read

83 - Miongoni Mwa Khutba Zake (A.S)

Miongoni Mwa Khutba Zake (a.s) - Ibn Shu’uba ameieleza katika Tuhaful’uquli’ uk. 146; Na Al-Qaadhi Al-Qudhaiy katika mlango wa tatu wa kitabu ‘Dasturu maalimil’Hukm’ uk. 59; Na Abu Na’im katika ‘Al’hilya’ Juz. 1, uk. 77; Na Al-Amidiy katika ‘Ghurarul’hukam.’

Nayo Ni Miongoni Mwa Khutba Za Ajabu, Na Huitwa ‘Al-Gharraau’:

“Ninamhimidi Allah (swt) ambaye amekuwa na daraja ya juu kwa nguvu Zake,1 na amekurubia kwa fadhila Zake,2 Mtoaji wa kila faida na fadhila, na muondoaji wa kila kubwa na dhiki. Ninamhimidi kwa ajili ya huruma na ukarimu Wake, na uwingi wa neema Zake. Na ninamwamini kwa kuwa ni wa mwanzo Aliye dhahiri,3 na ninamuomba mwongozo kwa kuwa yu karibu mwongozaji.

Na ninamuomba msaada kwa kuwa ni mshindi mwenye nguvu. Na ninamtegemea kwa kuwa ni mtoshelezaji, mnusuru. Na ninashuhudia kuwa Muhammad (s.a.w.w.) ni mja Wake na Mtume Wake, amemtuma ili kutekeleza amri yake, na kumaliza udhuru wake,4 na kutoa maonyo yake.5

“Nakuusieni! Enyi waja wa Mungu kumcha Mungu ambaye amekufanyiyeni mifano,6 na amekuwekeeni wakati maalumu wa maisha, na amekuvikeni riyasha (yaani vazi),7na ameyafaharisha maisha yenu8 na kuyaboresha, na amekuzungukeni kwa hesabu,9na amekuandalieni malipo, na amekutunukieni neema nyingi na takrima kwa wasaa. Amekuonyeni kwa hoja za wazi bainifu.

Amekufanyeni kwa idadi, na amekuainishieni muda, ndani ya nyumba ya balaa na mtihani, na kwenye nyumba ya mazingatio ninyi ni wenye kufanyiwa mtihani humo, nanyi mtahesabiwa matendo yenu.”

Kutahadharishwa Na Dunia

“Kwa kweli dunia kinywaji chake kimetibuka, chanzo chake kina udongo na tope. Mandhari yake yanavutia, na yanaangamiza.

Ni yenye kudanganya na kutoweka, na ni mwanga utowekao haraka na kivuli kipitacho, na ni nguzo iliyoelemea upande, mpaka anayeichukia aanzapo kuifurahia, na mwenye kuichukia aanzapo kuwa na matumaini, punde yainua miguu yake na kuirudisha chini na kumnasa mwanadamu kwa kamba yake, na kumuuwa pale pale kwa mishale yake, na kumfunga mtu,10 shingoni kamba ya kifo ikimuongoza kwenye malalo yaliobana (yaani kaburi), na marejeo ya upweke, na kuainisha mahali 11 - na thawabu za Aamali.12

Na hivyo hivyo waliokuja nyuma baada ya waliotangulia, kifo hakikomi kuziondoa nafsi, wala waliobakia hawakomi kutenda dhambi. Watafuatia mfano wao- (mfano wa waliotangulia katika matendo).

Wanapita kwa makundi mpaka upeo wa mwisho, na mwisho wa mambo, mpaka mambo yatakapokatika, dahari zitakapopita, na kukaribia kufufuka, Mungu atawatoa nje kutoka makaburini, na viota vya ndege, na maficho ya wanyama wakali, na katikati ya maangamizi.

Wataharakia kwenye amri Yake, wakienda haraka kuelekea maeneo yalioandaliwa kwa marejeo yao ya mwisho makundi kwa makundi, wakiwa kimya, hali wamesimama safu kwa safu, wakiwa katika kuonwa na Mungu wakiwa mahali mwitaji aweza kuwaita wamsikie.

Wakiwa na vazi la unyonge, wakifunikwa na unyenyekevu na udhalili, hila imekwisha, matumaini yamekatika, nyoyo zikiwa hazina furaha,13 sauti zikiwa zimedhoofu, hafifu, na jasho limekuwa kama hatamu,14 hofu imekuwa kubwa, na masikio yatakabiliwa na radi, kwa kelele ya sauti ya mfanya daawa, akiwaita kwenda kwenye upitishwaji wa maamuzi, na kupata malipo mbadala adhabu na kupata thawabu.”15

Kuwatanabahisha Viumbe

“Waja wenye kuumbwa kwa uwezo, na wamemilikiwa kwa kahari,16 na mamlaka, na watakufa kwa kuhudhuriwa na Malaika wachukuaji roho,17 na watawekwa kaburini, na hatimaye kuwa mifupa iliyochakaa, na watafufuliwa (kila mtu) pweke,18 na watalipwa malipo, na watafanyiwa hisabu kila mtu na yake 19 walipewa muda wa kujiepusha,20 na waliongozwa njia ya wazi,21 na waliruhusiwa kuishi na muda wa kutafuta maridhawa, na wameondolewa giza la shaka, na wameachwa kwenye medani ya mashindano ya farasi,22 na kuachwa wafikiri na kutafuta yahitajiwayo kwa mazingatio, kuwa na uvumilivu wa mtafutaji, anayejaribu kukipata kilichompotea, katika muda wa harakati za kazi kabla ya ajali.”

Ubora Wa Kukumbusha

“Mifano muwafaka ilioje na mawaidha yaponyayo! endapo yangeafikiana na nyoyo safi, na masikio sikivu, na rai zenye azma na akili thabiti!

“Mcheni Mungu uchaji wa mwenye kusikiliza na akanyenyekea, na atendapo ovu yu-atambua, na akiogopa hutenda yaliyo sawa, akiwa na hadhari huharakia kwenye mema, akiwa na yakini hufanya mema, akipewa mazingatio mara kadhaa huzingatia, akitahadharishwa hujihadhari, akikaripiwa hukaripika, aitwapo na wito wa mlinganiaji (kwa Mungu) hurejea kwake.

Arejeapo hutubu, na akifuata hufanya vizuri, akionyeshwa njia ya sawa huiona na yu aharakia akitafuta, na kuokoka mbio! na yuafaidika na mali, na kuwa na tabia njema, na kuyajenga marejeo, na akabeba masurufu mgongoni kwa ajili ya siku ya kuondoka kwake, na akaelekea njia aikusudiayo na hali ya haja yake, na mahali pa mahitaji yake, na kutanguliza mbele yake kwa ajili ya nyumba ya kubaki kwake.

Hivyo basi mcheni Mungu, enyi waja wa Mungu kwa upande wa lengo alilokuumbieni,23 na mjihadhari upeo wa kujihadhari na ambayo amekuhadharisheni nafsi yake,24 na kuweni wastahiki wa ambayo amekuandalieni,25 kwa kutekeleza ya wajibu,26 na kujihadhari na marejeo yake yanayotisha.”

Na Sehemu Hii Ya Khutba Kuwakumbusha Watu Neema Za Mungu

“Amekujaalieni masikio ili muweze kufahamu na kuyahifadhi aliyoyakusudia, na macho ili muweze kutandua tandabui ya giza giza, na viungo vya mwili vyenye kuwemo ndanimwe viungo vingine, na vyenye kulingana na umbo la mahali khusika katika muundo wa sura zake, na muda wa umri wao, na miili yenye kutekeleza manufaa yake, na nyoyo ambazo zimeshughulika kutafuta chakula chake, ndani ya neema zake zilizo funi- ka, na yawajibishayo upaji wake, na vizuizi vya afya yake.27

“Amekukadirieni umri aliousitiri mbali na (uelewa wenu) amekubakishieni mabaki ya athari za waliopita kabla yenu, ili iwe mwongozo kwenu, watu hao walistarehe na hisa zao kubwa, kwa nafasi bila ya kizuizi.28

Kifo kiliwachukua bila kufikia matumaini yao, (kifo) kiliwakata na kuwa’ngoa mbali nayo - matumaini - hawakujiandaa wakati miili iko salama, wala hawakuzingatia mwanzoni mwa umri wa ujana. Je wenye ngozi laini ya ujana wanangoja mpaka kupinda migongo kwa uzee!

Na ambao wana siha njema wanangoja kufikiwa na hali mbaya ya siha! Na walio na muda wa kubaki wanangoja mpaka uishe, pamoja na ukaribu wa kutoweka, na mbabaiko wa kutoweka, na kufikiwa na huzuni moyoni, na kusongwa na mate, na hofu ya mgonjwa na uchungu wa huzuni, na mbinyo wa mate.

Muda utafika wa kuomba nusra ya wajukuu na ndugu wa karibu, wapenzi na wenzi. Je! Ndugu wa karibu wamezuia, au vilio vimeleta nafuu!

Ameachwa mahali pa wafu amefungika, na kwenye malalo yaliyombana akiwa mpweke, wadudu wameirarua ngozi yake, na matukio yameuchakaza upya wake, na dhoruba itakuwa imefuta athari zake, na tukio litakuwa limefuta dalili zake, na miili itakuwa imehiliki baada ya kujaa kwake, na mifupa itakuwa imeoza baada ya nguvu zake, na nyoyo zitakuwa zimefungika kwa uzito wa mizigo (dhambi) yao, zitakuwa na yakini na habari zake zilizojificha, hazitotakiwa baada ya hapo kuzidisha Aamali zake njema29 wala hazitoombwa kutubia kwa ajili ya ubaya wa kuteleza kwake! 30

Je! Hamko wana wa kaumu hii, na mababa zao, ndugu na jamaa zao wa karibu? Mnafuata mifano yao na kuiga njia zao 31 na mwaenda njia zao, nyoyo ziko bado ngumu, zimeghafilika mbali na mwongozo wake, zaenda njia isiyokusudiwa! Kama kwamba mkusudiwa ni mwingine, kama kwamba mwongozo upo katika kukusanya dunia yake.”

Hadhari Ya Kitisho Cha As-Siiraat

“Na juweni kuwa mtapaswa kuvuka juu ya as-Siiraat nyayo zitateleza kiasi cha kumtupa mtu chini, na vitisho vya utelezi wake na mfululizo wa vitisho vyake.

Basi mcheni Mungu enyi waja wa Mungu uchaji wa mwenye akili, ambaye fikra zimeushughulisha moyo wake, na hofu imeutaabisha mwili wake, na sala ya tahadjudi imemfanya akeshe, na matumaini yamembakisha na kiu nusu ya mchana wa siku yake, (yaani anafunga mchana wake) na zuhudu imezuia matamanio yake, na dhikr ya Mungu imeufanya ulimi wake kuwa mwepesi, na ametanguliza hofu kwa ajili ya amani yake32 akajiepusha njia zilizo kombo kwa kufuata iliyo sawa, kwa ajili ya iliyo sawa, yu afuata njia iliyonyooka zaidi ili kuifikia njia ihitajiwayo; wala geuzo la ghururi halikugeuza fikra yake, wala mkanganyiko wa mambo haukumfanya asijue ukweli.

Akiwa katika hali ya furaha kwa bishara ya kufaulu neema ya maisha mema, katika neema kubwa ya usingizi wake, na siku yake yenye amani mno.

Akiwa amevuka kivuko cha hii haraka (dunia) mwenye kuhimidiwa,33 na akiwa ametanguliza masurufu ya baadaye akiwa na furaha, na ameharakia kutoka kwenye woga34 na akakaza mwendo katika muda wa uhai35 na akapenda kipaswacho, na kukiepuka kinachobidi, katika siku yake akaichunga kesho yake, na akaangalia yanayokuja mbele miongoni mwa a’amali, yaani akaangalia atakachokitanguliza miongoni mwa aamali.
Yatosha pepo kuwa ni malipo mema na mafanikio, na moto ni adhabu tosha na mateso, Mungu (swt) ni mlipizaji tosha na mnusuru! Na Kitabu (Qur’ani)36 ni hoja tosha na hasimu.

“Nakuusieni kumcha Mungu ambaye hakuacha udhuru kwa aliyoyaonya, na ametoa udhuru kwa onyo lake wazi,37 amekutahadharisheni na adui aingiae vifuani kwa kificho,38 na kupulizia masikioni kwa siri, kwa njia hiyo, amepotosha na kufanya uharibifu.

Atoa ahadi ya uwongo na kuyapamba maovu, na kudharau madhambi makubwa yaangamizayo, mpaka anapomporomosha kutoka daraja ya mwongozo mwenzi wake,39 naye atastahiki rehani yake, atakuwa yuakanusha aliyokuwa akiyapamba, na kuyakuza aliyokuwa akiyadharau, na kuyatahadharisha aliyokuwa akiyafanya yako salama.”

Miongoni Mwayo Maelezo Ya Kuumbwa Mwanadamu

Au mwangalie mwanadamu ambaye Mungu amemuumba ndani ya giza la mfuko wa uzazi na mifuniko ya sitara, ikibubujikiwa na manii, kisha likafanyika pande la damu lisilo na sura, baada ya hapo mimba, halafu kitoto kichanga kinyonyacho, kisha mtoto, baada ya hapo kijana, kisha amemtunukia moyo wenye kumbukumbu, ulimi wa kunenea, na macho yakuonea, ili aweze kufahamu na kuzingatia, apate kuacha kutenda maovu akijiziwia (kwa nguvu za mazingatio) afikiapo utu uzima, na kufikia kimo chake cha kawaida, na umbo lake kufikia kimo chake.

Akanusha kwa kiburi, aingiwa na ghururi na kubabaika bila kujali. Aijaza ndoo kubwa ya matamanio yake, afanya juhudi kukamilisha utashi wa dunia yake, katika matamanio yake, akienda na yanayomdhihirikia katika utashi wake. Kisha hakuogopa uovu wowote, wala kutishika wala kuwa na wasiwasi. Alikufa ndani ya maovu yake hali yukijana aliyeghurika. Aliishi akiwa makosani kwa muda mfupi. Hakufaidika na thawabu mbadala. Wala hakutekeleza wajibu wowote. Maradhi mabaya yalimkabili akiwa bado na ukaidi wake katika njia ya furaha yake kubwa, na alipitisha usiku akiwa kama amelewa.40

Alikesha akiwa katika shida ya majonzi na machungu, kufikiwa na uchungu na magonjwa, kati ya
ndugu na ndugu wa damu, na baba mwenye huruma, na mama anayelia akisema: ole wangu mwenye huzuni, dada apigaye kifua akiwa amefadhaika; na mtu yu katika sakarati ya mauti anataabika na shida ya kukatisha tamaa, na mvuto wa kuchukiza, na msukumo wa sakarati ya mauti.

Kisha yuatiwa ndani ya sanda akiwa mublisa41 mwenye kukata tamaa ya rehema ya Mungu avutwa kwa urahisi,42 kisha kutiwa ndani ya jeneza akiwa mwenye machovu ya kutupwa, na aliyekondeshwa na ugonjwa.

Akibebwa na wasaidizi vijana, na ndugu wasaidizi wambeba wakimpeleka kwenye nyumba yake ya upweke na na watu huacha kumzuru,43 na mahali pa upweke, mpaka wanaporudi waliokuwa wakimsindikiza na akarejea wenye huzuni, atakalishwa shimoni mwake akisemeshwa44 kwa faragha maswali ya kuduwaza, na mtihani wa kujikwaa.

Na balaa kubwa mno huko ni kuingia maji ya moto na kuteseka na Jahannam, na kutokota kwa moto, na ukali wa sauti ya moto, hakuna muda wa mapumziko, wala wa raha, wala nguvu ya kuzuia wala kifo cha kutuliza, wala usingizi wa kuliwaza, atakuwa kati ya aina mbalimbali za maiti,45 na adhabu za kila wakati na saa zote! Hakika tunajilinda na Mungu.

Enyi waja wa Mungu! Wako wapi ambao walipewa umri mrefu na kuneemeshwa! Walijulishwa na wakafahamu, na walipewa muda na wakaupoteza bure,46 walikuwa salama na wakasahau, walipewa muda mrefu wa maisha, waliumbwa kwa sura nzuri, walitahadharishwa machungu, waliahidiwa makubwa! Jihadharini na dhambi zinazoangamiza, na aibu zikasirishazo.

Enyi wenye macho na masikio na afya na mali! Je kuna upenyo! Au epuko, au kimbilio, au marejeo (yaani kurejea hapa duniani) au hapana? “Basi mpaka lini mwaibadilisha haki kwa batili?” (6:95) “Vipi mwaondolewa mbali na ibada ya Mwenyezi Mungu.” (40:62)
Au mwaghurika na nini! Hali ikiwa mmoja wenu hisa yake ya ardhi yenye urefu na upana ni kadiri ya urefu wake, mwenye kugusishwa shavu lake na mchanga (yaani maiti azikwapo ni sunna shavu lake ligusishwe mchanga kwa kuiondoa sanda aliyovikwa eneo la shavu lake).

Enyi waja wa Mungu! ni hivi sasa hali kamba haijakaza shingoni,47 na roho zimeachwa katika wakati wa kutaka mwongozo, hali miili iko na raha, na ukumbi wa kujikusanya,48 na muda wa maisha upo na mwanzo wa muda wa utashi,49 kuna nafasi ya kufanya toba, na nafasi ya wakati wa haja kabla ya shida, dhiki, hofu, na kubanwa, na kabla ya kuja mauti yanayongojewa na kabla ya shiko la Mwenye nguvu Muweza (swt).”

 • 1. Nguvu: Amekuwa na daraja ya juu kwa nguvu zake: Yaani ametukuka na kupaa kuliko kila kisichokuwa Yeye; kwa nguvu zake zilizo na mamlaka ya juu ya kuumba kuliko kila nguvu.
 • 2. Fadhila: Amekurubia kwa fadhila Zake: yaani Yeye pamoja na kuwa juu Kwake kwa utukufu, amesogea na kuwa karibu na viumbe Wake kwa fadhila Zake, yaani kwa upaji na ihsani Zake.
 • 3. Maana inakuwa: Namsadiki Mungu kwa kuwa yeye ni wa mwanzo kabla ya chochote katika kuwepo, kwa hivyo Yeye yu dhahiri dhati Yake na mdhihirishaji wa vingine, na mwenye kuwa hivyo kumsadiki kunakuwa hakuna shaka. Na aliye karibu na mwongozaji yapendeza aombwe hidaya, na muweza mshindi anafaa kuombwa msaada, kwa kuwa ndiye mwenye uwezo wa kusaidia. Na mtoshelezaji mnusuru ndiye wa kutegemewa.
 • 4. Kumaliza udhuru wake: Ni kufikisha kwake. Na udhuru hapa: Ni kinaya yamaanisha hoja ya kiakili na ya kunakili au kunukuu ukitaka, zilizowekwa kwa kutumwa kwake Nabii (s.a.w). Kwa kuwa mwenye kuhalifu sharia ya Mungu atastahili adhabu, na mwenye kuitekeleza anastahiki thawabu nyingi.
 • 5. Maonyo: Yaani utoaji habari wa ki-ungu wenye kuonya adhabu kwa kutenda maovu.
 • 6. Mifano ameileta katika maneno ili kuziweka wazi hoja na kuziimarisha ndani ya fahamu.
 • 7. Na sababu ya vazi kuwa neema: Kwa kuwa ni stara ya utupu, na ni hifadhi ya baridi na joto.
 • 8. Ameyafaharisha maisha, yaani ameyafanya kuwa ya hali ya juu yenye wasaa na kustawi.
 • 9. Amekuzungukeni kwa hesabu: yaani amejaalia hesabu za matendo yenu na kuyajua kama tendo la kuzungushia ukuta kiasi kwamba hamtotoka nje ya ukuta huo wala kuuvuka wala mtu yeyote kuachwa nje yake.
 • 10. Yaani imemtega na kumnasa kwenye mtego wa kamba zake yule mwenye kughurika nayo (dunia).
 • 11. Kuainisha mahali: yaani mahali ambapo mtu mukalafu - mwenye majukumu - atakapo fikia baada ya kifo, hapana budi kwa kila mtu mukalafu kuijuwa baada ya kifo hali yake itakavyo kuwa, peponi au motoni, na ataona mahali pake kati ya neema (za peponi) na (mateso ya) Jahannam.
 • 12. Thawabu za aamali: Anakusudia malipo kwa sura ya jumla yanayoienea furaha na mashaka.
 • 13. Nyoyo zimeporomoka: yaani hazina furaha wala matumaini ya kuwa na mafanikio, zikiwa kimya kwa kukabiliwa na mfadhaiko.
 • 14. Jasho limekuwa hatamu limekithiri kiasi cha kujaa midomoni kwa wingi wake na kuzuia uwezo wa kusema na kuwa kama hatamu.
 • 15. Mbadala: yaani ubadilishanaji wa malipo ya kheri kwa kheri na shari kwa shari.
 • 16. Iq’tisaran: wamilikiwa kwa ushindi: yaani wao kama vile walivyoumbwa kwa uwezo Wake Mungu (swt) na kwa nguvu Zake, pia wao ni wamilikiwa kwa mamlaka ya uwezo Wake, hawana hiyari katika hilo, na muda wao ujapo roho zao zitachukuliwa na kupelekwa Kwake (swt) na wanaohudhuria miongoni mwa watowao roho na nguvu yenye mamlaka juu ya uishaji wa viumbe.
 • 17. Asili ya kuhudhuria: ni kuhudhuria Malaika ili kuchukua roho. Na Waarabu walikuwa wakisema: Maziwa yemehudhuriwa, yaani yameharibika, wakimaanisha kwamba majini yamehudhuria na kuharibu yale maziwa, husemwa ‘al-Labanu muhtadhwaru faghatwi ina’aka’: Maziwa yamehudhuriwa, hivyo funika chombo chako.
 • 18. Watafufuliwa pweke: Yaani, kila mtu ataulizwa mwenyewe binafsi, haitozingatiwa jamii anayoungana nayo, kutokana na kauli Yake swt: “Walaqad ji’itumuna furada.” Hakika mmenijia kila mmoja pweke. (An-A’am: 94)
 • 19. Watafayiwa hesabu kila mtu na yake: Yaani kila mmoja atahesabiwa A’amali zake mbali na mwingine kutokana na kauli yake swt: “Na mbebaji hatabeba mzigo wa mwingine” 35:18): “Na enyi wakosefu! Jitengeni leo” (36:59)
 • 20. Walipewa muda: Yaani walingojewa ili watafute njia ya kutoka, yaani walingojewa warejee kwenye utii na watubu kwa ikhlasi, kwa sababu kufanya toba kwa ikhlasi ndio epuko la kutoka tanzi la maasi.
 • 21. Njia ya wazi: Ni njia ambayo sheria takatifu imeonyesha.
 • 22. Wameachwa: Yaani wameachwa uwanjani wanashindania heri. Na muda ambao uliowekwa. Na katika riwaya nyingine, ni mahali ambapo ni pa heri, yaani mahala ambapo wanashindana wachamungu kumridhisha Allah swt.
 • 23. Upande wa lengo alilokuumbieni: Yaani kusudieni upande ule ambao Mungu amekuumbeni kwa ajili yake huo, nao ni: Ibada, kwa sababu yeye swt amesema: “Sikuwaumba majini na watu ila waniabudie Mimi.” (adh-Dhaariyatu: 96) Yaani mcheni Mungu mkielekea upande ambao amekuumbeni kwa ajili yake, miongoni mwa matendo yenye kukunufaisheni yenye kubaki athari yake kwa watakaokuwa baada yenu.
 • 24. Ametuhadharisha nafsi yake (swt) tusijihusishe na yanayomghadhibisha kwa kuhalifu amri zake na makatazo yake.
 • 25. Kauli yake Amirul-Mu’minin (a.s.): “Kuweni wastahiki wa ambayo amekuandalieni: Yaani, mjijaalie binafsi wastahiki wa thawabu Yake ambayo amekuandalieni endapo mtatii.”
 • 26. Ukisema: Yatanajazul-haajata: Anaiharakia haja, anaifanikisha na anataka haraka yake, na An-Najizu: Al-Aajilu - ni mwenye haraka. Watanajuzu minal’mukallafina na kuharakia kwa Mukhallafin bisidqi miiadihi Sub’hanahu; kwa kusadikisha wajibu Wake (swt) Wa huwa muwadhabatuhum ala fi’ilil-wajibi, nako ni kudumu kwao juu ya tendo la wajiu, watajanubul-Qabiihi, na kujiepusha na maovu. Na uharakiaji huu wa matendo (mtu) huwa yuastahiki aliyowaandalia Mungu watu wema.
 • 27. Vizuizi vya afya: Yaani, afya inazuia madhara kwa ajili yenu.
 • 28. Na kadirio la maneno ni: Ameacha kwa ajili yenu mafunzo kutoka karne za watu waliopita, miongoni mwayo kustarehe kwao na hisa zao za dunia kisha kumalizika kwao, na miongoni mwayo ni wasaa wa kusongeka kwao na urefu wa muda walioachiwa, kisha mwisho wao ulikuwa ni kuangamia.
 • 29. Zitakuwa na yakini na habari zake zilizofichika: yaani zitakuwa zimefichukiwa na yaliyokuwa yamejificha miongoni mwa habari zake, na yaliyoandaliwa kwa ajili yake akhera, kwa kuwa mtu baada ya kifo chake hujua hali yake itavyokuwa kama ni peponi au motoni!
 • 30. Hawatokalifishwa baada ya hapo amali nzuri ya ziada, kwa sababu hapana amali baada ya umauti, wala haiombwi toba ya maovu; kwa sababu taklifu imetoweka.
 • 31. Al-Qidda: Husemewa kwa ajili ya kikundi cha watu wakiwa wako katika utashi wa aina moja, na kutokana na neno hilo, kauli Yake Mwenyezi Mungu swt: Wa kunna taraiqa qidada (al-Jinnu: 11). Na maana: mwafuata athari zao na mnashabihiana nao katika maten- do yao.
 • 32. Ametanguliza hofu kwa ajili ya amani yake: yaani ametanguliza hofu hapa duniani ili apate amani akhera, au ametanguliza hofu wakati ambao hofu yafaa wakati ule, kwa kuwa siku ikiwadia hofu haitomsaidia kitu mwenye hofu.
 • 33. Kivuko cha haraka: dunia na imeitwa kivuko cha haraka kwa sababu ni njia ambayo huvuka (mtu) kuiendea akhera, nayo ni ya baadae.
 • 34. Ameharakia kutoka kwenye woga: yaani ameharakia kutenda mema akiogopa asije kuyakuta yakutisha.
 • 35. Amekaza mwendo katika muhula wa uhai.
 • 36. Kitabu: ni Qur’ani. Na hoja na hasimu: yaani ni chenye kunaisha, kwa ambaye atak- wenda kinyume nacho atajikokotea maangamizi ya nafsi yake. Na inaweza ikakusudiwa kwamba kitabu ni yale yaliyoandikwa miongoni mwa a’amali za mtu atakapokabidhiwa Siku ya Hesabu.
 • 37. Ametoa udhuru kwa onyo lake. Au kwa maana ya: Ameondoa udhuru wa mtoa udhu- ru kwa onyo lake la hali ya matendo itakavyokuwa, na hoja upande wake imetimia dhidi ya wapotovu kwa yale aliyoyaweka wazi miongoni mwa njia za kheri na za ubora.
 • 38. Adui aliyetajwa: Ni Shetani, na kuingia kifuani ni tamthili ya uingiaji wa wasiwasi wake ndani ya nafsi, kwa hivyo yeye anayoyapamba yanakwenda mwendo wa pumzi, na anakwenda na anayokuja nayo kwa mwenendo wa marafiki kana kwamba ni mwandani anakupa siri na anakunong’oneza katika sikio lako ambayo unayadhania ni kheri kwako.
 • 39. Mwenzi hapa ni mwanadamu ambaye amekuwa mwenzi wa Shetani, Mungu (swt) amesema: “ni rafiki muovu mno!” (43:38)
 • 40. Na hapa makusudio yake (a.s.) ni: Maradhi yaliyomuangamiza, na hiyo ilitokea baada ya kukabiliwa na huzuni za kifo: nazo ni uzukaji wa maradhi ya kuangamiza yasababishayo kifo.
 • 41. Mublisu: Ambaye amekata tamaa ya kupata rehema ya Mungu, ukisema ablasa: yaani ni amekata tamaa. Na humo limechukuliwa neno Ibilisi. Na Iblis pia: ni kule kuingiwa na huzuni baada ya kukata tamaa kwa kila hali.
 • 42. Kuvutwa kwa urahisi hapa kunaishiria kuishiwa na uwezo kiasi cha kushindwa kukataa kitu.
 • 43. Nyumba yake ya upweke: ni kaburi lake. Na pia kukatika kwa ziara yake: kwa sababu kutembelewa kutakatika, hatofanyiwa ziyara.
 • 44. Atakalishwa shimoni mwake akisemeshwa: Hili ni tamko la wazi kuhusu adhabu ya kaburini.
 • 45. Akusudia machungu makubwa, na kila aina ya mateso miongoni mwa mateso ya adhabu, ni kama mauti kwa shida yake.
 • 46. Walipewa muda wakahadaika na kuacha kutenda mema, na hiyo baada ya kuwa wali- julishwa na kufahamu, na ilikuwa kwa muktadha wa kufahamu wasingedanganyika na muda na kuipoteza fursa!
 • 47. Yaani fanyeni mema hivi sasa mkiwa huru, mnao uwezo, kamba haijakazwa shingoni mwenu, na roho zenu hazijakamatwa.
 • 48. Ukumbi wa kujikusanya: Yaani, ninyi mpo katika uwanda ambao inakuwieni rahisi humo kushirikiana katika mema ninyi kwa ninyi.
 • 49. Ni mwanzo wa wakati wa azma ya kufanya jambo na kuchagua, lau kama mngepen- da kuanza tena utashi na azma ya kufanya mema mngeweza.