read

84 - Na Miongoni Mwa Khutba Zake (A.S)

Katika Kumuelezea Amru Ibnul-A’as

“Namshangaa ibn An-Nabighah! eti asema akiwa kati ya watu wa Syria (Sham) kuwa mimi ni mtu wa mzaha, na kuwa mimi ni mtu wa mchezo mwingi, najishughulisha na mieleka na kupigana na watu. Amesema batili na ametamka akiwa na dhambi.

Angalieni, (maneno ya uovu mno ni uwongo) naye yuasema na yuadanganya, anaahidi na yuaenda kinyume, anaomba kwa kung’ang’ania1na akiombwa yuafanya ubakhili, anavunja ahadi, na anaukata udugu. Awapo vitani yeye ni mkemeaji na muamrishaji!

Hapo ni ikiwa panga hazijachukua nafasi yake, na zikichukua nafasi yake, ujanja wake mkubwa ni kuwaonyesha maadui zake utupu wake. Ama mimi wallahi kukumbuka mauti kwanizuia kufanya mzaha, na kwa kweli yeye kimzuiacho kusema kweli ni kuisahau akhera, kwa hakika yeye hakumpa bai’a Muawiya mpaka alipompa sharti ya kupewa kitu.”2

  • 1. Anaomba na yuafanya ilhafu, kuomba kwa ilhafu ni kung’ang’a- nia kuomba. Mungu (swt) amesema: “hawang’ang’anii watu wakiwaomba” (2:273).
  • 2. Na makusudi ya chochote kitu hapa alichokuwa akitaka apewe ni kumfanya awe gavana wa Misri.