read

85 - Miongoni Mwa Khutba Zake (A.S)

Miongoni Mwa Khutba Zake (a.s) - al-Wasitiy ameitaja katika Uyunul-Hikami wal Mawa’idhy, na Ibn Sibt Jauziy katika Tadhkiratul-Khawa’is uk. 131.

Katika Kumwadhimisha Mwenyezi Mungu Na Kumtukuza

“Na ninashuhudia kuwa hapana apasaye kuabudiwa isipokuwa Allah swt. peke Yake, hana mshirika, ni wa milele (bila mwanzo) alikuwa yupo wakati hapakuwa na kitu kingine, na ataendelea kuwepo baada ya kutoweka kwa kila kitu, Yeye hana kikomo. Dhana haiambui kumpata na sifa, wala nyoyo haziwezi kumuelewa kwa aina, wala hapatwi na ufanywaji wa sehemu sehemu wala kufanywa kwa mfano kwamba hii ni baadhi ya sehemu ya Mungu. Hazungukwi na uoni wa macho na wa nyoyo.”1

Na Sehemu Yake Nyingine (Ya Khutba) Kuielezea Pepo

“Tabaka zinazo zidiana, na daraja zinazo tafautiana, neema zake hazikati- ki, atakayedumu humo hatozeeka, wala mkazi wake hatokuwa fakiri.”

  • 1. Katika mlango huu, pamoja na ufupi wake, kuna mas’ala manane miongoni mwa mas’ala za Tawhiid: Ya kwanza: Ni kuwa hakuna wa pili yake (swt) katika Uungu. Pili: Yeye ni wa milele yote tangu na tangu hana mwanzo wala mwisho. Tatu: Yeye ni Abadiyu: yaani dhati yake haina mwisho. Nne: kumkanushia sifa. Tano: kumkanushia jinsi. Sita: kuwa Yeye (swt) hagawanyiki, kwa kuwa Yeye sio mwili wala sio kiumbe ambacho si mwili kama vile uzito, na wepesi. Saba: Kuwa Yeye haonwi wala haipiti katika akili ya mtu kuwa yuko hivi. Nane: Dhati yake haijulikani.