read

86 - Na Miongoni Mwa Khutba Zake (A.S)

Na Miongoni Mwa Khutba Zake (a.s) - Ad-Dainuriy ameitaja katika al-Akhbar at-Twiwalu uk. 145; na ibn Shu’ba katika Tuhaful- Uqul uk. 100, na al-Barqi katika al-Mahasimu uk. 233.

Kuhusu Waadhi Wa Kujiandaa Kwa Ajili Ya Ulimwengu Mwingine Na Kufuata Amri Za Mungu

“Amezijua siri, na habari ndani ya dhamiri, yuakizunguka kila kitu, na mwenye kukishinda kila kitu, na mwenye nguvu juu ya kila kitu. Basi mtendaji miongoni mwenu na atende ndani ya muda wa (uhai) wake kabla ya kukabiliwa na ajali yake. Na atende wakati wa wasaa kabla ya kushughulishwa kwake, na wakati wa nafasi yake kabla hajashikwa koo.1

Ajiandae kwa ajili ya nafsi yake na safari yake, na aandae masurufu kutoka kwenye nyumba ya kituo chake (cha muda) kwa ajili ya nyumba ya kudumu kwake.

Mkumbukeni Mungu swt. enyi watu, kwa aliyokutakeni ndani ya Kitabu chake kuyazingatia, na haki Zake alizozihifadhi humo, kwa kuwa Mungu (swt) hajakuumbeni bure, na wala hajawaacheni bila ya faida, wala hajawaacha katika ujinga wala upofu. Amepandisha daraja ya athari zenu, na amejua amali zenu, na ameamua ajali zenu.

Na amekuteremshieni Kitabu kinachobainisha kila kitu, na amemrefushia umri nabii Wake kwa zama ndefu, kiasi cha kumkamilishia yeye na ninyi ujumbe - aliouteremsha Kitabuni mwake - ambao ni dini Yake ambayo ameiridhia nafsini Mwake; na amebainisha kwenu - kupitia ulimi wake - matendo mema na mabaya, makatazo Yake na amri Zake, na ameweka mbele yenu hoja Yake na kuondoa udhuru kwenu, amekukemeeni na kuwaonya na adhabu kali. Hivyo basi zidirikini siku zenu zilizobaki, na zifanyeni nafsi zenu zivumilie humo. Kwa kuwa ni chache katika siku nyingi ambazo mnakuwa katika mghafala, na kutotilia manani mawaidha, msiuachie muda, utawawekeni katika njia ya madhalimu, na msijipendekeze, kwa kuwa kujipendekeza kutawasukumeni kwenye maasi.

Enyi waja wa Mungu! Kwa kweli mnasihi mzuri mno wa nafsi yake katika watu ni yule mtii mno wa Mola Wake;2 Na kwa kweli mwenye kuighushi mno nafsi yake ni muasi sana wa Mola Wake;3 na mwenye kupunjwa ni yule ambaye ameipunja nafsi yake, na mwenye kutamani mfano wa hali ileile4 ni yule ambaye dini yake iko salama, na mwenye furaha ni mweye kuwaidhika na mtu mwingine, na dhalili ni mwenye kuhadaika na utashi wa nafsi yake na kughurika kwake. Jueni kwamba kuwepo kwa kiasi kidogo cha riya’a5 - ni ushirikina, na kukaa na watu wanaofuata matamanio ya nafsi zao - hawaa - yaliyoko nje ya maadili ya kisharia - kunasahaulisha imani, na ni mahudhurio ya Shetani.

Jiepusheni na uwongo, kwa kuwa ukando na imani. Mkweli yu ukingoni mwa wokovu na heshima, na muongo yuko katika kilele cha kuanguka na kudharauliwa. Msihusudiane, kwa kuwa husuda huila imani kama moto ulavyo kuni.

Msibughudhiane, kwa kuwa huko ni kwenye kufuta imani;6 na jueni kwa mba kuwa na matumaini mno - kunaisahaulisha akili na kumbukumbu.7 Basi yakidhibisheni matumaini kwa kuwa ni ghururi, na mwenye nayo ameghurika.”

  • 1. Kushikwa koo: Ni kinaya - yaani kule kubanwa wakati wa kuifariki dunia.
  • 2. Kwa kuwa yeye ameihifadhi isiadhibiwe, na kuiwajibishia thawabu, na huo ndio upeo wa nasaha.
  • 3. Mwenye kuighushi mno nafsi yake kati ya watu ni yule muasi mno kwa Mola Wake kwa kuwa yeye ameitumbukiza katika maangamizi ya daima, na huo ni upeo uwezekanao wa kuighushi na kuidhuru nafsi.
  • 4. Mwenye kutamani mfano wa hali ile ile hapa ni tafsiri ya: naye ni mtu aionaye neema kwa mwenzake naye akatamani apate neema kama ile bila ya kumtakia kinyume yule aliyetunukiwa neema hiyo.Waila itakuwa ni mwenye husuda.
  • 5. Riya’a ni kufanya tendo la kheri ili wakuone watu kwa ajili ya sifa hali moyo wako ulikuwa haupendi kufanya, (pia yawezekana moyo ulikuwa wapenda lakini mbele ya watu ukahamasika zaidi na ukaongeza mikogo katika tendo la kheri kutaka sifa).
  • 6. Kwenye kuifuta kila kheri na baraka. Na kwenye kung’oa ambayo huwajia kaumu kama kinyozi wa nyele.
  • 7. Matumaini ambayo husahaulisha akili na kumkumbuka Mungu na amri zake, na makatazo yake, ni kule kutuwama nafsi pale ilipofikia, haitazamii mabadiliko ya hali ya mambo, wala haina azma katika kazi.