read

87 - Na Miongoni Mwa Khutba Zake (A.S)

Na Miongoni Mwa Khutba Zake (a.s) - Zamakhshari ameieleza katika Rabiul-Abrar mlango wa al-izzu
wa sharaf.

Kuhusu Ampendaye Mungu Mtukufu

“Enyi waja wa Mungu! Kwa kweli miongoni mwa waja wapendwao mno na Mungu ni mja ambaye Mungu amemsaidia kupambana na nafsi yake, akawa yuaifanya huzuni ni shi’aru yake - vazi la ndani,1 na amevaa joho la hofu, kwa hiyo taa ya mwongozo ikaangaza moyoni mwake, na aka andaa takrima kwa ajili ya siku yake atakayofikia, kwa hivyo akasogeza kwa ajili yake kilicho mbali, na akapoza makali ya shida,2 ameangalia akatambua, akakumbuka na akakithirisha.3

Alipoza kiu kwa maji baridi aliyorahisishiwa maendeo yake, akanywa na kutosheka. Akapita njia iliyosawa, akiwa amevua vazi la matamanio, na kujiepusha na mahangaiko ya moyo, isipokuwa hangaiko moja pekee amebaki nalo,4 kwa hiyo akawa ametoka na kuwa mbali na sifa za upofu, na mbali na kushirikiana na watu wa matamanio, hivyo akawa miongoni mwa funguo za milango ya uongofu, na vifungio vya milango ya kuangamia.

Ameiona njia yake na akaipita njia hiyo, na akaijua miongozo yake, akaivuka bahari yenye maji mengi iangamizayo, na akashikamana na kishiko kwa umadhubuti, na miongoni mwa kamba iliyo ngumu mno, kwa hiyo yeye kwenye yakini yu kama mwanga wa jua, ameisimamisha nafsi yake kwa ajili ya Mungu (swt) katika mambo ya hali ya juu kabisa; kwa kulikabili kila limfikalo, na kuchukua kila hatua ihitajiwayo kwa hilo, na kulirudisha kila tawi kwenye shina lake.5

Ni taa ya giza jingi, mfichuaji wa upofu, ni ufunguo wa yaliyofumbika, mzuiaji wa shida, mwongozaji wa jangwani, akisema yuafahamisha, akinyamaza husalimika.

Amekuwa na ikhlasi kwa Mungu naye akamfanya makh’susi kwa ajili Yake, hivyo yeye ni chimbuko la dini Yake, na vigingi vya ardhi Yake. Amejiambatanisha binafsi na uadilifu, na ukawa uadilifu wake wa kwanza kujiondolea utashi wa kibinafsi.

Anaielezea haki na anaitendea kazi, haachi lengo la kheri ila atalikusudia, wala padhaniwapo kheri ila atapaendea. Amekishika Kitabu hatamu zake 6 nacho ndio kiongozi wake na Imamu wake. Anashuka pale ambapo kinapoifikisha mizigo yake, 7 na anateremka mahali pake pakufikia.”

Sifa Za Mtu Faasiqi

“Na mwingine amejiita mwanachuo hali akiwa si mwanachuo,8 amedondoa dhana za kijahili kutoka kwa majaahili, na upotovu kutoka wapotovu, na amewategea watu mtego uliotengenezwa kwa kamba ya udanganyifu, na maneno ya uwongo; anakichukuwa Kitabu-Qur’an - kwa maoni yake; na ukweli ameupindisha kulingana na utashi wake binafsi.

Anawafanya watu wajione wako salama watendapo makosa ya jinai, na hulichukua kosa kubwa kama ni kitu chepesi, anasema: ‘Nasita kwenye mambo yasiyo wazi,’ na humo yuajiingiza; na anasema: ‘najiepusha mbali na bid’a,’ na punde amejiingiza humo. Hivyo basi sura yake ni ya mtu, na moyo ni moyo wa mnyama, hajui mlango wa uongofu ili aufuate, wala mlango wa upotofu ili aufunge akiwa mbali nao, na huo ni umauti wa walio hai. “Basi mpaka lini mwaibadilisha haki kwa batili?(6:95) Vipi mwaondolewa mbali na ibada ya Mwenyezi Mungu.” (40:62)

Na alama zipo,9 Na aya ziko wazi, na minara imesimamishwa,10 mnapotezewa wapi! na vipi mnakuwa vipovu na kati yenu kuna itrah ya Nabii wenu!11 Nao ndio hatamu za ukweli,12 na ni alama ya dini, na ndimi za ukweli! Hivyo wawekeni daraja nzuri mno ya Qur’an,13 na muwaendee mwendo wa ngamia walio na kiu.14 “Enyi watu! Chukueni kutoka kwa Khatamun-Nabiyina - hitimisho la Manabii (s.a.w.w.): (Kwa hakika hufa afaye katika sisi na wala si mfu,15 na huoza aliyeoza katika sisi wala hakuoza) hivyo basi msiseme msiyoyatambua, kwa hakika ukweli mwingi upo katika myakanushayo.16

Kubalini udhuru wa msiye na hoja dhidi yake - naye ndimi - je sikuifanyia kazi kwenu thiq’lu kubwa!17 Na ninaiacha kwenu thiq’lu ndogo? Na nikasimika katika nyinyi bendera ya imani, na nimekusimasheni kwenye mipaka ya halali na haramu, na nikakuvisheni afya kutokana na uadilifu wangu, na nimekukukunjulieni mema kwa kauli yangu na vitendo vyangu, na nimekuonyesheni tabia njema za hali ya juu kutoka kwangu mimi mwenyewe binafsi. Hivyo msitumie rai katika ambayo hakifikiwi kina chake na macho, wala fikra haziingii.18

Na Sehemu Ya Khutba Hii Kuwahusu Bani Umayyah:

“Mpaka atadhania mwenye kudhani kuwa dunia imefungwa aqal, kwa Bani Umayyah, yawapa kheri zake,19 na kuwaongoza kwenye chemchemi safi za manyweo yake, na wala ummah huu hautaondolewa mjeledi wala upanga wake, na atakuwa ameongopa adhaniaye hivyo. Bali hilo ni tone la maisha ya ladha20 (watalila kwa muda kisha watalitema lote).”

 • 1. Huzuni ameifanya Shi’aru: Na shi’aru ni vazi la ndani. Kwa hiyo huzuni ameifanya kama vazi la ndani, na huzuni hapa ni uelewa wa kushindwa kutekeleza wajibu ipasavyo, nalo ni jambo la kiroho, athari yake haidhihiri kwa umbali ambao Mungu anaghadhibika, na kuharakia kutenda yanayomridhisha, na hiyo ni athari ya nje.
 • 2. Kujisogezea karibu kilicho mbali: yaani umauti udhaniwao uko mbali akausogeza karibu, kwa kutenda mema kwa ajili yake siku utakapomshukia, kwa hiyo akalegeza shida ya uvumilivu wa kuziacha ladha za mpito na kuwa makini kujipatia ubora wa juu kabisa, na hiyo ndiyo shida.
 • 3. Amemkumbuka Mungu akakithirisha matendo mema ili kumridhisha.
 • 4. Hangaiko moja, nalo ni la kubaki ndani ya mipaka ya kisharia.
 • 5. Kwa kuwa ambaye kwake la muhimu ni kubakia ndani ya mipaka ya Mungu, katika amri zake na makatazo yake, uoni wake hupenya mpaka kuufikia ukweli wa siri za Mungu katika hayo na anakuwa katika daraja ya ir’fani kiasi kwamba halimfikii jambo ila atalitoa kama lilivyo, wala halimtokei tawi ila atalirudisha kwenye shina lake.
 • 6. Kitabu ni Qur’ani, kushika hatamu zake ni tamthili, anamaanisha kuzitekeleza kwake hukumu zake, yeye anakuwa kama farasi na Kitabu kinamsukuma mahali kinapopenda.
 • 7. Mizigo hapa yakusudiwa: amri na katazo yanayobebwa na Kitabu.
 • 8. Huyu ni mja mwingine (mmoja katika aina nyingine ya watu) sio mja yule aliyemuelezea sifa zake zile za mwanzo, sifa za huyu zatofautiana na zake.
 • 9. Alama hapa: ni miujiza.
 • 10. Na minara hapa: Ile iliyosimamishwa ikiwa ni alama ya kheri na shari.
 • 11. Itrah ya Mtume ni kizazi chake, na si kweli isemwe kuwa ni ukoo wake japo wawe wa mbali. Na Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) aliwabainisha Itrah wake ni akina nani, pale alipowafunika shuka, na akasema: ‘inniy tariku fii kum athaqalayni’ akasema: ‘Itratiy ah’lu baytiy’ na katika kikao kingine alibainisha Ahlul-Bayt wake ni nani alipowafunika shuka na akasema ilipoteremka: “innama yuriidu llahu liyudh’hiba ankumur-rijsa ah’lal’bayti.” (33:33): Allahuma haulai ah’lubaytiy fadh’hib rijsa anhum, na kwa Itrah Amirul-Mu’minin alikuwa anajikusudia mwenyewe binafsi na watoto wake wawili; na asili yake kwa ukweli ni yeye mwenyewe, kwa kuwa watoto wake wamfuata yeye.
 • 12. Ameufanya ukweli kana kwamba wazunguka pamoja na wao wanakozungukia, kama ilivyo kwa ngamia, hutii na huielekea hatamu yake inakozungukia. Na Mtume (s.a.w.w.) alitoa habari ya ukweli wa kadhia hii kwa kauli yake: “na izungushe haki pamwe na yeye azungukiako”.
 • 13. Wawekeni daraja nzuri mno ya Qur’ani chini yake kuna siri kubwa, na hivyo ni kuwa yeye amewaamuru mukalafeena waipitishe Itrah katika kuitukuza, kuiadhimu na kuongoka na mwongozo wao, na utii wa amri yao kwa mwendo wa Qur’ani, anasema: iwekeni Itrah ya Nabii mioyoni mwenu mahala pa Qur’ani kwa kuiadhimu, kuitukuza na kuiheshimu, na kwa kweli moyo ni mahali pazuri pa materemkio ya Qur’ani.
 • 14. Mwendo wa ngamia wenye kiu: Yaani kuweni na hima kuchukua elimu na dini kuto- ka kwao, mfano wa hima ya ngamia wenye kiu sana wayaendeapo maji. Njooni kwenye bahari ya elimu yao haraka kama waharakiavyo ngamia wenye kiu maji.
 • 15. Ichukueni kadhia hii kutoka kwake, nayo ni: Mtu hufa kutoka miongoni mwa Ahlul’Bayti naye kiukweli si mfu, kwa sababu ya kubakia roho yake yamwetuka nuru kati- ka ulimwengu wa dhahiri.
 • 16. Mjinga huufunika ukweli na kuukanusha, na kwa hakika kweli nyingi ziko kwenye kina cha ndani zaidi.
 • 17. Thiq’lu hapa ni kitu chochote cha thamani kubwa, na limekuja neno hili katika hadi- ithi kutoka kwa Nabii (s.a.w) alisema: Nimekuachieni vya thamani viwili, Kitabu cha Mungu na Itrah yangu, yaani vyenye thamani viwili. Na Amirul-Mu’minina ameitendea kazi thiq’lu kubwa nayo ni Qur’ani na ataiacha thiq’lu ndogo nayo ni watoto wake wawili. Yasemwa: kuwa Itrah yake ni mwongozo kwa watu.
 • 18. Aliwakataza wasitumie rai kuyahusu aliyowaambia juu sifa bainifu za Al’Itrah na maa- jabu aliyowatunukia Mungu (swt). Akasema: Kwa kweli suala letu ni gumu akili haiwezi kulifikia, wala macho hayakifikii kina chake wala fikra haziingii kiasi cha kulifikia!
 • 19. Yawapa kheri zake: Yaani ameijaalia dunia kama ngamia aliyefungwa kwa ajili yao, ni kwa wao tu, ametiishwa kwa ajili yao, kana kwamba wao wamemfunga kwa aqal anawap- atia kheri yake, yaani anawapatia maziwa yake.
 • 20. Funda la maisha ya ladha: funda ni kiasi cha ujazo wa maji mdomoni kwa mara moja, mtu huyasukutuwa na haraka anayatema, huo ni mfano, na hapa imetafsiriwa kwa maana ya tone la asali limekuwa midomoni mwao kama linavyokuwa mdomoni mwa nyuki, wataionja kwa muda kisha wataitema. Kwa hiyo ni mfano wa maisha ya raha waliyopewa Bani Umayyah, ni mfano wa tone la asali limekuwa midomoni mwao kama linavyo kuwa kinywani mwa nyuki, wanalionja (utamu wake) muda, kisha wanalitema.