read

88 - Na Miongoni Mwa Khutba Zake (A.S)

Na Miongoni Mwa Khutba Zake (a.s) - al-Kailaniy ameieleza katika ar-Raudhwa uk.62, na Sheikh al-Mufiidu katika ar-Rishadu uk.173, na Ibn Athir amezitafsiri (hadith) ghariib katika an-Nihaya mada ya Azalu.

Katika Kuelezea Makosa Waliyonayo Watu

“Amma ba’ad. Kwa kweli Mungu hakupata kumuangamiza dhalimu wa zama fulani katu isipokuwa baada ya kumpa fursa na raha, wala hakuuganga mfupa wa yeyote katika wana umma isipokuwa baada ya dhiki na shida, na hakuwakabili kwa misiba na shida juu yao hata kwa kiasi kidogo kuliko ambacho kitawafikeni au tayari kimewafikeni, kinatosha kuwa somo. Wala sio kila mwenye moyo ni mwerevu, wala sio kila sikio ni sikivu, wala sio kila aangaliaye ni mwenye kuona.

Ajabu ilioje! Nitakuwaje nisistaajabishwe na makosa ya vikundi hivi kwa tafauti za hoja zao katika dini yao! Hawafuati athari ya Nabii (wao) wala hawaongoki na matendo ya waswii, wala hawaamini ghaibu, wala hawajiepushi na jambo la aibu, wanatenda katika mambo yanayoshakiwa, na wanakwenda na matamanio.

Kwa wao jema ni lile wanalolipenda wao, na ovu kwao ni walikataalo,1 kimbilio lao katika matatizo ni kwao wenyewe binafsi, mategemeo yao katika mambo yanayoshakiwa ni rai zao. Kama kwamba kila mmoja ni imamu wa nafsi yake,2 amejiamulia ayadhaniayo kuwa ndiyo tegemeo, na ni sababu thabiti.”

  • 1. Yaani waliona zuri walipendalo, na kuliona baya waonalo binafsi kuwa baya, bila ya kurejea kwenye dalili iliyo bayana, au kwenye sharia iliyo wazi, kila mmoja wao anajiamini kwa mawazo ya binafsi, kana kwamba ameshika kishiko madhubuti, kwa ule ujinga na kasoro walizonazo.
  • 2. Kana kwamba kila mmoja kati yao ni Imamu mwenyewe binafsi, yaani kuwa wao hawachukui shauri kwa mwanachuoni, wala hawamuulizi mjuzi, bali kimbilio lao pindi yatokeapo mambo yenye mushkili ni kwao wenyewe binafsi na rai za kibinafsi. Na hii ni sifa ya anayejigamba kuwa ameelimika na kuwa yu mbora.