read

89 - Na Miongoni Mwa Khutba Zake (A.S)

Na Miongoni Mwa Khutba Zake (a.s) - al-Qummiy ameisema katika Tafsiir yake uk. 3, na al-Kailaniy katka Usuli, uk. 69.

Azielezea Hali Za Watu Walivyokuwa Kabla Ya Bi’itha:

“Amemtuma wakati wa mwanya baada ya mitume,1 na usingizi mrefu kati ya umma, na kukithiri kwa fitna, na kuenea kwa mambo, na kulipuka kwa vita, na dunia imetoweka nuru, ghururi imejitokeza; wakati jini lake limekuwa manjano, na kukatishwa tamaa na matunda yake.2
Na kutoweka maji yake, minara ya uongofu imefutika, na zimejitokeza alama za kuangamiza, na zimefinya nyuso zao,3 mwenye kukunja uso mbele ya mwombaji wake, tunda lake ni fitna, na chakula chake ni mzoga,4 na nguo yake ya ndani ni woga, na nguo yake ya juu ni upanga,5hivyo zingatieni enyi waja wa Mungu, na (ikumbukeni ile) 6 ambayo baba zenu na ndugu zenu wako rehani,7 kulingana nayo watahesabiwa. Kwa umri wangu, muda wenu haujapishana sana na wao, wala haijapita kati yenu na wao miaka wala ummah, wala ninyi hii leo na siku mlizokuwa migongoni mwao sio mbali.

Wallahi Nabii hakuwasemesha kitu ila hii leo na mimi ni mwenye kuwasemesha nacho, na ambalo mmelisikia leo haliko tafauti na walilo sikia jana. Macho hayakuwa wazi kwao, na mioyo iliyokuwa kwa ajili yao wakati ule, ni sawa na ile mliyo nayo hivi sasa.

Wallahi hamkuwa mmeambiwa chochote baada yao ambacho hawakuwa wanakijuwa, na hamkupewa chochote ambacho wao walinyimwa, na kwa kweli balaa imewashukieni,8 inayumba hatamu yake, kamba yake iliyolegea. Isi kughurini hali waliyo nayo watu walioghurika, kwani hicho ni kivuli kilichopanuka mpaka muda uliopangwa.9

  • 1. Ni muda wa kukatika kwa risala na wah’yi, na ilikuwa kati ya Muhammad (s.a.w.w.) na wakati wa zama za Masihi (a.s) ni muda mrefu. Waliowengi miongoni mwa watu wanasema ni miaka mia sita.
  • 2. Neno hilo na la baada yake ni methali ya kugeuka kwa dunia na kuwa i karibu na kutoweka, na watu kukatishwa tamaa na starehe yake zama za jahilia.
  • 3. Ufinyaji wa nyuso: Yaani mtu alipokeapo jambo asilolipenda sura yake huwa imekunjamana.
  • 4. Yaani haina natija isipokuwa fitna, chakula chake ni mzoga: yaani chakula cha zama za jahiliya ni mzoga kwa sababu ya kudharurika sana, au ni kwa istiara, yaani chakula chake ni kibaya mno. Na kuna riwaya yasema: “chakula chao ni hofu”.
  • 5. Ameifanya hofu na upanga kuwa ni shiaru na ditharu, yaani nguo ya ndani na ya nje, kwa hiyo shiaru ni ile inayoambatana na mwili na dithari huja juu yake, kwa hiyo ameifanya hofu kuwa nguo yake ya ndani kwa sababu ni ya karibu mno na mwili, na kuifanya nguo ile ya juu inaifuata ya ndani, hivyo basi hofu iko ndani na upanga upo nje waziwazi. Na haya ni maneno safi mno.
  • 6. Yaani ikumbukeni dunia, au amana aliobebeshwa mwanadamu na akaibeba, au ni ishara ya matendo maovu, na itikadi batili na matokeo mabaya.
  • 7. Wako rehani yaani wamewekwa mahabusi kwa matokeo yake duniani kama vile udhalili na unyonge.
  • 8. Yaani mtihani mkubwa, alikusudia fitna ya Muawiyah na Bani Umayyah.
  • 9. Kwa kweli hicho ni kivuli kilichopanuka, mpaka muda uliowekwa: Ameyafanya walio kuwa nayo walio ghurika mfano wa kivuli kwa kuwa yametulia katika muono wa jicho hali yakiwa katika hali ya haraka katika ukweli wake, yaendelea kupungua, kwa hivyo yashabihiyana na dunia.