read

90 - Na Miongoni Mwa Khutba Zake (A.S)

Na Miongoni Mwa Khutba Zake (a.s) - al-Wasiti ameisema katika Uyunul-Hikami, na al-Aamidi katika Ghuraru-Hikami uk. 185, na Ibn al-Athir katika an-Nihaya, Jalada la 2, uk. 345.

Kuhusu Baadhi Ya Sifa Za Viumbe

“Shukrani ni zake Mungu (swt) aliye maarufu bila ya kuonwa, na ambaye ni muumba bila ya kufikiri,1 na ambaye hakukosa kuwapo yu thabiti daima; 2 pindi hapakuwa na mbingu zenye njia kuu za sayari (zodiac), wala pazia zenye vifungo vikubwa vya fahari,3 wala usiku wenye giza, wala bahari tulivu, wala jabali lenye njia, wala njia yenye kupinda pinda, wala ardhi yenye tandiko, wala viumbe wenye nguvu na kutenda kwa makusudi na utashi, Yeye ndiye mwenye kubuni uumbaji na mwenye kubaki baada yao, Mungu wa uumbaji na mtoaji wa riziki.

Jua na Mwezi vinatembea kwa uthabiti katika ridhaa Yake. Vinakifanya kikuukuu kila kipya, na kila kilicho mbali vinakisogeza karibu.

“Amezigawa riziki zao, na amedhibiti kwa idadi athari zao,4 na amali zao, idadi ya pumzi zao, na ishara za kukonyeza kwao, na ambayo yafichwa na vifua vyao miongoni mwa dhamiri,5 Anajua makazi yao ya muda, na mahali pa makazi yao ya kudumu, hali wakiwa katika matumbo ya uzazi na migongoni,6mpaka wafikiapo mwisho wao.

“Yeye ndiye ambaye adhabu Yake itakuja kuwa kali kwa maadui zake japokuwa huruma Zake ni zakutosha. Na rehema Zake zimewaenea wapenzi wake japokuwa adhabu Yake ni kali. Humdhibiti anayekusudia kumshinda Yeye.

Muangamizaji wa anayempinga, na humdhalilisha amuendae kinyume, mshindi wa amwendeaye kwa uadui. Humtosheleza amtegemeaye, na mwenye kumuomba humpa, na mwenye kumkopesha anamlipa, 7Na mwenye kumshukuru humlipa.

Enyi waja wa Mungu! Jipimeni wenyewe kabla hamjapimwa, na jihesabuni kabla hamjahesabiwa, na pumuweni kabla ya koo halijasonga. Ongokeni kabla ya kusukumwa kwa nguvu.8
Na jueni kuwa asiyesaidiwa na nafsi yake kiasi cha kuwaidhika nayo na kuwa mwenye kujikemea, hatowaidhika kutoka kwa mwingine, si mkemeaji wala si muwaidhi.” 9

  • 1. Yaani Yeye (swt) hutambulika bila ya macho kujiangika kwenye dhati yake na hayawezi, kwani asema (swt): “Hafikiwi na uoni wa macho wala wa fikra” na yu aumba bila ya kuchemsha bongo au kuwa na ramani ya kumwongoza.
  • 2. Thabiti daima: Linatokana na al-Qa’imu al-Qayumu: Aliye thabiti ambaye hatoweki, na limetafsiriwa kutokana na maana ya kauli yao: ‘Fulanun Qa’imun bi amri kadhaa,’ yaani fulani ni mwenye kulitawalia na kulishika lisiyumbe.
  • 3. Anakusudia kwa neno pazia zenye nguzo, ni pazia za nuru zilizowekwa kati ya Ar’shi Yake tukufu na malaika wake; na yawezekana akawa yuakusudia hujubu mbingu zenyewe; kwa sababu zimekuwa hijabu dhidi ya Shetani wasijue waliyonayo malaika.
  • 4. Yawezekana ikakusudiwa athari zao, athari za kukanyaga kwao ardhini, au harakati zao na matendo yao.
  • 5. Ni ufafanuzi wa yafichwayo na vifua, na hiyo ni yenye kufichika mno kuliko ishara ya konyezo za jicho.
  • 6. Anajua makazi yao, makazi hapa ni tafsiri ya neno ‘Mustaru’: yakusudiwa katika tumbo za uzazi. Na ‘Mustaudau’: Yaani katika migongo. Na yawezekana ikasemwa: Alikusudia ‘Mustaruhum wa maawahum,’ - juu ya mgongo wa ardhi, na ‘Mustaudauhum’ yaani ndani ya tumbo la ardhi baada ya umauti, na ‘Al-Arham wa dhuhuur’ matumbo na migongo: yaani ndanimwe.
  • 7. Amejaalia kutanguliza matendo mema kupo katika daraja sawa na kukopesha, na thawabu ni sawa na kulipa deni, ili kudhihirisha kuwa malipo ya matendo mema yamethibiti; Amesema Mungu (swt) “Ni nani atakayemkopesha Mwenyezi Mungu mkopo mwema, ili amzidishie mzidisho mwingi?” (2:245)
  • 8. Yaani ongokeni kuyaelekea mnayotakiwa kuyafanya mkihimizwa kwa upole kabla hamjasukumwa kwa nguvu na ukali.
  • 9. Yaani ambaye Mungu hakumsaidia kuonyeka na kujirudi yeye mwenyewe, uzinduzi wa mtu mwingine hautomnufaisha kitu.