read

91 - Na Miongoni Mwa Khutba Zake (A.S)

Na Miongoni Mwa Khutba Zake (a.s) - Ibn Abd-Rabi ameitaja katika al-Iqdul-Farid, jalada la pili, uk. 406, na al-Saduq katika at-Tawhiid, uk. 34.

Ijulikanayo Kuwa Ni Khutba Ya Al’ash’baahu, Nayo Ni Miongoni Mwa Khutba Tukufu Mno:

Al’ash’baahu: Al’ash’khaasu ni watu, na waliokusudiwa hapa ni malaika, kwa sababu khutba ndanimwe muna utajo wa malaika.

Mas’adah bin Sadaqah ameeleza akinukuu kutoka kwa as-Sadiq Ja’far bin Muhammad (a.s), kuwa yeye alisema: Amirul’mu’minina (a.s) aliitoa khutba hii juu ya mimbari ya (mji wa) Kufa hivyo ni kwa sababu mtu mmoja alimjia na akamwambia: ‘Ewe Amirul-Mu’minin! Tusifie Mola wetu iwe kama twamuona bayana ili tuzidi upendo na kumtambua.’

Hapo alighad- hibika (a.s) na akanadi: ‘Asalaatu jaamia,’ Hivyo watu walijumuika kwake kiasi cha kuwa msikiti ulijaa watu, hapo basi (a.s.) alipanda mimbari akiwa ameghadhibika, rangi imembadilika, alimuhimidi Mungu na kumsifu na alimsalia Nabii sala llahu alayhi wa Aalihi, kisha akasema:

“Alhamdu-lillahi - utukufu ni wake Mungu ambaye kuzuia na ubahili hakumzidishii utajiri, wala kutoa na ukarimu hakumfanyi kuwa fakiri, kwa kuwa kila mtoaji asiye kuwa yeye ni mwenye kupungukiwa, na kila mzuia- ji ni mlaumiwa mbali na yeye. 1
Na yeye ni mtoaji sana wa faida za neema, na rejea za ziada na mgawanyo. Wamtegemeao ni viumbe, amechukua dhamana ya riziki zao, na amekadiria vyakula vyao, na amefanya njia kwa wapendao kuziendea, na kwa watakao yaliyo kwake, wala si mkarimu sana kwa aliloombwa kulinganisha na asiloombwa.2 Ni wa Mwanzo ambaye hapakuwa na wa kabla hata iwe kabla yake kulikuwa na kitu, na ni wa Mwisho ambaye hana wa mwisho baada yake hata iwe kuna kitu baada yake, ni Mwenye kuizuia mboni ya jicho isiambue kitu Kwake au kumdiriki, Kwake hazibadililki zama kiasi cha kumfanya Yeye abadilike hali, au awe mahali ili iwe jaizu Kwake kugura.

“Lau angetoa ambavyo madini ya milima imevipumua,3 Na zimemchekelea chaza za bahari mfano wa dhahabu, fedha, na madini ya fedha ya aina makhsusi, na dhahabu iliyo halisi, na mtawanyiko wa lulu na mavuno ya marijani. Hilo lisingeathiri kitu katika ukarimu wake, wala usingekwisha wingi wa aliyonayo, na Kwake kungekuwa hazina ya wanyama ambayo isiyomalizwa na mahitaji ya viumbe, kwa kuwa Yeye ni Mpaji ambaye hamalizwi na ombi la waombaji, wala kunga’ng’ania kwa waombaji hakumfanyi awe bakhili.

“Basi ewe muulizaji, zile ambazo Qur’ani imekujulisha katika sifa Zake msifu nazo na faidika na mwanga wa mwongozo wake, na elimu ambayo Shetani amekutwisha nayo ambayo haiko Kitabuni wajibu wake juu yako, wala ndani ya Sunna ya Nabii (s.a.w.w.) wala athari ya Maimamu waongofu, iwakilishe elimu yake kwa Mungu (swt), kwa kuwa huo ni mwisho wa haki ya Mungu kwako.

Na tambua kuwa waliojikita katika elimu ndio ambao Mungu amewatosheleza kwa kutoivamia milango iliyofungiwa ya yasiyojulikana. Kukiri jumla ya wasioyajua ni tafsiri ya ghaibu iliyofichikana, Mungu akawasifu kutambua kwao kushindwa kuyapata wasiyo yazunguka elimu yake.

Amekuita kuacha kuzama katika wasiyokalifishwa kutafuta kumjua alivyo kuwa ni kuimarika, hivyo basi tosheka na hayo, usiupime utukufu wa Mwenyezi Mungu (swt) kwa kipimo cha akili yako utakuwa miongoni mwa wenye kuhiliki.

“Naye ni Muweza ambaye endapo fikra zimekwenda ili ziudiriki mwisho wa uwezo wake, na fikra zilizoepushwa na hatari ya wasiwasi zikajaribu kutaka kuiona hakika ya dhati Yake, na nyoyo kuwa na shauku ya kutam- bua hakika ya sifa Zake, na maingilio ya akili kuwa mazito, kwa kuwa sifa hazimfikishi ili kuipata hakika ya dhati Yake, anazirudisha nyuma. Na zitarudi hali zimeshindwa, hali zikitambua kuwa uhakika wa ilimu yake hauwezi kufahamika kwa njia iliyopotoka, wala hauingii akilini mwa wanafikra fikra yeyote, katika kukadiria ukubwa wa utukufu Wake.”

Kuumba Ulimwengu

“Ambaye amebuni viumbe bila ya mfano aliofananisha,4 wala hakuchukua kipimo na kulinganisha kutoka kwa muumba muabudiwa aliyekuwa kabla yake, na akatuonesha milki ya uwezo Wake, na ajabu zili- zotamkwa na athari ya hekima Yake. Na kwa viumbe wote kutambua kuwa ni wahitaji (hawana) ila awashike kwa nguvu Zake. Jambo ambalo limetufanya tumjue ni kuthibiti hoja ya dhahiri kwetu (dhidi yetu) na dalili ya kumtambua, japo viwe viumbe visivyosema.

Hivyo basi hoja yake ni kwa mazingatio yatamkayo, na dalili yake kwa muumba ipo wazi.5
“Hivyo basi nashuhudia kuwa mwenye kukushabihisha na mtengano wa viungo vya miili ya viumbe Wako, na kushikana ncha za mifupa yao iliyositiriwa ili kuizingatia hekima Yako, dhamira yake haijawa na maari- fa ya kukutambua Wewe, na wala moyo wake haujagusa yakini kuwa hauna kifani, kana kwamba hakusikia kujitakasa kwa wafuasi mbali na wenye kufuatwa watakapokuja kusema: Wallahi! Kwa yakini tulikuwa katika upotovu ulio bayana. Tulipokuwa tunakufanyeni ni sawa na Mola Mlezi wa walimwengu wote!’ (26:96-97)*

“Wamedanganya wanaokulinganisha, walipokushabihisha na sanamu zao, na wakakupamba na mapambo ya viumbe kwa dhana zao, na wakakufanya (uko) sehemu sehemu ufanywaji sehemu wa vitu vyenye miili kwa fikra zao, na wakakulinganisha na viumbwa vyenye kutofautiana nguvu kwa uwezo wa fikra ya akili zao. Na ninashuhudia kuwa mwenye kukufanya uko sawa na kitu chochote katika viumbe wako anakuwa amekufanyia mfano, na mwenye kukufanyia mfano ni kafiri wa yaliyoteremka miongoni mwa aya Zako za wazi na kuelekezwa na ushuhuda wa hoja Zako zilizo bayana, (pia nashuhudia) kuwa Wewe ni Mungu haujafungwa kwenye mabano ya akili ili uwe kwenye mwelekeo wa kifikra mwenye kugeuka geuka,6 wala katika fikra yake mwenye namna, wala si katika mawazo yake mwenye mipaka, mwenye kukubali kubadilika.”

Baadhi Ya Sehemu Ya Khutba Hii Hii

Kuhusu ukamilifu mkubwa wa uumbaji Wake (swt): “Miongoni mwayo: Amekadiria alivyoviumba na kuimarisha makadirio Yake, na amepanga na akaufanya mpango mzuri, na akaelekeza mwelekeo wake, wala haukuvuka mpaka wa ngazi yake, wala kuzembea kwa kutokufikia lengo lake, wala haikuona vigumu kutii utashi wake.

Na itakuwaje hali ikiwa mambo yametokea kulingana na utashi wake! Mbunifu wa sam- puli za vitu bila ya kuvuta fikra, wala kudhamiria kwa msukumo wa silka,7 wala hakufaidika na uzoefu wa matukio ya zama, wala hakusaidiwa na mshirika kubuni mambo ya ajabu, umbo lake likatimia, na kutekeleza utii wake, na kuitikia wito wake, na viumbe vikaitika wito wa muumba, kulingana na wajibu wa maumbile yake bila ya ujahili akavinyosha vitu vilivyopinda, na aliainisha mipaka yake na kwa uwezo wake ameunganisha kati ya vinavyopingana, na aliziunganisha (kamba za nafsi) na kuifarikisha jinsi tofauti katika mipaka na makadirio, silka na namna, ubunifu wa viumbe akaimarisha umbo lao, na ameviumba alivyopenda na kuvibuni.”

Na Miongoni Mwayo Kuihusu Sifa Ya Mbingu

“Na amefanya mwanya (swt) kati ya miili - yaani sayari za angani - moja na nyingine miongoni mwa sayari za angani na kuiweka katika nidhamu bila ya kuuangika moja na nyingine na bila ya kuifunga na ala ihisiwayo. Na amesawazisha miatuko ya mianya yake,8 na akafuma kati ya kila sayari na miili mienzake inayowiana nayo na kufanana miongoni mwa miili mingine katika tabaka la juu na chini kwa vifungo vinavyozishika (vifungo vya maanawiy, sio vya kimwili) vya mwinuko na vya bonde na akaziba mianya ya miatuko yake na amefuma (swt) kati ya kila mbingu na miili yake na inayofanana nayo.

Na amerahisisha kuikurubia miinuko yake kwa (malaika) wateremkao na amri yake, na kwa wapandao wakiwa na amali za viumbe Wake. Mgumu upandaji wake.

Aliziita hali zikiwa bado mvuke ulio bayana,9 mara moja viungo vyake viliungana na aliifungua milango yake hali ilikuwa imefungwa, na aliweka walinzi wa angani10 yaani vijinga vipenyavyo kwenye njia zake, na akazishika zisiyumbe katika mapito ya upepo kwa mkono (uwezo) wake.

Na akaiamuru isimame kusalimu amri Yake, na amejaalia jua kuwa ni alama yenye kuangaza kwa ajili ya mchana wake, na mwezi ni alama yenye kufutwa katika baadhi ya usiku.11 Na akazipitisha sayari mbili (jua na mwezi) kwenye mzunguko wake na akakadiria khatua za mienendo yao kwenye mapito yao, ili (kwa viwili hivi) aweze kubaini kati ya usiku na mchana na ipate kujulikana idadi ya miaka na hisabu kwa makadirio yao (jua na mwezi), kisha akaangika katika anga lake falaki (njia za sayari) na akaiambatanisha humo mapambo yake, miongoni mwa nyota zake (zajulikana kwa jina la “Duriyu”) nazo ni nyota zin’gaazo sana, na taa za nyota zake (hizi ni nyota ndogo ndogo), na aliwatupia waibao usikizi vijinga vyenye mwanga upenyao, na akazipitisha kwenye njia alizoziweka sawa kwa ajili ya iliyothibiti (miongoni mwa nyota zilizo thabiti mahali pamoja) na kwa ajili ya zenye kwenda kwa ziendazo (yaani tano zenye nuru, kwa kuwa daima ni zenye kwenda) kuporomoka kwao na kupanda kwao, na zile za ndege mbaya na ndege njema.”12

Miongoni Mwayo Kuhusu Sifa Ya Malaika

Kisha (swt) aliumba viumbe ili awafanye kuwa wakazi wa mbingu zake, na kuzifanya mbingu ziwe na wenyeji tabaka za juu za milki yake, viumbe wapya, nao ni miongoni mwa malaika wake, na aliwajaza maeneo ya wazi katika mabonde yake, na aliwajaza sehemu tupu za anga Zake, na kati ya mwanya miongoni mwa hiyo mianya kuna kelele za sauti za (malaika) wafanyao tasbiihi wakiwa ndani ya maboma matakatifu,13 na pazia za utukufu, na nyuma ya hayo kuna mtikisiko ambao masikio huziba, na tabaka za nuru zinakiwisha macho yasifike na kubaki yamezuilika kwenye mpaka wake, yaani zinapoishia nguvu zao, amewaumba wakiwa katika sura zilizo tofauti, na uwezo ulio tofauti, wenye mbawa wanautakasa utukufu wa enzi Yake, hawajidaii uungu binafsi, wala hawajigambi kuwa wanaumba kitu pamoja na Yeye miongoni mwa aliyojitenga nayo “Bali hao (wanaowaita wana) ni watumwa walitukuzwa. Hawamtangulii kwa neno, nao hufanya kwa amri Zake.” 21:26-27

“Mungu amewajaalia kuna ambao ni waaminifu kwa ajili ya wahyi Wake, na kuwatuma kwa manabii Wake wakiwa wabeba amri Zake na makatazo Yake.

Amewahifadhi dhidi ya kuwa na shaka ya utata, hivyo basi hapana yeyote miongoni mwao anayepotoka kando na njia ya maridhawa Yake.

Amewapa jinsi ya kufaidika na msaada na kuzifunika nyoyo zao adabu na unyenyekevu na amani, na amewafungulia milango laini ya kumtukuza, na amewasimamishia minara ya wazi ikiwa ni alama za tauhiidi Yake, uzito wa dhambi haukuwatopea, wala kupokezana kwa usiku na mchana hakujawamaliza au kuwageuza.

Wala shaka hazijashambulia kwa mishale uimara wa imani zao, dhana hazija songamana kwenye misingi ya yakini yao, wala chuki haijawasha moto kati yao, wala mbabaiko haujawapokonya walichoambatana nacho miongoni mwa maarifa Yake kwa dhamira zao, na kilichotulia miongoni mwa utukufu Wake na haiba ya utukufu Wake ndani ya nyoyo zao, wala wasiwasi haukuwa na tamaa kwao ya kuwatandazia kutu yake kwenye fikra zao.

Miongoni mwao kuna ambao wako katika uumbaji wa mawingu mazito ya maji, na walio kwenye milima mirefu, na walio katika maficho ya giza linaloduwaza. Na miongoni mwao kuna ambao nyayo zao zimetoboa ardhi ya chini nazo zikiwa kama bendera nyeupe zilizopenya kwenye penyo za hewa na chini yake kuna upepo uliotulia yaifunga kwenye mipaka inakoishia.

Shughuli za ibada Yake zimewatenga, hakika ya imani imekuwa wasila kati yao na maarifa Yake, yakini na Yeye imewakata na kuwafikisha kuwa na shauku Naye, upendo wao kwa Aliyonayo haukuvuka na kuwafikisha kwa aliyenayo mwingine. Hakika wameonja utamu wa kumtambua Yeye, na wamekunywa kwa gilasi ipozayo kiu kwa mahaba Yake, na imekita kwenye kiini cha mioyo yao kamba ya kumkhofia.

“Wamepindisha unyofu wa migongo yao kwa sababu ya urefu wa utii. Kwa kweli urefu wa matumaini Kwake haukumaliza mada ya unyenyekevu wao, wala ukubwa wa ukaribu haujawafungua tanzi za unyenyekevu wao, wala hawakutawaliwa na fahari, kiasi cha kuwafanya wakithirishe waliyoyatanguliza miongoni mwa mema, wala unyenyekevu wao kwenye utukufu wa Allah hauwaruhusu kuthamini mema yao, hawajapitiwa na utepetevu muda wote wa kudumu kwao, raghba yao haikupungua hata wahalifu kumtarajia Mola wao, wala ncha za ndimi zao hazikukauka kwa urefu wa faragha,14 wala hawakukaliwa na la kuwashughulisha mbali na Mungu hata walazimike kunong’ona ili kuzipunguza sauti zao za juu kwa dua, wala mabega yao hayakutofautiana katika safu za utii, wala hawakuzipindisha shingo zao kwa raha ili kuzembea amri Yake, wala upuuzi wa mghafala haushambulii azma ya juhudi yao, wala hadaa za matamanio hazishambulii hima zao.

“Wamemfanya Mwenye Arshi kuwa ni akiba ya siku ya haja yao, na wamemkusudia Yeye kwa wayatakayo na matarajio pindi waja walipojitenga mbali na Yeye na kuwaelekea viumbe kwa wayatakayo, hawaufikii mwisho wa upeo wa ibada yake, kila wazidishapo utii wake huzidi msukumo wa kumuabudu miongoni mwa upendo na hofu.

Sababu za hofu hazijakatika mbali na wao, hata wadhoofu katika juhudi zao, wala hawakutekwa na tamaa hata watosheke na juhudi ndogo mbali na juhudi zao kubwa, hawakuuzingatia ukubwa wa amali zao zilizotangulia, lau wangezikuza hizo, matumaini yao yangefuta hali ya woga wao.

Wala hawajatofautiana katika Mola wao kwa kughilibiwa na shetani. Uovu wa kutengana kati yao haukuwatawanya. Wala chuki ya kuhusudiana haikuwatawala, wala shaka haikuwatawanya, wala hima tofauti hazikuwagawa, hivyo wao ni mateka wa imani, hauwaachii watoke nje ya tanzi lake, sio upotovu wala ukiukaji, wala udhaifu, wala utepetevu. Hakuna sehemu hata ndogo katika tabaka za mbinguni ila kuna malaika; ama yu katika sijida au yu kwenye juhudi mwenye haraka. Muda wote wa utii kwa Mola wao wanazidi elimu kumhusu Mola wao, na enzi na utukufu wa Mola wao Mlezi unazidi kuwa mkubwa nyoyoni mwao.”

Sehemu Ya Khutba Kuhusu Sifa Ya Ardhi Na Kukunjuliwa Kwake Juu Ya Maji

“Ameingiza ardhi (swt) kwenye harakati za mawimbi yaliyochafuka, na kilindi cha bahari iliyojaa, mawimbi yake yanapigana pigana yenyewe kwa yenyewe, na zinatoa povu mfano wa ngamia dume, upandaji wa maji yenye kupigana kwa sababu ya uzito wa mzigo wake ukarudi chini, na ukatulia mhemko wa kupigana kwake, pindi ardhi iliposhindilia kifua chake,15 ikanyenyekea ilipojigaragaza, ikawa baada ya kelele za mawimbi yake imetulia, yenye kushindwa na kuwa dhalili chini ya mateka ya unyonge, mateka mnyenyekevu.

Na ardhi ilitulia ikiwa imekunjuka katika mawimbi yake makubwa, na ikayarudisha mwinuko wake, na (ardhi) ilivunja nguvu ya maji baada ya kupanda kwake, na kuinua pua yake na kukithiri kuvuka kwake mpaka, na ikayazuia maji hali yakiwa yamesongamana, yakatulia baada ya msukumo wake, ikajiambatanisha na ardhi baada ya kuvuma kwake.

Na yalipotulia kuchafuka kwake pembeni mwake, na kuibeba milima mirefu mikubwa pembezoni mwake, ikatumbua chemchemi za milima, akayatawanya kwenye ardhi tambarare na mifereji, na alisawazisha harakati zake kwa majabali marefu miongoni mwa mawe magumu ikatulia kuyumba kwa kutumbukia majabali kwenye vipande vya sehemu zake, na kujipenyeza kwa maji na kuenea katika makorongo na tundu za pua, na kupanda kwake juu ya milima alipoitandaza ardhi yake na kupitisha amri yake, alimteua Adamu ( a.s) akiwa mteule katika viumbe Wake, na alimfanya wa kwanza katika umbo lake, na alimfanya kuwa mkazi wa pepo Yake, na alijaalia wasaa wa mlo wake, na alimuonya kabla katika aliyomkataza, na kumjulisha kuwa kuyaelekea aliyoyakataza ni kujiingiza katika kumuasi, na ni hatari kwa daraja yake.

“Alijiingiza kwenye aliyomkataza - kulingana na ujuzi Wake (swt) - alimteremsha baada ya toba, ili aikae ardhi Yake na kizazi chake, na kwake yeye iwe ni hoja kwa waja Wake. Hakuwaacha tupu wanadamu baada ya kumfisha yeye Adam. Ni katika yatiliayo nguvu juu yao hoja ya kuwa Yeye ni Mola Mlezi, na iwe kiungo kati yao na kumtambua Yeye, na kuchukua ahadi kwa ushahidi kupitia ndimi za walio wema miongoni mwa manabii wake, na wabeba amana ya risala Yake, karne na karne. Mpaka kutimia hoja yake kwa Nabii wetu Muhammad (s.a.w.w.), na suala kufikia udhuru wake kwa Muumba.16

“Amekadiria riziki, ameikithirisha na kuipunguza. Na ameigawa kwa dhiki na wasaa, akaiweka katika makadirio, ili kuwajaribu waitakao kwa wepesi wake na ugumu wake, kwa hilo anatahini shukrani na subira kwa tajiri na masikini.

Kisha ameambatanisha utajiri na shida ya ufakiri, na salama ameiambatanisha na misiba na maafa yake, na fursa ya furaha yake imeambatanishwa na taabu za huzuni yake. Na ameumba muda wa umri wa kuishi, ameurefusha na kuufupisha, na ameutanguliza na kuuchelewesha, na ameuunganishia umauti na kamba zake, na kuufanya wenye kuvuta kamba zake, na wenye kukata kamba yake imara.

“Ni mjuzi wa siri za dhamiri za wenye kudhamiria, na siri za wenye kuficha, na mawazo ya moyoni, na vifungo vya azma yenye uyakini, na yanayo ibwa na muangazo wa kope za macho, na yaliyomo ndani ya siri za nyoyo, na yaliyo kwenye kina, na yaliyosikiwa kwa kuibwa na tundu za masikio, na maeneo ya sisimizi ya kupitishia muda wa kiangazi, na makazi ya wadudu wakati wa masika.

Na kurejea kwa mimba ni miongoni mwa yahuzunishayo, na sauti hafifu ya nyayo, na mahali tunda linapokuwa, katika kifuniko cha ua, na maficho ya wanyama kwenye mapango ya milima, na mabonde yake, na maficho ya mbu kwenye mashina ya miti na magome yake, na maoteo ya majani kwenye matawi, na materemkio ya amshaji - tone la manii17 kwenye mtiririko migongoni mwanzoni mwa kutungika kwake na kujiambatanisha kwake.

“Na kutiririka kwa matone ya mvua kutoka kwenye mkusanyiko wake, na yabebwayo na upepo pembezoni mwake, na yanayofutwa na mvua kwa mafuriko yake, na kuelea kwa wadudu wa ardhini na ni kitulizo cha mchanga, na ni makazi ya wadudu wenye mbawa kwenye vilele vya majabali, na kuimba kwa wenye kutamka katika giza la viota, na vilivyokusanywa na chaza na kutotolewa na mawimbi ya bahari,18 na vilivyofunikwa na giza la usiku au kuchomozewa na jua la mchana na viliyotokomezwa na tabaka za giza na daraja za nuru, na athari za kila hatua na hisia za kila harakati, na rejea ya kila neno19 na - mtikisiko wa kila mdomo, na makazi ya kila mtu, na uzito wa kila chembe, na hima ya kila nafsi, na yaliyomo ardhini miongoni mwa matunda ya mti, au jani lililodondoka, au makao ya manii,20 au mahali panapokusanyika damu na mudh’ghah au mwanzo wa kuumba na kizazi21 hakupata mashaka katika hilo, wala hakukabiliwa na upinzani katika kuhifadhi alichokibuni miongoni mwa viumbe Wake, wala hakupatwa katika kutekeleza na mambo na kuwaratibu viumbe uchovu wala ulegevu, bali elimu yake iliwaratibu, na aliwajua idadi, na kuwaeneza uadilifu wake, na kuwaingiza katika fadhila zake japokuwa ni wachache wanaostahiki.

“Ewe Allah! Wewe ni mwenye sifa nzuri, na ukamilifu usio na idadi. Ukitumainiwa ni mtumainiwa bora, na ukitarajiwa ni mtarajiwa bora. Ewe Allah! Umenikunjulia nguvu hasa kiasi cha kuwa simsifu nayo mwingine asiyekuwa Wewe, na simtukuzi mwingine yeyote asiye kuwa Wewe, si elekezi wasifu kwa chimbuko la kutofaulu na mahali pa shaka shaka,22umeuepusha ulimi wangu mbali na sifa za wanadamu na kuwasifu waruzukiwa, wa lioumbwa.

Ewe Allah! kila mwenye kusifu ana haki ya ujira na fidia kwa anayemsifu, kwa hakika, nimekugeukia na macho yangu, nimekutarajia kuwa ni dalili ya kwenye akiba ya rehema na hazina ya msamaha.23

“Ewe Mungu Wangu! hapa ni mahali aliposimama ambaye amekupweke- sha kwa tauhiidi ambayo ni haki Yako, na wala hajamuona anayestahiki shukrani hizi na wasifu asiyekuwa Wewe. Mimi ni mhitaji Kwako, kwa kiwango ambacho hakiondoi umasikini wake isipokuwa fadhila Zako, wala cha kuepusha ufakiri wake isipokuwa ihisani yako na upaji wako, hivyo basi tupe sisi ridhaa Zako mahali hapa, na tutosheleze tusinyooshe mikono kwa asiyekuwa Wewe; (kwa hakika wewe umuweza wa kila kitu).”

 • 1. Hivyo ni kwa sababu Mungu (swt) humzuia ambaye hikma na mas’laha vyaelekeza anyimwe mwenye kunyimwa, si kama wazuiavyo wanadamu.
 • 2. Yaani ukarimu wa muumba sio kama ule uliopo katika njia ya wanadamu, ambao wanatikiswa na ombi, bali ukarimu wake ni wa jumla katika hali zote.
 • 3. Ambavyo madini ya milima imevipumua ni istiara, yaani ilivyotoa inakuwa kana kwamba mnyama apumuapo hutoka kifuani mwake na mapafu yake hewa. Imam hapo ame- tumia balagha ya hali ya juu kwa kuuita utokaji wa madini nje ya johari zake kuwa ni tana- fusan - kupumua, kwani aghlabu huwa hivyo – bali karibu mara zote - kutokana na mtik- isiko wa maada zinazowaka ndani ya ardhi na kutoka nje, nazo zikiwa katika hali ya kufanya mvuke zinashabihiana na - tanafusi - kutoa pumzi, kama alipotumia badi’iu katika kuita ufungukaji wa chaza na kukitoa kilicho ndanimwe kuwa ni kucheka.
 • 4. Kauli yake Ib’tada’al’khalqa: Amewabuni viumbe bila kuwepo na kitu, na kauli yake: “Ala ghayri mithaalin imtathalahu” (bila ya mfano alioiga) yawezekana awe amekusudia kwa neno: Imtathalahu mathalahu, na maana inakuwa Yeye (swt) hakujiwekea mfano kabla hajaanza uumbaji (kama vile ramani) wa ulimwengu; kisha iwe amefuata katika uumbaji ule mfano, na yawezekana awe amekusudia kwa neno: Imtathalahu kuwa amefuata nyayo na kuiga, na maana inakuwa: Yeye (swt) hakufanyiwa mfano na mtendaji mwingine kabla yake naye akamuiga na kufuata nyayo na kufanya kama alivyofanya.
 • 5. Na amejaalia haja ya wazi wazi kwa viumbe ili kuweka kuwepo kwao kwa kiwashika- cho miongoni mwa nguvu Zake kama mfano wa mtamkaji wa utambuzi huo wa kumtam- bua Yeye, yaani ametujulisha kumtambua Yeye kwa sababu kuwepo kwa hoja kumetulaz- imisha hivyo.
 • 6. Yaani Haujawa na ukomo ukiwa ndani ya mipaka kiasi cha kuzungukwa na akili kwa hali hiyo akili iko katika aina makhsusi.
 • 7. Silka: Yaani Yeye (swt) hana silka kama walivyo viumbe zenye hisia kwa mujibu wa hiyo (silka), viumbe husukumwa kutenda, bali Yeye (swt) ni mtendaji kwa muktadha wa dhati Yake sio kwa msukumo wa tukio la nje.
 • 8. Yaani ikiwa kwenye sayari moja kuna mwatuko anausawazisha (swt) na kuuweka sawa na hivyo inakuwa kama ilivyokuwa mwanzo wa kuumbwa kwa ardhi na kuiengua kutoka miili ya mbinguni na kuwa na mwanya kati ya miili ya juu na hiyo (ardhi), kiwacho na mwanya katika hiyo anasawazisha (swt). “Awa lam yara lladhiina kafaru annas samawati wal’ardha kaanataa rat’qan fafataqnaahuma” ‘Je hawatambui waliokufuru (waabudia sanamu) wao hutofautisha kati ya kuumba na kuratibu, wananasibisha uumbaji kwa Mungu (swt) na uratibu wa mambo kwa miungu - sanamu’ (Al’anbiyau: 30) Kuwa mbingu na ardhi zilikuwa zimeungana mwanzo wa kuumbwa kwao naye swt. akazitenga, na hiyo ni katika tad’biiri (kuratibu, kuongoza), basi vipi yawezekana uumbaji uwe kwa mmoja na uratibu wa mambo uwe kwa wengine?!
 • 9. Usemi wake: Naadaaha - aliziita, ni kurejea kwenye kubainisha baadhi ya jinsi ilivyokuwa kabla ya nidhamu. Anasema: Mbingu zilikuwa moshi unaoyumba, za shabihi- ana na moshi kwa mandhari yake, na kushabiahiana na mvuke kwa hali yake ya maada, hapo ndipo siri ya uumbaji ikajitokeza.
 • 10. Walinzi: Ni kaumu ya wanaoangalia kama walinzi, na kuwa walinzi ni katika vimon- do mwanzo wa kuumba viumbe, ni kama alivyosema Imam (a.s.) ni dalili ya ambalo lime- thibitishwa na elimu kuwa vimondo ni vyenye kupiga baadhi ya sayari.
 • 11. Mwanga wake hufutika baadhi ya nyakati za usiku baadhi ya nyakati au usiku mzima siku nyingine.
 • 12. Kwa kweli nyota zina athari, kupanda na kuteremka, katika mambo kwa sura ya jumla, kama kusababisha joto au baridi, au kujulisha maradhi au ukame kwa sura ya jumla, au mvua ya kudumu, na mfano wa mambo kama hayo miongoni mwa mambo ambayo hayahusiani na suala la mtu fulani peke yake. Na ambalo alilikanusha kwa aliyemshauri asiende vitani katika siku makhsusi, kwa ajili ya nyota kuwa na athari katika mambo au matukio ya watu mmoja mmoja au tukio la mtu binafsi, mfano wa safari kukaa mahali fulani, vita, amani, na mfano wake.
 • 13. Boma hapa ni boma la kuwahifadhi wanyama, nalo hapa limetumika kwa majaazi (istiara) yakimaanishwa makazi matakatifu ya roho zilizo tohara.
 • 14. Yaani ncha za ndimi zao hazikukauka kiasi cha kuwa hawawezi kuendelea kumdhukuru (swt).
 • 15. Kifua hapa ni istiara - anakusudia kile ambacho maji yamekipata kutoka ardhini.
 • 16. Yaani hoja imetimia baada ya kumtuma Muhammad (s.a.w.w.) kwa viumbe wote na jambo kufikia mwisho wake, hapajabakia baada yake Mtume mwingine anayetazamiwa; hivyo inakuwa udhuru na onyo kwa Mungu vimekamilika. Udhuru wake ni: Ule ubainisho wake kwa mukalafiina, miongoni mwa kuwaonya na adhabu Zake endapo wakiasi, na maonyo Yake: Ni kule kuwaonya Kwake kuhusu matukio.
 • 17. Amshaaju: Ni maji ya mwanamume yaliyochanganyika na maji ya mwanamke na damu yake, ni wingi wa neno Mashiij katika Kiarabu, limeitwa amshaaji kutoka na neno mashaja yanapochanganyika, kwa sababu mashiij ni mchanganyiko wa viini mbalimbali, kila kimoja kinafaa kutengeneza kiungo miongoni mwa viungo vya mwili.
 • 18. Kama ambari na mfano wake.
 • 19. Kirejeacho miongoni mwa maneno nafsini mwako na kurudia rudia fikirani mwako.
 • 20. Makao ya manii: kituliacho katika maji mahali, na nut’fa ni maji yenyewe, na yawezekana awe amekusudia manii, na hili latiliwa nguvu na alilotaja baada yake miongoni mwa mudh’ghah - bonge la damu.
 • 21. Kizazi yaani Sulala. Na Sulala: katika asili yake ni kilichotolewa kwenye kitu, na nut’- fa imeitwa Sulalatul-insaan, kwa sababu mtu anatolewa humo, na hivyo hivyo mtoto.
 • 22. Anakusudia kwa neno: ‘Ma’dinul-Khaiba’ - chimbuko la kutofaulu: ni wanadamu; kwa kuwa mwenye kuwasifu na kuwatumainia aghalabu hafaulu, na amewafanya kuwa ni mahali pa shaka, kwa kuwa wao hawaaminiki kwa hali yeyote ile.
 • 23. Anataraji amjulishe matendo (mema) ambayo yatamridhisha. Ameyafanya matendo mema mfano wa hazina ya rehema.