read

92 - Miongoni Mwa Khutba Zake (A.S)

Miongoni Mwa Khutba Zake (a.s) - Tabariy na Ibnul’Athiir wameisema katika matukio ya mwaka, 35 kukiwa na tofauti ndogo mno.

Watu Walipotaka Kumpa Bai’a Baada Ya Kuuliwa Uthmani

Na maneno haya sahibu zetu wanayachukulia katika hali yake ya dhahiri; Kwa hiyo wanasema: Kuwa yeye (a.s) hakuusiwa na Mtume (s.a.w.w.) awe Imam, japo kuwa awe ni mbora kwa jambo hili kuliko watu wengine, na ni mwenye haki zaidi kwa daraja aliyonayo. Kwa sababu lau angekuwa ameusiwa Uimamu na Mtume (s.a.w.w.), isingejuzu aseme: “Dauniy waltamisuu ghayriy” - Niacheni na mwombeni mtu mwingine; na aseme: “Wa la’Ali asmaukum waatwaukum liman walaytumuhu amrakum” au aseme: “wa anaa lakum waziran khayrun minniy lakum amiran.”

“Niacheni na mtafuteni mtu mwingine, kwa kuwa sisi twatazamia jambo lenye sura nyingi na rangi nyingi, nyoyo haziwezi kuvumilia wala akili haziwezi kulibeba.

Kwa kweli msitari wa upeo wa macho umefunikwa na mawingu, na njia iliyonyooka haijulikani tena.1 Na jueni kuwa endapo mimi nitawaitikieni nitawabebesheni niyajuayo na sitosikiliza kauli ya msemaji yeyote, wala lawama ya mwenye kulaumu.

Na mkiniacha mimi nitakuwa kama mmoja yeyote miongoni mwenu. Na huenda nitakuwa mwenye kumsikiliza na kumtii mno mtakayemtawaza hili suala lenu, na mimi kuwa waziri kwenu ni bora kuliko kuwa Amiir.”

Maelezo

Na Imamia wanauchukua usemi huu kwa maana nyingine, wao wanasema: Ambao walitaka kumpa kiapo cha utii (bai’a) ni wale waliokula kiapo cha utii kwa makhalifa waliokuwa hapo kabla; na Uthman aliwanyima walio wengi haki yao ya fungu lililokuwa wakipewa.

Kwa kuwa Bani Umayyah walikomba mali katika siku za Uthman; alipouliwa wakamwambia Ali ( a.s): “Tutakubai (kula kiapo cha utii kwako) kwa sharti kwamba uende na sisi mwendo wa Abu Bakr na Umar; Kwa kuwa wao hawa wawili walikuwa hawahodhi mali kwa ajili yao binafsi wala kwa ajili ya ah’li zao, kwa ajili hiyo walimuomba Ali ( a.s) wamfanyiye bai’a ili awagawiye mgao kutoka baytul’mali kama ule wa Abubakar na Umar; Hapo ndipo akawakatalia na akawataka wamchague mtu mwingine ambaye atakwenda mwendo wa hawa wawili.

  • 1. Njia iliyonyooka haijulikani, kwa sababu alama zake zimebadilika, kwa hiyo ikawa haijulikani tena, na maana inakuwa: Shub’ha imezitawala akili na nyoyo, na watu walio wengi wamekuwa hawaijui ilipo njia ya kweli! Na hiyo ni kwa sababu tamaa imewaingia watu wengi katika utawala wa Uthman kutokana na kuboreshwa katika upewaji wa ruzuku, kwa hiyo haiwi rahisi kwao kuwekwa sawa na wengine, hivyo basi lau wangetendewa uadilifu wangemponyoka na kutaka vurugu ya fitna; kwa tamaa ya kupata utashi wao. Na hao aghalabu ndio maraisi katika kaumu.
    Endapo Imam (a.s) atawapitishia kama walivyokuwa katika kuboreshwa atakuwa ameleta dhulma, na kuihalifu sharia, na walipizao kisasi kwa Uthman walikuwa wanataka insaafu, vinginevyo watachochea fitnah, hivyo basi wapi aelekee ili kuifikia haki akiwa salama bila ya fitna! Na yalitokea baada ya bai’a yake aliyokuwa akiyabashri kabla yake.