read

93 - Miongoni Mwa Khutba Zake (A.S)

Miongoni Mwa Khutba Zake (A.S) - Abu Na’im amesema katika Hilyatul-Auliyai, jalada la kwanza, uk. 68, na Ibn Wa’dhwih katika Ta’arikh yake, jalada la tatu, 182.

Ndani Ya Khutba Hii Amirul-Mu’minin Anabainisha Ubora Wake Na Elimu Yake. Na Anabainisha Fitna Ya Bani Umayyah

“Baada ya kumhimidi Mungu na kumtukuza! Enyi watu! kwa hakika mimi nimetoboa jicho la fitna,1 na hangethubutu mwingine yeyote asiyekuwa mimi baada ya kutanda giza lake.2 Shari yake na maudhi yake yamekuwa makali.

“Hivyo basi niulizeni kabla hamjanikosa, namuapa ambaye nafsi yangu iko mkononi Mwake kwamba hamtoniuliza kitu tokea hivi sasa na siku saa itakapofika, wala kuhusu kikundi kitakachowaongoza watu mia moja na kuwapoteza mia nitakupeni habari nani mlinganiaji wake na kiongozi wake na mhamasishaji wake na mashukio ya ngamia wake, na kituo cha msafara wake, na ambao watauwawa miongoni mwa watu wake, na ambao watakufa kwa kifo cha kawaida.

“Na mtakaponikosa na mtapofikwa na shida ya vita na mambo magumu waulizaji wengi wangenyamaza na kuinamisha vichwa chini, na kuogopa wengi miongoni mwa watakaoshika nafasi za kuulizwa, na hivyo itakuwa viishapo vita vyenu, ikiwa na magumu kwenu, dunia itakuwa imebana kwenu, siku za balaa mtaziona ndefu, mpaka Mungu atakapowapa ushindi baadhi ya watu wema waliobaki miongoni mwenu.

“Kwa kweli fitna inapoingia utata hujitokeza.3

Ikigeuza mgongo hutambulika;4 haitambuliki inapokuja, na hutambulika inapotoweka.5 Na yazunguka mzunguko wa upepo, unaisibu nchi na kuikosa nchi.

“Jihadharini, kwa hakika fitna ninayoihofia sana mimi kwa ajili yenu ni fitna ya Bani Umayyah. Kwa kuwa hiyo ni fitna pofu yenye giza: Jambo lake limeenea6Na balaa lake limekuwa kwa sura makh’susi. Na wakapatwa na balaa humo wenye kuitambua haki.7 Balaa litamuepuka asiyejua.

Namuapa Mungu kwamba mtawakuta Bani Umayyah ni watu waovu kwenu baada yangu kama ngamia jike mzee mwenye tabia mbaya, yuang’ata kwa mdomo wake na apiga kwa mkono wake na kupiga teke kwa miguu yake ya nyuma na yu azuia kukamuliwa maziwa yake.

“Watabakia juu yenu mpaka hawatomuacha miongoni mwenu isipokuwa yule wa manufaa kwao, au asiye na madhara kwao. Balaa lao litaendelea juu yenu mpaka kiasi cha kuwa kuomba nusura kwa mmoja wenu dhidi yao ni kama kuomba nusura kwa mtumwa dhidi ya bwana wake8- na kwa mfuasi dhidi ya amfuataye, fitna yao mbaya na ya kuogofya itakujieni na sehemu ya jahiliya, hakuna humo alama za muongozo, wala dalili ionekanayo. Sisi ni Ahlul-Bayt (wana wa nyumba ya Mtume) twaepukana na hayo, wala si wanusuru wa hayo.

Kisha Mungu atakuondoleeni kama iondolewavyo ngozi kutoka kwa wenye kuambatana nayo kwa madhila, na kuwasukuma kwa mabavu, na kuwanywesha kikombe kichungu, hatowapa ila upanga, na wala hatowavika isipokuwa hofu.

Hapo Makuraishi watataka hata kwa gharama ya dunia yote na yaliyomo humo ili wanione mimi japo kwa mara moja tu lau kwa kadiri ya muda ule wa kuchinjwa ngamia ili niwakubalie lile ambalo hivi sasa nawaomba sehemu tu lakini hawako tayari kunipa.”9

Kisha alisema (a.s): “Niulizeni kabla hamjanikosa.” Bwana mwenye Kitabu cha Al-Isti’ab naye ni Abu Umar Muhammad bin Abdil-Bari ameeleza akinakili kutoka kwa jamaa wasimuliaji na wanahadiithi, wamesema:

‘Hakupata kusema yeyote miongoni mwa masahaba (r.a): ‘niulizeni’ isipokuwa Ali bin Abi Talib. Na Sheikh Abu Ja’far Al-Iskafi ameeleza ndani ya Kitabu Naq’dhul-Uth’maniyah akinakili kutoka kwa Ali bin Al- Jahdi kutoka kwa Ibin Shubrimah, Amesema: ‘Hawezi yeyote miongoni mwa watu kusema juu ya mimbari ‘niulizeni’ isipokuwa Ali Bin Abi Talib (a.s).

  • 1. Faqa’atuha: Nimeyachana (macho) na kuyang’oa. Hayo ni maneno ya mfano akiwa anamaanisha kuishinda fitna, hivyo ameijaalia fitna kama kiwa chenye macho makali watu wanayachelea, yeye alithubutu, akayapasua macho yake ikatulia baada ya kucharuka kwake, na hii ni miongoni mwa istiara, na hiyo ilikuwa baada ya kuumaliza mgogoro wa An-Nah’rawani na kuwashinda kwake Khawarij.
  • 2. “Al’ghayhabu”: Giza, na “maujuha”, ni kutanda na kuenea kwake, hivyo basi maana inakuwa baada ya kutanda na kuenea upotovu, kwa hiyo amedokeza badali ya upotovu akatumia neno “Al-ghayhabu’’na badali ya kutanda na kuenea ametumia neno “at-Tamauju.”
  • 3. Shabbahat: Utata huingia, yaani haki haitambuliki kwa kuchanganyika na wingi wa batili.
  • 4. Hujulikana ikigeuza mgongo yaani ikienda, kwa sababu zajulikana baada ya kupita kwake na hufichuka ukweli wake kwa hiyo huwa funzo.
  • 5. Mfano wake ni fitna ya vita vya Jamal, na fitna ya Al-Khawarij - wenye kujiengua - watu wengi kuyahusu matukio hayo mawili mwanzoni walisita, na hali ya mambo ilitata kwao, mpaka vita vilipokwisha ikawabainikia kwa kumtambua mpotovu mbali na muongofu.
  • 6. Kuenea kwa jambo hili kwa kuwa ni uongozi wa sura ya jumla, na balaa lake limekuwa kwa sura makh’susi kwa Ahlul’bayti, kwa sababu ni kuporwa kwa haki yao.
  • 7. Kwa mwenye kuitambua haki humo balaa la kisasi humshukia kutoka kwa Bani Umayyah.
  • 8. Yaani kunusurika kwa watu wanyonge si kunusurika; kwa kuwa mtumwa hanusuriki dhidi ya bwana wake kamwe.
  • 9. Huku ni kutoa habari za kudhihiri kwa “Musawudatu” na kumalizika kwa ufalme wa Bani Umayyah: yaani Bani Abbasi ‘kaulimbiu’ yao ilikuwa ni: Assawadu. Na habari aliyoielezea (a.s.) kuhusu wao ilitokea, imekuwa kweli kauli yake: “tawad Quraishi:…” - wanatamani Maquraishi - wamenakili wana historia wote kuwa Marwan bin Muhammad siku ya Zaabbu alipomuona Abdullah bin Ali bin Abdillahi bin Abbas mbele yake katika safu ya Khurasani alisema: “Ningependa Ali bin Abi Talib angekuwa chini ya bendera hii badala ya huyu kijana.”