read

94 - Na Miongoni Mwa Khutba Yake (A.S)

Na Miongoni Mwa Khutba Yake (a.s) - Ibn Abd-Rabi ameieleza katika al-Iqdul-Farid, jalada la 4, uk. 74, na al-Saduq katika Tawhid, uk.20.

Kuhusu Sifa Za Manabii

“Ametukuka Mwenyezi Mungu1 ambaye umbali wa mtazamo na fikra haumfikii, wala dhana ya utambuzi haimpati. Wa mwanzo ambaye hakuna upeo iwe anaishia huko wala hana mwisho iwe yuamalizikia hapo.

Na miongoni mwa hutuba hiyo: “Amewaweka weko bora na akawafanya watuwame kwenye tuwamo la kheri, imewanakili migongo mitukufu na kuwafikisha mifuko ya uzazi iliyo tohara; kila wapitapo - wafapo - waliotangulia, waliobaki kati yao hutekeleza dini ya Mungu, mpaka heshima ya Mungu (swt) imeishia kwa Muhammad (s.a.w.w.); akamtoa kutoka kwenye asili iliyo bora, na asili yenye heshima kuu, na kutoka mti ambao manabii Wake wametoka humo, na akachagua kutoka humo waaminifu Wake, Itrah yake ni miongoni mwa itrah; kizazi cha nyumba ya Mtume Mtukufu (s.a.w.w) zilizo bora. Na familia yake ni miongoni mwa familia zilizo bora. Na mti wake ni katika miti bora; umeinukia katika utukufu. Una matawi marefu; na matunda yasiyofikiwa;2yeye ni imam wa wenye kufanya taq’wa, na ni mwanga wa wapendao mwongozo.

“Ni taa ambayo umemweta mwanga wake, na kimondo nuru yake imeangaza, na kipekecho cha moto ambacho mwanga wake umeangaza, sira yake ni insafu na sunna yake ni mwongozo, na maneno yake ni upambanuzi, na hukumu yake ni uadilifu; alimtuma wakati wa mwanya kati ya mitume3 na wakati ambapo umma umepotoka na kupotoka kimatendo, na kutoelewa kati ya umma.

“Fanyeni mema - Mungu awarehemu - kwa mwanga wa wazi, njia ni ya wazi inaitia (watu) kwenye nyumba ya amani, (yaani pepo) hali mkiwa ndani ya nyumba ya kutafuta ridhaa (za Mungu), mkiwa na muda na fursa, na vitabu viko wazi (vitabu vya kuandika matendo ya waja), na kalamu ziko mashughulikoni (kalamu za malaika), na miili iko na siha, ndimi zikiwa huru, toba zinapokelewa, na aamali zinakubaliwa.”

  • 1. Tabaaraka-llahu, wanasema tabaraka ina maana mbili: moja ya hizo mbili ni: kheri Yake imebarikiwa, na neema Zake na hisani Zake zimezidi. Hii ni dua, na ya pili iwe yakusudiwa: kuzidi na kutukuka dhati na sifa Yake, kwa maana ya kwamba hawezi kulinganishwa na mwingine; na huu ni utukuzo.
  • 2. Hakusudii kuwa matunda yake hayana manufaa yeyote, kwani hiyo sio sifa njema, bali amekusudia kuwa matunda yake hayafikiwi kwa mabavu, wala hayachumwi kwa kupora.
  • 3. Fitra: Mwanya: ni wakati uliopo kati ya manabii, yaani huyu aliopo muda wake umekwisha kabla ya kuja mwingine.