read

Na Miongoni Mwa Khutba Zake (a.s) - at-Tabari ameieleza katika Ta’arikh yake katika matukio ya mwaka wa 37 H.A., na Ibn Muzahim katika Swifiin, uk. 256.

Baadhi Ya Siku Za Siffiin

“Kwa kweli nimeona kukimbia kwenu na kutawanyika kwenu mbali na safu zenu za vita, mkizungukwa na watu fedhuli na duni, na mabedui wa (Shaam) Syiria, ingawaje ninyi ni watangulizi katika waarabu na ni kilele cha utukufu na kilele cha ubora, na mna daraja ya juu mfano wa ile ya pua, na ule wa nundu kubwa ya ngamia.

Uhemaji wa moyo wangu utapoa tu niwaonapo mnawazunguka kama walivyokuwa wamewazungukeni, na mnawaondoa mahali mwao kama walivyokuondoeni, mkiwauwa kwa mishale na kuwachoma kwa mikuki, hivyo msitari wao wa mbele uangukie juu ya msitari wao wa nyuma, kama ngamia walioshikwa na kiu waliofukuzwa kutoka kwenye manyweo yao, na kuzuiliwa maendeo yao ya kunywea maji!”