read

13. Hukumu Za Ndoa

Kwa mujibu wa fatawa za Alhaji Sayyed Ali Hussein Sistani, Najaf- Ashraf, Iraq.

Kwa sababu ya mkataba wa ndoa ndipo mwanamke anahalalishwa kwa mwanamme na vile vile mwanamme anahalalishwa kwa mwanamke na mkataba huu upo wa aina mbili; mkataba wa kwanza ni wa kudumu na mkataba wa pili ni muta'. Tofauti baina ya mikataba hii miwili ni kwamba katika mkataba wa daima mwanamke anapoolewa hautambulishwi muda fulani kwa hivyo inadumu umri wao mzima, na muta' humo kunatajwa muda wa kuishi kwa ndoa hiyo; yaani mtu wanaweza kuoana na mwanamke kwa mapatano ya kwa saa moja au siku moja au mwezi mmoja au mwaka mmoja au muda mwingine wowote; lakini muda huo usizidi umri wa mwanamke au umri wa mwanamme kwa sababu katika sura hii ndoa hii itakuja kuwa batil; na ndoa hii inajulikana kama ndoa ya muta'. Ndoa hii ya muta' itazungumziwa peke yake katika kitabu hiki katika sehemu ya pili hivyo kwa habari zaidi na undani zaidi vitapatikana katika sehemu ya pili ya kitabu hiki.

(2372) Ndoa iwe ya kudumu au ya muda mfupi ni lazima sigha isomwe, kwa mwanamke na kwa mwanamme kuwa radhi nakuandika kwao hakutoshi. Itambidi mwanamke na mwanamme wasome wenyewe hiyo sigha ya ndoa ama wamtafute wakili ambaye atasoma kwa niaba yao.

(2373) Wakili huyo sio lazima awe mwanamme vile vile mwanamke anaweza akawa wakili wa upande wowote huo.

(2374) Hadi hapo mwanamke na mwanamme watakapokuwa yakini kuwa mawakili wao wameshai soma sigha ya ndoa basi hapo huyo mwanamke na mwanamme watakuwa hawaja halalishwa na hivyo hawawezi hata kutazamana, na kwa kukisia kuwa mawakili wao wamesoma sigha vile vile haitoshelezi lakini mawakili wao wakisema tumesoma sigha lakini wao kama hawakuridhika au hawakuyakini basi kuamini ni swala la mashaka.

(2375) Iwapo mwanamke atamteua wakili wake amsomee sigha amsomee nikah na mtu fulani kwa muda wa siku kumi na hakumtajia mwanzo wa siku kumi hizo basi wakili siku atakayoichagua ndio itakuwa mwanzo wa siku kumi hizo, lakini iwapo wakili huyo atajua mwanamke huyo alikuwa akikusudia siku fulani au saa fulani basi itambidi asome hiyo sigha kwa mujibu wa yule mwanamke alivyotaka.

(2376) Katika ndoa ya daima au ya muda mfupi inawezekana mtu mmoja akawa wakili wa upande wa mwanamke na mwanamme na vile vile mtu anaweza kuwa wakili wa mwanamke wakati yeye mwenyewe anamuoa huyo mwanamke lakini ni ehtiyate mustahab kuwa ndoa isomwe na watu wawili.

Namna ya kusoma sigha ya ndoa

(2377) Iwapo mwanamme na mwanamke watapenda wajisomee wenyewe sigha ya ndoa yao basi itawabidi kwanza watambulishe kiasi cha mahari yao na ndipo mwanamke aseme: "Zawwajtuka nafsi alaa sidaaqil ma'alum" yaani mimi kwa mahari ambayo imekubaliwa nimejifanya mke wako.

Hapo mwanamme atasema Qabiltu tazwija-yaani mimi nimekubali wewe kuwa mke wangu. Na katika sura hii ndoa yao ni sahihi.

Iwapo sigha ya ndoa hii itasomwa na wakili yaani iwapo jina la mwanamme ni Ahmad na jina la mwanamke ni Fatima na hapo wakili wa mwanamke akasema: "Zawwajtu muwakkilaka Ahmad muwakkilati Fatima 'ala sidaaqil ma'alum" na katika upande wa wakili wa mwanamme atasema "Qabiltu tazwija li-muwakkili Ahmad 'alaa sidaaqil ma'alum" Na hapo ndoa hiyo itakuwa sahihi.Vile vile ni ehtiyat-i-mustahab kuwa itambidi mwanamme au wakili wa mwanamme atamke maneno kwa mujibu wa maneno yaliyotamkwa na mwanamke au wakili wake mfano iwapo mwanamke atatamka "zawwajtu" basi mwanamme naye itambidi aseme "Qabiltu tazwija" na wala asiseme 'Qabiltu nikah.'

(2378) Iwapo mwanamme na mwanamke watapenda wajisomee sigha ya ndoa yao hivyo baada ya kuafikiana muda na mahari wanaweza kujisomea wenyewe. Hivyo mwanamke ataanza "zawwajtuka nafsi fi muddatil ma'alumat 'alaal mahril ma'alum" na hapo akimaliza mwanamme atasema "Qabiltu." Kwa hapo ndoa itakuwa sahihi na iwapo wataweka mawakili wao basi wakili wa mwanamke atamwambia wakili wa mwanamme "zawwajtu muwakkilati fil muddatil ma'alumati 'alaal mahril ma'alum." na hapo wakili wa mwanamme baada ya kusubiri kwa punde atasema: "Qabiltu tazwija limuwakkili ha-kadhaa " na ndoa yao itakuwa sahihi.

Masharti ya ndoa

(2379) Ndoa ina masharti na machache ndiyo yameorodheshwa kama ifuatavyo:-

1. Katika misingi ya ihtiyat, sigha isomwe katika Kiarabu kilicho sahihi na lau mwanamke na mwanamme hawataweza kusoma katika Kiarabu basi wanaweza kusoma katika lugha nyingine wanayoijua wao vyema ambamo maana ya maneno zawwajtu au Qabiltu inafahamika vyema kwao. Na si lazima kuweka wakili.

2. Mwanamme au mwanamke au mwakilishi wao, ambaye anasoma nikah yao, awe na nia ya 'insha' (yaani ikifanywa kutekelezwa papo hapo). Katika maneno mengine iwapo mwanamme na mwanamke wanasoma wenyewe, nia ya mwanamke anaposema zawwajtuka nafsi ikimaanisha kuwa amekuwa mke wake papo hapo; na mwanamme kwa kusema Qabiltu tazwija basi huyo mwanamme amemkubalia papo hapo huyo mwanamke kama mke wake. Na iwapo wakili wa mwanamke na mwanamme ndiye anaye soma nikah ndoa, nia zao wanaposema zawwajtu na Qabiltu ziwe kwamba mwanamke na mwanamme waliowateua wao kuwawakilisha, papo hapo wamekuwa mtu na mke wake.

3. Mtu yeyote asomaye nikah ama iwe yake mwenyewe au awe wakili wa mtu mwingine, lazima awe mtu mwenye akili na fahamu timamu, na kwa tahadhari, awe baleghe pia.

4. Iwapo nikah inasomwa na mawakili au walezi wa mwanamke na mwanamme, lazima wawatambulishe mwanamke na mwanamme kwa kuwataja majina yao au kwa kutoa ishara ya kuwatambulisha wao. Hivyo iwapo mtu ana mabinti zaidi ya mmoja na yeye akamwambia mwanamme: zawwajtuka ihda banaati (yaani nimekuoza mmoja wa mabinti wangu kuwa mke wako) na mwanamme akasema Qabiltu yaani nimekubali (hapo ndoa hiyo itakuwa batil kwa sababu hakuna msichana aliyetambulishwa ni msichana yupi.

5. Ni lazima mwanamme na mwanamke wawe radhi kuingia katika mkataba wa ndoa. Lakini iwapo mwanamke ataonekana akisita kutoa ruhusa ya ndoa hiyo, lakini inaonekana kuwa kimoyo amekubaliana nayo, basi ndoa hiyo iko sahihi .

(2380) Iwapo katika kusoma nikah hata herufi moja ikisomwa isivyo sahihi, kubadilika kwa maana, basi ndoa hiyo itakuwa batil.

(2381) Mtu yule ambaye anasoma nikah na anajaribu kuleta maana kwa ujumla, wakati akiwa na nia ya maana hiyo hiyo, hiyo ndoa itakuwa sahihi. Si lazima kwa mtu huyo kuelewa maana halisi ilivyo ya kila neno au kujua kanuni za lugha ya Kiarabu.

(2382) Iwapo ndoa ya mwanamke itasomwa bila ya ruhusa yake lakini baadaye mwanamme na mwanamke wakakubaliana na ndoa hiyo wakaridhiana, hiyo ndoa ni sahihi.

(2383) Iwapo mwanamme na mwanamke au mmoja wao, amelazimishwa kuingia katika mkataba huo, na wakaridhia baada ya nikah kusomwa basi ndoa hiyo itakuwa ni sahihi, ingawaje ni vyema iwapo nikah hiyo itasomwa tena.

(2384) Baba au babu wanaweza kufanya mkataba wa ndoa kwa ajili ya mvulana au msichana walio wadogo, au kwa niaba ya mvulana au msichana aliye na akili kasoro, lau watakuwa wamebaleghe na baada ya watoto kubaleghe au huyo mwenye akili kasoro akawa na akili timamu, basi wao wana uwezo wa kuiweka hiyo ndoa ikaendelea au kuikatisha iwapo kuna mambo maovu yaliyopo katikati. Lakini iwapo mmoja wa watoto hawa ambao bado hawajabaleghe watakataa hii ndoa, basi katika hali hii udharuri wa tahadhari talaqa au kusomwa tena kwa ndoa, hali itakayokuwapo lazima isomwe.

(2385) Iwapo msichana atafika wakati wa kubaleghe na bado yu bikira na yuko Rashida (yaani anaweza kuamua kwa ajili ya masilahi yake) anataka kuolewa, basi itambidi apate ruhusa ya baba wake au ya babu wake mzaa baba, ingawaje atakuwa yeye akijitazama mwenyewe katika maswala yake. Hata hivyo si lazima kwake kwa msichana huyo kupata ruhusa ya mama au kaka yake.

(2386) Katika sura zifuatazo haitakuwa lazima kwa mwanamke kupata idhini ya baba au babu mzaa baba kabla ya kuolewa:

1. Iwapo yeye si bikira

2. Iwapo yeye ni bikira lakini baba au babu mzaa baba yake wanamkatali idhini ya kuolewa na mwanamme ambaye ni mwema katika macho ya Shariah na vile vile katika tamaduni na desturi zao.

3. Iwapo baba na babu mzaa baba hakubali kushiriki katika ndoa.

4. Iwapo baba au babu mzaa baba hawako katika hali ya kutoa idhini, mfano hawana akili timamu, n.k.

5. Haiwezekani kupata idhini yao kwa sababu ya kutokuwapo kwao, au kwa sababu zingine kama hizi, na mwanamke anataka kuolewa haraka.

(2387) Iwapo baba au babu mzaa baba watafanya mkataba wa ndoa kwa niaba ya mtoto wao wa kiume ambaye hajabaleghe bado na huyo mtoto wa kiume atakapo baleghe itabidi kumlipia gharama zote mke wake. Na hata kabla ya kubaleghe kiasi kwamba huyo anakuwa na umri wa kuweza kuona raha ya mwanamke huyo na mwanamke asiwe mdogo sana kiasi kwamba asiweze kuwa na uhusiano wa kusuhubiana na bwana wake. Na katika hali mbali na hizi, kuwe na dalili za kuthibitisha kuwa anahitaji kugharamiwa mume wake hivyo kuwepo na maafikiano ikiwa ni njia ya tahadhari.

(2388) Iwapo baba au babu mzaa baba wataingia katika mkataba wa ndoa kwa niaba ya mtoto wao asiyebaleghe itawabidi walipe mahari iwapo mtoto hana uwezo wake, au iwapo mmoja wao atakayechukua jukumu la kulipa mahari hayo. Katika hali nyingineyo, baba au babu mzaa baba wanaweza kulipa mahari kutoka milki ya mtoto, lakini kisizidi kiasi cha mahari ya kawaida inayotolewa katika sura kama hii. Lakini iwapo hali ya wakati huo itadai kulipiwa mahari zaidi, basi watalipa kutoka milki ya mtoto, na sivyo vinginevyo, hadi hapo mtoto mwenyewe atakapokubaliana nayo baada ya kubaleghe.

Bibi na bwana wanaweza kuvunja ndoa

(2389) Iwapo mwanamme atakuja kujua baada ya kusomewa nikah (ndoa) kuwa mke wake wakati wa kusomewa mkataba wa ndoa alikuwa na kasoro mojawapo ya sita zifuatazo basi anaweza kubatilisha ndoa:-

1. Kichaa (hata kama kinakuja kwa muda fulani),

2. Ukoma

3. Magonjwa mabaya ya ngozi

4. Kipofu

5. Mlemavu, hata kama sio kiasi cha kutambaa ardhini,

6. Kuwapo kwa kipande cha nyama au mfupa katika ndani mwa sehemu za siri za mwanamke jambo ambalo linaweza au lisiweze mwanamke kuingiliwa au kushika mimba na iwapo mwanamme atatambua kuwa mke wake wakati wa kusomewa nikah, alikuwa ana ugonjwa unaoitwa Ifza'- yaani njia ya mkojo wake na vipindi vya damu vimekuwa moja au njia yakupitia damu ya haidh na njia ya kupitia choo imekuwa moja, katika sura hii mwanamme hawezi kubatilisha ndoa yake. Kwa tahadhari ya lazima itambidi kumpa talaqa iwapo itabidi kuvunja ndoa hiyo.

(2390) Mwanamke anaweza kubatilisha ndoa katika sura zifuatazo hata bila ya kupewa talaqa:

1. Iwapo atajua kuwa mume wake hana sehemu zake za siri (uume wa mwanamme).

2. Iwapo atajua kuwa uume wa bwana wake umekatwa kabla au baada ya kusuhubiana.

3. Iwapo bwana wake ana ugonjwa unaomfanya asiweze kusuhubiana, hata kama ugonjwa huo umetokezea baada ya ndoa au baada ya kusuhubiana.

(2391) Iwapo mwanamke atavunja ndoa kwa sababu ya mume wake hawezi kusuhubiana naye, basi itambidi muume ampe nusu ya mahari waliyopatana. Lakini iwapo mwanamme au mwanamke atavunja ndoa kwa sababu ya kasoro moja au nyingine kama zilivyoelezwa hapo juu, na kama hawajasuhubiana, basi mwanamme hatatakiwa kumlipa chochote mwanamke. Lakini iwapo bibi na bwana walisuhubiana, basi itambidi mwanamme amlipe huyo mke wake mahari kamili. Iwapo mwanamme atavunja ndoa kwa sababu ya kasoro kama zilivyoelezwa katika mas'ala 2389, basi katika sura hii kama hawajasuhubiana mwanamme hatatakiwa kulipa chochote. Na iwapo mwanamme alisuhubiana na mke wake basi itambidi amlipe mahari kamili.

Wanawake ambao kuwaoa ni haramu

(2392) Wafuatao ambao ni mahram kwa mwanamme ni haramu kuwaoa, nao ni:- Mama mzazi, dada yake, binti yake, shanghazi na wifi wake, binti wa kaka yake, binti wa dada yake na mama mkwe.

(2393) Mwanamme anapomuoa mwanamke kuanzia hapo mama mkwe, bibi mzaa mke wake, bibi mzaa baba wa mke wake na wanawake wote walio katika mstari huu ni mahram wake,
( maana yake ni wale wasioruhusiwa kuolewa na yeye), hata kama huyo mwanamme atakuwa hakusuhubiana na mwanamke huyo aliyemuoa.

(2394) Mtu anapooa mwanamke, na akasuhubiana naye, basi watoto wa huyo mke wake na wajukuu wa mke huyo (wa wanaume au wasichana ) na kizazi mfululizo kinachotokana hapo kuanzia huyo mwanamme wote kwa pamoja wanakuwa mahram. Bila ya kujali kuwa hao wote walikuwapo wakati wa kusomwa ndoa au walizaliwa baada ya ndoa yao.

(2395) Iwapo mwanamme ataoa mwanamke, na hakusuhubiana, basi ni tahadhari ya lazima kuwa muda utakao dumu ndoa yao, asimuoe mtoto wa mke huyo.

(2396) Shanghazi na wifi wa mwanamme kwa upande wa baba na mama yake, na shanghazi na wifi kwa upande wa baba yake, na shanghazi na wifi wa mababu zake, na shanghazi na wifi wa mama yake na shanghazi na wifi wa bibi mzaa mama, na vile mfululizo unavyoendelea nyuma, hao wote ni mahram wake.

(2397) Baba na babu wa mume, hata mfululizo huu utakavyo kwenda ni mahram wa mwanamke wa bwana huyo.Vivyo hivyo watoto wa kiume na wajukuu wa kiume (watoto wa watoto wa kike), vyovyote vile mfululizo huu utakavyokwenda chini, pia ni mahram wake, bila kujali iwapo hao walikuwapo wakati wa ndoa yake au walizaliwa baadaye.

(2398) Iwapo mwanamme atamuoa mwanamke, (iwapo ndoa yao ni ya kudumu au ndoa ya muta') kamwe hawezi kumuoa dada wa mke wake, wakati mwanamke huyo bado ni mke wake.

(2399) Iwapo mwanamme atampa mke wake talaqa inayoweza kurudiwa, kama vile itakavyokuwa inaelezwa katika Shariah zinazohusiana na talaqa, basi hawezi kumuoa dada wa mke wake wakati mke akiwa katika Iddah. Lakini iwapo hiyo ni talaqa isiyoweza kurudiwa, basi anaweza kumuoa dada wa mke wake. Na kama ni Iddah ya muda mfupi (muta'),tahadhari ya lazima ni kuwa mtu hapaswi kumuoa dada wa mke katika kipindi hicho.

(2400) Mwanamme haruhusiwi kumuoa binti wa kaka au dada wa mke wake bila idhini ya mke wake. Na lau kama ataoa bila idhini ya mke wake, na hapo baadaye mke wake akaridhia ndoa hiyo, basi itakuwa ni sahihi.

(2401) Iwapo mwanamke atakuja kufahamu hapo mbeleni kuwa bwana wake ameoa binti wa dada yake au kaka yake huyo mwanamke na akakaa kimya, na hapo baadaye akaridhia ndoa hiyo, itakuwa ni sahihi. Na lau mwanamke huyo hataridhia hapo baadaye, ndoa hiyo itakuwa batil.

(2402) Iwapo mwanamme kabla ya kumuoa binti wa shanghazi au wifi yake (Mungu atuepushe nayo) akasuhubiana na mama mkwe, basi hawezi kumuoa huyo msichana kwa misingi ya tahadhari.

(2403) Iwapo mwanamme ataoa watoto wa wifi au watoto wa shanghazi wake na baada ya kusuhubiana na mke wake akasuhubiana na mama wa mke wake huyo, basi tendo hili halitakuwa sababu ya kuachana (ndoa yao itaendelea). Na Shariah kama hii itatumika iwapo huyo mwanamme atasuhubiana na mama wa mke wake baada ya kusomewa ndoa, lakini kabla hajasuhubiana na mke wake, ingawaje tahadhari iliyosisitizwa mno katika sura hii ni kwamba huyo mwanamme ajitoe mbali kwa kumpa talaqa.

(2404) Iwapo mwanamme atafanya zinaa pamoja na mwanamke mbali na shanghazi na wifi wake, ni tahadhari iliyosisitizwa mno kuwa asioe binti wa mama. Kwa hakika, na kama atamuoa, na atafanya zinaa na mama wa mke wake kabla ya kusuhubiana na mke wake, basi tahadhari iliyosisitizwa mno ni kwamba ajitenganishe naye, lakini iwapo huyo mwanamme akasuhubiana na mke wake baada ya ndoa, na hapo baadaye ndipo akaja akafanya zinaa na mama wa mke wake, basi katika sura hii sio lazima kwake kutengana na mke wake.

(2405) Mwanamke wa Kiislamu hawezi kuolewa na mwanamme asiye Mwislamu, na vile vile mwanamme wa Kiislamu hawezi kumuoa mwanamke asiye Mwislamu ambao sio katika Ahlul kitab. hata hivyo hakuna ubaya kwa kuingia katika mikataba ya ndoa ya muda mfupi (muta') pamoja na wanawake wa Kiyahudi na wanawake Wakristo, lakini tahadhari ya lazima mwanamme wa Kiislamu asiwachukue hawa katika ndoa yao ya kudumu; zipo baadhi ya madhehebu kama Khawarij, Ghulat, na nasibi ambao wanajitambulisha na kudai kuwa wao ni Waislamu, lakini wametenganishwa kuwa si Waislamu. Wanaumme Waislamu na wanawake hawawezi kuoa au kuolewa ndoa ya kudumu au muta' pamoja na watu hao.

(2406) Iwapo mwanamme atafanya zinaa pamoja na mwanamke ambaye yupo katika Iddah ya talaqa inayoweza kurudiwa, kama tahadhari huyo mwanamke atakuwa ni haramu kwa ajili yake. Na iwapo huyo mwanamme atafanya zinaa pamoja na mwanamke ambaye yupo katika Iddah ya muda mfupi, au ndoa isiyoweza kurudiwa, au katika Iddah ya kifo cha mume wake, basi anaweza kumuoa huyo mwanamke hapo baadaye, ingawaje ni tahadhari iliyosisitizwa mno kuwa yeye asimuoe mwanamke huyo.

Maana za talaqa za kurudiwa na kutokurudiwa, na Iddah za muta' na Iddah za kifo, zinazungumziwa vyema katika vitabu vya fiqhi katika sura za talaqa.

(2407) Iwapo mwanamme atafanya zinaa pamoja na mwanamke ambaye hajaolewa na ambaye hayuko katika Iddah yoyote ile, kama tahadhari huyo mwanamme hawezi kumuoa huyo mwanamke hadi hapo amefanya tawba ya Allah swt na ameomba msamaha kwake. Lakini iwapo atatokezea mtu mwingine wa kumuoa huyo mwanamke kabla ya mwanamke huyo hajafanya tawba ya kuomba msamaha kwa Allah swt, basi hakuna mushkeli. Iwapo mwanamke huyo akaja kujulikana kuwa ni malaya katika sura hii haitaruhusiwa kumuoa huyo mwanamke hadi hapo amefanya tawba wazi wazi na kuomba msamaha wa Allah swt.

Na katika misingi hiyo hiyo haitaruhusiwa kuolewa na mwanamme ambaye anajulikana kuwa yeye anajihusisha katika mambo ya malaya hadi hapo huyo mwanamme atubu kidhahiri na aombe msamaha wa Allah swt. Na iwapo mwanamme atataka kumuoa mwanamke ambaye amejulikana kufanya zinaa pamoja naye au amezini pamoja na mwanamme mwingine basi itambidi kwa misingi ya tahadhari, asubiri hadi huyo mwanamke awe tohara kutokana na haidh.

(2408) Iwapo mwanamme atamuoa mwanamke ambaye yuko katika Iddah ya mwanamme mwingine, na lau wote kwa pamoja wanajua au mmoja wao anajua kuwa Iddah ya mwanamke huyo haijaisha, na wanatambua waziwazi kuwa kuoa mwanamke akiwa katika Iddah ni haramu, hivyo huyo mwanamke atakuwa ni haramu kwa milele kwa ajili ya mwanamme huyo hata kama huyo mwanamme baada ya kusomewa ndoa atakuwa hajasuhubiana na mwanamke huyo.

(2409) Iwapo mwanamme atamuoa mwanamke ambaye yuko katika Iddah ya mwanamme mwingine, na atasuhubiana naye, basi mwanamke huyo atakuwa haramu kwa ajili yake milele, hata kama yeye mwanamme atakuwa hakujua yeye mwanamke alikuwa katika Iddah, au hakujua kuwa ni haramu kumuoa mwanamke akiwa katika Iddah.

(2410) Iwapo mwanamme atamuoa mwanamke huku akijua kuwa mwanamke huyo anaye bwana, basi itambidi ajitenganishe naye na asimuoe kamwe maishani mbeleni. Na Shariah kama hiyo ndiyo itatumika katika misingi ya tahadhari, kama yeye mwanamme hakujua kama yeye mwanamke ameolewa na anaye bwana, na vile vile huyo mwanamme alikuwa amesuhubiana na mwanamke huyo baada ya ndoa yake.

(2411) Iwapo mwanamke aliyeolewa akafanya zinaa, yeye katika misingi ya tahadhari, atakuwa ni haramu wa milele kwa mtu aliyefanya zinaa naye, lakini hatakuwa haramu kwa mume wake aliyemoa na ndoa halali. Na lau huyo mwanamke hatafanya tawba, na ataendelea na tabia yake hiyo ya kufanya zinaa basi itakuwa ni afadhali kwa bwana wake ampe talaqa, ingawaje itambidi amlipe na mahari yake.

(2412) Katika sura ya mwanamke ambaye amepewa talaqa au mwanamke ambaye yuko katika ndoa ya muta' na bwana wake amekiachia kipindi kilichobakia, au iwapo kipindi cha ndoa ya muta' kimekwisha, na baada ya muda akaolewa na bwana mwingine na hapo akaijiwa na shaka iwapo wakati wa ndoa yake ya pili lau Iddah ya bwana wake wa kwanza ilikwisha au haikuisha, basi itambidi apuuzie shaka hiyo.

(2413) Iwapo mwanamme aliye baleghe atafanya Ulawiti na kijana wa kiume, basi mama, dada na binti wa mtoto huyo atakuwa haramu kwa ajili yake. Na Shariah kama hii itatumika wakati ambapo mtu ambaye amelawitiwa ni mwanamme mtu mzima, au wakati mtu anayelawiti ni kijana ambaye hajabaleghe. Lakini iwapo mtu atakuwa na shaka iwapo kikofia cha uume wa mwanamme umeingia katika sehemu za choo au haikuingia, basi katika sura hiyo mwanamke katika kikundi cha hapo juu hawatakuwa haramu kwa ajili yake.

(2414) Iwapo mwanamme atamuoa mama au dada wa kijana mvulana, na akamulawiti huyo mvulana baada ya ndoa kwa misingi ya tahadhari hao watakuwa ni haramu kwa ajili yake.

(2415) Iwapo mwanamme ambaye yuko katika hali ya ihram (ni amri moja wapo inayotimizwa wakati wa kuhiji) akaoa mwanamke, basi ndoa hiyo ni batil, na lau alijua kuwa kuoa katika hali ya ihram ni haramu, basi mwanamme huyo hawezi kumuoa mwanamke huyo.

(2416) Iwapo mwanamke ambaye yuko katika hali ya ihram anaolewa na mtu ambaye hayuko katika hali ya ihram, basi ndoa yake ni batil. Na iwapo mwanamke huyo alielewa kuolewa katika ndoa ya ihram ni haramu, katika misingi ya tahadhari ya faradhi, yeye mwanamke hawezi kamwe kuolewa na mwanamme huyo tena.

(2417) Iwapo mwanamme hafanyi tawaf-un-nisa (ni amri mojawapo ya kutimizwa katika Hajj na umra mufrada ) basi mke wake na wanawake wengine watakuwa haramu kwa ajili yake, vile vile iwapo mwanamke hatafanya tawaf-un-nisa, basi bwana wake na wanaume wengine watakuwa haramu kwa ajili yake. Lakini iwapo wao (mwanamme au mwanamke )watatekeleza tawaf-un-nisa hapo mbeleni, basi watakuwa halali.

(2418) Iwapo mwanamme atafunga ndoa pamoja na msichana ambaye bado hajabaleghe ni haramu kusuhubiana naye kabla hajatimiza umri wa miaka tisa. Lakini iwapo atasuhubiana naye basi huyo msichana ambaye ni mke wake hatakuwa haramu kwa ajili yake hapo atakapobaleghe, hata kama atakuwa amedhurika na Ifza (sura iliyoelezwa katika hukumu Na 2388) ingawaje katika misingi ya tahadhari itambidi, ampe talaqa.

(2419) Mwanamke ambaye amepewa talaqa mara tatu, atakuwa haramu kwa ajili ya mume wake. Lakini ataolewa na mwanamme mwingine, kwa mujibu wa Shariah na kanuni zinazoelezwa vyema katika vitabu vya fiqh katika sura ya talaqa, bwana wake wa kwanza anaweza kumuoa baada ya bwana wake wa pili kufariki, au kumpa talaqa mwanamke huyo na itambidi akamilishe kipindi cha Iddah.

Hukumu za ndoa ya kudumu

(2420) Kwa mwanamke ambaye ameolewa katika ndoa ya kudumu, ni haramu kwa ajili yake kutoka nje ya nyumba yake bila ya idhini ya bwana wake, ingawaje kutoka kwake huko nje hakutavunja haki za bwana wake.Vile vile itambidi ajitolee kwa ajili ya kusuhubiana na bwana wake, na kamwe asimuzuie mume wake kusuhubiana naye bila ya kuwa na sababu ya kiadilifu. Na kiasi kwamba mwanamke huyo hataondoka katika misingi ya kutimiza wajibu wake, ni wajibu kwa mume wake kumpatia chakula, mavazi na nyumba ya kuishi na lau bwana wake hatampatia vitu hivyo, bila ya kujali kama ana uwezo wa kumpatia vitu hivyo au hana basi atakuwa anadaiwa deni na mke wake.

(2421) Iwapo mwanamke hatimizi wajibu wake wa kindoa kwa mume wake, basi hana ulazimisho wa chakula, nguo au nyumba kutoka kwa bwana wake hata kama akiishi naye. Lakini iwapo atagoma kumtii katika nyakati mbalimbali basi hukumu ya kiakili yetu inasema kuwa huyo mwanamke hatakuwa na haki ya kudai chochote kutoka kwa bwana wake. Lakini hukumu hii ni swala la ishkal. Katika sura yoyote ile haimaanishi kuwa inapoteza haki zake za mahari.

(2422) Mwanamme hana haki ya kumlazimisha mke wake kufanya kazi za nyumbani.

(2423) Gharama za usafiri za mwanamke ni lazima zilipwe na bwana wake, iwapo zitazidi kuliko gharama za nyumbani na iwapo atakuwa amesafiri kwa ruhusa ya bwana wake. Lakini kwa gharama za kusafiri kwa gari au kwa ndege n.k. na gharama zinginezo ambazo ni dharura katika safari, zitachukuliwa na mke mwenyewe, isipokuwa wakati ambapo bwana mwenyewe atataka kumchukua mke wake pamoja naye katika safari, ambapo katika sura hii bwana ndiye atakaye gharimia gharama zote.

(2424) Iwapo bwana ambaye anawajibika kumlisha na kumtunza mke wake, hatimizi wajibu huo kwa mke wake, basi mke huyo anaweza kutoa gharama zake za maisha kutoka kwa milki ya bwana wake hata bila ruhusa ya bwana wake. Na lau sura hii haitawezekana, na atalazimika mwanamke huyo kufanya kazi na kujilisha mwenyewe, na mwanamke huyo hawezi kupeleka swala lake mbele ya mujtahid (kadhi au Hakimu wa Shariah) ambaye atamlazimisha huyo mwanamme (hata kwa kumtishia kwa kifungo cha jela) kulipa gharama za mwanamke, basi kuanzia pale mwanamke huyo atakapoanza kuchuma maisha yake haitakuwa faradhi kwa mwanamke huyo kumtii bwana wake.

(2425) Iwapo mwanamme kwa mfano ana wanawake wawili na hupitisha usiku kwa mmoja wao, hivyo ni wajibu kwake yeye kupitisha usiku mmoja kati ya usiku nne kwa mke wa pili; katika hali mbali na hii, si wajibu kwa mwanamme kuwa pamoja na mke wake. Hivyo, ni lazima kwa mwanamme kutojitenga na mke wake kabisa. Na katika misingi ya tahadhari inambidi mwanamme apitishe usiku mmoja kati ya usiku nne akiwa pamoja na mke aliyemuoa kwa ndoa ya kudumu.

(2426) Hairuhusiwi kwa mwanamme kutokusuhubiana kwa zaidi ya miezi minne pamoja na mke wake kijana na ambaye ameolewa kwa ndoa ya kudumu isipokuwa wakati kusuhubiana kule kunaleta madhara kwake au inahitaji nguvu na juhudi zaidi, au wakati ambapo mwanamke mwenyewe anakubali kutokusuhubiana kwa kipindi hicho au sharti liliwekwa na bwana wakati wa kufunga ndoa. Na katika Shariah hii, hakuna tofauti ya sura ya bwana anakuwapo au anapokuwa safarini au mwanamke huyu ameolewa kwa ndoa ya kudumu au kwa ndoa ya muta'.

(2427) Iwapo katika ndoa ya kudumu mahari haijaafikiwa, basi ndoa hii ni sahihi na katika hali hiyo bwana alisuhubiana na mke wake, basi itabidi amlipe mahari yote kamili ambayo itakuwa kwa mujibu kuwa mahari anavyolipwa mwanamke kwa kawaida kwa daraja lake. Ama kuhusiana na muta' hata hivyo kama mahari haijaafikiwa kuanzia mwanzoni basi ndoa hiyo itakuwa batil.

(2428) Wakati wa nikah ya ndoa ya kudumu, kulikuwa hakujaafikiwa wakati wa kulipa mahari, basi mwanamke ana ruhusa ya kumzuia bwana wake asisuhubiane naye hadi hapo atakapomlipa mahari yake, bila ya kujali iwapo bwana wake anaweza kumlipa au hana uwezo wa kumlipa. Lakini iwapo huyo mwanamke atamkubalia mume wake asuhubiane naye kabla ya kupokea mahari, na mume wake akasuhubiana naye, basi kuanzia kusuhubiana kwao kwa mara ya kwanza mwanamke huyo kamwe hawezi kumzuia mume wake asisuhubiane naye bila ya kuwa na sababu za kuridhisha.

Muta'

(2430) Kufanya muta' (ndoa ya muda mfupi) pamoja na mwanamke ama kwa ajili ya kutaka raha ya kusuhubiana, au kwa sababu nyingine yoyote ile, basi ni sahihi.

(2431) Ni tahadhari ya faradhi kuwa mwanamme asikose kusuhubiana naye mwanamke aliyefanya naye muta' kwa kipindi cha miezi minne yaani inambidi isipite kipindi hicho bila kusuhubiana na mwanamke aliyefanya naye muta'.

(2432) Iwapo mwanamme aliyefanya muta' na mwanamke, ataweka shuruti kuwa mume wake huyo hatasuhubiana naye basi ndoa hiyo itakuwa ni sahihi na vile vile shuruti lake hilo pia linakubalika, kwa hivyo mume atafaidika kwa starehe zinginezo tu bila ya kusuhubiana naye. Hata hivyo iwapo atakubali kusuhubiana naye hapo baadaye, mwanamke anaweza kusuhubiana na bwana wake huyo, na sharti hili linatumika katika ndoa ya kudumu.

(2433) Mwanamke aliyeolewa kwa muta' hawi mustahiki wa kupewa gharama zake hata kama atashika mimba.

(2434) Mwanamke aliyeolewa kwa muta' hastahiki kulala na bwana wake, na wala hana urithi na bwana wake na wala bwana wake pia hamrithi mke wake aliyeolewa kwa muta'. Hata hivyo iwapo mmoja wao anaweka sharti na kurithiana basi swala hilo ni ishkal, lakini hata hivyo lazima ichukuliwe tahadhari katika kuweka maanani na utekelezaji wake.

(2435) Iwapo mwanamke ambaye ameolewa kwa muta' alikuwa hajui kuwa yeye si mustahiki wa gharama wala kulala na bwana wake lakini ndoa yake itakuwa sahihi bado, na kutokujua kwake (kuwa yeye si mustahiki) bado hatakuwa na haki ya kudai chochote kwa bwana wake.

(2436) Iwapo mwanamke aliyeolewa kwa muta' atatoka nje ya nyumba bila ya ruhusa ya bwana wake na kwa vyovyote vile haki ya bwana wake itakuwa imevunjwa basi kutoka kwake nje ni haramu. Na iwapo haki ya bwana wake itakuwa imesalimika ichukuliwe tahadhari iliyosisitizwa kuwa mwanamke huyo asitoke nje ya nyumba bila ya ruhusa ya bwana wake.kuwa

(2437) Iwapo mwanamke atampa ruhusa mwanamme ya kuwa wakili wake katika kusoma nikah ya muta' pamoja na mwanamke huyo kwa kipindi fulani na kwa kiasi fulani cha mahari, na badala yake huyo mwanamme yaani wakili akasoma nikah ya kudumu pamoja na mwanamke huyo au anasoma nikah ya muta' pamoja na mwanamke huyo bila ya kubainisha wazi wazi kipindi cha muda au kiasi cha mahari, basi ndoa hiyo itakuwa batil. Lakini iwapo mwanamke ataridhia na kutoa ruhusa kwa mapatano hapo mbeleni basi ndoa hiyo itakuwa sahihi.

(2438) Ili kutaka kuwa mahram (yaani ambaye huwezi kumuoa na anakuwa ni jamaa wako wa karibu), baba au babu mzaa baba wanaweza kumuingiza mtoto wao asiyebaleghe au msichana wao asiyebaleghe katika ndoa pamoja na mtu mwingine kwa kipindi kifupi, ili mradi haitatokezea ufisadi. Hata hivyo, iwapo wao watamuoza mvulana mdogo au msichana mdogo ambaye kwa vyovyote vile hawezi kupata starehe ya kusuhubiana katika kipindi hicho, basi katika sura hii usahihi wa ndoa kama hiyo ni ishkal.

(2439) Iwapo baba au babu mzaa baba wa mtoto asiyekuwapo, wakamuoza kwa mtu ili kutaka kuwa mahram, bila kujua iwapo mtoto yuko hai au amekufa, basi kusudi litapatikana iwapo katika kipindi cha ndoa, mtoto atakuwa na uwezo wa kusuhubiana. Iwapo hapo baadaye itakuja kujulikana kuwa mtoto huyo hakuwa hai wakati wa kusomwa ndoa hiyo basi itachukuliwa kuwa ni batil. Na wale wote ambao walikuwa ni mahram sasa watakuwa si mahram.

(2440) Iwapo bwana atakuwa amempatia zawadi bibi wake aliyemuoa kwa muta' katika kipindi hicho, na atakapokuwa amemuachia na kama alikuwa amesuhubiana naye basi itabidi ampatie vitu vyote vile alivyokuwa ameahidi kumpa. Na lau kama alikuwa hajasuhubiana naye basi itambidi ampe nusu ya mahari yake, ingawaje achukue tahadhari iliyosisitizwa mno kuwa itambidi ampe mahari kamili.

(2441) Iwapo mwanamme ataingia katika muta' pamoja na mwanamke na mwanamke atakapokuwa katika kipindi cha Iddah kabla ya kuisha basi inaruhusiwa mwanamme kumuoa mwanamke huyo kwa ndoa ya kudumu au ndoa ya muta'.

Kuwatazama wale wasio mahram

(2442) Ni haramu kwa mwanamme kutazama mwili au nywele kwa mwanamke ambaye siyo mahram bila kujali iwapo ana nia ya kuona raha au sivyo, na kama kuna hatari ya kuangukia katika tendo bovu la kutenda madhambi au siyo. Vile vile ni haramu kutazama uso na mikono mpaka kufika katika vipingili vya mkono ya wanawake kwa nia ya kuona raha au kuna hatari ya kuangukia katika madhambi, na katika hatua ya tahadhari iliyosisitizwa ni kuwa mtu asitazame sura zao au mikono yao hata kama ni bila sababu kama hizo. Vivyo hivyo ni haramu kwa mwanamke kutazama mwili wa mwanamme asiye mahram kwake, isipokuwa sehemu zile ambazo kwa kawaida huwa hazifunikwi, kama uso,mikono, kichwa, shingo na miguu. Mwanamke huyo anaweza kuona sehemu hizi za mwanamme bila ya kuwa na nia ya kutaka raha au iwapo hakutakuwa na hatari ya kutumbukia katika matendo ya madhambi.

(2443) Kuangalia mwili wa mwanamke ambaye hajali kuhusu hijab hata kama atakuwa ameshauriwa si haramu, ili mradi haitamtumbukiza mtu katika matendo ya madhambi au raha ya kusuhubiana au kushangazwa, wala si kwa nia; na katika Shariah hii, hakuna utofautisho baina ya mwanamke wa Kiislamu au mwanamke asiye Mwislamu; na vile vile sehemu zile kama uso mikono ambayo kwa kawaida huwa haifunikwi na sehemu zinginezo za miili yao.

(2444) Inambidi mwanamke afunike mwili wake na nywele zake kutokana na mwanamme ambaye sio mahram kwake na tahadhari iliyo faradhi, kuwa ajifunike mzima dhidi ya wavulana ambao hawajabaleghe na ambao wanaweza kutambua baina ya mema na mabaya na labda wanaweza kuvutiwa katika mambo ya kusuhubiana. Lakini anaweza kuacha uso wake na mikono mpaka juu kidogo viganja visifunikwe mbele ya mtu ambaye sie mahram kwake, ili mradi huku kusimpelekee mtu katika mtego wa madhambi, kwa macho mabaya au yeye kufanya jambo lolote ni haramu; kwa hali zozote hizi itambidi yeye afunike sehemu hizo zote.

Ni haramu kutazama sehemu zake za siri za Mwislamu aliyebaleghe, hata kama itatazamwa nyuma ya kioo au kutokana na kioo kwa mbele, au maji safi yaliyotulia n.k. Kama tahadhari ya lazima, ni haramu vile vile kutazama sehemu za siri za mtu ambaye si Mwislamu na kijana ambaye hajabaleghe na ambaye anaelewa mema na mabaya. Hata hivyo bibi na bwana wanaweza kutazama mwili wa mwenzake.

(2446)Iwapo mwanamme na mwanamke ambao ni mahram kwa kila mmoja, hawana nia ya raha ya kusuhubiana, wanaweza kuona mwili mzima wa mtu na mwenzake isipokuwa sehemu zake za siri.

(2447) Mwanamme hatakiwi kuangalia mwili wa mwanamme mwenzake kwa kupandwa na matamanio ya Ulawiti, na vile vile ni haramu kwa mwanamke kutizama mwili wa mwanamke mwenzake kwa nia ya kutaka kuingiliana naye.

(2448) Iwapo mwanamme anamfahamu mwanamke ambaye siye mahram kwake, basi itambidi kama tahadhari asitazame hata taswira yake n.k.,ili mradi mwanamke huyo hayupo miongoni mwa wanawake mwa wale wasiovaa hijab.

(2449) Iwapo mwanamke anataka kumpiga enema mwanamke mwingine au mwanamme mbali na bwana wake, au kusafisha sehemu za siri za mwanamke au za mwanamme kwa maji, basi itambidi avishe kitu mikono yake ili mikono yake isiguse sehemu hizo za siri za mwanamke au mwanamme. Na vivyo hivyo inatumika kwa mwanamme ambaye anataka kumpiga enema mwanamme au mwanamke mwingine mbali na mke wake, au kusafisha sehemu za siri za mwanamke au mwanamme kwa maji.

(2450) Iwapo mwanamke atakuwa ameugua na anaweza kutibiwa na mganga wa kiume vyema zaidi, basi anaweza kutibiwa naye. Na iwapo daktari huyo mwanamme itabidi amtazame ili kumtibu, au kumgusa mwanamke huyo kwa sababu hizo basi hakuna ishkal yoyote. Hata hivyo, iwapo ataweza kumtibu kwa kumwangalia itambidi asimguse, na kama ataweza kutibu kwa kumgusa mwili wake, basi asimtazame mwanamke huyo.

(2451) Iwapo mtu itambidi atazame sehemu za siri za mgonjwa wake akiwa mwanamke au mwanamme kwa ajili ya matibabu, basi itambidi katika misingi ya tahadhari iliyo faradhi, aweke kioo mbele yake mbele ya mwanamke au mwanamme. Hata hivyo, na kama hakuna njia nyingine bila kuangalia moja kwa moja katika sehemu za siri za mwanamke huyo au mwanamme, basi hakuna mushikeli. Vivyo hivyo iwapo kutachukuliwa muda zaidi kuangalia sehemu hizo za siri kupitia kioo kuliko kumwangalia moja kwa moja, basi anaweza kumtazama moja kwa moja.

Hukumu mbalimbali kuhusu maswala ya ndoa

(2452) Iwapo mtu atakuwa ametumbukia katika matendo (zinaa) ambayo yameharamishwa kwa sababu ya kutokuwa na mke, basi ni faradhi kwake yeye kuoa.

(2453) Iwapo bwana ataweka sharti kabla ya ndoa kuwa mwanamke lazima awe bikira, na baada ya ndoa ikaonekana kuwa si bikira, basi anaweza kuvunja ndoa hiyo. Hata hivyo anaweza kukata kiasi cha mahari yanayolipwa kwa kawaida kwa ajili ya mwanamke aliyebikira au asiyebikira.

(2454) Ni haramu kwa mwanamke na mwanamme ambao si mahram kuwa pamoja katika sehemu zile ambazo hakuna mtu mwingine, iwapo kuna hofu ya kutumbukia katika ufisadi, au hata kama ni mahali ambapo anaweza kutokezea mtu kwa ghafla. Lau kutakuwa hakuna hatari yoyote ya ubaya basi hakuna mushkeli wowote.

(2455) Iwapo mwanamme ndiye atakayepanga mahari ya mwanamke wakati wa ndoa, lakini hana nia ya kumlipa, basi ndoa hiyo itakuwa ni sahihi lakini atakuwa ana deni na mke wake.

(2456) Mwislamu ambaye anaukana Uislamu na kuingia katika dini ya wale wasio Waislamu, ni kafiri na hao ni wa aina mbili; fitri na milli . Kafiri fitri ni yule ambaye wazazi wake au mmoja wao alikuwa Mwislamu alipokuwa amezaliwa, na yeye mwenyewe alikuwa Mwislamu hadi hapo alipofika umri wa kutambua baina ya mema na mabaya na hapo baadaye akaja akawa kafiri. Na kafiri milli ni mtu aliyetofauti kabisa yaani kinyume cha kafiri fitri.

(2457) Iwapo mwanamke atakuwa kafiri baada ya ndoa, ndoa yake itakuwa batil na iwapo mume wake atakuwa hajasuhubiana naye, basi hatakiwi kubakia katika Iddah. Na hali hii itakuwa vivyo hivyo iwapo yeye atabadilika baada ya kusuhubiana na mume wake, au yeye amefikia ugumba (Ya'isa), au alikuwa bado mdogo. Na lau kama atakuwa hajafikia ugumba, basi itambidi atimize Iddah kama vile inavyoelezwa katika hukumu za talaqa. Na ni jambo la kawaida iwapo yeye atakuwa Mwislamu tena akiwa katika kipindi cha Iddah, ndoa yake itasalimika. Hata hivyo inaweza kuchukuliwa kuwa sahihi, na hivyo tahadhari isiachwe. Mwanamke anayeitwa Ya'isa ni yule ambaye amefikia umri wa miaka hamsini (50) na kwa sababu ya umri huo mkubwa anaacha kupata haidh na wala hategemei kuyapata maishani mwake.

(2458) Iwapo mwanamme atakuwa kafiri fitri baada ya ndoa, mke wake atakuwa haramu kwa ajili yake; na huyo mwanamke anatakiwa kuingia katika Iddah (kama ile ya baada) ya kifo cha mume wake maswala ambayo yanaelezwa vyema katika Shariah za talaqa.

(2459) Iwapo mwanamme atakuwa kafiri milli baada ya ndoa, ndoa yake itakuwa batil. Na kama alikuwa hakusuhubiana na mke wake, au mwanamke huyo amekuwa Ya'isa, au kama bado ni mdogo basi hatatekeleza Iddah. Lau kama huyo mwanamme ataingia katika ukafiri baada ya kusuhubiana na mke wake, mke wake akiwa katika hali ya mwanamke yule ambaye anapata haidh kama kawaida, basi itambidi aingie katika Iddah ya talaqa, maswala ambayo yanaelezwa vyema katika maswala ya talaqa. Inachukuliwa kawaida iwapo bwana wake atakuwa tena Mwislamu kabla ya huyo mwanamke kumaliza Iddah basi ndoa yao itasalimika. Hata hivyo haitegemei kuwa hii itakuwa sahihi, lakini tahadhari isiachwe.

(2460) Iwapo mwanamke wakati wa ndoa ataweka sharti kuwa bwana wake asimchukue nje ya mji (utakaotajwa), na mwanamme akakubalia hilo sharti, basi asimchukue mke wake nje ya mji huo bila ya idhini yake.

(2461) Iwapo mwanamke ana mtoto wa bwana aliyemtangulia huyu bwana, basi huyo bwana anaweza kumuoza huyu binti kwa mtoto wake wa kiume, ambaye si mtoto wa mke huyo. Vivyo hivyo iwapo mwanamme atamuoza mtoto wake (wa kiume) kwa msichana, basi yeye akiwa kama baba anaweza kumuoa mama wa binti huyo.

(2462) Iwapo mwanamke atashika mimba kwa sababu ya zinaa, basi haruhusiwi kuangusha mimba hiyo.

(2463) Iwapo mwanamme atafanya zinaa na mwanamke asiye na bwana, wala yeye hayuko katika Iddah, na baadaye akamuoa na mtoto akazaliwa wakiwa bado pamoja na hawajui iwapo huyu mtoto ameingia katika mimba ya mama akiwa wamesuhubiana kihalali au kiharamu basi mtoto huyo atachukuliwa kama mwana halali.

(2464) Iwapo mwanamme hajui kuwa mwanamke huyo yu katika Iddah na akamuoa na mwanamke huyo vile vile hajui kuwa yeye yuko katika Iddah na mtoto akazaliwa kwao, basi huyo mtoto atakuwa ni mwana halali kwa mujibu wa Shariah ni mtoto wao wote. Hata hivyo iwapo mwanamke anajua kuwa yeye alikuwa katika Iddah, na katika kipindi hicho cha Iddah ndoa hairuhusiwi mtoto atakayezaliwa atakuwa ni mtoto wa baba na kwa hali yoyote ile ndoa yao itakuwa batil na wao watakuwa ni haramu kwa kila mmoja.

(2465) Iwapo mwanamke atasema yeye kuwa amekuwa gumba (Ya'isa), maneno yake yasikubalike lakini akisema kuwa yeye hana bwana basi maneno yake yakubalike, isipokuwa pale anapojulikana kuwa haaminiki, katika hali hiyo uchunguzi utahitajika.

(2466) Iwapo mwanamme atamuoa mwanamke baada ya mwanamke kusema kuwa hana bwana, na ikatokezea mtu mwingine akaja akadai kuwa huyu ni mke wake basi madai yake hayatakubaliwa hadi hapo ithibitishwe kwa mujibu wa Shariah.

(2467) Hadi hapo msichana au mvulana anamaliza umri wa miaka miwili, baba yake hawezi kumtenganisha na mama yake. Na kama tahadhari, mtoto asitenganishwe na mama yake hadi umri wa miaka saba.

(2468) Iwapo mtu anayetaka kuoa anajulikana kwa wema na imani yake, basi inasisitizwa kuwa ombi lake hilo lisikataliwe. Mtume Mtukufu s.a.w.w. ameripotiwa kusema: "Popote utakaposikia, popote utakapopokea maombi ya kumuoza mtoto wako kwa mwanamme ambaye sifa zake na ucha Mungu wake unakufurahisha wewe, basi muoze mtoto wako. Na lau hautafanya hivyo, basi ufisadi na maovu yatajaza dunia."

(2469) Iwapo mwanamke ataafikiana na mume wake kuhusu mahari yake, kwa masharti kwamba mwanamme huyo hataoa mwanamke mwingine, basi ni faradhi kwa mwanamme kutokuoa mwanamke mwingine na kwamba mwanamke huyo asidai mahari yake tena.

(2470) Iwapo mwanaharamu ataoa, na mtoto atazaliwa basi mtoto huyo atakuwa ni mwana halali.

(2471) Iwapo mwanamme atasuhubiana na mke wake katika funga za mwezi wa Ramadhani au wakati mwanamke huyo atakuwa katika vipindi vyake vya mwezi (haidh), mwanamme atakuwa ametenda dhambi lakini iwapo mke atashika mimba katika hali hiyo basi mimba hiyo ni halali.

(2472) Iwapo mwanamke atakuwa na uhakika kuwa bwana wake amekufa akiwa safarini na akaolewa na mwanamme mwingine baada ya kukamilisha Iddah ya kifo (mambo yanayoelezwa vyema katika maswala ya talaqa) na baadaye mume wake wa kwanza akatokezea kutoka safari, basi itambidi mwanamke huyo papo hapo ajitenganishe na bwana wake wa pili na huyo mwanamke atakuwa ni halali kwa bwana wake wa kwanza. Lakini iwapo bwana wake wa pili atakuwa amesuhubiana naye, basi itambidi atekeleze Iddah na bwana wake wa pili itambidi ampe mahari yake kamili kwa mujibu wa mwanamke wa kikundi hicho, lakini hastahiki kulipiwa gharama na bwana wake wa pili katika kipindi hicho cha Iddah.