read

17. Usamehevu

Kama iliyoelezwa hapo awali, hisia za mwanamke ndizo zinazotawala akili zao. Iwapo msichana hatakuwa amelelewa vyema kwa mujibu wa desturi na tamaduni za Kiislamu, basi kuna uwezekano mkubwa sana kuwa atakuwa ni msichana mwenye hasira na ulimi mkali.

Kwa upande mwingine mwanamme sio wa desturi hiyo, kwa hiyo Uislamu umemfaradhia mtu awe na subira na usamehevu wakati wa hasira za mke wake. Inambidi mwanamme amvumilie mke wake kwa kuweka maanani udhaifu wake na kwa kukumbuka kuwa mwanamke anatawaliwa na hisia zake.

Allah swt anatuambia katika Qurani tukufu sura An-Nisaa 4:19 "... na kaeni nao kwa wema..."

Hatuwezi kukanusha kuwa kazi hii ya kupewa ni ngumu sana na wakati mwingine inataka subira nyingi sana.

Allah swt anatuambia tena katika Qurani, sura Al-Baqarah 2: 201

"... Mola wetu! Tupe mema duniani na mema Aakhera,na utulinde na adhabu ya Moto."

Miongoni mwa ufafanuzi zaidi wa aya hii, Imam Amirul-Mu’miniin Ali ibn Abi Talib a.s. amesema:
"Mema katika dunia hii inamaanisha mwanamke mwenye silka nzuri na mema katika Aakhera inamaanisha hurul-ain na adhabu za moto inamaanisha mwanamke mwenye silka mbaya." (Tafsiri -Safi ).

Kusema kuwa mwanamke mwenye tabia, silka na desturi mbaya, mke mwenye hasira kali ni adhabu ya motoni. Lakini inatubidi sisi pia tuwe tukiitazama hii Hadith:-

"Kwa hakika Mtume Ibrahimu a.s. alimlalamikia Allah swt dhidi ya hasira za mke wake Sarah. Hapo Allah swt alimtumia ujumbe ukimwambia kuwa kwa hakika mfano wa mwanamke ni mfano wa ubavu; iwapo utajaribu kuunyoosha utavunjika; na lau iwapo utauachia ubavu wako ulivyo, basi utafaidika nao."

Kwa kifupi aya nyingi mno za Qurani tukufu na Hadith nyingi mno zinatuusia, zinatuamrisha kuwa muungano wa bibi na bwana uimarishwe na kufanywa madhubuti mapenzi yao na umoja wao kiasi wanapokuwa wameungana kindoa, hata kama itabidi mmoja ajinyime kiasi fulani na vile vile kujaza kwa subira inayozidi uwezo wa mtu mwenyewe.
Na kwa kufuata kwa kanuni kama hizi ndipo wanadamu wataweza kufaidi matunda ya amani humu humu duniani vile vile Aakhera.