read

20. Ufumbuzi Wa Masuala Mengi

1. Wanaume kuingiliana na malaya

Wanaume wengi mno wenye ndoa huwa na tabia ya kuingiliana pamoja na wanawake nje ya ndoa yao (malaya) ilhali wakijua kuwa kufanya hivyo ni kinyume na Shariah za Dini na ni ghunah-i-kabirah (dhambi kubwa mno). Pamoja na hayo kuna madhara mengi mno ya kimwili pia na hatimaye mtu kufikia hatua ya hatari kwa siha yake. Ni dhahiri kuwa raha na starehe za huyo malaya pia zinatolewa na mke wake na mke wa nyumbani huweza kutoa hata zaidi ya hayo.

Tumeona daima kuwa wanaume waendao na malaya huwa wana adhiriwa na kudhalilika katika jamii inayothamini ndoa halali na hatima yao huwa mbaya kwani huwa wamefilisika kimali na vile vile miili yao pia inakuwa imekwisha.Yaani kudhoofika na kupatwa kila aina ya magonjwa kama magonjwa ya ngozi, ukhanithi na siku hizi ugonjwa wa ukimwi, kwani malaya huwa hana bwana mmoja ila kila mwenye chochote ndiye bwana wake, ukitoka wewe ataingia mwingine kwani wao wanataka kila wakati wapate 'kipya' nao pia hawataki kula pilau kila siku kama wewe unavyodai.

Baada ya mwanamme huyo kujitumbukiza na kujiangamiza yeye mwenyewe katika magonjwa mabaya kabisa huwa ambukiza wake na watoto wake na hata familia yake nzima inaweza kuteketezwa kwa kutokana na maovu yake. Hivyo inampasa kila mwanamme amwangalie mwanamke malaya kama nyoka mwenye sumu kali na hivyo inambidi kujiepusha naye kabla hajapata sumu hiyo mwilini na maishani mwake.

Mara nyingi mno sababu za kumfanya bwana aende kwa malaya huwa ni wake zao nyumbani. Kwani kwa kutokana na magomvi au kutoelewana vyema baina ya bwana na bibi au kwa kutokuwa na programu nzuri ya maisha ya nyumbani.Vile vile imewahi kuonekana kuwa huwa mmoja wao hataki kusuhubiana wakati fulani ambapo mwenzake anataka kwa nguvu na katika hali kama hii ndipo inamfanya kufikiria njia ya kutaka kwenda nje kujiridhisha.

Hivyo inawabidi bibi na bwana kuwajibika vyema katika masuala haya. Na daima tukumbuke kuwa katika maisha yetu yote, mapenzi kati ya bibi na bwana ni nguzo mojawapo ya maisha yetu na iwapo itadhoofika nguzo hiyo, basi itaweza kuporomosha maisha yetu. Na swala la kusuhubiana ni nyeti mno katika maisha ya ndoa.

Tujaribu kuelewa falsafa ya 'kuridhika' na 'kutosheka' ndipo maisha yetu yatatengemaa. Iwapo katika tembeatembea yako umeona gari moja ambalo limekupendezea na ukawa unao uwezo wa kulinunua na ukalinunua hilo gari. Basi utajisikia una raha mno wakati ukiliendesha ambapo kabla yake ulikuwa unapata shida kubwa ya usafiri na huduma zinginezo. Lakini ikifika siku ukaanza kuidharau, basi utaanza kutukana badala ya kuisifu kama hapo awali na raha uliyokuwa ukipata sasa itakuwa imegeuka kuwa udhia na kuanza kula kichwa chako. Utaanza kutamani magari mazuri mno ya watu wengine wakati uwezo hauna.Sasa je! utakwenda kuiba ambapo unajua hatima yake ni kule kushikwa gari na wewe kwenda kizimbani--maisha yako kupotea na kuteseka?

Maisha yetu kuhusu kusuhubiana huwa ni sawa na kula, kunywa na kulala. Iwapo mtu atakuwa mroho katika kula na kunywa ambapo kamwe haridhiki,basi utaona anapenda kula kila mahala na kila wakati yaani anakuwa mroho asiyekinaika.

2. Kuhusu kusuhubiana mara ngapi

Wataalamu na madaktari wanasema iwapo mtu atataka kuitunza siha yake vyema na kujilinda kabisa,basi inambidi asuhubiane mara moja kwa mwaka, lakini kipindi hiki ni kirefu mno ambapo nadhani hakuna mtu afanyaye hivyo.

Hata hivyo kumwaga manii mara moja kila siku ingawaje haishauriwi, lakini inawezekana kwani manii huwa inakusanyika sehemu tatu. Kumwaga mara moja kunapunguza sehemu moja ya manii iliyokomaa ambapo kunakuwa bado sehemu mbili zinazoendelea kukomaa. Na kumwaga kwa mara ya pili kunatokwa na manii iliyo bado kukomaa na kumwaga kwa manii mara ya tatu kunatokwa na manii changa kabisa na kumwaga kwa mara ya nne ni kutoa damu tu. Hivyo kumwaga manii kwa zaidi ya mara moja kunamdhoofisha mwanamme na hatimaye kuwa khanithi.

Kuna watu wengi mno ambao siku hizi hawaoni raha ya kusuhubiana na wake zao hadi hapo watazame filamu za watu uchi wakifanya hayo.Watambue wazi wazi kuwa mwelekeo wao ni mbaya. Bwana anaanza kuwatamani wake wa nje na bibi kuwatamani wanaume wa nje na vile vile kuna hatari kubwa mno ya mwanamme kupoteza nguvu zake za kiume. Sasa raha za dakika chache tu zikikufikisha katika hatari hiyo, je! litakuwa ni jambo la busara? Hebu tukae na kutafakari swala hili vyema ili tusije tukajikuta tumeangamia kabisa.

Kama vile ilivyokwisha elezwa hapo awali,wazazi ambao wanapenda sana kusuhubiana, kizazi chao kitakuwa dhaifu na hivyo wazazi wanawajibika mno kuhakikisha kuwa vizazi vyao vinakuwa vyema na vyenye mustakbali mzuri.

3. Kumwaga manii kwa mikono

Ni ghunah-i-kabirah kuchezea sehemu ya uume wa mwanamme hadi kutokwa na manii kwa sababu tu siyo kuwa inadhoofisha mishipa yao bali inaleta madhara makubwa mno ambayo ni hatari zaidi kwa siha yao. Ikumbukwe vyema kuwa vijana wanamwaga na kuzitupa jawhari kutoka mwilini mwao. Na anapoingia katika tabia kama hii anakuwa ndiye muuaji wake mwenyewe bila hata ya yeye mwenyewe kutambua hivyo anajifurahisha kipuuzi kwa kupoteza uzima wa milele.

Tabia kama hiyo haina mipaka kwani kila wakati tu atakuwa akitamani kujitoa manii ambapo ni hatari kwa siha yake. Akifanya utafiti ataona kuwa anajitoa damu tu na je, kwa kujitoa damu si kutamponza tu? Sasa mwanamme mzima akiupoteza uume wake atakuwa na faida gani?

Kwa kutokwa na manii kupita kiasi kutampatia tabia ya kutokwa na manii haraka mno wakati wa kusuhubiana ambapo atakuwa daima hakutimiza hamu ya kusuhubiana. Si kwamba yeye tu atakuwa hana raha vile vile mke wake atakuwa na hamu isiyotoshelezwa, hivyo si kutamwelekeza mke wake kutafuta wanaume wengine? Je! mtu atapendelea hivyo?

Fikiria wewe ni mtu mmoja uliyesoma sana na unaoa mwanamke ambaye anafurahi mno kusikia sifa zako. Lakini mutakapoingia kitandani kusuhubiana anakukuta huna nguvu za kiume za kumridhisha. Je! mwanamke si atajiambia kuwa "afadhali ningeolewa na jahili ambaye anaweza kunitimizia haja yangu kuliko huyu aliyesoma ambaye hawezi kuniridhisha?" Maisha yamepotea bure!

Kuna baadhi ya vijana wanatokwa na manii katika ndoto, mkojo au katika hali ya ugonjwa au mshtuko na hali kama hii inatokea miongoni mwa vijana kwa sababu ya ugonjwa ambao unatokana na: (1) kujitoa manii (2) kujiweka pamoja na wanawake na (3) kuwa na mapenzi ya wanawake bila ya kuwapata.

Hivyo inawabidi vijana wote wajirekebishe na kuacha mbali tabia hizo mbaya ambazo zitawa angamiza na kuwapotezea nguvu zao za ujana wao.

Kile ukifanyacho sasa hivi bila ya kufikiria, ni hatari kwa maisha yako ya mbeleni, fikiria bado ni miaka mingapi utakayoishi. Hebu chukua mfano wa mtu amwambie kijana wa miaka 18 kuwa ang'oe meno yake yote. Sasa kijana huyo atafikiria iwapo atang'olewa meno yote umri huo basi ataufikiaje umri wa miaka 40 au 60 au zaidi bila ya meno?

Hivyo fikiria na uyajenge maisha yako kuanzia sasa kabla haujachelewa!

4. Ulawiti wa kila aina

Kwa mujibu wa Shariah za Kiislam, ulawiti na wanaumme kuingiliana wenyewe kwa wenyewe ni matendo ya Ghunah-i-Kabira na hivyo kaviwekea adhabu kali mno hapa duniani na Aakhera. Iwapo kutapatikana watu wakifanya hivyo,basi wote wachinjwe. Hapo Hakim-i-Sharah (Hakimu wa Kidini) anaweza kutoa amri ya kuchinjwa kwa panga, kufungwa mikono na miguu na hatimaye kutupwa kutoka juu au kuchomwa moto, kupigwa mawe hadi kufa au kuangushiwa ukuta. Vile vile anaweza kutoa adhabu zingine pamoja na kuchomwa moto.

Ulawiti baina ya mwanamke mmoja na mwanamke mwingine pia inachukuliwa na Shariah kuwa ni dhambi kubwa kabisa kama vile ilivyo ulawiti baina ya wanaume. Iwapo wanawake wenye kutenda hivyo ni wenye akili na fahamu timamu,basi wapigwe viboko mia moja kila mmoja. Adhabu hii imewekwa kwa ajili ya wanawake wote wale walioolewa na wasioolewa.

Iwapo mwanamke atapatikana na makosa kama haya kwa mara ya nne, basi atachinjwa. Na iwapo mwanamke atakapopatikana na kosa kama hili na akakiri na kutubu,basi Imam anaweza kumsamehe au kumpangia adhabu. Vile vile Naibu wa Imam anayo mamlaka kama haya. Lakini siku hizi hakuna ad­habu kama hizi.

5.Kutafuta mwenzako katika ndoa

Binadamu anafanya kila aina ya utafiti na jitihada ya kutafuta mwenzi wa kila mnyama anayemfuga kuwa watoto watakaozaliwa na hawa farasi, ng'ombe na mbwa wawe madhubuti na wenye siha nzuri lakini jambo la kushangaza ni kuona kuwa sisi tumejipuuza kutafuta mwenzetu katika swala hili !

Lakini leo tunatafuta bibi na bwana kwa kuzingatia urembo na utajiri, halafu hata kama mmoja wao atakuwa na tabia mbaya au magonjwa ya kuweza kurithiwa katika watoto.

Iwapo hawa watu wawili yaani mwanamme na mwanamke wanapotaka kuoana watakuwa ni watu wenye kasoro fulani za kitaalam ambazo zinajulikana basi hawashauriwi kuoana, huyu mwanamme asimuoe huyo mwanamke na huyo mwanamke asiolewe na huyo mwanamme. Hata hivyo watu wengi hawawezi kuelewa vile magonjwa ya kurithiwa yaliyomo miongoni mwao yaani mwanamme hawezi kuelewa mwanamke anayetaka kumuoa ana magonjwa gani ambayo yanaweza kurithiwa na watoto au mwanamke hawezi kuelewa mwanamme anayo magonjwa gani yanayoweza kurithiwa na watoto wao; basi watu wanaoana.

[Kutokana na maendeleo ya sayansi, iko uwezekano yakufanya utafiti na kuweza kujua kama mtu anabeba jeni (genes) ya magonjwa ya kuweza kurithiwa katika watoto na hivyo tunaweza kuepuka na hayo. Lakini lazima jamii ielimishwe kuhusu mambo haya na mengineyo yanayo elezwa katika makala hiyo].

Umuhimu juu ya mali, kabila na mambo mengine na mara nyingi ndoa kama hizi ndiyo sababu kubwa za kuzaliwa kwa watoto waliodhaifu kwa sababu katika kuchagua mpenzi, afya au siha iliachwa [haijapewa uzito]. Mwanamme aliye na siha nzuri anastahili kumuoa mwanamke aliye na siha nzuri, bila ya kujali kuwa huyo mwanamme ni tajiri au amesoma au hakusoma sana kwani jambo kubwa ni siha.

Ndoa ndiyo msingi wa furaha za maisha; ni jambo la kipumbavu kupanga ndoa baina ya watu wawili bila ya kutazama mambo ya mbele na nyuma. Inabidi wahusika wa sehemu zote mbili watilie maanani siha zao, tofauti kati ya umri na silka zao, kabla ya kukubaliana baina yao kwa sababu siha na silka au tabia zinazo-oana baina yao ndizo zinazofanya maisha yakawa yenye furaha na kama siha na silka zao zitatofautiana basi maisha yao yamepotea na kila mara watakuwa katika mizozo. Mambo mengi sana yapo ya kuzingatia kabla ya mtu hajakubaliana na mwenzake kuoana. Litakuwa ni jambo la kipumbavu kutafuta msichana mwenye umbo zuri, kiuno kidogo mwembamba kama sindano ati huyo ndiye anaonekana mzuri. Mara nyingi mwanamke kama huyo hawezi kuzaa watoto wenye afya nzuri.

Kwa kifupi mtu anapochagua mwenzake akiwa mwanamke au mwanamme asiangalie utajiri, urembo na ukabila ilimradi macho yake yanamdanganya, lakini inambidi amwangalie mwenzake ana siha gani. Na je! tabia na silka za huyu mwenzake ziko sawa na zimeoana kama tabia zake mwenyewe ili waweze kuelewana hapo mbeleni. Na iwapo ataoa mwanamke mrembo au tajiri lakini asiye na siha nzuri, basi hatakuwa na faida naye.

6. Uislamu haujakataza kupanga ndoa ya utotoni

Yaani watoto wanapokuwa wadogo katika mila nyingi wanapanga ndoa. Uislamu haujakataza lakini kuna mambo mengi ya kuzingatia yaliyo na faida na yenye hasara katika hali hii.Ndoa hizi za kupangwa za utotoni zimesababisha vijana hawa wawili wakose kuendelea na masomo yao na maendeleo mengi hawawezi kuyafikia kwa sababu wanaoana bado wakiwa wadogo.

Vile vile wanapokuwa wadogo wanaweza kuwa wanacheza pamoja, wanaweza kuwa marafiki sana kwa sababu wanakuwa na akili ya kitoto bado lakini vile wanavyoendelea kukua na baada ya kuwa wakubwa mara nyingi unaona wanatofautiana kwa mawazo na mmoja anakuwa na tabia tofauti na mwenzake na mara nyingine mmoja anaweza kumpenda mwenzake wakati mwingine anamchukia kwa sababu wakati huo wana akili timamu kwa hivyo kuna uwezekano wa hali hiyo kutoendelea vyema. Kwa hakika ndoa kama hizi zinaishia katika hali ya vurugu na mara nyingi kupeana talaqa.

Kuna hali nyingine za ndoa ambazo zinapangwa na wazazi au ndoa zingine zinapangwa na wataalam katika fani hii ya kuoza na katika sura hii mwanamke na mwanamme yaani bibi na bwana mara nyingi sana wanakuwa hawana raha ya maisha kwa sababu mwanamme na mwanamke wanatoka mahala tofauti na inawezekana mara nyingi hawajuani wanashtukia wameshapangiwa ndoa au bibi ameshatafutiwa bwana au bwana ameshatafutiwa bibi, ilhali anaona wakubwa wake wameshamtafutia anakubali!

Lakini mawazo na mapendo yao yanatofautiana, mwingine anakuwa na tabia tofauti na mwenzake kwa hiyo daima wanakuwa katika hali ya vurugu. Na katika maisha ambayo hayana raha, uelewano, mapenzi na uwiano baina ya bibi na bwana kuna sababisha watoto watakaozaliwa wasiwe watoto kamilifu kwa sababu watoto akiwa bado tumboni mama akili zake zinakuwa zimevurugika kwa sababu mama huwa hafikirii mambo mengi mazuri kila wakati utamuona mara ana hasira mara anafikiria matatizo anayoyapata; na hali hii inamuathiri mtoto na hata mtoto akishazaliwa hawezi kupata mapenzi ya baba na mama kwa sababu wote wawili wako katika hali ya mvurugano kwa hiyo hata watoto mawazo yao yanakuwa yameharibikiwa.

Ama wao wale wanao olewa wakiwa bado wadogo kabla ya kufikia ubaleghe hawawezi kuzaa ingawaje katika hali ya usichana, msichana wa miaka kumi na moja imerekodiwa kuzaa watoto. Hata hivyo kifuko cha msichana wa umri huo haijatangamaa kikamilifu kwa hivyo tusitegemee kuwa mfuko wa mama huyo ambao haujatengamaa sawa sawa ukaweza kuzaa mtoto na kumlisha mtoto kikamilifu. Kwa sababu mfuko wake bado unakasoro sio madhubuti kwa hivyo mtoto huyo hatapata mahitajio yake sawasawa yungali tumboni.

7. Hali ya kutooa kabisa

Kwa mwanadamu kimaumbile alivyoumbwa na Allah swt anategemewa aishi kama binadamu na hivyo mwanamme au mwanamke anapokataa kuoa au kuolewa kwa hakika hapo ni kinyume na kimaumbile aliyoumbiwa na Allah swt.Wataalam wamedadisi kuwa watu wanao oa au wanao olewa wanaishi maisha marefu zaidi kuliko wale ambao hawaoi wala kuolewa.Na wale wasiooa wana uwezekano wa kupata magonjwa mengi ya hatari kuliko wale wanaooa hivyo ni jambo la busara kuoa au kuolewa pale mtu anapoingia katika umri wake huo. Ni jambo la kudura za Allah swt kuwa mwanamme na mwanamke wanatamaniana.

Uwiano wa wanawake kwa waume imebadilika na takwimu ina onyesha wanawake ni wengi kwa hiyo mara nyingi hawaolewi sio kwamba hawataki, na ikiwa hivyo basi ni kumshukuru Mwenyezi mungu na kuomba dua. Hivyo watahifadhika kutoka magonjwa.

8.Dua za kuomba watoto

Zipo Dua nyingi mno kwa ajili ya mwanamke kushika mimba na hapa chini nitawaleteeni Dua chache ambazo zitakuwa zenye manufaa kwa wale bibi na bwana ambao kwa bahati mbaya hawakujaaliiwa watoto; ninatumaini kuwa kwa kusoma duaa na kwa kufuata miongozo michache ifuatayo Allah swt atawajaalia hiyo neema.

Mtume s.a.w.w. amesema: "Watoto ni sawa na maua ya peponi kwa hivyo uwema wa mtu ni kutokana na vile anavyozaa watoto."

Mtu ambaye hajabahatika kupata watoto, aende katika hali ya sijda na asome Dua ifuatayo:-Rabbi habli min ladunka dhurriyatan tayyibatan Innaka samiud-Dua', Rabbi la-tadharni fardan wa anta Khayrul Warithiin.

Na mtu ambaye anataka mke wake ashike mimba basi inambidi baada ya sala ya Ijumaa asali rakaa mbili na katika kila rakaa, rukuu na sijida arefushe na baada ya sala, asome Dua ifuatayo:-

Allahumma inni as-aluka bima sa-alaka bihi Zakariyya:Rabbi la tadharni fardan wa anta khayrul warithiin, habli minladunka dhurriyatan tayyibatan, Innaka akhadhtaha fa fadhayat fi rahimiha waladan, faj’alhu ghulaaman mubaarakan zakiyyan wala taj'al lishaytani fihi shirkan wala nasiban.

Mtu mmoja alimwijia Imam Muhammad Baqir a.s. na kumwambia:"Ewe mjukuu wa Mtume! Mimi sina watoto, "hapo Imam a.s. alimjibu kuwa: "Kila usiku au kila wakati wa mchana usome Istighfaar mara mia moja na Istighfaar ifuatayo ndiyo itakuwa vyema zaidi. 'Astaghfirullah rabbi wa-atubu ilaihi'.

Ili kutaka watoto kwa wale ambao hawajabahatika inawabidi daima asubuhi na jioni wafanye ifuatavyo: asome mara kumi,
Astaghfirullah rabbi wa-atubu ilaihi na baadaye asome mara tisa Subahanallah na baadaye asome mara moja Astaghfirullah rabbi wa-atubu ilaihi.

Mmoja wa wenye kuripoti anaelezea kuwa watu wengi wamefanya majaribio hayo na wameweza kuzaa watoto wengi.

Imam Ja’afer Sadiq a.s. amesema kuwa mtu yeyote mwenye kutaka watoto, kila anapoamka asome Istighfaar mara mia moja na lau atasahau hapo baadaye asome kwa nia ya Qadhaa.

Mtu mmoja alisema:"Ewe Imam mimi sina watoto." Imam a.s. alimwambia:"unapopanga kusuhubiana na mke wako soma duaa ifuatayo: Allahumma inruzaktana dhakaran sammaytuhu Muhammadan.

Mtu mmoja alimwijia Imam Ridha a.s na kumwambia: "Ewe mwana wa Mtume ! Mimi daima huwa niko mgonjwa na sina watoto." Hapo Imam a.s alimjibu: "Uwe ukisoma adhaan nyumbani kwako kwa sauti kubwa”. Yule mtu baada ya miaka kupita alimwijia Imam na kumwambia: "Mimi nilikuwa nikifanya hivyo na ninamshukuru Allah swt nimepona na nimekuwa mzima na sasa hivi nina watoto wengi."

Mtu mmoja alikuja kwa Imam Ja’afer Sadiq a.s. na kuleta malalamiko yake, "Ewe mwana wa Mtume ! Mimi sipati mtoto wa kiume." Hapo Imam a.s. alimjibu: "Popote pale unapokuwa umepanga kusuhubiana na mke wako (kumuingilia mke wako) basi usome Aya ifuatayo mara tatu na baada ya kusoma mara tatu ndio usuhubiane na mke wako. Allah swt atakujaalia watoto wa kiume.

Na Aya yenyewe ni hii ifuatayo:-Wadhan-nuuni Idh-dhahaba mughadhiban fadhanna an lan nakdira alayhi fanaada fidh-dhulumaati, 'an-Lailaha illa Anta Subhanaka inni kuntu minadh-dhalimiin, fastajabna lahu wa najjainaahu minal ghammi wa kadhalika nunjil mu'miniin, Zakariyya idh-naada Rabbahu Rabbi la tadharni fardan,wa anta Khayrul warithiin.

Katika Hadith inapatikana kuwa mtu yoyote ambaye hapati watoto inambidi afanye niyyah kama ifuatavyo:- "Iwapo mimi nitapata kijana wa kiume jina lake nitaliweka Ali" basi Allah swt atamjaalia mtoto wa kiume.

Imam Zeinul Abeidin a.s. amenakiliwa akisema mtu yeyote atakayesoma Dua ifuatayo atapata chochote kile atakacho lau atataka mali, au watoto na wema wa dini na dunia, basi Mwenyezi Mungu atamjalia vyote hivyo na Dua yenyewe ni kama ifuatavyo:-

Rabbi la tadharni fardan,wa anta Khayrul warithiin wajalni minladunka wayarithuni fi hayati wayastaghfiruli ba’ada mauti waj-alha khalqan sawiyyan wala taj-al lishaytani fiha nasiban. Allahumma Inni astaghfiruka wa atubu ilayka, Innaka antal ghafurur-Rahiim.

Na kwa hakika imependekezwa mno kusoma Dua hiyo mara sabini kwa ajili ya wale wanaotaka watoto.

Mtu mmoja alimwijia Imam Muhammad Baqir a.s. na alikuja akilalamika kuwa anao watoto wachache. Hapo Imam alimjibu: "Kila siku kwa muda wa siku tatu baada ya sala ya asubuhi na sala ya Isha usome subahanallah mara sabini na Astaghfirullah mara sabini. Na baadaye usome Dua inayofuata:- Astaghfiru Rabbakum Innahu kana Ghaffara, yursilussama' alaykum midraara,wa yumdidkum bi amwalin wa baniin wa yaj-alkum anhaara.

Baada ya kukamilisha utaratibu huo kwa muda wa siku tatu kwa usiku huo wa siku ya tatu ndio usuhubiane na mke wako na Allah swt atakujaalia watoto wema kwa ajili yako.

Mtu mmoja alikuja kwa Imam Ja’afer Sadiq a.s. na kumwambia: "Ewe mjukuu wa Mtume! Allah swt amenijaalia wasichana wanane lakini mpaka leo sijabahatika kuona sura ya mtoto wa kiume. Imam a.s. alimwambia: "Wakati wa kusuhubiana, ukae katikati ya miguu ya mke wako, wakati huo mkono wako wa kulia uwe upande wa kulia mwa kitovu chake na usome sura ya Inna-an- zalnahu ... mara saba na baada ya kusoma ndio usuhubiane na mke wako. Mtu huyo anasema kwa kufanya hivyo Allah swt alimjaalia watoto saba wa kiume”. [cha muhimu ni kwamba wakati unasoma sura katika hali iliyoelezwa usisahau ile heshima usomaji wa Qurani inayo stahiki].

Imam Hasan a.s. amesema: "Yeyote yule anayependa kuzaa watoto wa kiume basi inambidi afanye Istighfaar kwa wingi kabisa."

Hapo tumeona duaa za kupata watoto vile vile kuna mambo mengine yanayochangia katika sura hii.

Wakati mzazi anapopata mimba hali yake ya kiakili na siha yake ya kimwili inaathiri sana mwili na akili ya mtoto aliye tumboni.

Inamlazimu mwanamke akae mbali na bwana wake katika kipindi cha haidh. Mfano wa gogo liki­tupwa mtoni halirudi nyuma bali linaendelea mbele (yaani halirudi kule maji yanakotoka bali huenda kule maji yanakokwenda), vivyo hivyo iwapo manii zitaingizwa ndani ya mwanamke haitafika katika sehemu za kushika mimba hivyo hakutakuwa na maana ya kusuhubiana. Na lau kimaajabu mwanamke akitokea akashika mimba katika hali hiyo ya kusuhubiana wakati akiwa katika kipindi chake cha damu ya siku za mwezini, mtoto ataweza kufa azaliwapo. Iwapo mimba itashika siku ya pili mtoto atazaliwa akiwa na kasoro ya viungo na umri wake utakuwa mdogo sana. Na mimba itakayoshikwa baada ya kumalizika kwa damu hiyo mtoto atakuwa mzima mwenye siha nzuri na maisha mazuri.

Hivyo inashauriwa sana kwa wanawake kuweka akili zao safi na wayaondoshe mawazo yao mabaya na wasijiingize katika mambo machafu, vile vile inawabidi wavae mavazi mazuri, masafi yenye kupendeza, wajipake manukato mazuri waonekane nadhifu,wajiepushe na harufu mbaya na mawazo ya kutisha.

Mwanamke huyo asile vyakula vilivyoharibika au vilivyolala. Inambidi asitoke toke nje ila kikazi na aende katika mazingira ya kupendeza na kamwe asiende katika mazingira ambayo yanatisha yenye mashetani, majini n.k. na kamwe asipige makelele na mayowe na wala asijitaabishe kimwili pia, kwa muhtasari inambidi ajiepushe na kila aina ya tabia na hali ambayo itamuathiri vibaya mtoto tumboni.

Mwanamke mwenye mimba asilale juu ya vitanda virefu. Inambidi kitanda anacholalia kiwe na nafasi ya kutosha na ni lazima kuwa matandiko yawe mazuri na masafi. Na inambidi alale na mavazi mepesi, chakula chake kiwe cha kawaida na chenye afya yaani kiwe na mahitaji ya kutengeneza chakula cha mtoto tumboni.

Mwanamke mwenye mimba huwa na matamanio na yasipo timizwa yanamuathiri sana mtoto. Masikitiko,hasira, kutoridhika na mambo, yote kama haya yanamathiri akili na ubongo wa mtoto aliye tumboni.

Imeshauriwa sana kwa mwanamke kujiepusha na:-

1. Kupanda farasi au tembo

2. Kupanda miinuko mikubwa

3. Kufanya mazoezi magumu

4. Kwenda kwa mwendo wa haraka haraka au kuruka ruka

5. Magomvi ya kila aina

6. Kula vyakula vyenye harufu mbaya au kula vyakula vilivyo moto na kula vitu vichachu sana
na vile vile kula vyakula ambavyo ni vizito.

7. Kuchuchumaa na mambo kama hayo.

Inashauriwa ale matunda kwa wingi zaidi kiasi awezavyo.

Baada ya kushika mimba mwanamke anakuwa na hamu sana ya kula aina nyingi ya vyakula.
Wakati huo, inabidi kufanya subira hata kama uwezekano upo kwa kuwafikiria wengine wasio kuwa na uwezo. Kwa kiasi fulani apatiwe hizo chakula kwa kuwa inamsaidia kukaa katika hali ya furaha nayo ni hali inayomsaidia mtoto aliye tumboni.

Jambo hili linategemea uwezo wa mtu kifedha. Kama haiwezekani, inabidi mja mzito afanye subira na mwenyezi mungu atambariki mtoto mwema inshallah.

Wazazi tabia zao pia zina athiri sana akili na hali ya watoto. Iwapo wazazi watakuwa wakigombana wakati wa kushika mimba, basi kuna uwezekano wa mtoto atakayezaliwa atakuwa mgomvi. Walevi mara nyingi wanazaa watoto wenye kasoro na wasio na maendeleo. Inatokea pia kwa baadhi ya watoto wanaozaliwa wanakuwa wamepoa na wenye fikra kidogo za kinyuma nyuma wakati watoto wengine wanaoendelea kuzaliwa wanakuwa hodari na wenye siha nzuri.
Sababu zote hizo tunaweza kuzipata katika mazungumzo tuliyoyazungumza huko nyuma na mengineyo mengi. Kwa hivyo inatulazimu sisi tuende na wakati kwa sababu iwapo tutataka watoto wazaliwe wenye siha nzuri, wenye akili nzuri, wema wenye sifa nzuri basi itatubidi tujirekebishe katika kipindi hicho, tuwe tahadhari na hali ya baadaye.

9. Khatna yaani kumkalisha sunna mtoto

Imefaradhishwa katika Islam kukata sehemu ya ngozi ya mbele ya uume wa mtoto mwanamme. Kufanya hivyo kuna faida nyingi sana ambazo zinaelezwa hata na madaktari wa siku hizi. Daima kunakuwa na maji yenye kunatanata na yenye harufu mbaya mbele ya uume wa mwanamme. Lau itaachwa hali hiyo uchafu huo uendelee kuwepo hapo basi kuna hatari ya kutokezea vipele na kuzuka magonjwa mabaya yatakayo athiri uume wa mwanamme. Hivyo iwapo hiyo ngozi ya mbele itakatwa basi hakutabakia uchafu hapo mbele na hivyo sehemu ya uume wa mwanamme daima utakuwa msafi na utakuwa hauna hatari ya kupata madhara kama haya.

Mwanamme aliyetahiriwa yaani aliyekatwa ile ngozi ya mbele ya uume anatoa manii kwa nguvu zaidi kuliko ya yule mwanamme ambaye ngozi yake haijakatwa.Manii iliyomwagwa haibakii katika sehemu ya ngozi ya mwanamme sehemu ya mbele kwa wale waliokatwa ngozi na wale wasiokatwa ngozi uchafu huo unabaki pale pale na unaweza kuleta madhara makubwa zaidi. Wale wanaume ambao hawajakatwa ile ngozi ya mbele (kutahiriwa) hawawezi kusafisha ndani mwa sehemu hizo hivyo kuna hatari nyingi ya kufuga magon­jwa hapo na vile vile kuna uwezekano mkubwa sana wa kufuga magonjwa yanayotokana sehemu za siri za mwanamke na mwanamme.

Hivyo Shariah za Uislamu zina hekima , zina busara, na zimefanywa kwa ajili ya masilahi na ubora wa binadamu kwa yeyote yule atakaye kufuata atapata mafanikio na wala hakuna hasara au ubaya ndani yake.

10. Pombe

Katika Uislamu unywaji wa pombe na zinaa vyote hivi ni katika madhambi makubwa.

Unywaji pombe umezungumziwa sana katika Qurani na Hadithi na riwaya mbalimbali. Kabla ya kutaka kuzungumzia madhara na maovu ya pombe kwa mujibu wa dini ya Kiislamu tujaribu kuangalia sayansi na matibabu yanasemaje kuhusu haya.

Daktari mashuhuri Arnel-Wared anaandika katika mpangilio wa sayansi kuwa yeye alipokuwa akifanya kazi katika Hospitali mashuhuri ya Edinberg, hospitali yake ilikuwa ikiwanywesha pombe wagonjwa wenye magonjwa ya Pneumonia hivyo ilibidi watumie mabilioni ya mapaundi kwa ajili ya kuwanunulia wagonjwa pombe. Baada ya miaka michache kupita Profesa Sir Thomas wa Edinberg University alizuia matumizi ya pombe katika kutibu ugonjwa huo hivyo gharama ya matumizi ya pombe ilipungua sana ikabakia katika paundi chache tu.

Sababu kubwa yakukatiza utumiaji wa pombe katika kutibu ugonjwa wa pneumonia ni kwamba: "Pombe hiyo ilikuwa ikiwadhoofisha Phagocytes ambao wanasaidia sana katika kuua vijidudu vya Pneumonia. Kwa hakika hao phagocytes wanapokuwa dhaifu basi kuna uwezekano mdogo sana kwa mgonjwa kupona na hivyo hatima yake ni kifo. Baada ya uvumbuzi huo hospitali nyingi za Ulaya ziliacha kutumia pombe katika matibabu ya ugonjwa huo na badala yake maziwa yalianza kutumika. Hata hivyo hawakosi madaktari wengi mno ambao bado wamekalia desturi ya kizamani ya kushauri wagonjwa wenye Pneumonia kutumia pombe. Hata hivyo katika hospitali nzuri na zenye maendeleo mazuri zinakataa utumiaji wa pombe kwa sababu pombe zinaaminiwa na inasadikiwa kuwa ni adui wa mwanadamu hadi leo hii.

Profesa Machincalf wakati wa maonyesho ya siha huko London katika mwaka 1906 alisema kuwa phagocytes ni kitu kimoja bora katika damu yetu, lakini inapopata sumu juu yake basi inaharibika. Vile vile amethibitisha kuwa pombe inaiteketeza hiyo nguvu yake kama vile ‘opium’ inavyofanya.

Wakati mtu anapoumwa na ugonjwa wa ‘mbwa kichaa’ au anapopigwa sindano ya \kichaa cha mbwa’ basi huyo mtu ambaye si mlevi inamsaidia vyema kabisa kuliko yule ambaye ni mlevi na mara nyingi haiwasaidii. Utumiaji hata kiasi kidogo cha pombe kinawateketeza phagocytes.
Na hii ni sawa sawa na kuteketeza uwezo wa mwili wetu sisi wenyewe.
Baada ya uvumbuzi huo madaktari waliokuwa wakiamini kuwa pombe inasaidia katika kuivisha chakula mwilini wameondoa mawazo hayo ya kuwa pombe ni yenye faida badala yake wameamini kuwa pombe inaleta madhara zaidi mwilini .

Pombe inaathiri vibaya sana hali ya uzalishaji wa kemikali katika tumbo. Kemikali hizi zinafanya kazi kubwa sana ya kutengeneza chakula chetu kuingia katika damu yetu. Hivyo kwa kunywa pombe kunaharibu nguvu za kemikali na hivyo kutukosesha sisi faida yote kutokana na vyakula vyote tunavyopata.

Athari za pombe kwa mama wanaonyonyesha maziwa

Miaka ya nyuma madaktari walikuwa wakiwashauri wanawake wanao nyonyesha maziwa watoto watumie pombe ili kuongeza maziwa katika matiti yao. Hata hivyo, wamebadilisha mawazo yao na maoni yao. Ni kweli kuwa pombe inaongeza kiasi cha maziwa katika matiti ya mama, lakini sio sababu nyingine isipokuwa ni sababu ya utumiaji wa maji, ambayo ndiyo inaongezea kiasi cha maziwa katika matiti ya mama. Kwa hivyo kuna vinywaji vingi sana vyenye afya na vyenye siha nzuri ambavyo vinaweza kutumika na vyenye manufaa zaidi kuliko pombe. Je! kwa nini tuanze kumnywesha mtoto pombe yungali mchanga kwa kupitia katika maziwa ya mama?

Pombe inakausha maji maji mwilini. Na hii ndiyo maana tunawaona wanywaji wa pombe kuwa wanahitaji kunywa maji mengi sana na wanakuwa na kiu kingi kuliko mtu wa hali ya kawaida. Sababu nyingine ya kiu kikubwa kama hicho ni kwamba pombe inaathiri vibaya sana kemikali zinazotengenezwa na tumbo kwa ajili ya kuivisha chakula na kufanya chakula kisiweze kuiva vizuri; chakula kinageuka kuwa sumu kwa mnywaji wa pombe. Na sababu hii ni mojawapo ya kusababisha sumu hii kuingia katika damu kumfanya awe na kiu hasa ya vinywaji baridi. Na vile vile tumeona kuwa mtu mwenye homa huwa ana kiu sana kwa sababu ya sumu hiyo inayoingia katika damu yake. Hata hivyo ukinywa maji hiyo sumu iliyoko ndani ya damu ya mtu mwenye homa inapungua hivyo kila sumu inavyozidi kupungua katika damu ndivyo homa inavyoendelea kupungua.

Mlevi wa pombe huwa anawashwa sana tumboni na ndio maana watu wengi utawaona wanakunywa pombe kwa kuiongezea maji na hii inakuwa na athari kidogo kuliko mtu anayekunywa pombe kavu kavu. Hata hivyo nawashauri hao watu waache kunywa pombe na wanywe maji tupu kwa sababu maji yanafaida sana kuliko pombe yao hiyo.

Sasa nitaomba tuangalie kidogo vipi Dini yetu inatuambia nini kuhusu unywaji wa pombe. Sisi tumebahatika mno kuwa wafuasi wa Dini ambayo imetuangalizia mambo mengi yenye faida na manufaa kwetu ambayo yote yanatuletea maendeleo katika maisha yetu.Vivyo hivyo Dini yetu hii imetuambia mambo mengi yaliyo mabaya na maovu na yenye hatari kwa ajili ya maisha yetu. Wataalamu katika fani ya madawa katika miaka ya nyuma walikuwa wakiwacheka Waislamu kuwa Dini yao imewanyima vitu vyenye faida kubwa kama vile pombe. Lakini baada ya utafiti kuendelea zaidi leo wanakubali kuwa Mtume Muhammad s.a.w.w. kwa hakika ametumia hekima na busara sana kwa kuwaharamishia Waislamu pombe kitu ambacho ni chenye madhara makubwa sana.

Mtume s.a.w.w. amesema kuwa: "Watu wa vikundi vitatu hawataingia kamwe peponi , nao ni:-

1. Wale wanaokunywa pombe daima

2. Wale wanaotumia uchawi

3. Wale ambao wanavunja uhusiano na majamaa zao

Mtu yeyote anayetumia pombe atapewa kinywaji kutoka mto unaoitwa Guta. Kinywaji hiki kitakuwa kina uchafu na usaha kutoka kwa malaya na kitakuwa kikitoa harufu mbaya sana na kwa hakika kitakuwa kiki­wauma sana wale wote watakaokuwa wakiishi Jahannam.

Mtume s.a.w.w. amesema kuwa: "Mtu yeyote atakayekuwa akiwauzia pombe Mayahudi, Wakristo, au makafiri basi huyo mtu atakuwa anapata madhambi sawa na yeye mwenye kuinywa pombe hiyo”. Kwa hiyo mtu asiseme kuwa ninawauzia pombe makafiri hivyo mimi sina madhambi, pombe ni kitu kibaya kwa binadamu wa kila aina awe Mwislamu, awe kafiri; kwa hivyo atakayewauzia pombe hata makafiri atapata madhambi sawa sawa na mtu anayekunywa pombe yenyewe.Vile vile Mtume s.a.w.w. amesema kuwa: "Watu wasiende kumwangalia na kumjua hali mgonjwa ambaye ni mlevi na wala wasiungane katika mazishi ya mlevi huyo”.Vile vile ameendelea kusema “ushahidi wa mlevi usikubaliwe na wala msiwaoze watoto wenu kwa walevi”. Ameendelea kusema Mtume s.a.w.w. kuwa: "Chochote kile kisikubalike kutoka kwa mlevi."

Imam Ja’afer Sadiq a.s. amesema: "Mlevi siku ya Qiyama uso wake utakuwa umegeuka kuwa mweusi na ulimi wake utakuwa umevutwa ukining'nia mpaka mate yatakuwa yakimdondokea kifuani mwake.” Mlevi huyo atakuwa akipatiwa maji au kinywaji kutoka kisima ambacho kitakuwa kimejaa usaha wa miili ya watendao maasi yaani malaya. Allah swt, Malaika, Mitume na waumini wote kwa pamoja wanawalaani walevi. Wakati mtu anapokuwa amelewa imani yake inamtoka na nafasi hiyo inachukuliwa na mashetani.

Imam Muhammad Baqir a.s. amesema: "Mtu yeyote anapolewa ibada zake za siku arobaini hazikubaliki. Na lau hatasali basi atapata adhabu mara mbili."

Imam Ja’afer Sadiq a.s. amesema kuwa: "Mlevi sala zake za siku arobaini hazikubaliwi na iwapo atakufa katika kipindi hicho basi ataingizwa katika Jahannam moja kwa moja."

Abu Salehe alimuuliza Imam Ja’afer Sadiq a.s. iwapo kuna ubaya wowote katika kumnywisha mtoto mchanga azaliwapo pombe kwa sababu ilikuwa katika desturi na mila zao. Basi Imam a.s. alimjibu: "Allah swt atawanywesha maji moto sana yakutokota wale wote watakaowanywesha watoto wa­changa pombe".

Imam Ja’afer Sadiq a.s. amesema: "Mtu yeyote atakayemuoza binti yake kwa mlevi, basi huyo mtu amejibu­ruta katika Jahannam.” Vile vile amesema mtu yeyote asimuoze binti wake kwa mlevi na wala asimkubali binti wa mlevi kwa harusi na wala mtu yeyote asiende kumwangalia mlevi anapougua. Mlevi siku ya Qiyama uso wake utaonekana mweusi, macho yake yakiwa majivu, uso wake ukiwa hauna sura nzuri ukiwa umeoza na ulimi ukiwa umening'inia chini. Amesema ni dhambi kabisa kunywa pombe. Mtu anapokunywa pombe anaacha sala, hamtambui mama, dada au binti yake na daima huwa amepoteza fahamu zake.

Ameendelea kusema iko nyumba ya maasi na nyumba hiyo ina mlango uliotiwa kufuli na ufunguo wa nyumba hiyo ni pombe. Kwa hiyo inamaanisha kuwa pombe ni mama wa maovu yote. Mtu yeyote anayekunywa pombe ni sawa na mtu anaye abudu miungu. Kwa sababu katika hali hiyo hakubali Qurani kuwa ni kitabu kilicho kweli kwani lau akikubali kuwa ni Kitabu kilicho kweli na sahihi basi asingekunywa pombe kitu ambacho kimeharamishwa katika Qurani tukufu.

Ameendelea kusema Imam a s. kuwa: "Mtu yeyote atakayempa mlevi punje ya chakula au hata tone la maji, basi Allah swt atamuwekea kaburini nge mkubwa sana mwenye meno ambayo yatakuwa marefu kiasi cha mikono mia moja na kumi na atakuwa akipatiwa maji kutoka Jahannam.” Kutimiza mahitajio ya mlevi ni sawa na kuwaua waumini elfu moja na kuibomoa Al-Kaaba kwa mara elfu moja. Malaika elfu sabini wanamlaani yule mtu anayemsalimia au anayemheshimu mlevi. Jibrail, Mikail, Israfil,Mitume na Maimamu wote wanawalaani wale watu wote ambao wanachukua pombe hata tone moja.

Siku ya Qiyama atatokezea nge mkubwa mno katika uwanja na atasema: "Wako wapi wale watu ambao walikuwa wakipigana na Allah swt na Mtume wake?" Jibrail atamuuliza ni akina nani alikuwa akiwatafuta. Nge huyo atasema: "Yeye alikuwa akiwatafuta watu wa aina tano."

1. Wale ambao wameacha sala

2. Wale walioacha kulipa zaka

3. Wale wanaopokea riba

4. Wale walio na tabia ya kunywa pombe

5. Wale ambao wamezoea kuzungumzia mazungumzo ya dunia wakiwa misikitini.

Mtu mmoja alimwuliza Imam Ja’afer Sadiq a.s. kuhusu kuwapo kwa pombe juu ya meza ya chakula. Imam alimjibu: "Ni haramu kula chakula juu ya meza hiyo." Vile vile Imam a.s. amesema: "Watu wasiwe wakikaa na walevi kwa sababu walevi daima huwa wanalaaniwa na wale wanaokaa nao pia wata athirika kwa laana hizo."

Imam Mohammad Baqir a.s. amesema kuwa Allah swt anawalaani watu wa aina kumi wanao shirikiana ka­tika utengenezwaji wa pombe nao ni:-

1. Wale wanaopanda mbegu ya miti ambayo mazao yake yanatumika katika kutengenezea pombe

2. Wale ambao wanaangalia na kuitunza miti hiyo

3. Wale wanaotengeneza juisi yake

4. Wale wanaohudumia, wanaotawanya wanaogawa pombe

5. Wale wanakunywa hiyo pombe

6. Wale wanaopakia au kusafirisha hiyo pombe

7. Wale wanaochukua hiyo pombe

8. Wale wanaouza hiyo pombe

9. Wale wanaonunua hiyo pombe

10. Wale wanaolipia hiyo pombe

Allah swt anazuia matendo mema yaliyofanywa na mtu katika kipindi cha miaka arobaini ya mtu ambaye anawasalimia au anawatolea heshima au anayepeana mikono na walevi. Ameendelea kusema: "Kumsaidia mlevi ni sawa sawa ni kuwasaidia wale ambao wanataka kuuvunja na kuuharibu Uislamu," na vile vile amesema: "Kumpatia mkopo mlevi ni sawa sawa na kumuua Mumiin."

Hivyo msomaji tumejaribu kuangalia kwa muhtasari tu kuhusu maovu na hatari na vile Uislamu unavyosema kuzungumzia pombe kwa kuwa kitabu hiki kidogo kinazungumzia mambo mengine kuhusu mambo ya ndoa n.k. hivyo hatuna muda wa kuzungumzia mambo juu ya pombe, hata hivyo maudhui haya yamezungumziwa na watu wengi Mashekh na madaktari kwa mapana zaidi na vile vile ukiweza kubahatika unaweza kutuandikia kwa anwani yetu juu ya kitabu kinachozungumzia mambo mawili ambayo yameungan­ishwa katika Qurani: pombe na kamari maovu haya mawili katika jamii yetu ni maovu sana na mimi nimetunga kitabu kimoja juu ya mada ya ‘kamari’ peke yake na kipo kitabu kingine kinazungumzia juu ya habari ya pombe na anwani yangu ipo hapo nyuma katika ukurasa wa maneno machache. Lau utapenda kupata kitabu hicho usisite kutuandikia tutajitahidi kukutumia.

11. Zinaa

Kama vile Uislamu unavyolaani pombe vile vile inalaani vikali sana zinaa, kwa uchache ninawaletea mazungumzo na Hadithi juu ya suala hili.

Allah swt ametuamrisha katika Qurani kuwa siku ya Qiyama mwenye kutenda zinaa ataadhibiwa mara dufu na daima atakaa katika moto wa Jahannam.

Imeelezwa katika kitabu Tafsir-i-Safi kuwa miongoni mwa chemichemi za Jahannam moja inaitwa Asam ambamo badala ya maji inatiririka shaba iliyoyeyushwa. Maumivu yanayosikika na ya chemichemi hizi inazidi hata adhabu za akhera na adhabu za Jahannam. Wale watakaotupwa katika chemichemi hii inayotokota ni wale ambao wanamwabudu mtu mwingine mbali na Allah swt, na wale ambao wamewaua wale watu ambao wameharamishwa kuuawa na wale watu watendao zinaa.

Imam Ja’afer Sadiq a.s. amesema: "Allah swt ameweka adhabu sita kwa wale watendao zinaa ambapo adhabu za aina tatu wanazipata humu humu duniani na zinazobakia hizo tatu wanazipata huko Akhera.”

Adhabu hizo zilizowekewa humu duniani ni:-

1. Wanapoteza nuru

2. Wanakuwa maskini

3. Maisha yao yanakuwa mafupi.

Adhabu tatu zilizowekewa Akhera ni:-

1. Allah swt atakuwa amewakasirikia mno

2. Watahesabiwa siku ya Qiyama kwa Shariah kali

3. Wataishi milele Jahannam

Mtume Mtukufu s.a.w.w. amesema: "Manukato ya Jannat yataweza kusikika hadi umbali wa miaka. Hata hivyo yule mtoto ambaye amekanushwa na wazazi yaani wazazi wamesema sio mtoto wao tena, na mtu yule ambaye haonyeshi huruma kwa jamaa zake na yule mtu mzee anafanya zinaa, hao ndio watu hawataweza kusikia manukato ya Jannat."

Kuna Hadithi isemayo kuwa mwenye kufanya zinaa na mwenye kufanya Ulawiti watakuwa wakinuka kama nyama ya mizoga siku ya Qiyama hadi watakapoingizwa Jahannam. Na kwa kweli watu wataudhika na kud­hurika kwa harufu zao hizo mbaya. Na wala hakuna matendo yao mema yeyote yatakayokubalika na kwamba matendo yao yote hayo yatakuwa yametupiliwa mbali. Watapigiliwa misumari katika masanduku ya maiti. Watakuwa wamepewa adhabu kubwa kweli kweli kiasi kwamba iwapo mishipa yao watafungwa watu laki nne wote watakufa kwa kuathirika na adhabu watakuwa wakipata watu kama hao. Na watu kama hao ndio watakaopata adhabu kubwa kabisa katika wakazi wa Jahannam.

Mtu yeyote iwapo ni mtumwa au mtu mwingine yeyote afanyapo zinaa na Mwislamu, Myahudi, Mkristo, au mwanamke mwingine, Allah swt atamfungulia milango laki tano katika kaburi ambamo wataingia nyoka, nge na miale ya mioto ambavyo vyote hivyo vitakuwa vikimuadhibu na kumteketeza humo hadi siku ya Qiyama wakati watu wote watakapokuwa wamekusanyika siku ya Qiyama, watu kama hawa watakuwa wakitoa harufu mbaya katika sehemu zao za siri, kiasi kwamba watu wengine wote watakuwa wakiona udhia, na harufu hii itaendelea kutoka hadi watakapoingizwa Jahannam.

12. Magonjwa

Wanawake: Leucorrhoea

Kuna wakati wanawake wanatokwa na maji meupe au ya rangi ya njano yaani maji maji hayo ni kama usaha kutoka sehemu zao za siri na maji haya yanakuwa yenye kuondoa raha mwilini nayo yanaitwa Leucorrhoea.
Wanawake walio na ugonjwa kama huo wanaweza kuingizwa katika makundi manne yaani:-

1. Wasichana wadogo

2. Mabinti waliokua

3. Wanawake walioolewa

4. Wanawake wenye umri mkubwa

1. Wasichana wadogo

Wasichana hawa wanaanza kutokwa na maji kama hayo kwa sababu ya uvimbe unaotokea katika sehemu zao za siri. Inaweza kuonekana iwapo msichana atalala kwa wima na ukiangalia sehemu yake ya siri utaona imevimba imekuwa rangi nyekundu na imejawa na usaha na maji maji kama haya na sababu kuu zinazofanya hali hii kutokea ni kama zifuatazo:-

(i) Kuna jarasimu za aina nyingi sana juu ya ardhi ambapo uchafu umechanganyikana hivyo jarasimu hizo zimeingia katika sehemu za siri za watoto kwa sababu wanapokuwa wakicheza kwenye udongo nje na wanakuwa hawakuvaa chupi na matokeo yake ni uvimbe wa aina hiyo. Na lau hali hii haitapewa umuhimu wa kutibiwa basi utaishia katika ugonjwa Leucorrhoea.

(ii) Kuna vijidudu vya aina fulani ambavyo vinaishi katika majumba ambayo haina upepo wa kutosha. Na minyoo hiyo inawauma watu wanapokuwa wamelala hivyo minyoo hiyo inapouma sehemu za siri za msichana pia inaweza kusababisha ugonjwa huo.

(iii) Majeraha yanayopatikana kwa sababu ya ajali katika sehemu ya siri ya mwanamke pia inasababisha ugonjwa kama huo.

(iv) Hali ya baridi pia inachangia katika ugonjwa huu.

Katika kutibu sehemu hizi inabidi zioshwe vyema kabisa na kusafishwa na pamba au kitambaa safi kilichochovya katika maji ambamo borax imechanganywa. Borax ni aina ya dawa inayotumika katika matibabu kama haya na lau hakutaonekana dalili ya kupona ugonjwa huo basi inashauriwa kumuona daktari haraka sana iwezekanavyo.

2. Wasichana wa makamu

Sehemu za siri za wasichana wasioolewa pia huwa inavimba na kutoa maji maji kama hayo wao pia hupata maumivu madogo madogo katika sehemu ya chini ya tumbo lao na huongezeka pale wanapokaribia vipindi vyao vya damu ya mwezi ( haidh ). Kwa sababu moja kubwa ya ugonjwa huo katika kikundi hiki kuwa matamanio yao yanakuwa hayakutimizwa.

Katika hali ya wasichana kama hawa hakuna matibabu yake. Hata hivyo wanatakiwa wapewe mapumziko, vyakula vizuri na vile vile wawe wakilala kwa kiasi wakiwezacho. Jambo tunaloshauri suluhisho kama hili ni kuwa msichana wa hali kama hii waozwe haraka iwezekanavyo.

3. Wanawake walioolewa

Wanawake walioolewa wanapopata maumivu wakati wa kusuhubiana basi wajue kuwa ni onyo kuwa watapata ugonjwa huu. Hivyo waume zao inawabidi wawe wavumilivu na wenye subira kwa sababu kusuhubiana kupita kiasi kutaleta ugonjwa huu wa Leucorrhoea.

Wakati mwanamke anapozaa, mdomo wa mfuko chake unapanuka na moja ya sababu ya ugonjwa huo ni hiyo na lau mwanamke huyo atatibiwa vyema basi ataweza kuepukana na ugonjwa huo lakini kama hakupata mati­babu sahihi basi ugonjwa huu unaweza kutokezea.

Mwanamke kutopata haidh, kusuhubiana wakati huo na kushindiliana zaidi kunasababisha ngozi za sehemu za ndani ya sehemu za siri ya mwanamke kuvimba na hii pia ni sababu mojawapo.

4. Wanawake wenye umri mkubwa

Si kwamba wasichana wadogo na wanawake ndio wanaopata ugonjwa huu bali hata wanawake wa makamu wanaathirika na ugonjwa huu. Kutokujali vyema katika umri wa vijana, ugonjwa wa kisukari na mabadiliko katika umri wa mwanamke huyo inachangia katika ugonjwa huu kwa wanawake wa makamu.

Matibabu

Ugonjwa huu ni kwa sababu ya uvimbe unaotokana katika sehemu za siri ya mwanamke ndani mwake na sababu kubwa inatokana na damu yake kuwa chafu, kutoiva chakula vizuri tumboni, yabisi, n.k.Hivyo sababu hizi ziondolewe wakati huo huo kunapofanywa matibabu yaani dawa zake.

Inaonekana kuwa mwanamke anapata raha kidogo wakati anapochukua pamba iliyorowanishwa katika maji yenye kemikali ya borax na kuweka katika sehemu za siri za mwanamke kwa muda wa masaa ishirini na manne hadi arobaini na nane kwa hivyo iwapo hili halitamsaidia basi aonane na madaktari au awaulize wazee wanaoweza kumsaidia kwa madawa ya kienyeji ili akapona na aweze kujisikia raha starehe.

Wanaume: Spermatorrhoea

Imeonekana kuwa vijana wengi wana matatizo wa ugonjwa huo wa spermatorrhoea. Kuna malalamiko ya aina mbili katika kupungua nguvu kwa kiume katika kusuhubiana, nazo ni:-

1. Manii inamwagika wakati mtu akiwa usingizini au katika mkojo

2. Mwanamme, ingawaje anakuwa na hamu ya kusuhubiana na mwanamke hawezi kuusimamisha uume wake au anapousimamisha, hatokwi na manii. Hivyo katika kufanya matibabu ya magonjwa kama haya inabidi mtu afanye dawa ambayo itamsaidia. Hata hivyo kabla ya kufanya matibabu hayo inabidi mtu mwenye magonjwa ya yabisi n.k. ayatatue kwanza. Itambidi mtu aangalie hali ya hewa ya wakati na hali ya mwili wake na mazingira kabla ya kuingilia matibabu ya matatizo yake hayo.