read

2.Utangulizi

Zipo riwaya nyingi mno ambazo zimenakiliwa kutoka Mtume s.a.w.w. na Maimamu a.s. ambazo zinasema kuwa:

‘mwenye kuoa’ atakuwa amejidhibiti vyema katika Islam na amejilinda nusu ya Imani yake na nusu ya sehemu nyingine ya imani, inambidi afanye jitihada ili aweze kuiimarisha.

Na rakaa mbili za mwenye kuoa ni afadhali kuliko rakaa' sabini za mtu asiyeoa. Aliyeoa ni mpenzi wa Allah swt.

Mtume s.a.w.w. amesema kuwa mtu asifanye uchelewesho katika kuoa kwani watoto watakaozaliwa (baada ya ndoa) kama watakuwa wakimtii na kumtukuza Allah swt, basi ujira wake utakuwa wanapatiwa wazazi wao na mema yao pia yatakuwa yakilipwa wazazi wao.Vile vile amesema kuwa tuuendeleze Ummah wake ili aweze kuwa na fak­hari Siku ya Qiyama. Na iwapo mwanamke mimba yake itaanguka basi Siku ya Qiyama mtoto wake huyo atakataa kuingia Jannah (Peponi) hadi hapo wazazi wake waingizwe nae pamoja”.
Limetolewa onyo kuwa "kufa bila ya kuoa ni vibaya mno."

Imam Ja’fer Sadiq a.s. amenakiliwa akisema kuwa "iwapo nitakuwa na dunia pamoja na vitu vyake vyote vikawa vyangu, bali na kupitisha usiku mmoja bila mwanamke,basi mimi siridhii hayo yote.Ni afadhali ku­kosa vyote hivyo kuliko kukosa mwanamke. Vile vile sala ya aliyeoa ni afadhali kuliko sala za kila siku pamoja na saumu za asiyeoa."

Vile vile kuna riwaya isemayo kuwa mtu atakapo kujitakasa mbele ya Allah swt, basi inambidi afanye harusi na kuoa hata akiwa katika hali ya umasikini na ufukara, hii itakuwa ni kuthibitisha imani na uaminifu juu ya Allah swt; kwani Allah swt amesema "Oeni hata katika hali ya umasikini na ufukara kwani nitawaghaniisha." (nitawatajirisheni)

Ipo katika riwaya kuwa ‘muoe wake wazuri’ na mtu atakayeoa mwanamke kwa sababu ya tamaa ya mali au uzuri, basi atakosa vyote. Na atakayeoa kwa kuangalia dini na imani ya mwanamke, basi atapata vyote, yaani mali na uzuri.

Sifa za mwanamke mzuri ni kuwa yeye ni bora kuliko dhahabu na fedha na mwanamke mwovu ni mbaya sana kwani hata mchanga ni afadhali kuliko yeye. Mwanamke mwenye gharama ndogo, mahari ndogo na vilevile akizaa watoto kwa ura­hisi, huyu basi ni mwanamke mwema; na mwanamke mwenye gharama kubwa na mwenye kuzaa watoto kwa mushkeli na mwenye mahari kubwa, basi mwanamke kama huyo si mwema.

Ni Sunnah kusoma nikah wakati wa usiku, kwani Allah swt ameufanya usiku kuwa mapumziko na starehe na inapoangukia Qamar dar Aqrab (mwezi iwapo katika Nge) basi msifanya nikah na kunapokuwa joto ka­li, iwapo kutakuwapo na ndoa, basi kuna uwezekano wa kuachana.Vile vile kusifanywe ndoa usiku wa baada ya siku ya jumanne ( yaani kuamkia jumatano), kwani siku hiyo ni mbaya mno. Iwapo hiyo (usiku wa baada ya siku ya jumanne) itakuwa ni siku ya kuzaliwa kwa Ma'sum a.s. basi hakuna shida yoyote. Haifai kuoa katika tarehe 26, 28 na 30 za kila mwezi.

Kuoa si faradhi lakini iwapo kuna hatari ya kutumbukia katika maasi, basi itakuwa ni faradhi kuoa na kwa mjane kuolewa si vibaya, kwani kubakia pekee mara nyingi inakuwa mushkeli kimaisha na hivyo haitakiwi kujitumbukiza katika magumu ya maisha ambapo tunaweza kujiepusha. Kwa hakika ni jambo la kusikitisha kuona katika jamii yetu wajane wakitupwa bila kuwajali na kudharauliwa kama ni wenye nuksi ambapo inatubidi sisi kuwajali, kuwatunza na kuwaoza inapowezekana ili wao nao waweze kuishi maisha kama wengineo wote.

Ipo Hadithi inayosisitiza mno kabisa kumfanyia na kumgharamia mtu harusi na nikah kwani inayo thawabu adhimu. Kila neno litakalosemwa, kila tendo litakalotendwa na kila hatua itakayochukuliwa, Allah swt atampa thawabu za sala za usiku na saumu za mwaka mzima. Na huko Jannat atampatia Hur al-Ain elfu moja wakiwa na majumba yaliyorembeshwa kwa Yaquti na vito vya thamani.

Ipo riwaya inayosema kuwa atakayemwozesha mjane, basi Siku ya Qiyama atakuwa miongoni mwa wale waliorehemiwa na Allah swt.

Atakaye suluhisha baina ya bibi na bwana,basi Allah swt atamjaalia thawabu za mashahidi elfu na hatua zo­zote zile atakazozichukua katika kufanyisha sulhu na matamshi yote yatakayotoka atapatiwa thawabu za ibada za mwaka mzima.