read

3. Ndoa Na Maisha Ya Starehe

1) Mafunzo ya awali

Iwapo mimi nikitaka niwe daktari au niwe mhandisi basi itanilazimu kwa mfululizo kwa kiasi cha miaka miwili, au mitatu au mitano, kumi au kumi na tano nisome kwa kupitia vyuo mbalimbali, kufuatia mazoea tofauti tofauti hadi niweze kuwa daktari au mhandisi ambapo nitaweza kukabili hali ya kazi zangu bila matatizo na vile vile iwapo nitapata matatizo nitakuwa ninajua njia za kuweza kuyarekebisha, kusahihisha na kuleta maendeleo mazuri katika fani yangu.

Lakini katika zama hizi ni jambo la kusikitisha mno kuona kuwa wanaume wanataka kufuzu na kupata stashahada ya kuwa yeye ni mume bila ya kupitia mafunzo na kujitayarisha vyema kwa ajili ya mustakabali huo mpya. Kwa hakika mwanamme au mwanamke akitaka kuwa mume na mwanamke akitaka kuwa bibi inawalazimu wajifunze mambo mengi na namna ya kukabili mustakabali huo mpya; hivyo inawabidi wapitie mawaidha, nasiha na mazungumzo ya wazee na kujionea maisha yalivyo na wakati waliopo. Lakini tunaona wengine wanaoa kimchezo na baadaye maisha yanakuwa magumu huko mbeleni na hatimaye ndoa zao kuvunjika na hivyo maisha ya pande zote mbili kuharibika, kujaa kwa chuki na kukosa raha kabisa. Hivyo katika taarifa zinazofuata nitajaribu kuzungumzia namna ya kutengeneza ndoa yetu ikawa raha na mustarehe.

2) Ndoa ni kazi ya kikundi

Ndoa ni sawa na farasi wawili wakivuta kigari. Kama ukiwaona farasi wawili wamefungwa kigari nyuma yao, utaelewa zaidi vile wanavyotembea kwa sababu farasi wote wawili itawabidi wainue miguu yao kwa mpangilio na wote itawabidi waelekee upande mmoja; huwezi kuona farasi mmoja akielekea kushoto na mwingine kulia; gari hilo haliwezi kwenda, farasi wote wawili watabaki hapo na kigari kitabaki hapo hapo.
Hivyo tumeona katika maisha yetu ya ndoa kuwa baada ya kuoana, bwana (mume) anakwenda kushoto na bibi (mke) anachukua mwelekeo wa kulia kwa hivyo lile gari lao wanalolivuta haliwezi kutembea, wote wataangamia, na kwa hakika hii sio sababu ya ndoa. Kwani sababu kubwa ya ndoa ni bibi (mke) na bwana (mume) kushirikiana na kwenda hatua kwa hatua pamoja kuendeleza maisha yao na ya familia yao hapo baadaye.

3) Kuendesha maisha ya ndoa

Kwa hakika ndoa iliyofanikiwa na yenye raha inamgeuza mtu akajihisi kama yuko peponi na hiyo ndiyo baraka kubwa ya Allah swt na neema kubwa, kisha wajitahidi kiasi wawezacho kujionyesha kama kweli wao wako katika mazingira hayo (ya furaha) ili mazungumzo wanayozungumza, vitendo wanavyotenda vionekane kama ni kweli.

Kwa hivyo mtu anaporudi kutoka ofisini inambidi aje nyumbani na uso wenye bashasha hata kama amekumbana na mambo mengi yaliyomuudhi, yaliyomvuruga wakati akiwa ofisini na kwa hakika akija na uso wenye bashasha nyumbani, nyumba nzima watakuwa wachangamfu watakuwa wakicheka, atapenda aongee, wajadiliane, wazungumze, wabadilishane mawazo na kwa hakika hiyo itamfanya huyo bwana asahau uchovu wake wa siku nzima.

Lakini fikiria ukija nyumbani umenuna,umevimba uso kama papai, nyumbani wakishakuona tu umekuja umepandisha, wote watakukimbia, hata kama mmoja wa familia atakuwa amewazia ukija azungumze kitu fulani, hatazungumza mtu yeyote na wewe maana wanajua wakikuzungumzisha wewe ni sawa sawa na kuwatemea moto; kwa hivyo wewe mtu mmoja tu, ukija nyumbani unaweza kuigeuza nyumba yako ikawa bustani nzuri au unaweza kuitengeneza nyumba yako ikawa ni chumba cha adhabu kwa sababu kila mmoja anakuogopa; wote wamenuna umewatia katika adhabu na huu sio uadilifu kwa upande wa mwanamme. Na hakuna sababu ya mwanamme kuleta hali mbaya kama hii katika nyumba; mwanamme inambidi akirejea kutoka nje arudi na furaha ndani.

4) Furaha ya milele

Mwanamme ni bingwa katika utumishi wake lakini mtumishi aliyebobea katika utumishi, daima anatenda kiasi cha kumfurahisha mwanamke na kujiona yeye ni mtu maarufu.

Bibi na Bwana wanaelewana vizuri kuliko mtumishi, lakini inawabidi wote wawili wawe ni watumishi waliobobea katika fani yao; bibi kwa bwana na bwana kwa bibi. Kamwe usimfanye mke wako ahisi kuwa wewe unaelewa kasoro zake na wala yeye asifanye hisia kuwa anaelewa kasoro zako;. daima kila mmoja awe akimfunika mwenzake. Kwa hakika maisha ya furaha yanaweza kupatikana katika ndoa pale bibi na bwana wanapokuwa na moyo wa kutoa na wala si wa kuchukua.

5) Tofauti ya maoni

Ni jambo la lazima kuwapo na tofauti ya maoni na uhodari wa mabishano miongoni mwa watu waliokuwa wanaishi pamoja. Hasira ni jambo la kutokea lakini haifai pande zote mbili kuwa na hasira wakati mmoja; labda mmojawapo akipatwa na hasira au akichukiwa, basi mwingine lazima adhibiti hamaki yake. Yaani, yule anayeweza kwanza adhibiti na mara nyingine mwenzake. Kwa sababu, mmoja anapokuwa ameingiwa na hasira na mwenzake akawa ametulia hapo balaa na maafa mengi yataweza kuepukwa.

Kwa hakika nimeona maneno ya kupooza magomvi katika majumba yetu ni machache na matamu sana yaani kusema: "samahani nisamehe," . Na kwa hakika mtu anayesema maneno hayo ya "samahani nisamehe," ni mtu mwenye busara sana na anahisi raha moyoni mwake, hasa wakati anajua yeye hayuko kwenye hatia wala hana makosa lakini anaomba msamaha; na kuna msemo mashuhuri usemao 'anayetoa msamaha kwa mwenzake ni mpenzi wa Mungu'. Kwa hakika mtu mwenye moyo mkubwa ni yule anayekubali makosa yake, anayekubali lawama na kuomba msamaha.

Jambo lingine linalostahili kuandikwa kwa wino wa dhahabu ni "kamwe usimlaumu mwenzako". Njia nionayo iliyo rahisi kwa ajili ya kuelewana katika magomvi na kutoelewana katika sura mbali mbali ni kwanza ukubali kufanya maelewano japo kuwa liwe ni jambo dogo.

Halafu, baada ya mambo kutulia mnaweza kuendelea mkafanya marekebisho na maongezi zaidi katika maelewano yenu hayo, na hatimaye kila mnapokuwa mkiendelea kupanua maelewano yenu itafika wakati mtaona kuwa mambo ambayo mliokuwa hamkuelewana yatatoweka na kutakuwa na uelewano tu.

6) Kamwe usikemee bali ushukuru

Kamwe usiwaseme vibaya upande wa mke wako au upande wa mume wako. Kwa sababu iwapo mwanamme atakuwa akiwasema vibaya jamaa za mke wake basi mke ataanza kuwachukia jamaa wa mume wake. Kamwe usiwe na hasira dhidi ya mwenzako na wala usikubali hisia kama hizo ziingie mwilini mwako. Daima uwe ukishukuru, ukionyesha furaha sio kwa sababu ya mambo mazuri ya mwenzako bali hata ikitokea jambo mbaya ni muhimu sana uonyeshe subira. Kwa kufikiria mambo mazuri kila mara, hata kile kibaya kitatatulika vizuri.

7) Kufukia tofauti ndogo ndogo

Kutofautiana kwa maoni na mawazo na magomvi ni sehemu ya maisha. Mshairi mmoja maarufu amesema: "Je maisha ni nini, Je mauti ni nini, na kufufuka ni nini?" Urafiki wako, magomvi yako, na kukutana kwako tena."

Kisha hakikisha kuwa ugomvi wenu haubaki mpaka wakati wa chakula kinachofuata, yaani mkigombana asubuhi mpaka chakula cha mchana kiwe kimeshakwisha , na wewe hutakiwi kukwepa mlo huo. Ni lazima ukubali kuwa Allah swt ametujaalia neema kubwa ya muda huo wa kula chakula pamoja ambamo tunaongezea uhusiano na uelewano wetu na kumaliza tofauti na ugomvi wetu.

Lazima tuwe tahadhari kuwa kamwe tusianze mazungumzo ambayo yataleta ubishano mkali wakati tukiwa tunakula. Kwa sababu kunaweza kuanza mazungumzo ambayo yanaweza kuleta mzozo na watu wasiweze kula chakula chao, hivyo kila mtu aachilie mbali mazungumzo hayo hadi baadaye ili wote waweze kula vizuri na washibe ili waweze kumudu maisha yao na kazi zao hapo baadaye.

8) Mapenzi na mapenzi ya kusuhubiana

Kupendana na kucheza kwa bibi na bwana ni moja ya siri kubwa ya ufanisi wa maisha ya ndoa na kwamba inaweka hai moyo wa ndoa. Kamwe usijitupe ukajisahau bali inakubidi daima uwe ukijiweka vyema, vizuri kiasi cha kumvutia mwenzako ili daima awe akikutamani na kukupenda bila ya kujali umri wako.

Kusuhubiana kwa bibi na bwana ni gurudumu moja muhimu katika mtambo huu wa maisha ya ndoa. Kusuhubiana kutakuwa na mafanikio na raha zake zitapatikana pale bibi na bwana watashirikiana katika mazingira hayo. Inabidi ikumbukwe pia unapokuwa na mawazo mengi, kunapokuwa na mvurugano na mtu anapokuwa na matatizo, raha na hamu ya kusuhubiana hufa. Hivyo hamu na raha ya kusuhubiana inapatikana katika hali ya mtu kuwa mchangamfu na namna ya kujiweka mwenye raha.

Mtu anapochokozana kimapenzi na mwenzake basi kimchezo mchezo mapenzi yao yanaongezeka na hatimaye yanafika mbali mathalani bibi na bwana wanaweza kuwa wamelala katika mazungumzo, wanaweza kuanza mapenzi ya mmoja kumbusu mwenzake na wakawa na hamu wakaingiwa na hamu kwa wote wawili hadi kufikia hatua ya kusuhubiana kwa furaha; kwa sababu pande zote mbili wanakuwa na hamu.

Vile vile ni jambo la muhimu sana kila mmoja yaani bibi na bwana kukumbuka tarehe ya kuzaliwa ya mwenzako ili inapofika tarehe yake ya kuzaliwa unaweza kumpa salamu za kuzaliwa au ukampa zawadi. Hili ni jambo linalovutia na inadhihirisha kuwa kweli unamfikiria; pia ni vizuri kukumbuka tarehe ya kufunga ndoa ili mweze kuapiana salamu za heri ifikiapo tarehe ya ndoa. Mambo haya ni muhimu sana kuona kuwa unamjali sana mwenzako. Na kamwe uchunge vioja vidogo vidogo na tofauti ndogo ndogo ambazo haziishi na zikaleta balaa kubwa nyumbani. Tuwe na moyo wa kusameheana na wala tusiwe na moyo wa kukomoana kwa sababu kila inapo ongezeka hasira na chuki ni sawa na kumwaga mafuta juu ya moto.

9) Mabishano na ugomvi mbele ya watoto

Panapokuwa na watoto katika familia ni lazima kabisa kwa bibi na bwana kuheshimiana na kuonekana kuheshimiana mbele ya watoto wao; na kamwe wasionyeshe tofauti zao mbele ya watoto. Ugomvi na mzozano wa bibi na bwana mbele ya watoto una athari mbaya kabisa kwa watoto kwa ajili ya siha ya akili zao, jambo ambalo ni muhimu sana kwa watoto kuliko siha ya mwili.Vile vile matishio ya kumpiga mke ni mambo ambayo hayawezi kusameheka.

10) Kusahau yaliyopita

Hakuna faida ya kukalia makosa yaliyopita au mambo yaliyopita; itakuwa ni vyema lau utasahau na kusameheana ili mjenge maisha mema.

11) Mkaidi dhidi ya kuvumiliana

Ukaidi hauleti manufaa yoyote kwa bibi na bwana na familia nzima kwa ujumla, lakini kuvumiliana na kupeana mkono kwa bibi na bwana ni jambo moja ambalo linasaidia kusukuma gurudumu la maisha bora na utengemano ambayo hatima yake ni ya bibi na bwana kuelewana vyema na kuishi maisha ya starehe.

12) Kugawana kazi

Nyumba ni mahala pa mke na biashara au kazi au taaluma ni maswala ya bwana.Hivyo kama mwanamke anaishi nyumbani tu anafanya kazi za nyumbani na mwanamme anafanya kazi za biashara au ofisini basi wasiingiliane bali kila mmoja amwachie mwenzake aendeshe kazi inayompasa; hiyo haimaanishi kuwa bwana asiwe na picha ya mazingira ya nyumbani na mwanamke asiwe na picha ya mazingira ya kazi bali kila mmoja inabidi wasaidiane washirikiane waishi maisha mazuri ili bibi aweze kuendelea na kazi zake vizuri na bwana aweze kuendelea na kazi zake vizuri bila ya kuzozana.

13) Yote yale yang'aayo

Ni kweli kuwa ‘umbali unavutia’. Mara nyingine twaona wanandoa fulani huishi maisha ya juu.
Kwa hivyo utaona bibi na bwana hawa wanatuvutia na wanaonekana kwamba wao wanaishi vizuri kuliko sisi kwa hiyo tukazane kwa sababu sisi hatuishi vizuri, hatuelewani kama wale wanavyoishi kwa raha na starehe.

La sivyo hivyo inawezakana wao mbele ya watu hawaonyeshi tofauti zao bali wanaonyesha wako raha na starehe na hakuna tofauti baina yao. Ingawa kunaweza kuwepo raha na starehe pamoja na tofauti miongoni mwao; hivyo basi kwa kuwatazama wengine tusianze kuzua magomvi kwetu vile vile usione wengine wanaishi maisha ya kifahari na sisi baada ya kuyaona tukatamani kuishi hivyo bila kujali hali ya uchumi wa waume wetu au matatizo mengine yanayokabili familia kwa ujumla.