read

6. Uhakika Anaotakiwa Bibi Kuzingatia

(a) Kuwa mcheshi, kuimarisha mahusiano na kufundisha mambo mema. Na haya ndiyo maneno yenye busara kubwa.

(b) Unatakiwa uwe na uhusiano unaoitwa ‘uhusiano wa pembe tatu’ yaani pembe tatu hiyo iwe imetengenezwa kwa kona tatu, pembe ya kwanza ni Allah swt, ya pili ni bwana wako na ya tatu ni wewe mwenyewe; yaani kabla kutenda kitendo chochote kile, mwanamke afikirie kuwa haiko nje ya radhi ya Allah swt na radhi ya mume wake.

(c) Vita vikuu vya dunia vilivyopiganwa lau ukitaka nikuambie wapi na lini hutaipata katika ramani ya ulimwengu, ni vita vilivyopiganwa na akina mama kwa wanaume, kwa hiyo tuwe makini yasitutokee sisi.

(d) Tafuta vitabu, magazeti, maprogramu na mambo ambayo yatakufanya wewe uwe mke mwema zaidi, mama mwema, rafiki bora na Mwislamu bora.

(e) Qurani Tukufu inatuambia sura An-Nisaa, 4: 34

"....Basi wanawake wema ni wale wenye kutii,wanaojihifadhi wasipokuwapo waume zao..."

Vile vile Qurani Tukufu inatuambia katika sura Al-Ahzab, 33: 59

"Ewe Mtume ! Waambie wake zako,na binti zako na wanawake wa Kiislamu, wajiteremshie uzuri nguo zao."

1. Ndoa nzuri ni muujiza wa maisha

Kwa hakika kwenye siku yako ya harusi akili yako inageuka kwa siku za baraka zijazo. Ndoa nzuri ni muujiza wa maisha yote. Kwa hakika wewe na mpenzi wako hamuwezi kujua vile maisha yenye baraka na fanaka yatakavyokuwa mbeleni.

2. Uwe mke sio mama

Mke mpenzi, daima uwe ni kama mke kwa bwana wako na wala usiwe kama mama yake kwa sababu bwana wako aliyekwisha kua anahitaji mke na wala si mama. Na juhudi yoyote ya kujifanya kuwa wewe ni mama mbele ya bwana wako italeta athari mbaya kuliko nzuri. Hakuna mtu yeyote anayeweza kuwa mama na mke kwa mtu mmoja papo hapo kwa hivyo kwa bwana wako uwe kama mke wake. Utambue wazi kuwa bwana wako anaye mama wake na lau wewe ukitaka kujifanya kama mama yake basi ujue kuwa utakuwa ni kama mama wa kambo.

3. Ushangilie juhudi zake wala usimbishie

Kwa hakika mwanamme amezaliwa akiwa mtawali, na hivyo mwanamke inambidi awe mcheshi ili kuendesha maisha yao vyema. Mwanamme amezaliwa kuongoza na inavuruga akili na kumvuruga yeye pale anapoamrishwa na mke wake atii amri za mke wake.

Mwanamke hodari ni yule ambaye anaweza kumuathiri bwana wake kwa mbinu mbali mbali kiasi kwamba bwana wake asiweze kuhisi iwapo yeye anaelekezwa au anashutumiwa au anaburutwa na mke wake. Bwana yeyote hawezi kukubali kutii amri kutoka kwa mke wake na lau akichafuka, mambo yanaweza kuwa mabaya kabisa kwa hivyo mwanamke mwenye busara anajaribu kujiepusha na majanga ya maisha ya ndoa ili yasiharibike bali yaendelee vizuri na yenye mustarehe.

4. Kuonyesha hisia

Inambidi mwanamke amfanye bwana wake ahisi kuwa mke wake ni mtu mmoja ambaye anamjali kabisa maishani mwake.Unaweza kuwa na mawazo na matatizo mengine ya familia na watoto lakini baba watoto lazima apewe nafasi ya kwanza, kiasi kwamba asihisi kuwa yeye ametupwa, haumjali. Hivyo pamoja na kuwa na shughuli za nyumbani nyingi zilizokutinga kamwe usisahau kumjali bwana wako pale anapoondoka kwenda kazini katika harakati za kutafuta riziki, na kwa hakika mwanamke mwenye busara atamsindikiza hadi mlangoni na ataweza kumuaga vyema. Vile vile atakaporejea kutoka kazini uwe ni wakati muhimu katika maisha yako inakubidi umpokee kama shujaa na unamkaribisha kama mgeni muhimu kwako huku ukijionyesha umefurahia sana na kurudi kwake kwa moyo wako na bashasha usoni.

5. Usimkaribishe kwa matatizo yako

Kamwe, usianze kuongea mambo ya matatizo yako pale bwana wako anaporudi kutoka kazini. Kwa sababu bwana wako atakuwa ametoka katika vurugu za maisha, matatizo na mawazo ya siku nzima yaliyokuwa yakimzonga akilini huku akiwa amerudi nyumbani ikiwa kama ni peponi hivyo bibi umkaribishe vyema na furaha. Mkaribishe vyema ajihisi kama kweli amepata utulivu katika moyo wake na akili yake na baadaye kadiri muda unavyokwenda atakujali vyema.

6. Usiwe mtafuta makosa

Kamwe usiwe mtu mwenye mzozo, usiwe mtu mwenye kuzua mizozo na katika maswala nyeti na bwana wako kamwe usiseme:“Je si nilikwambia hayo .........".

7. Nyumba ni ngome yako usiiache

Kamwe usiiache nyumba yako katika hali ya mzozo wowote ukaenda nyumbani kwa mama yako. Hii nyumba ni ya kwako hivyo itakubidi ufanye marekebisho kuliko kuiacha. Magomvi na mizozano yote itakuwa imepoteza makali yote siku inayofuata yaani mambo yatakwenda yanatulia kila muda utakavyokuwa unaendelea kupita.

8. Familia ndio wajibu wako

Mwanamke aliye elimika na kuerevuka lazima akumbuke kuwa iwapo yeye anataka familia, na maisha ya kifamilia basi itambidi kujitolea mhanga ya utaalamu wake kwa sababu ya bwana wake na watoto wake; yaani iwapo mwanamke ni mhandisi au mwalimu au ni mtaalam katika fani yoyote ile na iwapo anataka familia na lau itambidi abaki nyumbani kuitunza familia yake basi itambidi atoe mhanga wa utaalamu wake kwa ajili ya familia yake hiyo. Kwa hakika kimaumbile mwanamke ni mtu mwenye kuheshimiwa na makusudio ya maisha yake ya msingi ni kuzaa watoto, kuwalea na kutengeneza nyumba yake. Adhma yake katika maisha ni kuwa mke na mama.

9. Uonekane mwenye kuvutia

Daima itakubidi uwe mwenye kupendeza na kuvutia mbele ya mume wako. Hakuna mtu yeyote anayeweza kujigeuza au kutokujali mbele ya mwanamke anayependeza na kuvutia yaani kila mwanamme anavutiwa kwa mwanamke anapopendeza na anapovutia, lau wewe hautaweza kumuweka katika mvuto wako basi utambue wazi kuwa kuna mwingine atamvutia. Itabidi tukumbuke kuwa hakuna mwanamke aliye ovyo isipokuwa huyu mwanamke asiojua namna ya kujirembesha na kujifanya mwanamke mwenye kuvutia na kupendeza.

10. Uridhike kwa kidogo

Bwana wako anaweza kufanya kila juhudi kwa uwezo wake ili akupatie kile kilichobora kabisa. Lazima daima uwe unafikiria kuwa wewe uko katika hali ya afadhali kuliko mwanamke mwingine. uelewe kuwa majumba ya fahari na gari, havifanyi maisha ya bibi na bwana yakawa ya furaha na mustarehe hata kidogo isipokuwa kinachofanya nyumba ya bibi na bwana kuwa raha na mustarehe ni kule kuridhika hata kama kitakuwa ni kiasi kidogo kwa sababu tumeona kuwa kuna familia nyingine matajiri kabisa lakini hawana raha nyumbani, bibi ana njia yake na bwana ana njia yake. Pamoja na kuwa na gari, majumba ya fahari kila kitu wanacho lakini ile raha ya maisha ya ndoa hawana.

Na vile vile tumewaona watu wengine wanaishi maisha kwa tabu tabu kimapato, lakini wanaishi kwa mapenzi, wanapendana na humo ndimo kuna baraka za Allah swt. Kwa sababu wote wawili wanaishi maisha ya kutosheka, wanakinai. Amesema Mtume Mtukufu s.a.w.w. kuwa: "Asiyekinai kwa kidogo hashibi kwa kingi."

Inatubidi tutosheke, turidhike kwa kile alichotupa Allah swt na hii ni neema moja kubwa ya Allah swt na wala usisikitike kwa kile usichonacho. Daima uwe na moyo wa kusema kuwa wewe unacho kila kitu na moyo kama huu ndio utakupa maisha mazuri.

11. Malengo ya maisha yawe kujirekebisha

Kamwe usijaribu mawazo yako potofu yakakufanya uwe mwenye fahari mbele ya mwenzako katika maisha ya unyumba, daima uishi vile nafasi yako katika familia ilivyo yaani isiwe wewe mwanamke unataka kujifanya wewe ukachukua nafasi ya mwanamme katika nyumba. Mwanamme ana nafasi yake na wewe mwanamke una nafasi yako, hivyo kila mtu ana cheo chake. Na hii ndiyo itahakikisha maisha yawe mema kwa sababu tunaona magomvi makubwa ndiyo hayo, bwana ataanza kusema mimi mke wangu anataka kuniendesha, anataka kunitawala, ananitolea amri mbali mbali, mimi siwezi mwanamke kama huyu na hatima yake ni kuachana na kuishi katika hali ya ugomvi na kutokuelewana.

12. Daima uwe ukishirikiana naye

Daima uwe mcheshi pale unapomuona ametingwa na mawazo, anamzigo kwenye akili yake ambao unamchanganya. Lazima umpunguzie uzito wake mwilini pale unapoona amelemewa. Mashitaka kutoka kwako yawe machache sana iwezekanavyo na daima uwe ukitafuta njia yenye mafanikio katika kumkaribia na katika maongezi yako na yeye. Inakubidi uitengeneze nyumba iwe ni mahali ambapo kwa hakika yeye ndipo anapotaka kwenda yaani unaweza kuigeuza nyumba yako ikawa ni mahala ambapo yeye akija amechoka anakuja anaona anaweza kupumzika na akatuliza akili yake na wala usiigeuze nyumba ikawa ni mahala akija ndio kunaanza vita na ugomvi. Kwa kifupi hiyo nyumba uigeuze iwe Jannati au Jahannam, uamuzi ni wako utaona utakavyoweza kufanya wewe.

13. Mfanye akufurahie

Kwa kumtukuza ni jambo muhimu sana na kila bwana anapenda kuwa mke wake amsikilize na amkubalie mambo yake, anapenda pia ubashasha wa mke wake na shukurani zake. Na pale utakapo ona unaweza kutimiza yale mambo yaliyo moyoni mwake basi utambue wazi kuwa daima atakuwa anakupa kila kitu kilicho bora kabisa. Iwapo bibi atamtukuza bwana wake kwa hiyo bwana ataona kuwa nikitaka kufanya kitu hiki atasema hapana mke wangu ananipenda na kunitukuza hivi basi wacha nimpe kitu kilicho bora zaidi.

Hivyo tunaona hata hawa masikini wanaokuja kuomba mitaani na majumbani, akikuona hakuambii nisaidie shilingi moja, hapana, huyo masikini kwanza ataanza kukusifu, “ ahaa! bwana habari za siku nyingi hujambo?vipi watoto nyumbani hawajambo, mama hajambo! Ehee! siku hizi vipi nasikia ulikuwa unaumwa?” Anakuzungumzisha kidogo unafurahi baadaye kidogo anakwambia, “haloo! bwana nina shida, nisaidie senti kidogo”, kwa hiyo utafikiria kuwa huyu mtu nimezungumza naye vizuri, badala ya kumpa shilingi moja ngoja nimpe shilingi kumi au mia moja, basi hii ndivyo ilivyo unamthamini mtu kufuatana na kauli yake.

Katika sura nyingine mtu mpumbavu anapokuuliza, je! mimi ni mpumbavu? na lau utamwambia kuwa wewe ndiye mpumbavu wa mwisho duniani, nadhani wewe ndiye utakuwa adui wake wa mwisho na mtagombana sana. Na iwapo utamwambia kuwa nani amekuambia kuwa wewe ni mpumbavu, wewe ni mtu mmoja mwerevu sana katika watu ninaowajua na ninaowaheshimu, wewe mtu mmoja mwenye busara sana basi utaona pale anacheka na anafurahi na kweli kwa hakika wewe ndiye utakuwa rafiki yake sana, pamoja na upumbavu wake ule lakini atakuheshimu; kwa hivyo itakubidi wewe kama mwanamke ushirikiane naye katika kujenga mazingira ya nyumba hiyo yenye ndoa.

14. Hata wapenzi wa kweli wana matatizo

Kwa hakika hata mapenzi ya kweli hayana dhamana ya kukosa matatizo. Hata kama bibi na bwana wanapendana kiasi gani haiwezi kusemwa kuwa hakuna matatizo miongoni mwao, lakini jambo la ajabu ni kwamba wao pamoja na kuwa na makosa na matatizo miongoni mwao wameshikamana vyema na wanasonga mbele. Na hayo ndiyo maendeleo ya kweli.

15. Uwe mpishi bora

Kujishughulisha na mambo ya vyakula unachukua masaa mengi kwa siku na kwa jumla kuliko kazi nyingine zozote za nyumbani. Katika hali hii kuna sura mbili:

1. Ama kuchukia na kusababisha kupika chakula songa mbele.

2. Au kufurahika na kazi ya mapishi na katika hali hii lau utapika mapishi kwa furaha na moyo mkunjufu basi utapika bila kuona tabu yoyote na utaweza kupika vyakula vya aina aina ambavyo vitafurahisha nyumba nzima .

Upishi unaonekana kwamba ni jambo ambalo ni nzito sana katika baadhi ya majumba lakini mimi ninaona upishi ni fani moja kubwa yenye kufurahisha na yenye kumchangamsha, jambo ambalo linadumu maisha.

Na kutaka kuwa mpishi mzuri au mtaalam, kwanza itakubidi utambue umuhimu wake. Pili itabidi ujifunze na kutambua, na tatu inabidi utende kimatendo yaani uyapike hayo mapishi.

Je! hatuelewi sisi umuhimu wa mapishi katika maisha ya ndoa ya ustarehe na yenye fanaka? Je! hayana umuhimu katika kujenga familia zinazoishi kwa raha? Wanaume wengi sana nimewaona na kuwasikia wanapotoka majumbani mwao wanakwenda kunywa chai katika vioski na mahotelini wakati wamewaacha wake zao nyumbani wamelala usingizi mnono na mtu ambaye hana habari na kinachotendeka.

Vile vile wako wanaume wengine wanaoamka na kujipikia chai yao na vitafunio. Loh! Jambo la kushutua sana na la kuaibisha. Inawezekana mwanamke huyo haimbidi kuamka mapema kiasi ambacho mwanamme anaamka lakini anaweza kutumia ustaarabu huo wa kuamka na kumtengenezea chai na vitafunio bwana wake anywe ashibe aende kazini akafanye kazi vizuri, na baadaye huyu mke anaweza kurudi chumbani kulala au anaweza kulala mchana. Hebu fikiria chai na kitafunio kilichotengenezwa na mke wako mcheshi mwenye roho nzuri mwenye moyo wenye kukupenda wewe na huku akitoa maongezi matamu matamu asubuhi itakavyokusaidia wewe katika siku yako hiyo nzima; bwana anatoka nyumbani amefurahi, siku nzima yake itakwenda vyema kabisa. Na bwana kama huyo ambaye amepata chai na vitafunio na maneno matamu ya mke wake, jioni anaporudi anakutana na mke anamchekea vizuri anaongea naye vizuri na kukuta amepikiwa chakula chake vizuri cha jioni basi mimi hapa sina maneno ya kuelezea hali ya starehe na ya ufanisi wa maisha ya ndoa inavyokuwa.

16. Wajibu wa mama kwa binti

Mama anaweza kuwa athiri watoto sana katika mapishi na kazi za nyumbani. Inawabidi akina mama wachukue muda wao katika kuwafunza mabinti zao kuhusu mapishi na kazi za nyumbani wafanye nao.

Akina mama watambue wazi kuwa watoto wao wanapo olewa na wanapokuwa na mikono yao myeupe haimfurahishi bwana isipokuwa kazi anazozifanya nyumbani na kutunza nyumba na ule mpango, akili na moyo wa kufanya na kufanyisha kazi ndio unaopendwa na bwana. Kwa hiyo mwanamke ambaye hafanyi kazi na nyumba inakuwa chafu, hapiki au hajui kupika basi unyumba wake utakuwa na matatizo na katika hali hii magomvi hayawezi kuisha.

Inawabidi akina mama watumie akili na busara yao kutaka kuishi maisha mema wawafundishe mabinti wao vitu hivyo ili wao pia wakienda kwa mabwana wao waweze kuishi maisha mema na mazuri.Hakuna mama anayetaka binti wake akiolewa apate taabu huko, hivyo ili kuepukana na swala hili itabidi muwafundishe mabinti wenu mapishi, kazi za nyumbani, mapenzi ya bwana na ufamilia, ili kuhakikisha maisha yao yatakwenda vizuri. Watoto wa siku hizi wanalelewa vibaya na wazazi wao na hatimaye tunaona magomvi ya familia hayaishi, na mara nyingi mabinti wengine wanarudishwa kwa wazazi wao kwa sababu ya kukosa uhodari katika fani hizo.

17. Kufanya kazi nje ya nyumba

Akina mama inawabidi kufanya kazi, na miaka ya nyuma akina mama walikuwa wanafanya kazi ngumu na kwa masaa mengi. Wanawake walikuwa wakifanya kazi katika maduka madogo au mashambani na pia walikuwa wakifanya kazi pamoja na mabwana zao na watoto wao wote walikuwa wakifanya kazi kwa pamoja. Kwa hivyo kila wakati mama alikuwa pamoja nao na Yeye alikuwa daima akipatikana pale alipokuwa akihitajika na mtoto wake; aliweza kuwaacha baba na watoto dukani akaenda nyumbani kumshughulikia mtoto wake. Na kazi yake ilikuwa ni kwa mujibu wa kutaka kuishughulikia familia yake na ilikuwa ni kazi za kifamilia.

Lakini kazi za siku hizi ni kazi tofauti kabisa ni mbali na nyumba, ni mbali na bwana (na kwa kawaida kazi hizo ni pamoja na mabwana wa wanawake wengine).Na mara nyingi wanaume wanapokosa mapenzi na uvutano wa wake zao, wanaingia katika mtego wa wanawake wengine.

18. Mama anapofanya kazi ni mbali mno na watoto

Kama Akina mama hufanya kazi, inambidi kuajiri walezi, na walezi wa watoto wanakaa kidogo kisha wanabadilika mmoja baada ya mwingine. Kwa hiyo katika maendeleo ya mtoto hafaidiki kiasi anachotakiwa na upole na mapenzi ya mama hayapatikani pale mtoto anapokuwa mgonjwa au anapokuwa katika shida. Hali hizi kwa siku hizi ndizo zinazoleta matatizo makubwa katika familia zetu hizi.

Lakini ninaona kuwa akina mama inawabidi watambue hivyo kabla ya kukubali kufanya kazi kama hiyo. Labda inawezekana wakatafuta njia nyingineyo ya kupata mapato ilihali bado wakiwa nyumbani. Daktari Habibu Nathan kutoka Chuo kikuu cha Florida amefanya utafiti juu ya matokeo ambapo mama anapomuacha mtoto wake nyumbani kabla ya kuanza shule. Yeye amegundua kuwa kuna matokeo mengi sana ambayo ni kinyume na tabia za kijamii kwa mfano udanganyifu,wizi na uporaji, kutokuwa na adabu ya kutambua baina ya usawa na ubaya, uharibifu na mara nyingi wakiwa wakijishughulisha wenyewe na miili yao. Na watoto kama hawa mara nyingi imeonekana hawapendelei kujitambulisha na wazazi wao.

Ukitaka kusoma zaidi juu ya maudhui haya,rejea sehemu ya pili ya kitabu hiki juu ya muta'.