read

7. Hiki Na Kile Katika Maisha Ya Ndoa

Kwa vijana

1. Majukumu yanayo ambatana na maisha ya kuoana inahitaji uangalifu sana. Uvumilivu, na hisia za kijana ambaye hana uzoefu anaweza kuona kuwa anajitwisha (kama ataoa) mzigo wa matatizo ulio hafifu kuliko pale anapokuwa peke yake. Lakini ule moyo na hali wa kutaka mtu kuunganisha na mwenzake ndio siri kubwa ya maisha ya ndoa ambayo itafanya maisha hayo kuwa kama bustani ya maua mazuri ya kupendeza.

2. Katika maisha ya awali ya ndoa kunakuwa na mawazo kuhusu mapato ya familia hasa fedha za kununulia vitu vya nyumbani na gharama zinginezo. Na katika hali ya kushirikiana, maswala ya kifedha ni ya wote wawili na bibi na bwana wanaweza kuunganisha vichwa vyao kwa pamoja na kuweza kutatua maswala yao yanayowazonga kwa pamoja kama vile mapangilio ya kazi, matumizi ya fedha n.k.

Ni lazima tukumbuke kuwa mwanzoni mwa maisha ya ndoa hakuna mtu ambaye ana mapato ambayo yanaingia tu bila yeye kutafuta na kushughulikia na ni jambo la furaha mno kuona mtu anakusanya senti moja moja hadi hapo wanafanikiwa hata kujenga nyumba.Usisahau kuwa wazazi wako pia wameanza vivyo hivyo na wao pengine hawakuwa na chochote kile wanachokihitaji pale ulipokuwa bado mdogo. Na kwa hakika ni jambo la kawaida kuwa sisi inatubidi tujue namna ya kuweka akiba na maswala ya akiba ni nyeti katika maisha ya familia ili kujenga maisha ya baadaye kwa ajili yetu na kwa ajili ya watoto wetu.

3. Katika kupunguza mawazo na mvutano wa maisha, watu wengi wanakuwa na mapenzi katika mambo fulani fulani ambayo kwa hakika hatuwezi kuelezea umuhimu wake katika maisha ya ndoa hususani mapenzi au mazoea ya tabia baina ya bibi na bwana wanaweza kushirikiana kwa pamoja. Lau tabia ya mapenzi kama hayo yataanzia katika ujana wao kwa wote pamoja kwa hakika litakuwa ni jambo la kufurahisha mno katika miaka ya baadaye.

Umri wa kati

4. Katika umri wa kati yaani baada ya miaka chache ya kuoana, bibi na bwana wanakuwa katika umri wao mzuri sana na maisha yao yanaweza kuwa maisha ya peponi.

5. Hapo kuna anza kutokea matatizo ya watoto wanaokua lau itakumbukwa kuwa watoto ni matokeo ya ushirikiano wao na hivyo ni wajibu wa kila mmoja wao katika kuwaongoza na kuwaelekeza kwa hivyo hakutakuwa na matatizo yoyote katika umri huu na hivyo itafanya maisha yao yawe yameimarika zaidi.

6. Katika miaka ya kukua mwanamke anaweza kukabiliana na matatizo kwa sababu uzazi wake unakwisha na mwili wake inabidi ubadilike kwa ajili ya hali hiyo. Na katika hali hii ya kipindi kifupi anaweza kujisikia mzito asiye na raha na asiyejipenda na hata maisha hayapendi kwa sababu atakuwa haoni raha katika kila hali hivyo wakati huu ndiyo utunzaji bora na mapenzi ya bwana wake ndiyo yanayoweza kumsaidia akapita kipindi hiki ingawaje na daktari anaweza kusaidia katika swala hili.

Kwa kifupi, kila mabadiliko ya mwili wa mwanadamu iwe bibi au bwana, wanatakiwa wawe tayari kama waokozi wa mwenzao katika hali itakayo kuwa ikimghilibu mwenzao. Bibi akiona bwana anapita katika kipindi fulani anamsaidia na kumfariji na kumpa hima na vile vile bwana pia itabidi kufanya vivyo hivyo.

7. Katika umri huu wa katikati mwanamme ndio huwa yuko katika kilele cha wajibu wake kama bwana au baba akiwa kama mkuu wa familia; kwa ujumla hivyo ataonekana yuko mashughuli (anashughulikia) sana katika kutimiza malengo na mipango ya kifamilia ambayo alikuwa akiadhimia akiwa anayo adhma kutoka muda uliopita. Hivyo inambidi huyo bwana awe akitia maanani pia kuwa familia inamhitaji hata wakati huo, hivyo asijisahau na kuisahau familia yake. Kuwa na uwiano sawa na shughuli na familia ndio kutaleta maendeleo mazuri katika maisha ya kifamilia, hivyo haitakuwa vyema kushindwa upande mmoja wa ’vita vya nyumbani’ kwa ajili ya upande wa pili. Kwa sababu tunaelewa vyema kuwa athari, mapenzi, maongozi na maongezi ya baba katika familia kwa ajili ya watoto wake na kama bwana kwa ajili ya mke wake ni vitu ambavyo vina umuhimu sana katika familia na lau watoto watakosa vitu hivi watakuwa na hasara kubwa sana na wata athirika vibaya mno, mambo ambayo hayana suluhisho katika maisha ya mbeleni.

Miaka hii ndiyo wakati mwanamme yaani mume au akiwa kama baba anaanza kuweka msingi ya baadaye wa maisha ya watoto; wakati huu ndio bwana anamalizia mipango ya kujenga nyumba kwa ajili ya mke wake na watoto wake na wakati huu huu ndio watoto wanapokuwa wamekua kidogo kwa hiyo yupo katika mipango ya kuwasomesha masomo ya juu zaidi au kuwapeleka katika masomo ya fani mbalimbali. Hivi ndivyo vinavyomtinga kwa kipindi hiki. Namna ya kukabili mambo hayo yote na namna ya kutimiza adhma aliyokuwa akiipangia miaka yote iliyopita, ushirikiano wa mke na watoto kwa bwana au baba katika hali hii ni jambo moja jema kabisa ambalo litamsaidia kutimiza malengo haya kwa uzuri na vyema kabisa, bila ya kuhisi kuwa amebeba mzigo huo peke yake.

8. Wakati huu ndio tunawaona wanawake wengi wakiwa wajane wanafiwa na mabwana zao hivyo tuombe kwa Allah swt asiwajaalie wake zetu kupata matatizo.
Kuna wajane wengi sana wanaozurura mitaani, wanaofanya kazi vilabuni, wajane kila mahali tunakutana nao, na hayo hawapendi kuyafanya lakini kwa sababu ya mazingira magumu wanapotoka katika njia zao.

Kwa ajili ya uzeeni

9. Kuna msemo wa wahenga usemao kuwa:"Mwanamke ni mzee vile aonekanavyo na mwanamme ni mzee kama vile mishipa yake inavyoonekana, ni kweli." Kwa sababu mwanamme ni mzee kiasi kile anachokihisi yeye na kuhisi mwenyewe ni jambo moja muhimu sana katika maisha ya mwanadamu na hiyo hisia ndiyo inayobadilika kuwa jambo la ukweli linalo onekana kwa hivyo iwapo mwanamme atapendelea ajionyeshe kama kijana na akajiweka kama kijana basi atakuwa anaonekana kama kijana kabisa, na mishipa yake ya damu ya mwili iwe minyororo inawezekana kwa kuzingatia mambo ya vyakula na mazoezi.

10. Ni jambo la kawaida kwetu sisi kuona mtu ameishi miongo sita au zaidi kuwa ni mzee na mambo ambayo tunaona kuwa huyu mtu anastahili kustaafishwa hata kazini. Kwa hakika hili zoezi sio sahihi. Tusiangalie mtu ameishi miaka mingapi ili tujue uzee wake bali tuangalie ameishi namna gani, ndilo jambo lililo la muhimu mno. Tunawaona watu wengi sana wanasayansi pia na watu wanaotoa mihadhara na wataalamu katika fani mbalimbali ambao wamechangia kwa kiasi kikubwa mno na kwa muda wa miaka mingi katika fani zao na wametoa michango yao katika kuiendeleza fani zao hizo ambao baada ya kupita miaka yao hiyo ya uzee sisi tunaouhesabia na bado wako wachangamfu na wakakamavu.

Kwa hiyo kama tunasema mtu miaka sitini ndio anastaafu sio sahihi kwa sababu katika miaka hiyo sitini hatujui ni miaka mingapi amefanya kazi, kinachotakiwa kuangaliwa si miaka mingapi amefanya kazi bali ana uwezo bado! Kwa sababu mimi naona mtu mwenye biashara yake kamwe hakujistaafisha katika umri huo na bado anaendelea vizuri kabisa na miaka mingi itakayokuja.

11.Utafiti wa siku hizi umegundua kuwa mtu ambaye anajiweka mkakamavu kiakili na kimwili katika shughuli mbalimbali basi anakuwa amejiepusha na matatizo ya uzeeni, hivyo hata mwishoni wa maisha yake bado anaweza kuwa na nguvu na kuendeleza shughuli katika hali yoyote ile, iwe ya kiakili au kimwili.

Hivyo maisha ya ndoa ambayo yanaendelea daima ni baraka na neema kubwa ya Allah swt. Na kukua kwa watoto kusiwaletee hofu na mashaka kwa upande wao. Iwapo mtu atataka maisha yake yawe mema na mazuri zaidi atokane na tamaa ya umashuhuri, kujitakia nafasi, kutaka mamlaka au utajiri; kwa hakika raha ya kuishi itaweza kupatikana na mwenzako ambaye ameshirikiana na wewe katika hali tofauti tofauti za maisha.

Inabidi mtu aende na maisha yake au aende na wakati; mtu anapokuwa kijana anaweza kujitafutia nafasi, pesa, nguvu na umashuhuri n.k. kwa sababu ana uwezo wa kufanya mambo kama haya na anakuwa na nguvu za kukabiliana na mambo kama haya na matatizo yoyote yatakayotokana nayo; na vile umri wake unavyoendelea kukua ile nguvu ya kustahmili ya kukabiliana na mambo kama hayo inapungua. Pia nguvu za mwilini mwake zinapungua.
Hivyo yanapotokea matatizo yoyote yanamuathiri sana kiakili na kisiha; mara nyingine katika hali ya uzee mtu anapata ugonjwa wa moyo, au hata kupoteza fahamu (akili) n.k. na kukosa usingizi ni mambo ya kawaida, hivyo inabidi mtu kupunguza kasi zake za harakati za ujana ili anapozeeka, akili yake isiwe inaathirika ambayo itahatarisha maisha yake ya uzeeni.

12. Kuna sheria au kanuni zingine zisizo za kistaarabu (zimetungwa ili kuboresha fursa za ajira kwa vijana) ambazo zimembainisha mtu kuwa ni mzee ati kufikia umri fulani (kama sitini) yaani nkuonyesha kuwa amezeeka. Na hali hii inaweza kuleta athari mbaya sana kwa mtu ambaye mpaka siku hiyo amekuwa daima akijishughulisha na gurudumu hili la maisha na sasa anakatizwa na mpangilio wake na tabia aliyoizoea katika maisha.

Lakini inaweza hali hii ikamsaidia mtu (kama alikuwa ameshapanga) kujiandaa na utaratibu mwingine baada ya kuachana na shughuli aliokuwa akiendelea nao kwa miaka mingi.
Kwa sababu kama hajapanga mapema kuwa ataendelea vipi baada ya kusimamishwa kazi, tumeona watu wengi waliokuwa wakifanya kazi na kuishi vizuri nje na ndani ya nyumba baada ya kustaafishwa wanapata mshtuko na wanaona maisha yanakuwa magumu hawana raha na mustarehe ndani na nje ya nyumba zao. Kisha watu kama hawa wanajiona kwamba wao hawana ’status’ hali miongoni mwa watu kwa sababu wanakaa wanaota kila wakati ndoto za siku zilizopita na mambo yalivyokuwa mema wakati ule.

Na vile vile anaona vigumu sana kuchanganyikana na watu wengine, anakosa uchangamfu na badala yake anaona afadhali abakie nyumbani tu. Hivyo kwa matokeo yake atakuwa amejipoteza kwake mwenyewe kwa familia na jumuia yake nzima kwa pamoja. Hivyo inambidi mke wake ajitayarishe katika kumuandaa bwana wake na kumpa hima katika hali hiyo ya kustaafishwa ili kujaribu kupunguza athari mbaya baada ya kustaafu, jambo lisilozuilika.

Mwanamme daima amekuwa ni mtu wa kuhisi kuwa yeye ni mkubwa na mtu ambaye ana uwezo wa kila aina katika miaka ya nyuma na lau leo atakuwa amestaafishwa hivyo katika maswala ya mapato na mambo mengineyo atakuwa amekwama na katika hali hii mwanamke (mke wake) itambidi aendelee kumtukuza na kumpa heshima vile vile alivyokuwa.Mapenzi ya mke yanahitajika sana wakati huo. Kumshutumu na kumsuta katika umri huu kwa matendo yaliyopita yana athari mbaya kabisa. Na hali hii ya bwana kuadhirika ni kwa muda mfupi tu, na lau mke wake atashirikiana naye vizuri katika kipindi hiki inaweza kuwa kipindi kifupi zaidi na katika kipindi hicho maisha yanaweza kuwa mazuri na yenye raha na fanaka bila ya kujali uzee wanaopitia.

13. Kama nilivyoelezea awali ni vizuri kuwa na (interst) mapenzi katika fani mbalimbali hasa katika umri huu wakati mtu anaona hana shughuli ya kufanya anapitia katika kipindi kigumu baada ya kustaafishwa inambidi awe na mapenzi ya jambo fulani ili kupoteza mawazo yake; mfano mtu mwingine anakuwa na tabia au mapenzi ya uchoraji. Kuna mfano wa mtu mmoja ambaye katika miaka ya nyuma alikuwa mchoraji, na uchoraji huu ameuanza alipokosa kazi maana mawazo yalikuwa yakimsumbua kwa hiyo akajitafutia hoja ya kujituliza kimawazo, akawa mchoraji na kwa hali hii alinunua kibokisi kimoja cha rangi na brashi kidogo na makaratasi mengi na akaanza kazi ya uchoraji. Na baada ya kutayarisha vitu hivi akajiingiza katika fani hii ya uchoraji hivyo maisha yake yakawa yanaendelea vizuri bila kuharibikiwa na akili. Mambo kama haya wote tunaweza kuyafanya.

14. Imesemwa kuwa ujana wenyewe unavutia lakini bora zaidi ni kuwa na shukurani katika uzeeni.