read

8. Mambo Katika Maisha Ya Ndoa

1. Bibi na bwana kustiriana

Allah swt anatuambia katika Quranii Tukufu sura Al-Baqarah, 2: 187

"... Wao ni (kama) nguo kwenu, na nyinyi ni kama (nguo) kwao."

Familia inaanza katika bibi na bwana wenye mpangilio wa maisha ambayo yanawaelekeza wote wawili katika njia iliyo bora hapo mbeleni, tunaona katika jamii ya siku hizi kuwa kuna mapambano katika jamii zetu, baina ya Mashariki na Magharibi mawazo haya yanatofautina au tunaweza kusema kuna tofauti baina ya mawazo ya Kiislamu na mawazo yasiyo ya Kiislamu, kwa sababu jamii ya Kiislamu imeeleza waziwazi vile mfumo wa familia unavyotakiwa kuwapo na kwa kuwa watu wanaacha tabia na tamaduni zao za Kiisilamu na kukimbilia tamaduni za kimagharibi au zile zisizo za Kiisilamu ndipo matatizo na upotofu unapoanza hivyo ni ushauri kwa wote kwanza wazingatie mfumo wa jamii katika Uislamu ndipo hapo baadaye wajaribu kuingia katika mfumo wa kimagharibi halafu shauri lake kama atapata kupotoka au atapenda kurekebisha maisha yake ili hadi mwisho wake, yawe yenye fanaka na baraka.

2. Kimaumbile shughuli za mwanamme na mwanamke

Ni wazi wazi kuwa Allah swt amemuumba mwanadamu, ana mambo mawili ya kuyafanya:

1.Kuendeleza kizazi ili kisi ishe, binadamu waendelee kuzaana.

2. Kutimiza mahitaji yao.

Kwa upande mwingine tunaona Allah swt amegawanya wanadamu katika makundi mawili mwanamme na mwanamke.Naona kwa maumbile mwanamme ameumbwa kwa ajili ya shughuli za nje za kutafuta mahitaji na kutafuta riziki kwa ajili yake na familia yake nzima wakati mwanamke hakupewa jukumu huo. Papo hapo tunaona kimaumbile mwanamke ametengenezwa makhsusi kwa ajili ya uzazi na malezi.

Itakuwa ni jambo lenye ugumu sana kwa mwanamme kufanya kazi za kulea na kutunza familia na kupika chakula na mambo mengineyo ambayo mwanamke anayafanya vyema zaidi na vile vile kimaumbile ni vigumu sana kwa mwanamke kufanya kazi ngumu za kupambana na maisha katika kuchuma fedha kwa ajili ya kulisha familia yake. Na nyanja zote hizi mbili zinapingana.

Kwa mwanamme kubaki nyumbani, kulea watoto, kutunza nyumba na usafi n.k. anaweza akachoshwa katika muda wa madakika tu na papo hapo anaweza kukumbana na maswala magumu zaidi akiwa nje ya nyumba katika kutafuta riziki na kutafuta mahitajio ya familia yake; hayo mambo mazito na magumu hatayajali bali atayakabili na kuyapita, na upande mwingine mwanamke kutoka nje ya nyumba kwenda kutafuta mapato kwa ajili ya riziki na mahitajio ya familia yake ni kazi moja ngumu sana kwake kimaumbile lakini anaweza kushinda nyumbani siku nzima, akilea watoto, akifanya usafi na mapishi n.k. bila kusikia uchungu au uchovu wowote.Hivyo mwanamme awe ni mwanamme na mwanamke abakie kuwa ni mwanamke.

3. Faida za ndoa

Mazungumzo yaliyotangulia yametuonyesha waziwazi majukumu katika maswala haya ya ndoa hivyo tuendelee na mazungumzo yetu kuhusu faida za ndoa na hizo ni kama ifuatavyo:-

(a) Faida ya kwanza

Kazi za mwanamme na kazi za mwanamke kama zilivyo elezwa hapo juu zina kamilisha uwiano wa majukumu katika familia, hivyo hizo ndizo faida za mkataba wa ndoa.

Katika mkataba huu mwanamme anachukua jukumu la kufanya shughuli fulani na mwanamke anakubali kufanya shughuli fulani ili familia iweze kuishi kwa baraka, amani na fanaka. Mwanamme atatumia uwezo na nguvu zake zote katika kutafuta mapato kwa ajili yake na familia nzima na mwanamke atatimiza wajibu wake upande wa nyumbani na hivyo sehemu zote mbili zitakuwa sawia. Allah swt anatukumbusha jambo hili katika Qurani sura An-Nur, 24: 32

"...kama watakuwa mafakiri,Allah atawatajirisha katika fadhila Zake..."

Imam Ja’afer Sadiq a.s. amesema kuwa riziki na baraka ipo pamoja na wanawake na wale wanaowategemea. "Usemi huu unasema uhakika kuwa fani ya unyumba ni uhifadhi wa mwanamke na kwa ufanisi wao katika fani hii wanaweza kufanya mapato ya mwanamme yakafika mbali sana. "

(b) Faida ya pili

Pande zote mbili baada ya kuungana kwa ndoa inawabidi wahakikishe uendelezaji na ubakiaji hai wa binadamu. Ingawaje mzigo mkubwa uliomuhimu katika hatua hii upo juu ya mabega ya mwanamke, lakini haiwezekani shughuli hii ikafanyika kuanzia mwanzoni iwapo mwanamme hatashirikishwa.

Ni faida hii ambayo Mtume Mtukufu s.a.w.w. amesema katika Hadithi mashuhuri, "Muoe,musaidiane, mustarehe na muongeze idadi yenu."

(c) Faida ya tatu

Faida ya tatu ya ndoa ni kutimiza mahitajio ya hamu ya mwanadamu kwa njia zilizo za heshima (tusiwe kama wanyama tukaanza kutumia njia kama za mbwa n.k.).

Ingawaje watu wengi mara nyingine wanajaribu kutimiza mahitaji yao ya jinsia bila ya ndoa, lakini faida mbili zilizoelezwa hapo juu zitakuwa vigumu sana kuzitimiza bila ndoa, na wakati mwingine haiwezekani kabisa, kupata bila ya ndoa. Na kwa sababu hizi ndipo hata makabila au watu wasioendelea duniani wanatimiza ndoa hawaishi bila ndoa na wanaiheshimu sana.

Na kwa sababu kama hizi na faida kama hizi ndipo Mtume s.a.w.w. amesema: "Mtu mbaya au mtu mwenye bahati mbaya kabisa katika watu waliokufa miongoni mwenu ni yule ambaye hajaoa au hajaolewa."(Watu wengi wanasema kuwa mtu anapokufa bila kuoa au kuolewa basi hata Mwenyezi Mungu hampokei kule na katika tamaduni mbalimbali swala hili linashughulikiwa kitofauti, katika tamaduni za Wahaya mtu anapokufa bila ya kuoa au kuolewa wanamzika na mgomba ati akiwa mwanamke huo mgomba ni bwana wake na lau yeye ni mwanamke basi huo mgomba utakuwa ni mme wake kwa hivyo wanathamini sana kuoa na kuolewa lakini mazingira ya uchafuzi wa akili zetu ndizo zinazotufanya tutupilie mbali maswala ya kuoa tusiyape umuhimu, kwa sababu mafunzo ya dini tumeyaacha, mila na desturi za mababu zetu tumeziacha tumeingia katika desturi na mila za kigeni ambazo zinatupotosha ).

Hivyo labda tunaweza kuilewa Aya ya Qurani Sura Al-Baqarah 2: 187

"... Wao ni (kama) nguo kwenu, na nyinyi ni kama (nguo) kwao."

Kwa kutaja mavazi tunaelezwa madhumuni matatu yaani inapendeza, inafunika sehemu za mwili na inamuhifadhi mtu kwa baridi na joto.

Bibi na bwana kwa kuungana pamoja wanajaribu kufunika maswala madogo madogo wanayokumbana nayo, na umoja huu ndio unaowahifadhi dhidi ya magumu na matatizo ya mtu anapokuwa peke yake; "nuru ya furaha na fanaka inang'ara katika maisha yao." Na wote kwa pamoja kwa juhudi zao za pamoja wanatimiza wajibu wao kama zilivyo katika sheria za kibinadamu.