Table of Contents

Neno La Mchapishaji

Kitabu kilichoko mikononi mwako ni tarjuma ya kitabu cha Kiingereza kiitwacho, The Journey to the Light kilichoandikwa na Sayyid Abbas Noor Eddine. Sisi tumekiita, Safari ya Kuifuatia Nuru.

Kitabu hiki kinazungumzia maisha ya Imam Mahdi (a.s.) na Ughaibu wake, jinsi ulivyotokea na anavyoishi sasa katika maisha hayo ya kutoonekana. Waislamu wamehitalifiana juu ya Ughaibu wake na jinsi anavyoendelea kuishi akiwa katika Ughaibu.

Mwandishi wa kitabu hiki amejaribu kuelezea kwa lugha nyepesi juu ya hitalafu hizo, na hatimaye kwa kuonesha jinsi alivyozaliwa mpaka kuingia kwenye Ughaibu, jinsi anavyoishi Ughaibuni huko na jinsi wafuasi wake (ambao ni Waislamu) wanavyonufaika naye pamoja na kwamba yuko Ughaibuni.

Tumekiona kitabu hiki ni chenye manufaa sana, hususan wakati huu wa maendeleo makubwa ya elimu katika nyanja zote, ambapo uwongo, ngano za kale na upotoshaji wa historia ni mambo ambayo hayana nafasi tena katika akili za watu.

Kutokana na ukweli huo, Taasisi yetu ya Al-Itrah Foundation imeamua kukichapisha kitabu hiki kwa lugha ya Kiswahili kwa madhumuni yake yaleyale ya kuwahudumia Waislamu, hususan wazungumzaji wa Kiswahili.

Tunamshukuru ndugu yetu, Selemani Salum Matumula kwa kukubali kukitarjumi kitabu hiki. Vilevile tunawashukuru wale wote walioshiriki kwa njia moja au nyingine hadi kufanikisha kuchapishwa kwake.

Mchapishaji:
Al-Itrah Foundation
S. L. P. 19701
Dar-es-Salaam, Tanzania.