Table of Contents

Utangulizi

Kitabu hiki ni utambulisho mfupi juu ya mtu mkubwa sana na mwenye shakhsiya isiyofanana na mwingine aliye na siri nyingi zilizofichika na kubwa mno. Wale waliopata kumfahamu na wanaomuamini maisha yao yamebadilika kabisa, na kuna uhusiano maalum kati yao na mtukufu huyu.

Hatuwezi kujua kiwango cha mabadiliko haya kwa sifa zake na ukubwa wake, kwa sababu yanatofautiana kati ya mtu na mtu. Hata hivyo, kadiri tunavyofahamu, ni mageuzi makubwa, na mfano wake asilan usingeweza kutokea kwa mahusiano yeyote mengineyo.

Mtukufu huyu anangojewa na ulimwengu wote, na anatajwa na wafuasi wote wa dini zinazoamini kwamba Mwenyezi Mungu ni Mmoja kwa majina mbalimbali. Waislamu humuita Mtukufu huyu kama “Al–Mahdi” (a.s), na baadhi yao wanalijua jina lake kamili na mambo mengi kuhusiana na yeye.

Waislamu Mashi’a wanafahamu kwamba ni Imam Muhammad bin Al- Hasan” (a.s). Walikuwa wakiieneza siri hii (ya jina lake sahihi) miongoni mwao wenyewe, wakikataza kuitangaza siri kwa hofu ya kuhatarisha maisha ya mwenye jina hili. Na wakati walipokuwa na uhakika kwamba hakuna hatari yoyote ambayo ingeweza kumpata waliruhusu na kuanza kulieneza bila woga au hofu ya kukamatwa kwake.

Mtukufu huyu ndiye yupi basi, ambaye idadi kubwa sana ya watu, wanaozidi milioni mia moja, wanaunganishwa na yeye, kiasi kwamba wamenasibishwa na jina lake na wanatambulika kwa jina hilo? Mashi’a hususan hujulikana kama Shi’a Imamia,” jina linalotokana na huyu Imam.

Ni vipi mataifa mengine yalipata kuwa na uhusiano na Mtukufu huyu, na vipi wamekuwa wakimzungumzia? Kwa nini jina lake limefichuliwa na kwa nini siri nyingi zinazohusiana na yeye zimefichuliwa, hususan kwa Mashi’a peke yao tu? Na kwa nini Mashi’a wamekuwa wakijiamini sana na hata kuwa na ari ya kuutangaza ujumbe huu kwa mataifa yote ya Ulimwengu?

Maswali haya ya kuvutia yatajibiwa ndani ya kurasa za kitabu hiki pamoja na maswali mengine ambayo yatatokeza kadri tutakapokuwa tukiendelea.

Na ni kwa vile Mashi’a ndio ambao wanamtaja mtu huyu wa ajabu mara kwa mara, na wakiwa na mambo mengi zaidi kwa undani kuhusiana naye, tutaanza na wao ili tuweze kuyatolea ufumbuzi maswali haya.
Kama maswali haya yataachwa bila ya majibu ya kutosheleza, wale ambao wanafanya utafiti ili waupate ukweli watakuwa wamewekwa katika hali ambayo watakuwa hawajui wafanye nini, kwa kutopewa fursa muhimu ya kubadili maisha yao kuwa bora zaidi, maisha yaliyo na mengi yanayopendeza na mengi yanayovutia.

Nimeshawahi kupata kuwaona baadhi ya hawa Mashi’a ambao wanamfa- hamu vyema mtukufu huyu, na wamekuwa na uhusiano wa karibu zaidi na yeye.

Nimeshayaona maisha yao yakiwa yamejaa mno matumaini huku wakiwa ni wenye kusubiria hiyo siku itakapofika, wakiwa hawajakata tamaa, wala hawana hofu wala kufadhaishwa na maisha ya kipuuzi, zaidi ya matumaini hayo makubwa. Nimewaona watu hawa wana ari na ushujaa.

Nimepata kuwajua watu ambao mfano wake haupatikani popote pale ulimwenguni. Ingawa watu wengi kutoka mataifa mbalimbali humtaja Mtukufu huyu na humuamini, maisha yao hayajabadilika na sijaona chochote kwao kama ambavyo nimeona kwa Mashi’a. Siri ya jambo hili, na siri yote hii hasa ni habari zenye maelezo kwa undani zaidi.

Ni vipi Mashi’a walikuja kumfahamu Imam Mahdi (a.s)? Je, wengine walikuja kumfahamu?
Katika namna ambayo walivyomfahamu Imam Mahdi (a.s), Mashi’a wamegawanyika katika sehemu mbili:

Kundi la Kwanza: Waliomfahamu Imam baada ya kupita njia ndefu katika kupata elimu. Walimjua mwanzoni ambapo palikuwa na masuala mengi yaliyowaongoza wakamfahamu. Kwa sababu waliishi katika mazingira na mahali ambapo palikuwa na habari nyingi za kweli, na moja kwa moja wakatokea kumwamini Imam.

Wakazifahamu sifa zake njema, lengo na makusudio ya kazi yake anayoitekeleza na atakayoitekeleza, wadhifa wake na wajibu katika maisha yetu kwake.

Kundi la Pili: Ni wale ambao waliuona ukweli wa mambo yanayotokea hapa ulimwenguni. Walishuhudia dhuluma za kutisha, maafa ya kutisha, ubadhilifu, uongo na kutawaliwa kwa mabavu kwa wanyonge na wenye nguvu, kwa sababu walikuwa ni watu wenye hisia na waliweza kuhisi hali ya madhila na shida wazipatazo watu, hivyo walikuwa wakifanya utafiti wapate wokovu kuokoka na jinsi ya kuzuia haya madhila ambayo yalikuwa yakiwapeleka binadamu kuelekea mwisho mbaya.

Kutokana na hisia zao kubwa na jitihada zao njema walizokuwa nazo, ziliwaongoza kutambua kwamba upo mpango maalum unaotoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kuuokoa ulimwengu dhidi ya dhulma na ukandamizaji na baadae kuleta haki na amani. Jambo hili halikukawia sana kulitambua, kwani imani yao kwa Allah (s.w.t) iliwaongoza kuufahamu mpango huu.

Kama Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehma, katika kipindi chote cha maelfu ya miaka katika historia ya mwanadamu Aliwatuma watu waje kuwaokoa wanadamu, vipi asifanye hivyo tena? Je, huruma Yake imeisha? Au neema zake zimetoweka? Au je, hawezi kufanya chochote?

Maadam Mwingi wa Rehema, Mkarimu, Mwenye Nguvu Allah (s.w.t) ambaye Huruma Zake zisizo na kikomo na Ukarimu wake usiokwisha, na ambaye Ayafanyayo hayazuiliki, Yu Hai, Yu Mjuzi wa yatendekayo, Yu Aona na Yu Asikia, na Uumbaji Wake wanadamu kila siku ni uthibitisho juu ya hili, na ni alama ya wazi ya ukarimu Wake, na ni kutokakana na imani hii juu ya uumbaji Wake kwamba upo Mpango, ambao utekelezaji wake unangojewa.

Mtu Mtukufu, yaani mwanadamu aliye karibu zaidi na Mola wake, yaani Imam ambaye ndiye mwenye Mpango huu wa Mwenyezi Mungu Mwenye Huruma, hakika naye vilevile yu hai. Ama sivyo, Mwenyezi Mungu ana uwezo kwa wepesi mno kuumalizia mbali msiba huu kwa kuyasitisha maisha ya hapa duniani.

Je, Yuko Wapi Sasa?

Hapa kundi la kwanza walijaribu kujibu swali hili na kutueleza juu ya namna ya kumjua na kumtambua, kwa jina lake, kwa sifa zake na umbile lake!
Yeyote anayekulia na kulelewa katika mazingira ya wafuasi halisi wa madhehebu ya Shi’a, kwani kuna watu wengi wanajiita Mashi’a lakini hawajui chochote juu ya Ushi’a, na kukaa karibu na wanazuoni huweza kumfahamu Bwana Mlezi wa Ulimwengu (swt) ambaye wote humuabudu kwa namna ya kushangaza siku zote.

Zipo hadithi nyingi za Kishi’a zinazomhusu ambazo ni nzuri mno, zina- zoelezea namna Mwenyezi Mungu (s.w.t), anavyowatendea viumbe wake, na jinsi anavyohusiana nao, katika namna ambayo maarifa yanayopatikana kutokana na hadithi hizo, pamoja na hazina kubwa ya kisayansi ya Kiislamu humfanya mtu aweze kumaizi mambo yaliyofichika katika uhai na siri zake, kimahusiano na mfuatano, bila ukinzani wala kasoro.

Binadamu anapendwa na kuthaminiwa na Allah (s.w.t). Mapenzi ambayo yapo kati ya Allah (s.w.t) na viumbe wake ni jambo lisiloweza kuelezeka kwa maneno matupu. Mwenyezi Mungu (s.w.t), ameumba kila kitu kwa ajili ya binadamu, na Yeye atafanya lolote lile ili amuongoze, amuokoe, na kumfanya afikie kikomo cha furaha kubwa kabisa na ukamilifu.

Chochote kile kilichopo hapa ulimwenguni ni kutokana na kazi ya Allah (s.w.t) isipokuwa uovu ambao umefanywa na watu waovu na madhalimuna yote ayafanyayo Allah (s.w.t) ni kwa ajili ya maslahi ya huyu huyu mwanadamu.

Ingawa hatufahamu ni vitu vingapi vinavyoishi, na ni vitu vingapi vinavyotokea hapa Ulimwenguni, dunia hii imeumbwa katika namna ambayo kila chembe ina hisia za mapenzi kwa kiumbe huyu, na hutaka kumtumikia, na kumfanya awe mwenye furaha.

Hatujui ukweli wowote juu ya ndege anayelia kwenye tawi la mti bustanini kwetu kwamba humwomba Mola atusamehe dhambi zetu na kutupa Rehema na Baraka juu yetu. Allah (s.w.t) amemuumba kwa ajili ya kutuombea sisi Kwake.

Je, na vipi kuhusu miti na majani yake, majani ya ardhini na mimea yake na kila jabali na jiwe, na kila mlima na sayari? Akili hutulia unaposikia ukweli huu na moyo hujawa furaha unaposimuliwa hadithi hizo.

Mola wa Ulimwengu ni Mwingi wa Rehema na Mwenye Haki, Huongoza viumbe wake na humshika mkono yeyote yule atakaye uongozi na ambaye amechagua njia ya wokovu.

Huwatuma wajumbe wake wakiwa kama Mitume wake ambao hutoa mafunzo ya dini na kuonya, wakiwa na amri zitokazo Mbinguni na kutangaza mwongozo wa Allah na kueneza sheria za Mwenyezi Mungu ambaye ni Mmoja.

Hata kama Mitume watauawa, Rehema Yake haiishi asilan. Utoaji toka Kwake huendelea, na ule mstari wa Rehema ambao hukizunguka kila kitu baina ya mbingu na ardhi utaendelea kuwepo.

Ingawa Utume ulishafungwa na Bwana wa viumbe na Mbora Kabisa wa Mitume Muhammad ibn Abdillah (amani iwe juu yake na Aali zake), hii haina maana kwamba Rehema za Allah zitakwisha.

Mpango wa wokovu wa Ulimwengu, Utawala wa Mwenyezi Mungu na urithi na kuchukuliwa kwa dunia hii na wachamungu, ushindi wa wanyonge kushindwa kabisa kwa madhalimu, yote haya ni ahadi za Mola Mwenye Nguvu ambaye havunji ahadi yake asilan.

Hivyo, Mpango huu bado upo. Mwenyezi Mungu Allah (s.w.t) anasema katika Qur’ani:

قُلْ فَانْتَظِرُوا إِنِّي مَعَكُمْ مِنَ الْمُنْتَظِرِينَ {102}

“Sema (ewe Mtume wetu Muhammad): Subirini, hakika Mimi nipo pamoja na wenye kusubiri” (Qur’ani: 10:102).

Wanazuoni wa Kishi’a wametaja katika vitabu vyao kazi kubwa ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w) kwamba ilikuwa ni kuongoza watu, kuhifadhi Qur’ani na kuzuia kuifanyia mabadiliko na kuipoteza (ikiwa ndio Mwongozo wa maisha na Mpango wa kuleta mabadiliko), na majukumu haya yalihamishiwa kwa Maimamu Ma’asumu (amani iwe juu yao) baada ya kifo chake.

Na ili watu wasipotoke kwa kutowafuata wao, kama kweli walikuwa wanautafuta mwongozo, Mtume (s.a.w.w) aliwatajia majina yao na kuzitaja sifa zao. Maimamu kwa upande wao waliubainisha mpango huu kwa ufasaha, na walionyesha njia ya wokovu, huku wakiyataja mambo ya lazima ya kuzingatia.

Moja kati ya mambo ya muhimu ya Mpango huu ilikuwa ni kumtambulisha kiongozi wake, Msimamizi wa utekelezaji wake na mwenye kuhakikisha kwamba unaendelea kuwepo kama inavyotakiwa, ili uweze kukabidhiwa kwa kizazi ambacho kitakuja kutokea na kuutumia kwa ukamilifu kabisa ulimwenguni pote wakiwa pamoja na Imam.

Hili litatokea katika siku na muda aujuao Mwenyezi Mungu - Allah (s.w.t) tu peke yake.

Basi Kwa Nini Mashi’a Wa Kweli Wana Matumaini, Uhai Na Nguvu?

Ni kwa sababu tu hawakuridhishwa kwa kuona tu misiba ya hapa Ulimwenguni, na kulia kwa kutoa machozi na kuonyesha huzuni na simanzi. Katika hali hii hii ya vurugu, na kutokana na wingi na undani wa matukio haya maovu, waliweza kutambua kuwepo kwa Allah (s.w.t).

Allah (s.w.t) ambaye Yu-Kila Mahali ndiye Yeye ambaye anadhibiti kila kitu na hakuna chochote kinachotokea bali huwa ni kutokana na Mapenzi Yake na Hekima zake katika kuyaendesha mambo ya Ulimwengu na kuon- goza na kuwaokoa waumini.

Hivyo ni namna gani ambavyo sisi tunadhani hali ya mtu itakavyokuwa, ambaye amejifunza yote haya, na vile vile jinsi ambavyo rehema itakayoletwa na kuwafikia wote, na jinsi Allah (s.w.t) atakavyouondoa uovu kutoka hapa ulimwenguni.

Zaidi ya hapo, yule ambaye amejifunza, ikiwa ni pamoja na Mpango wa wokovu, sababu za kutokea kwa udhalimu na ufisadi, na sababu za kuendelea kwa huzuni na majonzi; baada ya kuyaona yote haya pamoja na habari sahihi, kwa uwazi kabisa na kwa undani, huwezesha kuipa mwanga na kuifungua njia yake na kumuita aweze kushiriki katika kuunusuru ulimwengu, kuuokoa na kuzitokomeza huzuni na machungu yake.

Lakini si wito tu; bali ni uteuzi katika nafasi hii na ni jukumu la kuwaita pamoja wale wote ambao wameuitikia wito huu.

Hivyo, Mashi’a huzihusisha imani zao juu ya Allah (s.w.t) na vile wanavyoyaelewa yale yanayotokea Ulimwenguni, yaani, hivyo ni kusema kwam- ba ni baina ya mambo yanayoonekana na yasiyoonekana (al-ghaib wa al-shahada), kati ya roho na vinavyoonekana (al-ruh wa al-dhahir) na kati ya moyo na matendo (al-qalb wa al-amal).

Kwao, imani kwa Allah (s.w.t) sio tu hisia za moyoni bali ni kuendelea kutafiti kuwepo kwa Allah (s.w.t) katika kila uwanja wa maisha yao na kuweza kupata kuifahamu Hekima Yake, Ayatendayo na namna anavy- ouendesha Ulimwengu.

Hawatenganishi hali ya kila siku na imani yao juu ya Allah; hivyo ndio kusema, wanaishi katika maisha yao wakiwa wanafahamu fika kuwa hivyo ndivyo Allah (s.w.t) anawataka wao waishi.

Hawadanganyani wala hawawadanganyi wengine kwa kujiamulia wao wenyewe kwamba yupi ni mwadilifu na yupi si mwadilifu.

Mizani wanayotumia ni Allah (s.w.t) ambaye kwao hayupo mbinguni tu basi. Kwa sababu hii wameamua mara moja kufuata tabia ambayo inalingana na mani yao na uhusiano wao na Allah (s.w.t).

Hivyo yeyote yule ambaye ni adui wa Allah (s.w.t) kwao pia ni adui yao, na yeyote yule amtakaye Allah (s.w.t) yu pamoja nao. Hivi ndivyo namna walivyopata kumjua Imam (a.s) na kumfuata na kuungana na Mpango wake.

Imam haonekani hivyo huwezi kupata hisia za kuwepo kwake; mtu hawezi kumuamini mpaka awe na imani juu ya yale yasiyoonekana.

Imam ni Uadilifu wa daraja ya juu kabisa; mtu hawezi kumuamini mpaka awe hana imani juu ya watawala madhalimu na kuacha dhuluma.

Imam ni Rehma ya upeo wa juu kabisa, mtu hawezi kumuamini mpaka ndani ya nyoyo zao ziwe hai kwa mapenzi juu ya wanaodhulumiwa na wenye shida.

Hii ndiyo habari ya Mashi’a na Imam Al-Mahdi (a.s) ambayo ni sehemu ya siri ya uhusiano wao uliopo na kushiriki kwao katika Mpango wake.

Hata hivyo ……

Endapo mtu anajifanya anamuamini Allah (s.w.t) lakini hafanyi utafiti wa kumjua alipo katika maisha yake ….

Endapo mtu anajifaharisha kwa kumpenda Allah na bado akawa haonyeshi huruma juu ya wanaodhulumiwa na wenye shida………..

Wakati mtu anajua ghadhabu za Allah juu ya madhalimu na bado akawa kimya kwa vitendo vyao wanavyovifanya……………….

Ndipo hapo bila ya kujali kwa kiasi gani anajifanya na anadai anapenda kumpenda Mwokozi na kutangaza na kumlilia, hataweza kumfikia wala kumjua wala kuwemo katika Mpango wake.

Mwokozi huyu si masimulizi ya habari ya mtu ya kihistoria au utabiri wa mambo yajayo; yeye ni mkubwa zaidi ya hapo na mtukufu wa daraja la juu zaidi kuliko hivyo, pamoja na kwamba ametajwa katika historia na amekuwa ni utabiri wa hapo baadaye.

Yeye ndiye aliye na Mpango, Majukumu na Lengo…………..

Yeye ndiye Mwadilifu wa upeo wa juu kabisa ambaye hatafanya mkataba wa amani na madhalimu.

Je, Ni Kwa Nini Siri Hii Imefichuliwa?

Tutasoma juu ya maisha ya Imam Mahdi (a.s) kwanza kabisa juu ya jinsi alivyozaliwa ambapo itatukumbusha alivyozaliwa Nabii Musa (a.s) ambapo Allah (s.w.t) alimficha ili Firauni na askari wake wasimuone.

Ni hadithi inayofanana… kwani kila baada ya dhuluma ya madhalimu kukikithiri, na watu kukata tamaa ya kutafuta ufumbuzi wao wenyewe, huwa na tamaa ambayo huwarudisha katika dini ili watafute njia ya wokovu. Hali hii ina athari kubwa katika kuhuisha suala la Imam Mahdi (a.s) kwa uwanja mpana zaidi baada ya kuwepo kwa watu wachache tu hapo kabla.

Watawala wa wakati huo kabla ya kuzaliwa Imam Mahdi (a.s) walielewa kuwa jambo hili ni la kweli na kwamba limeshaanza kuonesha tishio kali kwao kwa sababu tu ya hamu ya watu kwa ajili ya muundo mbadala wa utawala, vyovyote utakavyokuwa, utahatarisha ufalme wao. Kwani ni nini kama watu walichokuwa na hamu nacho ni Matumaini, Mwokozi, Uadilifu na Uislamu wa kweli!

Ndipo hapo kazi kubwa ya kutafuta kumtambua yule ambaye angeweza kuwa ndiye Imam, hata kama hawakumuamini. Hali ya watu kumsubiri mtu yeyote awaye yule ili awaongoze, kwa mtazamo wa watawala ulichukuliwa kuwa ni tishio kubwa kwa maslahi ya wafalme ambao wao aliupora utawala uliokuwa unapaswa kuwa ni wa Waislamu.
Baada ya kufanya upelelezi mbalimbali na uchunguzi iliwathibitikia kwamba tishio lingetokea kutoka kwa mtu atakayezaliwa kutoka katika nyumba ya Mtume (s.a.w.w.), aidha, waligundua kwamba kulikuwa na harakati za dhati hasa za watu katika kumfuata.

Kutokana na upelelezi wao huo unaoendelea, waliweza kuthibitisha lengo halisi. Hivyo walimfunga Imam Ali al Hadi (a.s) babu yake Imam al-Mahdi (a.s) na Imam Hasan al-Askari (as) baba yake Imam Al-Mahid. Hata hivyo, Allah (s.w.t) aliwaficha kuzaliwa kwa Imam mwenye kusubiriwa, kama vile ambavyo aliwaficha kwa Nabii Musa (a.s).

Katika kipindi hiki cha kuendelea kufuatia, ilikuwa ni kwa wale Mashi’a ambao waliifahamu siri hii wakalificha kabisa jina la Imam, ama sivyo maisha yake yangekuwa hatarini zaidi. Watawala wa wakati huo walijua kwamba Imam atatokea kutokana na watu wa nyumba hii, lakini hawakuweza kwa usahihi kuamua kwamba atakuwa ni nani.

Kwa maneno mengine, walijua kwamba kuna mtu ambaye anatarajiwa na watu kwamba atazaliwa, na iliwezekana kwamba wangeweza kumtangaza kwamba ndiye mwokozi na kiongozi wa Waislamu kutokana na amri ya Mtume (s.a.w.w).

Kufichwa kwa siri hii ilikuwa hakuna budi kwa vitisho hivi halisi. Uwekaji wa usiri huu na kufichwa huku kuliendelea kutoka kwenye ghaibu ya kimaajabu ya Imam mpaka kutokeza kwa waumini kumekuwa na uhakika kwamba hakuna madhara yatakayompata, kiasi kwamba suala la ulinzi wake linakuwa kitu kilichofichika sana.

Akatoweka machoni pa watu katika namna ambayo hakuna yeyote ambaye angeweza kumfikia.

Imefahamika kwa Mashi’a kuanzia sasa na kuendelea kutafuta sababu za kutoweka kwake, ambako kumekuwa kwa muda mrefu… katika wakati huu, suala la mwokozi kidogo kidogo likaanza kufifia, na likawa ni matumaini tu yaliyomo mioyoni mwa watu. Ashi’a wakagundua kwamba ghaiba ya Imam Mahdi (a.s) ya namna hii ni kutokana na ukosefu wa watu wanaomfuata.

Kama Imam alitaka kuutekeleza Mpango wake mkubwa ambao anao, basi angehitaji wafuasi. Wafuasi wake lazima wawe na tabia na sifa maalumu ambazo zingewawezesha kuutekeleza Mpango kwa uaminifu wa kiwango cha juu kabisa. Ni Mpango wa muda mrefu na ni mgumu kabisa, na suala hilo lahitaji watu imara kabisa, waadilifu kweli kweli.

Inasemekana kuwa, moja ya sababu za kutoonekana kwake ni watu kutofikia hali ya kuwa tayari katika kiwango kinachohitajika ili kuhimili na kuivumilia Serikali yake, ambayo ni ya haki tupu.

Hivyo, ni muhimu kuandaa mazingira yanayofaa kwa ajili ya kuja kwake, na kuyaweka mataifa katika hali ya kuwa kweli wanaihitaji Serikali hiyo.

Vipengele vyote hivi vikafanya utaratibu wa kutangaza kuhusu Imam na kuwajulisha watu haiba na ukweli wake kuwa ni suala lenye kuhitajika sana na muhimu kabisa, kwa sababu kurejesha matumaini mioyoni mwa watu kunahitaji uthibitisho wa kweli ambao hauwezi kupatikana kwa maelezo ya juu juu na visa vya kufikirika tu.

Kwa hiyo, wanachuoni walianza kutafuta hadithi zinazomhusu Mahdi (a.s) anayengojewa na mpango wake. Walizikusanya na wakaanza kuzisambaza kwa watu, na hivyo likawa suala lililotangazika na kuaminiwa na wale ambao wanazifahamu hadithi nyingi ambazo zimesimuliwa na Mtume na Ahlul Bayt (a. s).

Lengo Kuu La Imam Al-Mahdi (A.S)

Kama ambavyo ulivyo Mpango wa Imam Mahdi (a.t.f.s) ni Uislamu, Malengo yake vilevile ni malengo ya Uislam, na hapa ingefaa kuyaweka wazi malengo haya:

Hapana shaka kwamba Uislamu ni Mpango na sheria ya Allah (s.w.t). Allah (s.w.t) amewaumba wanadamu ili wawe na furaha, na kuufikia kamilifu wa furaha kubwa kabisa katika maisha yao yote.
Hivyo vipi furaha hii inaweza kufikiwa na ni utaratibu upi katika Uislamu ufuatwe ili kuweza kuipata furaha hii?

Furaha ya mwanadamu ipo katika kuufikia ukamilifu wa daraja la juu kabisa. Ukamilifu huu umekusudiwa na kutaraijwa katika maisha yao yote, na chochote kile zaidi ya hilo hakina maana yoyote. Binadamu atahusiana na chochote ambacho kinamwakilisha yeye katika ukamilifu huu, au iwe ni njia ya kupitia ili kuupata ukamilifu huo.

Kwa upande mwingine mwanadamu huyu hukikataa chochote kile ambacho huwa ni kikwazo kwake katika njia ya kuweza kuufikia ukamilifu huu. Hivyo chochote kile ambacho kinakuwa ni kikwazo, bila kujali kitakuwa karibu kiasi gani, kitachukiwa na kukataliwa.

Lengo kubwa la Uislamu ni kuuelezea ukamilifu huu na kuufichua uwongo na upotofu uliofikia kiwango cha juu kabisa. Binadamu wanaweza kuwa na uhusiano kama vile ambavyo watu wengi walivyo, na vitu ambavyo wanadhani ni vya ukamilifu. Hivyo fikra za mtu huyu lazima zielekezwe na kuongozwa ili kuufikia ukamilifu halisi.

Sehemu muhimu sana ya mafunzo ya Uislamu yanazunguka katika uwanja huu, na hicho ndicho sisi tunakiita ilmu ya kiroho (ma’rifa) na kutam- bua (wa’i). Uislamu haujaridhika na kuelezea ukweli tu, bali huweka wazi sababu za upotofu huu na jinsi watu wanavyoifikia hali hii mbaya kabisa.

Uislamu unatoa mpango wa kuwaokoa na kuwalinda kutokana na uongo huu, wakati karibu wanadamu wote kwa muda wote wamepotoshwa na fikra hizi potofu, si hivyo tu bali unautukuza mpango wake kwa kutoa miongozo ya jinsi ya kuufikia ukamilifu halisi na kuulinda.

Ni kweli kwamba mwanadamu kama mtu binafsi yupo katikati ya mpango huu, na kwamba kila mwanadamu anawajibika kwa ajili yake mwenyewe. Hata hivyo, jamii na watu wanaomzunguuka kwa kiasi fulani ni sehemu yake, kama ambavyo kuna msemo usemao kwamba, “Jamii ni kipengele kimoja cha mtu.” Au kipengele muhimu cha shakhsiya yake.

Hivyo kama mtu anawaacha wengine na hawajali basi atashindwa na atapata taabu sana. Anaweza hata asipate ukamilifu unaotakiwa na furaha kubwa ya kweli.

Jamii si idadi ya watu tu, au watu ambao tunahusiana nao tu, bali ni mfumo wa kiutawala, desturi na sheria, mfumo ambao jamii imo ndani yake, na kwa msingi huu, mahusiano yanajengwa na watu na watu wanashirikiana.

Mtawala au kiongozi wa jamii hufanya kazi ya kuweka na kulinda mfumo huu. Kwa sababu mfumo huhakikisha kwamba maslahi yake yanalindwa, yeye atakuwa ndiye mlinzi mkubwa kabisa. Atakuwa yupo tayari kuuwa na kuyatokomeza makundi ya watu endapo atawatilia shaka kwamba wanakwenda kinyume na mfumo wake!

Mtawala huyo, ambaye huitwa dhalimu atawaongoza wale wote ambao huukubali mfumo wake motoni kwenye Adhabu ya Akhera. Dhalimu ni adui wa Allah (s.w.t) na humwakilisha Shetani hapa duniani.

Watu hawawezi kujitenga na athari za mfumo huu wa utawala ambao wanaishi humo, na kuukubali mfumo wa maisha na kuishi kulingana na mfumo huo, maisha yao yatabadilika na kuwa maisha ya kidhalimu, maisha yenye uadui dhidi ya Allah (s.w.t ). Ni juu yao, na ni muhimu sana kuukataa mfumo huu. Kukataa huanzia ndani ya moyo, akilini na katika imani.

Katika hali fulani wakati mwingine haiwezekani kufanya chochote kwa kutokana na kuikataa hali hii; hata hivyo, kukataa kwa moyo kwabakia kuwa sehemu muhimu ili kumfungulia mtu milango iwe wazi mbele yake, na kumwekea njia iliyo wazi ili aweze kuufikia ukweli.

Endapo watu hawataweza kurekebisha hali hii, hata kama ni kwa kiwango cha imani na kwa moyoni, basi hawataweza kufanikiwa katika kurekebisha sehemu nyingine za shakhsia zao, na hivyo vikwazo vitabaki, vya kuwazuia wasiufikie ukamilifu.

Kwa hiyo, wanayo dhima kubwa kwa jamii, kwa maana ya kwamba dhima juu ya mfumo, na dhima juu ya wawakilishi wake wanaotenda kazi zao ili kuulinda mfumo huo.

Mfumo wa kidhalimu ambao upo kwa ajili ya kulinda maslahi ya mtawala – ama mtawala huyu awe mtu mmoja au kikundi cha watawala – ni mfumo wa kikatili, ambao huwadhulumu watu haki zao na kwa namna hii unawatawala watu na kuwafanya watumwa kwa kutumia hila mbalimbali.

Si kama ulivyokuwa utumwa wa hapo siku za nyuma huko Marekani kwa Waafrika; bali umebadilishwa na kuwa wa kisasa zaidi, uliojificha zaidi na wenye uovu zaidi.

Mfumo wa kisasa wa Utumwa upo katika kuhodhi uchumi, ambapo mtumwa anaonekana ana uhuru wa kufanya chochote apendacho, lakini ukweli ni kwamba hali yake ya kiuchumi imedhibitiwa barabara kabisa, na vile vile amedhibitiwa barabara kabisa na mfumo unaotawala uchumi.

Anachokula, asome wapi na asome nini, vipi apate pesa na vipi azitumie, afikirie vipi, ampigie kura kumchagua nani, yote haya yamepangwa kabla kwa makusudi kwa ajili yake, na yote haya ni kwa kisingizio cha uhuru na uhuru wa kuchagua.

Watu wachache sana wanaweza kuimaizi hali hii ya sasa ya utumwa. Dhalimu haishii hapa, kwani atazitafuta kanuni za ukweli na za haki na wale ambao wangeweza kuzitetea kutishia maslahi yake. Kwa hiyo ata- jaribu kuzivunjavunja hizi kanuni, hii ndio kusema kwamba atayaondoa yale katika yaliyobaki katika kulinda utu na furaha ya mwanadamu, na kuwaangamiza wale wanautetea ukweli.

Haiwezekani kumpata mtawala dhalimu anayeukubali ukweli. Ni upuuzi mtupu kudhani kwamba mtawala dhalimu angeweza kuishi kwa kufuata kanuni za maisha ya kibinadamu. Ni ujinga mkubwa kabisa na ni kiwango cha juu kabisa cha kukosa mazingatio!

Ni Wapi Yalipo Maadili Ya Hali Ya Juu Ya Mwanadamu, Na Ni Nani Ambaye Huudhihirisha Ukweli, Na Kuwafanya Watu Kuielewa Bayana Hali Yao Waliyo Nayo?

Kwa urahisi mno kabisa ni Uislamu ambao unaweza kufanya hivyo; dini ya Allah (s.w.t) na ujumbe Wake ambao umekuja kuwaokoa wanaodhulumiwa na wanaoteswa, wanaofadhaishwa na wanaonyonywa. Maadili yote na ukweli utapatikana kutokana na huduma ya wale ambao wamejitolea wenyewe kutoka kwenye minyororo ya mtawala dhalimu na mfumo wake.

Mtawala Dhalimu Anachofanya Tu Ni Kuufunika Na Kuuficha Ukweli.

Mtawala dhalimu anachofanya ni kuharibu tu maadili (hayo) ya hali ya juu na kuwapotosha wafuasi wake. Katika kivuli cha mazingira haya inawezekana kabisa kwa mtu kuungana na chanzo cha Nuru, Uongozi, Maadili na Ukweli. Mtu kwanza na kabisa huhitaji kuuacha huu mfumo hata kama ni kwa moyoni tu. Hata hivyo, uhuru kamili ndiyo njia pekee ya kupata wokovu wa mwanadamu.

Wamekosea wale wanaodhani kwamba unyoofu wa hali ya juu na maadili ya kiroho ya Kiislamu yanapatikana kwa wale ambao hujisalimisha mbele ya madhalimu na kuwakubali.

Wanajidanganya wale ambao hufikiria kwamba Swala na amali nyingine kubwa kubwa za kiibada zitakuwa na manufaa wakiwa chini ya utawala wa wakandamizaji.

Kwa hiyo tunaweza tukayatambua malengo ya Uislamu: Lengo kuu kabisa ni kuipata furaha ya mwanadamu.

Na furaha hii imo katika kupata aina zote za ukamilifu. Ili kulifikia lengo hili vikwazo vyote lazima viondoshwe Kikwazo kikubwa kabisa na cha hatari zaidi ni kuwadhulumu watu.

Mtawala dhalimu ni yule ambaye anaulinda mfumo wa kidhalimu na kuuimarisha, na zaidi ya hapo huwaongoza watu wake katika kuifanya dhulma hiyo.

Tunapoitumia nadharia hii iliyo dhahiri na rahisi katika kuupata ukweli ndiyo tunakuja kuyafahamu kwa wepesi malengo ya Imamu Mahdi (a.s). Pia tunakuja kujua siri ya kutoafikiana kati ya wale wanaoamini juu ya malengo yake.

Baadhi ya wanaomuamini hutilia maanani kipengele cha kiroho na unyofu katika kungojea kurejea kwake, na humchukulia yeye kuwa ni kiongozi wa kiroho ambaye atawachukua na kuwafikisha katika kilele cha ukamilifu wa kiroho.

Wengine huangalia juu ya jukumu lake kubwa katika kuwafundisha watu na kueneza maarifa na hekima ulimwenguni. Wengine humuona kama ni kiongozi mkubwa wa majeshi ambayo yataangamiza viti vya enzi vya tawala dhalimu na mifumo ya kidhalimu na ubadhirifu.

Wote hawa wapo sahihi, hata hivyo mawazo yao lazima yaongozwe ili kuweka wazi picha halisi. Upinzani dhidi ya dhulma ni hatua ya mwanzo kuufikia ukamilifu wa kiroho, uongozi na imani. Ni katika imani na ucha- ji (Mungu), maarifa yatazidi kukua na matawi yake mazuri yataendelea kumea.

Si ujumbe wa mapinduzi tu ambao Imam Al-Mahdi (a.s) ameubeba, bali anataka kuitoharisha ardhi kutokana na madhalimu na kuwazuia wasifanye ubadhirifu na kuuvuruga ulimwengu, kwa lengo la kupata mazingira yanayotakiwa ili kuwakamilisha wanadamu katika mambo yote ili waweze kuipata furaha ambayo wanaitafuta.

Maarifa haya yana umuhimu sana kwa maisha yetu… Kwa nini? Kwa sababu tunaamini kwamba Imam (a.s) tangu kilipoanza kipindi cha ghaiba yake alikuwa akiandaa mazingira yanayofaa kwa ajili ya kipindi atakapokuja kurejea na kufanya maandalizi ya kuumalizia Mpango wake ambao ulikuwa ndiyo ndoto ya Mitume (a.s) tangu hapo mwanzo wa wakati.

Je, Na Hii Itakuwaje?

Ni rahisi sana, maadam tumekwisha yafahamu malengo yake, basi tunaweza kuwajua wale waendao sawa sawa kufuatana na mpango wake huu mtukufu.

Maadam tunataka tuwe miongoni mwa wale ambao wanaandaa mazingira mazuri ya kurejea kwake kuliko na baraka na tuna imani juu ya umuhimu wa kumsaidia, basi hakika tutaungana na msafara wa wale ambao wanamuandalia arejee na hatutaingia katika mtego wa wanafiki na waongo.

Angalia jinsi gani ambavyo hisia zetu juu ya malengo ya Uislamu zinatuleta moja kwa moja kufika mahali ambapo tunapaswa tuwepo.

Kama tunamjua adui mkubwa kabisa na mwenye hatari zaidi ni mtawala dhalimu, hapo ndipo tutaweza kujua maadui zake na wale ambao watakuwa ni wasaidizi wa Imam na wanyoofu.

Hivi ndivyo jinsi tunavyojua hatua ya kwanza ya kumfuata Imam, na kama tutachukua hatua hii tutakuwa ni miongoni mwa wale ambao kwa hakika wanamngojea Imam, wakisubiri wokovu wetu wa kweli.

Wasioamini Kuwepo Kwa Imam Al - Mahdi (A.S)

Tunafahamu kwamba wale ambao hawauamini ukweli, kwa vyovyote uwavyo, wapo katika makundi mawili:

Kundi la kwanza: Ni kinzani na lenye kukanusha, wanaufahamu ukweli, lakini hawataki kuukubali kwa sababu utawaletea hasara kwenye maslahi na manufaa yao.

Kundi hili limekuwepo siku zote na bado lipo. Kukabiliana na watu wa aina hii kwa kutumia hoja na ushawishi hauna faida yoyote; bali ingelikuwa si busara kufikiria kuwa hoja hizo zingeweza kuleta matokeo mazuri.

Kundi la pili: Hukanusha ukweli kwa sababu wana mashaka na wamedan- ganyika, wakidhani uongo ndio ukweli, ambao huwazuia wao kutoufikia kweli.
Makundi yote haya mawili hayaamini kuwepo kwa Imam Al–Mahdi (a.s). Baadhi ya watu wanafahamu kutokana na hadithi za Mtume (s.a.w.w.) zilizosimuliwa kwao kwamba atakuja kuishi mjukuu wa Mtume (s.a.w.w) na jina lake ni Imam Al–Mahdi (a.s), na kwamba atatokea katika kipindi cha mwisho wa dunia ili kuujaza ulimwengu usawa na haki baada ya kuwa umeshajazwa dhuluma na uonevu.

Lakini watu hawa hufikiri kwamba kwa kuuonyesha ukweli huu utavuta nadhari ya watu kuwaelekea wasaidizi wa kweli wa Imam, na kusababisha wao kuwaacha. Kwa hiyo, huzificha hadithi hizi na hawazisambazi kwa wafuasi wao.

Kundi jingine la watu hudai kwamba wanaamini kuwepo kwa Imam (a.s) lakini wanakataa kabisa kuzungumzia wazi wazi juu ya jukumu lake na malengo yake, kwa sababu hii itawaongoza watu waweze kuwa wasaidizi wake wa kweli, kitu ambacho kitaharibu maslahi yao, kwani wao hupata fedha na manufaa mengine mengi kutoka kwa wafuasi wao. Hivyo kama wafuasi wale wakijua watu wanyoofu ni akina nani, hawatawapa tena pesa zao na watawapuuza.

Bila shaka baadhi ya wanaopinga hawaamini kuwepo kwa Imam (a.s) kwa sababu hawaamini baadhi ya itikadi, kanuni na mambo ya kweli ambayo kwa kweli ni utangulizi katika kuamini kuwepo kwake, tunamuomba Allah (s.w.t) afanye haraka kurejea kwake.

Watu hawa kamwe hawazungumzi habari zake, kwa vile kutokuwa kwao na imani juu ya mambo ya kweli ya kimsingi huwazuia wao katika njia hii moja kwa moja.

Imani ya ukaidi ina miundo na aina mbalimbali, na ina viwango mbalimbali; baadhi ya hivi vimejificha kuliko vingine. Hata hivyo, kinachovihusisha hivi viwango na aina zake ni mapenzi ya maisha ya dunia hii na kutanguliza mbele maslahi binafsi kuliko kuufuata ukweli.

Ama kwa kundi la pili la wasioamini, kwa sababu ya hadaa na fikra wali- zonazo, huona kwamba kumuamini Imam Al-Mahdi (a.s) ni upotofu.

Uongo mwingi huchangia kuifikia hali hii ya kutoamini na kutokukubali. Kabla hatujautaja uongo huu ni lazima tutambue ukweli kwamba tunaposhughulikia suala la Imam Mahdi (a.s) mbali kabisa na kanuni za Uislam kutaufanya utafiti kuwa mgumu, kama sio kutowezekana kabisa.

Kitu cha kwanza na muhimu kabisa kwenye kanuni hizi ni: Imani juu ya Allah (s.w.t) na kudra Zake kwamba hawezi kushindwa. Yeye, Mtukufu, ni Muweza wa kufanya kitu chochote.

Maadam suala la Imam Mahdi (a.s) linatokana na Mwenyezi Mungu, Allah (s.w.t), hivyo basi maisha yake marefu hapa duniani na yote yale ambayo yanamhusu yapo mikononi mwa Allah.

Kwa hiyo, kutokukubali juu ya kuwepo kwake hai, maisha yake kuwa marefu, ama kuweza kunusurika na kuishi katika kipindi hiki chote kirefu ambacho kinazidi zaidi ya miaka elfu moja, inaashiria kukataa na kutozijua Nguvu za Mwenyezi Mungu.

Kanuni nyingine ya Uislamu ambayo ni muhimu katika kulifahamu suala la Imam Al–Mahdi (a.s) na kulifanyia utafiti kwa usahihi ni: Imani juu ya Mtume wa mwisho, Umaasum wake na kazi yake ambayo inajidhihirisha yenyewe katika maisha yake, tabia yake na hadithi.

Hii inakusudia kumuiga yeye, na kukichukulia kila kitu akisemacho kwamba ni kweli, kwa sababu huyu ni Mtume Mkubwa (Amani iwe juu yake na Aali zake) na anao wajibu ulio muhimu katika kuteuliwa kwa Imam Al–Mahdi (a.s).

Kwa hiyo, tukienda moja kwa moja kwenye suala la anayengojewa Imam Al–Mahdi (a.s) bila ya kuzizingatia kanuni zilizotajwa hapo juu, ama kuzitegemea, yawezekana tusifikie mwisho wowote.

Wale wanaouamini Uislamu na Qur’ani, wanafahamu vyema kwamba hakuna jambo lolote geni kwa yale yanayoelezewa juu ya Imam Al-Mahdi (a.s), kama vile maisha yake marefu.

Kwa nini iwe hivyo? Kwa sababu Qur’ani ina mifano mingi kama hiyo, na wanachuoni wameyasoma mno mambo hayo katika vitabu vingi na wameweka mada hasa juu ya Imam Mahdi (a.s) kama ifuatavyo:

Kuwepo hai kwa Imam Mahdi (a.s), mwana wa Imam Al-Askari [ambaye ndiye mwana wa Imam Al-Hadi, mwana wa Imam Al-Jawad, mwana wa Imam Al-Ridha, mwana wa Imam Al-Kadhim, mwana wa Imam Al-Sadiq, mwana wa Imam Al-Baqir, mwana wa Imam Al–Sajjad, mwana wa Imam Al–Husein, mwana wa Imam ‘Ali ibn Abi Talib (Amani Iwe Juu Yao Wote), ambao ni warithi wa Mtume wa Allah (s.w.t), (kama ambavyo Mtume amesisitiza katika moja ya ujumbe wake) inathibitishwa kwa namna mbili; kupitia mapokezi na hoja za kiakili.

Katika mapokezi, zipo hadithi sahihi nyingi mno ambazo zinatoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w) na vipo vitabu vingi ambavyo humo mna hadithi ambazo zinathibitisha kuwepo kwa Imam.

Kwa hoja za kiakili, tunaweza kuthibitisha umuhimu wa kuwepo kwake, kwa kutumia hoja mbalimbali ambazo zote zimejengwa na msingi wa Imani juu ya Uwezo wa Allah, Huruma Yake, Hekima na Rehema ya Allah (s.w.t). Inasemekana kwamba imani juu ya Muumba na Sifa Zake thabiti bila shaka zitatufikisha kuamini juu ya Imam Mahdi (a.s).

Kinyume cha haya, wapimzani wa hoja hii – kwamba ni hoja ya kuwepo kwa Imam – inakuwa haiwezikani kupambanua kinachotokea Ulimwenguni na katika maisha ya watu, ingawa wanadai kumuamini Allah (s.w.t) na sifa Zake.

Kama tunavyosoma katika dua, Imam Mahdi (a.s) ni Rehema ya Mwenyezi Mungu ambayo kwamba Allah (s.w.t) ameileta Mwenyewe, na Ukarimu Wake ambao hauwezi kutenganishwa na Utukufu Wake na Uangalizi wa Ulimwengu huu. Pia tunawaeleza: Endapo Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa Rehema na Mwingi wa Hekima, na ameahidi kwa waja wake kwamba wachamungu wataurithi Ulimwengu huu, basi iwapi hiyo Rehema, Ukarimu na Hekima ya Allah (s.w.t) kutokana na hali ambayo imekuwa ikitokea!

Vipi Tutaweza Kuwa Na Uhusiano Wa Karibu Zaidi Na Imam?

Kama maarifa ya kumuelewa Imam (a.s) yatakuwa yameimarika kwa dhati ndani ya nafsi; hutokea kumfahamu kwa undani zaidi; na hamu ya kutaka kunufaika kutoka kwake na kutaka kuungana naye inakuwa kubwa zaidi.

Kama mtu huyu ataishuhudia hali halisi ya jamii ilivyo na kuja kuyajua matukio yanayotokea ulimwenguni na ukandamizaji na ubadhirifu ambao unafanyika, basi hamu hii itageuka kuwa kubwa mno na kuona huruma.

Yote haya ni kwa sababu yeyote amjuaye Imam na kumuamini kwa moyo wake na nafsi yake, haiwezekani aone watu wakiteseka na akaona si chochote si lolote!!

Imani huamsha asili ya mwanadamu, na vilevile kuwa na mapenzi kwa wengine na humfanya mtu mchamungu awe anawajali watu wengine na kuwa na moyo wa huruma. Anapoona hali ya kutisha ya ukandamizaji, mateso, majonzi, na huzuni ambazo zinavunja moyo na kuiua roho, basi mara moja ataelekea kwenye mambo mawili:

Kwanza: Ataulizia apate kujua ni nani anayesababisha majonzi yote haya.
Pili: Atautafuta wokovu, au mwokozi.

Hivyo, maadam imani ya mtu huyu ina utambuzi fika wa Imam na dhima yake katika maisha ya watu, moja kwa moja atamfuata mwokozi wa kweli ambaye ndiye aliye na mpango wa mageuzi ya ulimwengu na kuzitokomezea mbali aina zote za ukandamizaji na ubadhirifu. Kwa hiyo, hapa kuna nukta mbili za kuziangalia:

Kwanza: Kumtambua Imam.
Pili: Kiwango cha maarifa juu ya ulimwengu na jamii tuliyomo.
Haya mawili kwa pamoja humfanya mtu ageuke kwa kina kumwelekea Imam Al–Mahdi. Kama mtu mwaminifu anamtambua Imam kwa Utukufu wake, Umuhimu wake, na Hadhi yake aliyonayo mbele ya Allah (s.w.t) bila ya kupata kufahamu majonzi yaliyopo hapa ulimwenguni, basi inawezekana kwamba hamu yake kubwa ya kutaka kumfuata Imam ikawa ina upungufu na yenye kikomo.

Kwa upande mwingine, kama atajiingiza katika madhila ya wanadamu, shida za jamii, na moyo wake ukajawa na uchungu na simanzi kwa yale yanayotendeka, basi, hali yake kwa jinsi alivyo na katika kumtafuta ili kumfuata Imam kutakuwa na nguvu. Jina la Imam Al–Zaman (Imamu wa zama hii yetu) limeambatanishwa na dhima yake kubwa mno.

Ghaiba yake haikutokea katika karne zote hizi hivi hivi tu, bali ilikuwa ni kwa ajili ya kumuokoa mwanadamu. Hivyo kwa yule ambaye atauweka moyo wake uhisi taabu za ulimwengu, atakuwa karibu zaidi na Imam.

Je, Kuna Kitu Ambacho Mtu Anaweza Kukifanya?

Bila shaka, hisia za ndani peke yake hazitoshi kwa maisha haya, kwani zinaweza kutoweka. Kwa hakika, imani yoyote bila ya kujali kwamba namna gani imejijenga moyoni na akilini, kama haikufanyiwa kazi inaweza kusahauliwa kwa urahisi ama kukataliwa. Ni vitendo tu na harakati ambazo zinatokana na imani ndizo hujikita moyoni na kuhifadhika mwongozo wake.

Fikiria juu ya mtu aliyeuamini utukufu wa Imam Al–Mahdi (a.s) na daraja aliyonayo mbele ya Allah (s.w.t), lakini kwa upande mwingine akawa anajihusisha katika shughuli na vitendo vya wakandamizaji, na akawasaidia katika kutekeleza mipango yao, ambayo inaelekezwa katika kuwanyonya wanyonge pamoja na rasilimali zao.

Aidha, maslahi yake yakawa yana uhusiano na maslahi yao, kwani maisha yake na kipato chake kinatoka kwao. Je, tunaweza kumtegemea kwamba yeye awe anampenda, au mwenye kumngojea Imam al–Zaman, mwenye kuisambaza haki?

Kila namna ya mahusiano na wakandamizaji yanapunguza imani moyoni, na hali hii huendelea hadi kufikia kuwa mapenzi na imani kwa Imam hufutika vyote kabisa kwa pamoja. Kwa hiyo, kitu muhimu kabisa baada ya kumjua Imam ni kukiacha chochote kile ambacho kinaweza kuidhoofisha athari ya maarifa haya ya kumtambua Imam kwa mtu binafsi.

Hivyo, inawezekana kufanya baadhi ya mambo ili kuiimarisha na kuuongeza zaidi uhusiano na Imam, baadhi yake ni:

1. Kuwa Imara Katika Kumfuata Yeye:

Hii ina maana ya kujiwajibisha siku zote kuwa katika mwongozo wake na mwongozo wa wale ambao humsaidia, kufuata utaratibu wake, na kuweka mazingira yanayofaa kwa ajili ya kurejea kwake.

Imepokelewa kutoka kwa Imam Muhammad Al-Baqir (a.s), amesema kwamba: “Utakuja fika wakati kwa watu ambapo Imam wao atatoweka machoni mwao, baraka ziwe juu ya wale ambao watakuwa imara katika kutufuata sisi katika wakati huo. Malipo ya kiwango cha chini kabisa ambayo watayapata ni kwamba Allah (s.w.t) atawaita na kusema: “Enyi waja wangu, mmeiamini siri yangu, na mmeamini katika yasiyoonekana, hivyo shuhudieni malipo toka Kwangu.

Enyi waja wangu hakika nayapokea kutoka kwenu, na kwenu ninatoa msamaha, na ninawasamehe. Na kwa ajili yenu ninainyesha mvua kwa ajili ya waja wangu, na ninawaondolea mabalaa. Kama isingelikuwa ni ninyi, ningeliwashushia wao adhabu yangu.”1

Yeyote ambaye yupo imara katika kuifuata njia ya Ahlul Bayt (a.s) ndiye huyo ambaye amefungamana na mpango wao wa kuleta mageuzi ulimwenguni na huuchukulia kuwa huo ndiyo mpango wa maisha yake.

2. Kuepukana Na Maadui Zake:

Kuepukana kwa kweli ni kuachana nao kabisa na kukabiliana nao. Uadui na maadui wa Imam Al–Zaman huimarisha uhusiano naye, na humfanya mtu kuwa tayari katika kuufuata mwongozo wa Imam, kuepukana (bara’ah) na maadui wa mtu ni sawa na kumfuata (wilayah), na bila ya hivyo, kumfuata hakutakuwa kwa kweli au kwa hakika.

Mtume (s.a.w.w) amesema: “Ewe Ali! Naapa kwa yule ambaye amenituma mimi na utume na amenichagua mimi miongoni mwa viumbe vyote. Kama Mchamungu amefanya ibada kwa ajili ya Allah (s.w.t) kwa miaka elfu, hataweza kukubaliwa mpaka amekufuata wewe (wilayah) na maimamu kutokana na kizazi chako, na kukufuata wewe hakutakubaliwa bila ya kuepukana na maadui wa maimamu wa kizazi chako.

Hivi ndivyo Jibrili (Malaika Jibril) alivyonifahamisha Mimi. Ni juu ya mtu ama kuwa mwenye kukataa ama kuwa mwenye kuamini.”2

Kama mtu mwaminifu hawezi kusema waziwazi kuacha na kuepuka kwake hivyo itabidi chuki yake iwe kwa maadui wa Imam ili kuiweka nafsi iwe katika hali ya kuwa tayari.

Kusahau kutokuwa na chuki na kutoihisi kuendelea kuwepo kwake, maana yake mwisho wake ni kutoweka kwa Wilaya kutoka katika nafsi ya mtu. Kwa hiyo, Imam al–Sadiq (a.s) alimuusia mtu aliyemtembelea nyumbani akimtajia kasoro yake kwa kutokufanya chochote dhidi ya maadui, kwa kusema:

“Baba yangu aliniambia kwamba baba yake alimuambia kwamba babu yake alimuambia kwamba Mtume wa Allah (s.w.t) alisema: ‘Yeyote yule ambaye amedhoofu na hawezi kutusaidia sisi, Ahlul Bayt, lakini bado akawalaani maadui zetu katika nyakati zake za ibada kwa siri akiwa peke yake, Allah (s.w.t) ataifanya sauti yake iwafikie Malaika wote, kuanzia duniani hadi kwenye kiti cha enzi.

Wakati wowote ambao mtu huyu anawalaani maadui zetu malaika pia humsaidia katika kuwalaani wakifanya hivyo mara mbili yake, hivyo hivyo!

Kisha watasema: Ewe Allah (s.w.t) mbariki mja wako ambaye amefanya kile kilicho katika upeo wa uwezo wake, na kama angekuwa na uwezo wa kufanya zaidi ya hapo angefanya. Ndipo hapo sauti kutoka kwa Allah (s.w.t) itakuja, ikisema: Nimeipokea dua yako na nimelisikia ombi lako. Nimeibariki roho yake miongoni mwa roho na nimemfanya yeye kuwa kwangu Mimi miongoni mwa watu walioteuliwa na wenye upendeleo.”3

Pia imepokelewa kutoka kwa Mtume (s.a.w.w), akisema: “Furaha kubwa sana ipo kwa wale watakaomfikia Al-Qaim na kumfuata yeye katika kipindi cha ghaiba yake kabla ya kuonekana kwake tena. Wanaowafuata watu watukufu wanaomwakilisha, na wanaoonesha chuki dhidi ya maadui zake. Wao ni marafiki zangu na watu ambao nitawapenda, na ni watu wenye thamani kubwa sana katika umati wangu katika Siku ya Hukumu”.4

3. Kuwajibika Kwenye Sheria Za Kiislamu (Shari’ah) Katika Mambo Yote Ya Maisha:

Lazima tusisahau kwamba wakati Imam atakapojitokeza, ataifanya sheria ya dini kama ndiyo sheria inayofuatwa katika maisha ya mwanadamu na kwa kuiongoza jamii yote ulimwenguni.

Ni dhahiri kwamba wale wanaofuata Shari’ah, katika kila kipengele cha maisha yao, kabla ya kujitokeza kwake kulikobarikiwa, watakuwa tayari zaidi kukubali hii sheria kuliko wengine.

Watalifanya suala hili (la kufuata sheria za Mungu kama sheria ya kawaida) kuwa kubwa kabisa kama mafanikio ya Imam Al–Mahdi (a.s), kufuatia utekelezaji wa haki ulimwenguni.

Kama tutazingatia hadithi ambazo zinataja sifa na tabia za watu wanaomsaidia Imam Al–Zaman na wale ambao wanatayarisha mazingira mazuri ili ajitokeze, tutaona kwamba sifa muhimu kabisa kati ya hizi ni uchamungu (taqwa), ambao maana yake ni kutekeleza sheria zote za Mwenyezi Mungu katika kila hatua ya maisha.

Mtume wa Allah (s.w.t), amesema: “Mwishoni mwa umma huu wataishi watu ambao watapata malipo sawa kabisa na wale waliokuwapo mwanzoni, wataamrisha mema na kukataza maovu, na kupigana dhidi ya watu wapotovu.”5

Kama ambavyo tunajua kuamrisha mema na kukataza maovu ni mambo mawili ambayo ni ya wajibu katika Uislamu, ambayo ndiyo yaliyokuwa sababu ya umma wa Muhammad (s.a.w.w.) kuwa bora kuliko umma nyingine. Allah (s.w.t), anasema:

كُنْتُمْ خَيْرَ أُمَّةٍ أُخْرِجَتْ لِلنَّاسِ تَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَتَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنْكَرِ وَتُؤْمِنُونَ بِاللَّهِ ۗ{110}

“Ninyi ni kundi bora mliotolewa kwa ajili ya watu, mnaamrisha mema na mnakataza maovu, na mnamuamini Mwenyezi Mungu (s.w.t).” (Qur’ani, 3:110).

Kuutekeleza wajibu huu wa kidini ni uthibitisho kwamba hakika mtu anafuata barabara mambo mengine ya wajibu ya dini na sheria. Imepokewa katika hadithi kwamba Imam al–Baqir (a.s), amesema: “Kuamrisha mema na kukataza maovu ni njia ya Mitume na ni mwenendo wa wachamungu, na ni kazi kubwa. Kwa namna hii, majukumu hutekelezwa, makundi ya watu huwa salama, biashara huwa za halali, dhuluma huondoshwa, na ulimwengu hujengwa, na utulivu huimarika.”6

Kuuacha wajibu huu utamfanya Imam awe mbali na sisi, na muda wake wa kujitokeza kuongezeka, kwa sababu wakati atakapojitokeza atahitaji watakaomsaidia ambao wanaona wanao wajibu wa kuubadili ulimwwengu, kuugeuza na kutokomeza ubadhirifu ndani yake. Amirul Muuminin Imam Ali (a.s), amesema: “Msiache kuamrisha mema na kukataza maovu, ama sivyo Allah (s.w.t) atachagua watu miongoni mwenu kusimamia mambo yenu, mtaomba lakini maombi yenu hayatakubaliwa.”7

Imam Muhammad al–Baqir (a.s) amesema: “Laana ya Allah (s.w.t) kwa viumbe wake imetutoa sisi kuwa mbali nao.”8

4. Kuomba Du’a:

Kuomba Du’a kuna jukumu kubwa katika kuweka mawasiliano ya kiroho, na kuyaimarisha. Maombi huipa nafsi hisia muhimu ili iweze kuwa imara na kuendelea, hasa kama tutakuwa tunatambua kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameahidi kuyasikiliza maombi ya wale ambao wanamuomba kwa dhati. Kusikiliza hapa kuna maana kwamba Allah (s.w.t) atawafahamisha kwamba amewasikia na anajua ni yapi ambayo wamekuwa wakimuomba. Wakati muumin anapojua hili, ndipo hapo imani na kumuamini Allah itaongezeka.

Wakati waumini wakimuomba Mwenyezi Mungu juu ya Imam al–Zaman, na kuomba kuharakishwa kutokeza kwake, hii itaongeza hisia zao na imani kwamba Imam anaishi, yu hai na yupo. Hisia hii huwafanya wawe imara kuhusiana na kukaribia njia ya Imam.

Kumuomba Mwenyezi Mungu juu ya Imam Mahdi (a.s) ni muhimu sana, tunaona kwamba Maimamu wengine wa Ahlul Bayt (a.s) pia walikuwa wakimuomba Mwenyezi Mungu kwa ajili yake. Na hawakuridhika tu kwa kutuongoza sisi ili tumfuate Imam.
Maombi mengi muhimu yamesimuliwa kuwa yanatokana na wao.

Kama hili lingekusudia kitu kingine, basi lingekusudia kwanza kabisa, awali ya yote kwenye kazi kubwa mno ambayo Imam (a.s) atakuja kuimalizia, ambayo ndiyo ilikuwa lengo la Maimam wote Maasum (a. s) vilevile.

Baba yake Imam Mahdi (a.s) amesema: “Naapa kwa Allah (s.w.t) atakuwa ghaibu katika ghaiba ambayo hakuna hata mmoja ambaye atanusurika kutokana na uharibifu isipokuwa wale ambao Allah (s.w.t) amewaimar- ishia katika nyoyo zao imani ya Uimamu wake, na amewapa dua ya kuom- ba kuharakishwa kwa nusura yake (Imam)”9

Katika barua iliyoandikwa kwa hati ya mkono wake Imam Al-Mahdi (a.s) na kuwekwa saini yake imeandikwa: “Na ongezeni kuomba dua kwa ajili ya kuharakishwa kwa nusura (nusura ya Imam), kwani hiyo ni nusura yenu.”10

Zipo dua kwa idadi ya makumi kadhaa ambayo hulifanya suala hili la Imam Mahdi (a.s) kuwepo katika nafsi, na kuzifanya roho kuwa na tamaa kubwa ya kutaka kukutana naye, na kuyafanya mambo kulingana na mpan- go wake mkubwa. Tutazitaja baadhi ya hizi dua mwishoni mwa kitabu hiki. Ama kwa dua nyingine, zimo katika vitabu vya dua vinavyofahamika.

5. Kujiandaa Kwa Ajili Ya Kuja Kwake:

Hii ina maana kwamba tuendelee kutekeleza vitendo na mipango ambayo itakuwa ndiyo sababu ya kujitokeza kwake, na kuharakisha kujitokeza kwake. Yeyote ambaye anajua sababu za kughibu kwake atafahamu kwamba kujitokeza kwake kulikobarikiwa kwahitaji maandalizi na kuwapo katika hali ya utayari.

Watu wengine wataandaa mazingira ya kujitokeza kwake, na wengine watakuwa tayari kwa kujitokeza kwake. Hivyo msingi mkubwa ambao Imam atauhitajia kwa ajili ya kuleta mabadiliko ulimwenguni utakuwa upo tayari.

Imam Sayyid Ali Khamenei, mmoja kati ya watu muhimu sana kwa wakati huu kwa kuweka mazingira bora kwa Imam, anasema yafuatayo kwa wale wote ambao wanaelewa vyema maana ya wilayah:

“Wajibu wenu leo hii ni kuweka mazingira bora ambapo Imam Mahdi (a.s) atakuja na kuanza kazi yake kutokana na msingi uliokuwa tayari ambao umeshaandaliwa. Haiwezekani kuanza bila ya kuwepo na msingi wowote ule.

Jamii ambayo inaweza kukubali serikali ya anayengojewa, Imam Mahdi (a.s) - roho zetu ziwe sadaka kwa ajili yake - ni jamii ambayo ipo tayari na imejiandaa kwa jambo hilo. Vinginevyo, itakuwa na mwisho ule ule ambao umezipata jamii nyingi katika nyakati kama ilivyo katika historia.”

Anaendelea kusema:

“Kwa hiyo, inawezekana kuandaa mazingira. Kama mazingira haya yatazidi kuwa makubwa kwa uwezo wa Allah (s.w.t), ndipo hapo ambapo patakuwa pameandaliwa kwa ajili ya kujitokeza kwake Imam (a.s) (Baqiyatullah) - roho zetu ziwe mhanga kwa ajili yake - na kisha matakwa ambayo yalikuwa mioyoni mwa mwanadamu na Waislamu, yatapatikana.” (15 Shaaban, 1418 A.H.).

Hali hii ya kuwa tayari ndiyo maana halisi ya kungojea Faraja (Al Faraj). Yule ambaye hasa kweli anamngojea Imam Mahdi (a.s) ndiye ambaye ameweka mazingira bora na msingi unaofaa kwa ajili ya kujitokeza kwake.

Huwatafuta wale wengine wote ambao wanashughulika kwa kuipitia njia hii, na ya wale wote ambao wanasaidia kazi hii.
Zaidi ya hapo, muda wote ambao hutafuta njia hii bora ya kuandaa mazingira kwa ajili ya kujitokeza kwake, hajisikii kuwa ameridhika baada ya kuwa ameshafanikiwa katika sehemu ndogo tu ya kazi hii.

Amiir Muuminiin Imam Ali (a.s) amesema: “Matendo bora kabisa ambayo hukubaliwa na Allah (s.w.t) ni kungojea Faraja (faraja ya Imam).”11

Imam Musa al–Kadhim (a.s) amesema: “Ibada bora kabisa, baada ya kumjua na kumpenda Mwenyezi Mungu, ni kusubiri kuja kwa Faraja (Faraja ya Imam).”12

Imam al–Sadiq (a.s) anawasifia wale ambao kweli wanamngoja kwa kusema: “Furaha kamili (ni) kwa ajili ya wafuasi (Shi”a) wa Qaim ambao hungojea kuonekana kwake katika kipindi cha ghaiba yake, na wanamtii baada ya kutokeza kwake. Wao ni mawalii wa Allah (s.w.t) ambao kwao hawatakuwa na hofu wala kuhuzunika.”13

Hapana shaka kwamba maandalizi yanahitaji umoja na ushirikiano ili kusije kukatokea kutokuelewana na kutawanya nguvu.

Siku hizi, kama tutawaangalia watu wengi miongoni mwetu ambao wanadai kwamba wao ni wafuasi wa Imam (a.s) tunaona kwamba hawayajui masharti ambayo ni muhimu sana na sababu za kuja kuonekana kwake, ambako kunakubalika kwa pande zote, na kuachana kabisa na kujitenga. Utengano pia ni sababu kubwa ya kuchelewesha kuja kwa Imam na kurejea kwake kuliko na baraka.

Haimchukui mtu mwenye busara kufikiri sana kutambua kwamba njia bora ya kuudumisha umoja miongoni mwa wanaomsubiri Imam ni kuwa na uongozi imara wa mtazamo mmoja.

Sifa njema ni za Allah (s.w.t) ambaye ameuweka uongozi katika umma huu ambao ulimwengu wote unafahamu, na wote wanashuhudia kwamba unasimama imara dhidi ya maadui wa dini na ubinadamu.

6. Kuiadabisha Nafsi:

Wakati tunafahamu maana ya kuiadabisha nafsi tunatambua athari yake juu ya uhusiano wake na Imam al–Mahdi (a.s). Nafsi safi yenye tabia njema wakati wote ipo tayari kuukubali ukweli na matendo yake yakalingana na ukweli huo, tofauti na nafsi zilizo ovu hata kama zitakuwa na Imani sahihi.

Imepokewa kutoka kwa Imam Jafar al–Sadiq (a.s) amesema: “Yule ambaye amependezwa kuwa mmoja wa wafuasi wa wa al–Qaim, basi anapaswa akae akingojea, na matendo yake yawe ya uchamungu na tabia njema, wakati akingojea.

Basi kama atakufa na al–Qaim akatokeza (baada ya kifo chake) atapata malipo sawa sawa na yule ambaye amemuona al–Qaim, hivyo ajitahidi na asubiri.”14

Imam Khamene’i amesema: “Imani juu ya Imamuz-Zaman itakuwa ni kwa Mashi’a, kama watauelewa ukweli wake na kufanya kama wanavyopaswa, chanzo cha matokea ni nuru.

Imani hii pia itamuongoza kila Mwislamu na muumini na Shi’a kufanya jitihada kimawazo na kivitendo kuyalinda mahusiano yao na Imam kiroho na kiakili, na kusafisha nafsi zao katika namna ambayo itapendezwa na Imam wao Maasum.”

7. Kuhuzunika Na Kulia Kwa Ajili Ya Kughibu Kwake:

Tutaanza kwanza kwa kutaja kisa hiki chenye maana:

Sudair al–Sairafy, mfuasi wa Maimam (a.s) anasema kwamba: Siku moja bila ya kumpa taarifa kabla alifanya ziara ya kumtembelea Imam Jafar al–Sadiq (a.s) akiwa pamoja na al–Mufadhal ibn Umar, Abi Basiir, na Aban ibn Taghab, na walimuona akiwa amekaa chini kwenye mchanga katika namna ambayo si ya kawaida, akilia kama vile mama ambaye amefiwa na watoto wake wote. Uchungu ulionekana machoni usoni mwake na mashavu yake yalilowana kwa machozi, na alikuwa akisema:

“Ewe Maula, kughibu kwako kumeniondolea usingizi, kumekifinyanga kitanda changu, na kumeupokonya utulivu wa moyo wangu.
Ewe Maula, kughibu kwako kumefanya mateso yangu kuwa yenye mau- mivu ya milele.

Nahisi machozi yakinidondoka kutoka machoni mwangu, na udhaifu ukiunyong’onyeza moyo wangu kwa misiba inayoendelea na iliyopita…”

Mioyo ya wafuasi wake ikastushwa walipomsikia, wakapatwa na huzuni. Walidhani kwamba wamesikia jambo kubwa na msiba mkubwa, ndipo wakamuuliza:

“Allah (s.w.t) ajaalie usilie, Ewe mwana wa mbora wa wanadamu, ni kwa kutokana na jambo gani unalia na kutoa machozi, na ni hali gani imekufanya uwe katika hali hii ya huzuni?” Imam al–Sadiq (a.s) akashusha pumzi kwa nguvu, kisha akasema:

“Ole wenu. Nimeangalia katika kitabu cha Ilm Al–Ja’far asubuhi hii, kitabu ambacho kina maarifa yote juu ya vifo na misiba, na maarifa ya kuna nini na itakuwaje Siku ya Hukumu, ambacho Allah (s.w.t) amempa Muhammad na Maimamu baada yake (s.a.w.w) tu peke yao.

Nikatafakari juu ya kuzaliwa kwa al–Qaim wetu na kughibu kwake na kuchelewa kurejea kwake, na umri wake mkubwa na madhila makubwa watakayopata waumini katika muda huo, na chanzo cha shaka katika nyoyo zao kutokana na kughibu kwake kwa muda mrefu, na wengi wao kutoka katika dini na kuuacha Uislamu, kama Allah (s.w.t) alivyosema ndani ya Qur’ani:

وَكُلَّ إِنْسَانٍ أَلْزَمْنَاهُ طَائِرَهُ فِي عُنُقِهِ ۖ وَنُخْرِجُ لَهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ كِتَابًا يَلْقَاهُ مَنْشُورًا {13}

‘Na kila mwanadamu tumemfungia matendo yake shingoni mwake, na tutamtolea Siku ya Kiyama daftari atakayoikuta imekunjuliwa.’ (Qur’ani, 17:13).

Maana ya aya hii ni Wilaya. Huruma ikanijia na nikapatwa na uchungu.”15

Habari hii inaonesha ni kwa kiasi gani jinsi Maimamu wetu walivyokuwa na uchungu kwa kughibu kwa Imam Mahdi (a.s) ambako ni kukubwa, na kadiri ambavyo yeye akiwa yu katika ghaiba huu uchungu utaendelea kuwepo. Kama tutapata kufahamu yupi ni Shi’a wa kweli, basi tutajua uhu- siano uliopo baina ya kuhuzunika kwa ajili ya Imam na kuungana naye.

Imepokewa kwamba Amirul Mu’miniin Imam Ali (a.s) amesema: “Allah (s.w.t) alichunguza duniani na akatuchagua sisi, na akachagua wafuasi wa kutusaidia, na watafurahi tukiwa na furaha, na watahuzunika tukiwa na huzuni. Watatoa sadaka pesa zao kwa ajili yetu. Wao wanatokana na sisi na sisi tunatokana na wao.”16

Kinachotakiwa hasa ni huzuni ya kweli na mapenzi, si tu kwa kuijua huzuni ya Imam. Sayyid Ibn Tawuus ana kitu kizuri mno cha kusema kuhusiana na hili, anasema: “Nimemwona yule ambaye anadai kwamba ni wajibu kuwa na furaha kwa ajili ya furaha ya Imam, na kuwa na huzuni kwa ajili ya kuwa kwake na huzuni.

Baraka za Allah (s.w.t) ziwe juu yake. Anasema kwamba anaamini kwamba kila kitu ulimwenguni hapa kimeporwa kutoka katika mikono ya al–Mahdi (a.s), na watawala na watu wamevipora toka mikononi mwake.

Hata hivyo sijamuona mtu huyu akiwa ameathiriwa na kuporwa na kunajisiwa huku, kama ambavyo angeathirika kama angenyang’anywa dinari au dirham au ardhi au mali zake. Utiifu ulioje au maarifa yalioje ya Mitume na Maimamu katika kumjua Allah (s.w.t)?”

Matendo mengi yametajwa ili kuuimarisha huu uhusiano. Mojawapo ya kitabu chenye manufaa katika uwanja huu ni, “Wajibu wa muumini kwa Imam al Zaman”. (The responsibilities of a believer towards Imam al- Zaman), cha Sheikh Mahdi ‘Alaa’ al–Diin.

Maisha Ya Imam Mahdi (A.S) Kwa Ufupi.

Yeyote ambaye amepata kusikia juu ya Imam Mahdi (a.s) atajua kwamba maisha yake yamejaa miujiza na ni ya aina ya kipekee. Miaka kadhaa kabla ya kuzaliwa kwake, jitihada za kutaka kumjua na kumtafuta zilianza. Wale ambao walimuamini na waliamini juu ya kazi yake kubwa ya kuyaleta mageuzi ulimwenguni na kuuokoa ubinadamu walimsubiri kwa miaka kadhaa kabla bado hajazaliwa.

Na wale ambao walisikia juu ya yale ambayo angewafanyia, na namna ambavyo angewaangamiza walikuwa wakisubiri ili siku atakayozaliwa wamuuwe wakati akiwa bado mtoto anayenyonya.

Ama kwa waumini walikulia katika mikono ya Viongozi wa dini (a.s) ambao waliwapa habari njema juu ya mwokozi ambaye siku moja angeonekana. Maimam walisema mengi kwa watu juu ya sifa zake, nini kingetokea baada ya kuzaliwa kwake, na nini kingemtokea. Matumaini ya wengi yalikuwa mioyoni mwao, na walianza kusimulia toka kizazi kimoja hadi kingine.

Matumaini haya yaliongezeka kwa ahadi tukufu na mpango wa kisiasa. Ikawa ndiyo sababu ya kuwakusanya hao watu ambao wanamsubiri Imam, chini ya chama cha kisiasa chenye mtazamo wa kuleta mabadiliko ambapo wanaamini juu ya hoja ya kufanyika mabadiliko kutokana na ubadhirifu mkubwa, ambao watawala waovu na wenye sifa mbaya watawajibishwa.

Ama kwa maadui walifuatilia harakati za wanaomsubiri Imam kwa miaka kadhaa. Ndipo wakaja kujua kwamba waumini wanasubiri kuzaliwa kwa kiongozi wanayemwita Al–Mahdi (a.s) na ambaye angewaunganisha.

Walijua pia kwamba wanaomsubiri Imam wangeweza kuungana pamoja na kuleta nguvu kubwa ambayo ingeweza kuviyumbisha viti vyao vya enzi na kuzitishia tawala zao. Kwa hiyo, walizifuatilia habari za Imam Al–Mahdi (a.s) kama ambavyo waumini walivyofanya – lakini kwa nia tofauti!

Mtu anaweza kuuliza kwa mshangao, je, hii ina maana kwamba maadui walimwamini Al–Mahdi (a.s) na kwa ambayo angeyafanya, kama ilivyoahidiwa katika Hadithi na Aya? Kama walikuwa wanamwamini basi wasingelikuwa maadui zake. Je, si ndivyo hivyo? Kama hawakumuamini yeye na bishara zake njema, hivyo kwa nini basi wanajisumbua kiasi hicho ilihali wanajua kwamba mambo yote haya si chochote kitu bali ni imani potovu na hekaya za uongo?

Tumelitanguliza jambo hili katika kisa cha Firauni na Musa (a.s). Historia inakumbusha bayana kwamba Firauni aliota akiwa usingizini, mtoto wa kiume kutoka katika kabila la Wayahudi angezaliwa baada ya muda mfupi na angekuwa ndiye sababu ya kuumaliza ufalme wake hapo baadaye.

Baada ya Firauni kuwa na uhakika na tafsiri ya ndoto yake akatoa amri yake ya kikatili ya kuwaua watoto wote wa kiume ambao wangezaliwa kutoka katika kabila la Wayahudi. Askari wake walianza kumfuatilia kila mama mja mzito mpaka hapo atakapojifungua, na kama mtoto aliyezaliwa alikuwa ni wa kiume, walimuua mara moja.

Juu ya kitendo hiki sasa tunamuuliza Firauni mwenyewe! Basi wewe Firauni, amma hukuiamini ndoto hiyo, au uliiamini, bila ya kuwepo na uwezekano wa tatu. K

ama hukuiamini na ukadhani kuwa pengine ni uongo tu, au jinamizi ambalo mtu asiyepata usingizi mzuri huweza kulipata, sasa kwa nini unafanya vitendo hivi vya kikatili, unaleta balaa karibu katika nyumba zote za Wayahudi, na kumfanya kila mama mzazi awe mfiwa wa mwanawe?!

Ama sivyo, kama unaiamini ndoto, basi maana yake ni kwamba hiyo ndiyo yenyewe hasa na ni ya kweli, na hivyo hutaweza kuizuia ikija kutokea. Kwa hakika kabisa, mtoto huyu atakuja kuzaliwa, na atakua na kuja kuuvunjilia mbali ufalme wako. Hivyo, kwa nini basi unaamrisha vitendo vya uhalifu, na kumuua kila mtoto wa kiume aliyezaliwa? Je, hii itakuja kukusaidia nini?

Jibu pekee kwa swali hili ni kwamba Mafarao, Wafalme na watawala madhalimu hawana akili. Siku zote wamekuwa hivi na wataendelea kuwa hivyo. Wakati mtu akiwa mtawala dikteta, hupoteza uwezo wa kufikiria vizuri. Uovu na uhalifu humzidia kwa sababu hawezi kuona mbali ya upeo wa Ufalme wake na nguvu zake.

Hapana shaka kwamba watawala madhalimu katika kipindi cha kuzaliwa Imam Al–Mahdi (a.s) walikuwa wanajua kitu kingine zaidi ya njozi na majinamizi. Labda walihofu kitu ambacho wale wanaomsubiri Imam walikuwa hawakijui, Wakati huu historia ilitofautiana katika jambo muhimu sana.

Watawala hawakumuogopa Imam mwenyewe, kwa sababu waliweza kumfunga jela au kumuua kama ambavyo walifanya kwa baba zake Maasum, mmoja baada ya mwingine. Bali, waliogopa waumini kuungana na kuwa pamoja, na kuunda kwao kwa jeshi moja imara, nguvu kubwa ambayo sio rahisi kuishinda.

Waumini wenyewe hawakulijua jambo hili. Walikuwa wakimsubiri tu Imam kwa sababu ya kusikia kwao kutoka katika hadithi ambazo zilikuwa zikimzungumzia yeye; hata hivyo walikuwa hawafahamu vyema juu ya jambo hili (isipokuwa kwa wachache tu). Maadui walifahamu vyema sababu kubwa ya kuungana na kukusanyika kwa waumini, kinyume na waumini wenyewe walivyokuwa wakijua. Vipi basi hii ilivyotokea?

Ni vigumu kulifahamu vyema jambo hili labda mpaka sisi wenyewe tuwe ndiyo watawala, au tuwe na ufahamu mzuri wa hali ya kijamii na kisiasa. Watawala wanafahamu vizuri zaidi kuliko wengine nini kitahatarisha kutawala kwao.

Pia walifahamu vyema nguvu ya umma ya maadui zao. Ndiyo sababu tunawaona wakifanya vurugu na uhalifu. Kama ambavyo Imam ‘Ali (a.s) alivyosema: “Hakika yule ambaye hutawala kwa udhalimu ni dhaifu.”

Tunaamini kwamba wao wapo imara, wakiwa na nguvu ambayo haiwezi kushindwa, hata hivyo, wao wenyewe wanajua vyema kabisa ni kiasi gani walivyo wadhaifu. Hofu yao kubwa kabisa ni juu ya nchi wanayoitawala.

Angalia hali ilivyo sasa na katika historia, namna wafalme walivyokuwa wakizuia kwa vurugu tupu na mateso, harakati zozote za upinzani zilizojitokeza – bila kujali zilikuwa kidogo kiasi gani – hata kama zilitoka kwa mtu mmoja kati ya maelfu ya watu wengine waliokuwapo ambao waliishi katika nchi hiyo.

Sasa kama tutarudi katika wakati wa kabla tu ya kuzaliwa kwa Imam Al–Mahdi (a.s), kama imani juu ya kuja kutokea kwa mwokozi mkuu ilipoenea miongoni mwa watu, na tuichunguze hali kutoka kwa mtazamo wa watawala, tutaona kwamba kitu kimoja ambacho watu walikikosa ili waweze kufanya mapinduzi kilikuwa ni kukosekana kwa kiongozi.

Hata hivyo, kama tujuavyo, kiongozi alikuwepo, hata kabla ya kuzaliwa kwa Imam Al–Mahdi (a.s). Imam Hasan al-Askari (a.s) alikuwa na sifa zote ambazo anastahili kuwa nazo kiongozi, na hivi ndivyo ilivyokuwa kwa baba yake Imam al-Hadi (a.s), na ndivyo ilivyokuwa kwa Imam al–Jawad {a.s), na ilivyokuwa kwa Imam al–Ridha (a.s), na kabla yake baba yake Imam al-Kadhim (a.s), na kabla yake Imam al–Sadiq (a.s), na kabla yake Imam al–Baqir (a.s), na Imam al–Sajjad (a.s), na baba yake Imam al–Husein (a.s) ambaye aliuawa akiwa na wafuasi wake wachache huko Karbala, na pia Imam Hasan ibn ‘Ali (a.s). Kabla ya wote hao Amirul-Mu’miniin, Imam ‘Ali, amani iwe juu yao wote hao.

Nyakati zote hizi, kiongozi ambaye anaweza kuwaongoza waumini alikuwepo, na haukuwapo wakati ambapo hakuwepo kiongozi, tangu kifo cha Mtukufu Mtume (s.a.w.w). Je, Imam Hasan al–Askari (a.s) hakuweza kuwaongoza watu dhidi ya watawala dhalimu, na kuanzisha serikali tukufu ya haki?
Bila shaka Imam alikuwa ana sifa ambazo zilistahili kwa yeye kuitekeleza kazi hii kama ambavyo babu zake kabla yake walivyokuwa, Je, waumini katika nyakati hizo waliamini hivi? Historia inatueleza kwamba waumini katika jambo hili walikuwa wachache.

Jinsi Maisha Ya Ajabu Ya Imam Huyu Anayengojewa Yalivyokuwa!

Baba yake ilimbidi afiche kuzaliwa kwake, hata kwa watu wa karibu. Si hivyo tu, bali alimficha awe mbali na watu hata baada ya kuzaliwa kwake, kwa sababu alijua kwamba watawala madhalimu wasingechoka kumtafuta mpaka wamuone na wamuuwe kikatili.

Watawala madhalimu waligundua kwamba baada ya mwaka 255 Hijria waumini katika miji mbalimbali wangekuwa na mategemeo na matumaini makubwa.

Hii iliwafanya wawe vichaa kabisa. Walitaka kujua, kwa njia yeyote, wapi ambapo huyu Imam ambaye atayevunjavunja viti vyao vya enzi alikuwa.

Usiku wa siku ya Alhamisi, usiku wa mwezi kumi na tano Shaaban, Mwaka wa 255 Hijria, Nuru ilichomoza na kuuangaza ulimwengu ambao macho ya upelelezi hayakuweza kuambulia hata mpepeso wa mwale mmoja wa nuru hii.

Yeye ni mrithi wa Mtume na Maimam, alizaliwa katika namna ya kimiujiza, kama ambavyo Nabii Musa (a.s) alivyozaliwa, bila ya dalili yeyote ya ujauzito kuonekana kwa mama yake, ingawa mara kwa mara alikuwa akichunguzwa na maaskari wa Firauni.

Wanawake wote ambao walitumwa kuja kupeleleza katika nyumba ya Imam Hasan al-Askari, wakati akiwa katika kifungo cha nyumbani, walishindwa kujua juu ya tukio hili kubwa.

Kila mtawala dhalimu ambaye anataka kukaidi na kupingana na Allah (s.w.t), Allah atamleta katika nyumba yake yule ambaye atakuja kumpindua

Firauni alimtafuta katika kila nyumba adui yake ambaye angezaliwa karibuni, na Allah (s.w.t) akamleta Musa akiwa bado mtoto mdogo nyumbani kwake.

Firauni alikuwa hana uwezo wa kupingana na Mapenzi ya Mwenyezi Mungu. Ni amri ya Allah, na wakati ikija hakuna mtu awezaye kufanya chochote kuizuia bila ya kujali yeye ana nguvu kiasi gani.

Jinsi Gani Kulivyokuwa Si Kwa Kawaida Huku Kuzaliwa Kwa Huyu Imam!

Imam Hasan al–‘Askari (a.s) alijua kwamba huyu mtoto, ambaye alikwenda chini na kusujudu mara tu alipokuja katika uliwengu huu, ndiye Imam anayengojewa.

Alilijua hili muda mrefu kabla hata ya kuzaliwa kwake, na kwa hiyo akampa jina lililobarikiwa la Mtume wa Allah (s.w.t) ambaye alikuja kuwaokoa wanadamu. Akampa jina la Mtume na kun’ya yake (jina la heshima ya uzazi) Abal-Qasim Muhammad.

Mtume (s.a.w.w) anasema: “Al–Mahdi anatokana na kizazi changu, jina lake ni jina langu na kun’ya yake ni kun’ya yangu.”

Imam Mahdi (a.s) kwa mara ya kwanza kabisa katika historia ya mwanadamu, atauunganisha ulimwengu wa magharibi na ulimwengu wa mashariki. Baba yake anatoka Mashariki, na mama yake anatoka Magharibi. Imepokelewa kwamba mama yake Imam aitwaye Nargis “Malika,” alikuwa ni binti wa Yashua Ibn Qaisar (Caesar) Mfalme wa Rumi.

Mama yake, kwa upande mwingine alikuwa ni mmoja kati ya wato- to wa wanafunzi wa Nabii Isa (a.s) na kizazi chake kinaendelea kwa kurudi nyuma hadi kumfikia Shim’uun, mlezi wa Nabii Isa (Yesu).

Licha ya ukweli kwamba mama yake Imam aliishi mbali sana na kilipokuwa kitovu cha ulimwengu wa Uislamu, tukio lililomtokea katika maisha yake lilimfanya ageukie upande wa mashariki na kwenda huko ambako kulibadili maisha yake moja kwa moja.

Usiku mmoja akiwa usingizini aliona ndotoni kwamba Mtume wa Waislamu alikuwa anakuja na watoto wake na akamuomba aolewe na mwanawe wa kiume, ambaye baadaye alikuja kumtambua kwamba alikuwa ni Imam Hasan al–‘Askari (a.s).

Walimjulisha kwamba atapata baraka ya kupata mtoto wa kiume ambaye atautawala ulimwengu, mashariki na magharibi, na utaujaza kwa usawa na haki. Akaamka kutoka usingizini na moyo wake ukiwa umejawa na imani na nuru ikaing’arisha roho yake. Akapatwa na tamaa ya kuzipata hizi nuru alizoziona katika ndoto yake.

Akapata hisia ambazo hakuweza kuzielezea, kwamba amekuwa yeye ni mmojawapo miongoni mwao na kwamba nuru zao zilikwenda zikaingia rohoni mwake na kukaa hapo moja kwa moja.

Akaogopa kuwaeleza ndugu zake kwa yale yaliyomtokea, kwa sababu angeweza kudhaniwa kwamba amepatwa na kichaa, kwani uadui baina ya Rumi na Waislamu ulikuwa ni mkubwa mno. Ndoto hii ilikuwa katika mawazo yake wakati wote, na ikamfanya nafsi yake kujaa imani zaidi na kuwa na shauku zaidi kiasi ambacho alitaka aungane nao hata kama ni kwa njia isiyo ya kawaida.

Yuko wapi huyu mtu aliyemuona katika ndoto yake, ambaye ni mwana wa Mtume Mtukufu? Labda alikuwa akitawala Waislamu kwa sasa, au alikuwa ni kiongozi wa majeshi yao! Kwa hali hiyo, lazima atakuwa ni mtu mkubwa wa daraja ya juu miongoni mwa watu wake.

Lazima wawe wamempa mwana wa Mtume, ambaye Waislamu wanamtukuza katika namna ambayo haijatokea katika historia, amma ni mtawala wao au kiongozi wao mkubwa! Ndipo hapo wazo fulani likamjia.

“Waislamu na Warumi wanapigana vita wao kwa wao, na vita huanza muda wowote kati yao. Hivyo kama nitakwenda katika jeshi la Warumi wakati wa vita, nitaweza kuingia upande wa jeshi la Waislamu kama mateka.

Na Waislamu bila shaka watanichukua na kunipeleka kwa kiongozi wao, ambaye atakuwa ndiye mwana wa Mtume, na ndipo nitakapomueleza kilichotokea katika ndoto yangu na kumueleza kila kitu, Bila ya shaka kabisa atanielewa.

Aidha, atanifahamu kabla sijasema neno. Wazo zuri lilioje, nitafanya hivi hivi mara moja. Lakini subiri! Kama kujitokeza kwangu ni kama hivi, itajulikana kwamba ninatoka kwenye familia ya watu watukufu. Na Warumi watagundua kwa haraka kwamba nimekuwa mateka.

Kwa juhudi zote watadai nirudishwe, na watalipa fidia kubwa kwa kurudi kwangu! Ni lazima nijibadilishe na nionekane kama mtu mwingine ili mtu yeyote kati ya watu wangu asinijue, hivyo watadhani mimi nimepotea na wala sijakamatwa.”

Baada ya muda si mrefu mwenyewe akajibadili na kuvaa mavazi ya wahudumu na kujichanganya katika kundi lao. Wakati vita vilivyokuwa vikitarajiwa vilipoanza akajipenyeza na kuingia kwenye kundi la Waislamu, na mtu mmoja akadhani kwamba kajipatia mateka muhimu sana vitani, akamchukua kwa ajili yake mwenyewe.

Uvunjikaji wa moyo ulioje! Binti Mfalme hakujua chochote juu ya sheria za Waislamu. Alidhani kwamba angechukuliwa kama wafungwa wengine na kupelekwa kwa kiongozi wao mwenye cheo kikubwa, ambaye ndiye atakayempeleka kwa mtawala wa Waislamu kama ni ahadi ya utiifu kwake na kumthamini. Hakujua kile ambacho kingetokea.

Hofu ikamzidi na hakuna chochote kilichoipunguza hofu hiyo zaidi ya taswira za ile ndoto ambazo zilimpa utulivu moyoni mwake, kwani alikuwa yupo mbali zaidi na mistari ya mbele vitani, akiwa amechukuliwa kwenda kwenye nchi ambayo hakuijua kabisa!
Jambo jingine lililotokea ambalo hakulitegemea ni kwamba huyu askari aliyemchukua aliamua kumuuza sehemu iliyo karibu zaidi na hapo ambapo watumwa waliuzwa. Huyu askari aliona ni bora kurudi nyumbani akiwa na Dinari zake za dhahabu, badala ya kwenda na huyu mtumwa anayesikitisha. Binti Mfalme akawa hana matumaini ya kurudi katika nchi yake, ambapo aliondoka bila ya kurudi. Akifikiria kwamba kweli atafika nchi ambayo iliujaza moyo wake kwa nuru. Hakuliuliza hili, wala hakukipata alichokitarajia.

Kama isingekuwa ni kutokana na michomo ya nuru iliyokuwa ikimjia kila mara, kukata kwake tamaa kungesababisha kifo chake; uchungu mkubwa ungeweza kumuumiza. Mfanya biashara alimnunua, pamoja na wafungwa wengine, ndipo akauona mwisho usioeleweka kwake kutokana na ndoto yake ile unapotea hivi hivi mbele ya macho yake.

Safari nyingine ikaanza kuelekea kusikojulikana… lakini kwa nini huyu mfanya biashara alikuwa akimtendea kwa heshima sana, tofauti na wengine? “Je, Mimi si mtumwa tu masikini kama wengine, anaogopa hata kuniangalia usoni!”

Baada ya siku chache kupita, wakaingia katika mji wa Samaraa’. Ndipo hapo ambapo mtu anayeonekana ni mwenye kuheshimika akatokea, mfano wake alikuwa bado hajawahi kuuona kabla.

Alikuja karibu yake na akajitambulisha kuwa yeye ni Ali ibn Muhammad al–Hadi, na akamnunua kutoka kwa mfanya biashara yule.

Jinsi alivyostaajabu, yaani ilikuwa karibu na kupata mshtuko alipojitam- bulisha kwake, na yote hayo yalimtokea tangu mwanzoni… Je, hii inaweza kuwa na hekima ndani yake… huu ndio ufumbuzi… lakini hii ni nyumba ya kimasikini inayosikitisha… na siyo hekalu la mtawala mkubwa.

Na wakati alipoingia ndani ya nyumba ile, akaona ulimwengu mkubwa na mpana ambao hauwezi kupimwa kwa mbingu na ardhi. Ni Imam Hasan al-‘Askari ambaye alimchumbia akiwa ndotoni.

Haikuchukua muda kabla ya binti mfalme, ambaye alichagua jina la “Nargis” kama ndilo jina lake, akawa mtu muhimu katika nyumba ya Mtume. Juhudi zake kubwa zilimsaidia kunywa kutoka kwenye maarifa ya ufunuo (wahyi).

Kabla ya muda mrefu kupita, mtoto mchanga anayengojewa akatokeza katika ulimwengu huu kuzihuisha kumbukumbu za Mtume wa Allah (s.w.t) kwenye nyumba toharifu. Mbora wa waaminifu (Imam Hasan al-‘Askari) alimuona mtoto yupo sawasawa na alivyokuwa Mtume Mtukufu ambaye kimaumbile na sifa zake zilikuwa zikizungumziwa mara kwa mara.

Maisha Ya Ajabu Ya Imam Huyu!

Ilikuwa ni muhimu kwa Imam kutoweka haraka. Maadui walizidi kuhisi kwamba kuna kitu kisicho cha kawaida kinachotokea katika makundi ya wapinzani, ambao walikuwa wanapinga dhuluma.

Kwa sababu makundi haya hayakuungana; na waumini walihitaji kueleweshwa zaidi, kufahamu kwa undani, na kuwa na nguvu ya kumsaidia Imam. Zaidi ya hapo, kuuawa kwa Imam kungekuwa na maana kwamba ungekuwa ndiyo mwisho wa mpango mtukufu wa kuleta mageuzi ulimwenguni.

Hivyo ilikuwa ni lazima, kwamba Imam atoweke haraka asionekane baada ya kuuawa baba yake Imam Hasan al–‘Askari (a.s) katika mazingira ya kutatanisha.

Imam, akiichukua dhima hii mbali na kuwa umri wake ulikuwa bado ni mdogo; ilibidi kuchagua idadi ya watu wakati wa dharura hii ya kutoonekana ili aweze kuwasiliana na waumini na kuwapa moyo waweze kujitokeza katika muda muafaka. Watu hawa walijulikana kama Mabalozi (Sufaraa’), na walikuwa wanne.

Wakati wowote ambapo mmoja wao alipokufa, Imam katika makazi yake ya siri alimteuwa mwingine. Hii ilifanyika mpaka wa nne alipokufa. Imam akaona kwamba hali ilihitaji yeye kujitenga kabisa na watu. Hivyo mawasiliano yake na mabalozi yakasimamishwa, mpaka leo hii.
Wanazuoni wametaja matukio kadhaa na ripoti za kuthibitisha kwamba baadhi yao walipata heshima ya kuonana na Imam Al–Mahdi (a.s) tangu wakati huo. Mapokezi mengi yamesimuliwa yakiwa yamejaa mafunzo.

Hatua ya mwanzo ya kutoweka kwa Imam, ambapo alikuwa na mawasiliano na waumini kupitia kwa Mabalozi wanne, inaitwa ghaiba ndogo.

Hii ilikuwa sawa na kutua kwa jua, na mwanga wake ukiwa bado umebakia. Ama kwa hatua ya pili ya kutoweka kwake, ambayo ilianza baada ya miaka sabini ya ghaiba ndogo, iliitwa ghaiba kubwa.

Maimam walieleza bayana itakavyokuwa hatua hii, tabia na sifa za wale ambao watachukua dhima ya kuiongoza jamii ya Kiislamu na kuwaongoza kwenye malengo makuu ya Imam na kuandaa mazingira mazuri kwa ajili yake.

Majina ya Mabalozi wake (Sufaraa) wakati wa ghaiba ndogo ni: ‘Uthman ibn Sa’eed al–‘Amri. Anaitwa al-Samman (mchuuzi wa siagi), kwa vile sababu aliitumia kazi yake kuficha harakati zake za siri Muhammad ibn ‘Uthman ibn Sa’eed al-‘Amr Al-Hasan ibn Ruuh Abu al-Hasan ‘Ali ibn Muhammad al-Sumari.

Kuthibitisha Uhai Wake Na Ghaiba Yake

Mtume (s.a.w.w) amesema: “Kama hakuna chochote kilichobakia isipokuwa ni siku moja tu, Allah atamleta mtu kutoka katika kizazi changu ambaye ataijaza haki dunia hii, kama ambavyo itakuwa imejazwa na dhuluma.”

Hadithi nyingi zimepokelewa kuhusu kuzaliwa kwa Imam na ghaiba yake. Jumla ya hadithi 156 zimeandikwa katika vitabu sahihi vya Kisunni kuhusu Mahdi (a.s), na zaidi ya hadithi elfu moja zimo ndani ya vitabu vinavyotegemewa vya Kishi’a kuhusu kuzaliwa kwake, ghaiba yake, kwamba yeye ni Imam wa Kumi na Mbili na ni mtoto wa Imam Hasan al-‘Askari (a.s).

Takriban hadithi zote hizi zinafikiriwa kwamba ni miujiza, kwa sababu Maimamu Kumi na Mbili walikuwa wakimtaja wa mwisho wao, kuzaliwa kwake kwa siri, kwamba atakuwa na ghaiba mbili, ya pili itakuwa ni ndefu zaidi kuliko ile ya kwanza, na maelezo mengine yanayohitajika. Yote haya kwa hakika yametokea, ingawa bishara hizi ziliandikwa miaka kadhaa kabla ya matukio haya kutokea.

Imeelezwa kwamba wengi walijua kuhusu kuzaliwa kwake, na wafuasi wake wengi na watu waaminifu wamemuona (a.s) tangu anazaliwa mpaka leo hii, ambacho ndicho kipindi cha ghaiba kubwa. Kama ambavyo kuza- liwa kwa baba zake kunavyojulikana, kuzaliwa kwake pia kwajulikana.

Upuuzi wa wabishi na shaka zao kuhusu muda mrefu wa kutoweka kwake, kuzaliwa kwa siri, na umri wake mrefu uliobarikiwa si hoja imara za kutosha za kutoa majibu dhidi ya ushahidi imara ulio bayana.

Sheikh al-Saduuq Muhammad ibn Babawaiyh anasimulia kwa mfululizo wa mapokezi mpaka kwa Ahmad ibn Ishaq, kwamba amesema: “Nilimtembelea al-Hasan ibn Ali al-Askari, kutaka kumuuliza kuhusu mrithi baada yake.

Akaanza kwa kusema, ‘Ewe Ahmad ibn Ishaq; hakika Allah hajauacha ulimwengu tangu kuumbwa kwa Adam, na hatauacha mpaka Siku ya kufufuliwa bila ya mtu ambaye atakuwa ni hoja (Hujjah) kwa viumbe Wake. Kwa ajili yake yeye Hujjah, Allah ataondosha mabalaa kutoka kwa watu wa hapa ulimwenguni, na kwa ajili yake Allah atainyeshesha mvua, na kwa ajili yake Allah ataleta baraka hapa ulimwenguni.”

Akasema: Ndipo nikamuuliza, Ewe mwana wa Mtume wa Allah, basi ni nani ambaye ni Khalifa baada yako? Akasimama haraka na kuingia nyumbani kwake, kisha akarudi tena akiwa amembeba mabegani mwake mtoto wa miaka mitatu ambaye uso wake uling’ara kama mwezi.

Akasema: “Ewe Ahmad ibn Ishaq, kama si kwa ajili ya heshima yako mbele ya Allah na kuwathamini wale ambao ni hoja za Allah kwa viumbe wake, nisingemle- ta mwanangu kwako.
Jina lake ni jina la Mtume wa Allah, na ataujaza ulimwengu kwa usawa na haki, kama ambavyo ulikuwa umejazwa kwa dhuluma na ufisadi.

Ewe Ahmad ibn Ishaq, mfano wake katika umma huu ni mfano wa Khudhr, na kama Dhu Al-Qarnain. Naapa kwa Allah atakapokuwa ghaiba hakuna atakayesalimika na upotevu mpaka Allah ampe uimara katika imani juu ya Uimamu, na akampa uwezo wa kuomba kwa kuharakishwa kurejea kwake Imam.”

Ahmad ibn Ishaq akasema: Basi nikamwambia: Ewe Maula, na je, kuna alama yeyote ambayo moyo wangu unaweza kuithibitisha? Hapo mtoto akasema kwa lugha ya kiarabu fasaha kabisa: “Mimi ndiye Aliyebakia kwa Allah katika dunia Yake (Baqiyyat Allah), na mlipa kisasi kwa maadui Zake, Hivyo usiulizie alama nyingine zaidi yangu mimi, Ewe Ahmad ibn Ishaq.”

Kisha Ahmad ibn Ishaq akasema: Basi nikawa mwenye furaha na kucheka, na wakati siku iliyofuata nilikwenda tena kwake na kumwambia: “Ewe mwana wa Mtume wa Allah, furaha yangu imekuwa kubwa kwa sababu ya yale uliyonipa. Je, jambo gani lililo sawa baina ya yeye na Khudhr na Dhu Al Qarnain?”

Akasema: “Ewe Ahmad ni muda mrefu wa ghaiba.”

Nikasema: “Ewe mwana wa Mtume wa Allah, je na ghaiba itakuwa ya muda mrefu?” Akasema: “Kwa jina la Mwenyezi Mungu ndiyo, mpaka wengi kati ya wale wanaomuamini waiache imani yao, na hakuna atakayeweza kuihifadhi imani yake isipokuwa wale ambao Allah ameahidi wilaya yetu, na ameiandika imani katika mioyo yao na amewapa msaada wa roho kutoka Kwake.

Ewe Ahmad ibn Ishaq, hili ni katika mipango ya Allah, na ni siri kati ya siri za Allah, na isiyoonekana (ghaib) kati ya yasiyoonekana ya Allah, hivyo pokea ninayokupa, yafiche, na ushukuru kwa hayo utakuwa pamoja na sisi kesho mahala patakatifu {Illiyin)”.

Miujiza mingi imetajwa katika kipindi cha ghaiba ndogo na katika siku ambazo mabalozi na maswahaba mahsusi wa Imam walikuwa wakimtembelea mara kwa mara. Baadhi yake imetajwa katika kitabu cha ‘Muntaha al-Aamal’ cha Shaikh ‘Abbas al-Qummi, na vinginevyo katika ‘al-Thaqib’ cha Shaikh al-Nuuri.

Kisa

Imesimuliwa kutoka kwa Ali ibn Sanan al-Moosali, naye kutoka kwa baba yake kwamba amesema: “Wakati Abu Muhammad (Imam Hasan Al- ‘Askari) (a.s) alipokufa wajumbe fulani walitoka Qum na kiasi kikubwa cha pesa walichokuja nacho, na hawakujua kuhusu kifo cha Abu Muhammad al-Hasan (a.s), hivyo wakati walipofika Sir man ra’a (mji wa Samuraa’) walimuulizia.

Watu waliwajibu: “Amefariki.” Hivyo wakase- ma: “Na yupi ndiye mrithi wake?” Baadhi ya watu wakasema: “Jafar, kaka yake.” Wakamuulizia, wakaambiwa kwamba ametoka kwenda safari ya matembezi ya kujiburudisha kwenye boti katika mto Dajlah, akinywa pombe na akiwa pamoja na waimbaji wa muziki.

Msimulizi akasema: “Basi tulishauriana wote kwa pamoja, na kisha tukakubaliana kwamba hizi sizo sifa za Imam, na baadhi wakawaambia wengine turudi na turudishe pesa za watu kwa wenyewe. Muhammad ibn Jafar al-Qummi akasema: “Subiri mpaka tumjaribu ili kuthibtisha kama ndiye yeye hasa”

Msimulizi akaendelea: “Basi wakamwendea kumsalimia na kusema: Ewe Bwana wetu sisi tunatoka Qum na kati yetu kuna kundi la Mashi’a na watu wengine, na tumeleta pesa kwa Bwana wetu Abu Muhammad al-‘Askari (a.s)”

Akasema: “Zipo wapi?”
Tukasema: “Tunazo”
Akasema: “Nipeni”
Tukasema: “Hizi pesa zina sifa ya pekee”
Akasema: “Na inaweza kuwa ni ipi?”

Wakamwambia: “Hizi pesa zinakusanywa na ni Dinari moja na Dinari mbili kutoka kwa watu tofauti tofauti miongoni mwa Mashi’a, kisha huzi- weka katika mkoba na kuufunga kwa kuuwekea muhuri.

Hivyo wakati tulipokuwa tukizileta kwa Bwana wetu Abu Muhammad (a.s) alikuwa akitutajia kiasi cha pesa ni kiasi fulani na Dinari kiasi fulani, kiasi hiki ni kutoka kwa fulani na kiasi hiki ni kutoka kwa fulani na fulani, mpaka amewataja watu wote, na kukitaja kilichofungiwa kwenye muhuri ni kitu gani.” Jafar akasema: “Mnasema uongo, mnasema kitu ambacho kaka yangu hakuwa akikifanya. Huu ni ujuzi wa mambo yasiyoonekana.”

Msimulizi akasema: “Wakati lile kundi waliposikia Jafar alichokuwa akisema wakawa wanaangaliana.”

Akasema: “Nipeni pesa”

Wakasema: “Sisi ni kundi lililokodishwa, hatutoi pesa isipokuwa mpaka tupate dalili tunazozijua kutoka kwa Bwana wetu al-Hasan (a.s). Kama wewe ni Imam, basi uuthibitishe, la sivyo, tutazirudisha pesa kwa wenyewe, waamue wazifanyie nini.”

Kisha msimulizi akasema: “Jafar ibn Ali baadaye akaenda kwa khalifa ambaye alikuwa Sir man ra’a (mji wa Samuraa’), na kumlalamikia dhidi yao, wakati walipoletwa mbele ya khalifa, akasema: “Mpeni hizi pesa Ja’far.”

Wakasema: “Mwenyezi Mungu aurudishe ukhalifa katika hali yake nzuri, sisi ni kundi lililokodishwa. Sio wenye kumiliki pesa hizi. Ni za kundi la watu waliotuomba tubaki nazo mpaka tumeona dalili na ushahidi. Hii ndiyo kawaida alivyokuwa akifanya Abu Muhammad Al-‘Askari (a.s).”

Khalifa akasema: “Na uthibitisho ulikuwa upi?”

Kundi likasema: “Alikuwa akituambia Dinari na wenyewe walizozitoa, kiasi cha pesa na ni kiasi gani. Kama Jafar anaweza kufanya yote hayo basi tutampa.

Tumekwishafika kwa Abu Muhammad Al-‘Askari (a.s) mara kwa mara na hii ndiyo ilikuwa dalili yetu kwake. Sasa amekufa, na kama huyu bwana ndiye mrithi wake basi lazima afanye hivyo hivyo kama alivyokuwa akifanya kaka yake. Vinginevyo, tutazirudisha pesa kwa wenyewe ambao wametutuma.”

Jafar akasema: “Ewe Kiongozi wa Waumini, hawa watu ni waongo, wanasema uongo kuhusu ndugu yangu, kwa sababu huu ni ujuzi wa mambo yasiyoonekana.”

Kisha Khalifa akasema: “Hawa ni wajumbe na mjumbe lazima asifanye kitu kingine chochote zaidi ya kusema alichotumwa.”

Msimulizi akasema: “Jafar akastaajabu, na hakuweza kupata jibu.” Kundi likasema: “Ewe Kiongozi wa Waumini, tupatie ulinzi mpaka tumeondoka katika nchi hii.”

Hivyo akaamrisha wapewe ofisa ambaye aliondoka nao. Wakati wameishatoka nje ya mji, mtoto mwenye sura nzuri sana, akionekana kama mtumishi akatoka nje, na akawaita, Wee fulani na fulani, na fulani na fulani, Msikilizeni Bwana wenu.”

Wakasema: “Je, wewe ndiye Bwana wetu?”
Akajibu: “Najilinda kwa Allah, mimi ni mtumishi wa Bwana wenu, basi nendeni kwake.”
Wakasema: “Tulitembea pamoja naye mpaka tukaingia katika nyumba ya Bwana wetu al-Hasan ibn Ali (a.s), ambapo tukamuona mwanawe al Qaim, Bwana wetu amekaa kitandani. Uso wake ulionekana kama pande la mwezi, na alikuwa amevaa nguo za rangi ya kijani.

Tulimsalimia na akatujibu Salaamu zetu, kisha akasema: “Kiasi cha pesa ni Dinari kadha na kadha, na fulani na fulani wameleta kiasi kadha na kadha”. Akaendelea kututajia mpaka akawataja wote. Akatutajia nguo zetu na wanyama wetu tunaosafiria, na ni wa aina gani. Tukaenda chini na kufanya sijda kwa ajili ya Allah, na kuubusu udongo uliokuwa mbele yake.

Tukamuomba tulivyokuwa tukivihitaji, akatukubalia. Kisha tukampa pesa, na yeye (a.s) akatupa maagizo kwamba tusizilete pesa kabisa katika mji wa Sirr man ra’a (mji wa Samuraa’), kwa sababu atatuwekea mtu katika mji wa Baghdad ambaye itabidi tumpe pesa, na kutoka kwake yeye zitakuja sahihi (barua zilizowekwa sahihi za Imam)”.

Tukaondoka na akampa Abu al-Abbas Muhammad ibn Jafar al-Qummi baadhi ya vifaa vya kuhifadhia maiti, na sanda na kumwambia: “Allah akuzidishie thawabu kwako.”

Msimulizi akasema: “Na wakati tulipofika katika kizuizi cha Hamadan Abu al-Abbas alipatwa na ugonjwa na akafariki. Baada ya hizi pesa kupelekwa Baghdad kwa wawakilishi waliochaguliwa na yeye, na barua zenye sahihi za Imam walikuja kuzichukua.”

Baadhi Ya Dalili Za Kurejea Kwa Imam Al-Mahd (A.S)

Dalili za kurejea kwake zipo katika sehemu mbili: Dalili zilizo wazi na dalili zisizo wazi. Ama kwa dalili zilizo wazi, kwa jumla ni kama zifuatazo:

Kutokea Kwa Dajjal:

Huyu ni mtu aliyelaaniwa ambaye atadai kwamba yeye ni Allah, na kwa sababu yake Ulimwengu utakuwa katika machafuko na umwagaji damu, Vita vitaanza kati yake na jeshi la Imam, na atauawa na Imam (a.s), au Isa ibn Maryam (a.s) (Yesu).

Ukelele:

Hadithi nyingi zimepokewa zikitaja kwa uwazi ukelele toka mbinguni. Katika hadithi ya al-Mufadhil ibn Amr aliyeipokea kutoka kwa Imam Jafar Sadiq (a.s) kwamba amesema:

“Al-Qaim ataingia Makka na ataonekana pembeni ya nyumba (Kaaba), na wakati jua litakapochomoza na kuangaza Mpiga Ukelele atapiga ukelele kuwaeleza viumbe huku akiwa kati kati ya jua kwa lugha ya kiarabu fasaha ambayo vyote vilivyoko mbinguni na ardhini vitaelewa; Enyi watu kati ya viumbe, huyu ni Al-Mahdi, wa kizazi cha Muhammad (na atamwita kwa jina hilo hilo na kun’ya ya babu yake Mtume wa Allah, na ukoo wake unarudi mpaka kwa baba yake Al-Hasan, Imam wa kumi na moja, mpaka kwa Al-Hussain ibn Ali, amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yao wote), kuleni kiapo cha utii kwake na mtapata uongofu. Zifuateni amri zake, ama sivyo mtapotea.

Wa mwanzo kumbusu mikono yake watakuwa ni Malaika, kisha Majini, kisha viongozi watawala. Watasema: “Tumesikia na tumetii.” Hakutakuwa na kiumbe yeyote asikiaye ambaye atakosa kuusikia huo ukulele.

Na viumbe wote watakuja kuanzia wale wafugaji wanaohama hama kutafuta malisho ya mifugo hadi wale waliostaarabika, na kuanzia wale wa ardhini nchi kavu hadi baharini, watazungumza kwa kila mmoja wao, na kuulizana kwa kila mmoja kuhusu walichokisikia kwa masikio yao.

Na wakati jua litakapokuwa karibu na kuzama Mpiga Ukelele kutoka upande wa Magharibi atapiga ukelele akisema: “Enyi watu kati ya viumbe, Bwana wenu ameonekana katika bonde la ardhi kavu ya Palestina, naye ni ‘Uthman ibn ‘Anbah al-Amawi, anayetokana na kizazi cha Yazid ibn Muawiyah.

Kuleni kiapo cha utii na mtaongoka, na wala msiache kumtii yeye kwani mtapotea”.

Malaika, Majini na viongozi watawala wataupinga usemi wake na kuukanusha, wakimwambia: “Tumesikia na tunakataa”. Watu wote wasioamini, wenye shaka, wanafiki, na makafiri watapotea kutokana na ukelele huu wa mwisho”.

Kutokeza Kwa Al–Sufyani:

Yeye ni Mtu Mwenye Sura Mbaya. Kwenye sura yake kuna alama za ndui, na yeye anatokana na Yazid ibn Mu’awiyah. Mtu huyu aliyelaaniwa anamiliki miji mikuu mitano:

Damascus, Hams, Palestina, Jordan na Qanserinarin. Hutuma jeshi lake sehemu zote na miji yote. Machafuko (fit-nah) yatawapata sana wapenzi na wafuasi wa Ali ibn Abi Talib (a.s), hasa walioko pembezoni mwa miji hii.

Wakati jeshi lake litakapofika katika ardhi ya jangwa lililo baina ya Makka na Madina, Allah atamtuma Malaika katika ardhi hiyo na atapiga ukulele akisema: “Ewe ardhi wadidimize watu hawa waliolaaniwa,” na ardhi itawazamisha watu hawa pamoja na silaha zao zote.

Wakati al–Sufyani atakapolisikia hili atakwenda kutoka Sham kuelekea Kufah na atasababisha uharibifu hapo.

Baada ya kuwasili kwa al–Hujjah (a.s) (Huyu ni Imam Mahdi) hapo, al–Sufyani atakimbia kuelekea Shamu, na Imam atatuma jeshi kumfuata ambalo litamuuwa katika jiwe la Bayt al Muqaddas.

Kuuawa Kwa Mtu Mwenye Roho Safi (Al–Nafs Al Zakiyah):

Ambaye ni kutoka katika kizazi cha Mtume Muhammad (s.a.w.w) na ambaye atauawa baina ya nguzo na eneo takatifu (al–rukn wa al–maqam) katika Ka’aba tukufu.

Kutokeza Kwa Al–Sayyid Al–Hasani.

Yeye ni mtu anayeonekana ni mwenye umbile zuri, ambaye atatokea upande wa al–Daylani na Qazwin. Hasemi uongo wala hawaiti watu wamfuate. Yeye anatokana na wafuasi wa kweli wa Maimamu kumi na mbili. Anafuata shari’ah sahihi na hadai kuwa yeye ama ni mwakilishi au ni Al–Mahdi (a.s); lakini ni kiongozi anayetiiwa.

Kabla ya kutokeza kwake dunia itakuwa imejaa kufru na dhuluma, na watu watateswa na kuumizwa na madhalimu. Al–Sayyidal–Hasani ataomba misaada kusaidia dini ya Nyumba ya Muhammad (s.a.w.w). Waumini watamsaidia, na atatawala akiwa kiongozi anayefuata haki.

Kidogo kidogo ataanza kuwashinda watu madhalimu na tawala dhalimu na atauondoa uchafu wa madhalimu na kufru duniani.

Atakapofika Kufa akiwa na wafuasi wake atapata habari kwamba Al–Mahdi (a.s) ameisharejea, ndipo hapo al–Sayyid al–Hasani atakuja na wafuasi wake kwa Imam (a.s) na atamuomba atoe ushahidi kuthibitisha Uimamu na urithi kutoka kwa Mitume.

Imam al-Sadiq (a.s) amesema: “Na yeye (akiwa na maana ya Al-Sayyid al- Hasan) hakulihitaji hilo bali kuwaonyesha wafuasi wake baraka za Imam Mahdi (a.s) ili waweze kula kiapo cha utii kwake.”

Basi ndipo hapo Imam (a.s.) atawaonyesha ushahidi wa Uimamu na urithi toka kwa Mitume, na al-Sayyid al-Hasan na takriban wafuasi wake wote watakula kiapo cha utii cha kumfuata isipokuwa wachache.

Kupatwa kwa jua katikati ya mwezi wa Ramadhan, na kupatwa kwa mwezi mwishoni mwa mwezi wa Ramadhani.

Kutoafikiana kwa Bani Abbas, na kumalizika kwa utawala wao, ambao walikuwa wameuweka.

Ama juu ya alama zisizo dhahiri, zipo nyingi, baadhi ya hizo tayari zimek- wishatokea na nyingine bado. Hapa tutatoa baadhi yake kwa ujumla:
1. Ukame mkubwa kabla ya kuja kwake.

2. Tetemeko kubwa la ardhi, na kutokea kwa ugonjwa wa kuambukiza utakaoenea katika nchi nyingi.

3. Mauaji makubwa na umwagaji damu kwa sababu ya kuwepo kwa mataifa na majeshi mbalimbali.

4. Kutokeza kwa mataifa ya watu weusi toka Khurasaan.

5. Ulimwengu kujaa dhulma, kukosa imani (kufru), ubadhirifu na dhambi.

Qur’ani Tukufu Yasema Juu Ya Imam Al – Mahdi (A.S)

Qur’ani iliteremshwa kwa watu ili kuwaongoza katika mambo yao yote ya maisha na kuleta mageuzi katika jamii ya wanadamu, kuifanya jamii iweina haki na yenye mwongozo wa kumfuata Allah (s.w.t).

Mwongozo hautakuwa umekamilika mpaka kuwepo na mtu ambaye ataiongoza jamii na kukabiliana na majaribu ya kuipotosha Qur’ani, na kutafsiri Aya zake isivyotakiwa katika namna itakayowapendeza watawala waovu na madhalimu.

Qur’ani imemuelezea kwa kifupi mtu huyu ambaye ana dhima ya kuilinda Qur’ani ili tuweze kumjua, kumfuata, na tuongozwe na yeye. Qur’ani ina sehemu nyingi zinazomtaja ambazo mwanzoni huweza kuonekana kama maelezo yake yamejificha, lakini baada ya kutafakari na kufikiri kwa undani tutakuja kuona kwamba yanamhusu yeye.

Imebakia katika hali ya maelezo kwa kifupi ili madhalimu wasiweze kuivuruga Qur’ani na kuiondosha ili iwe mbali na watu. Maimam wa Ahlu–Bayt (a.s) walishaanza kuvielezea wazi wazi hivi vifungu vya habari vinavyomhusu Imam kwa watu, na kuwatafsiria watu wachamungu.

Tutaelezea hapa baadhi yao: Al–Mahdi ni nuru ya Allah (s.w.t): Allah (s.w.t) anasema:

يُرِيدُونَ أَنْ يُطْفِئُوا نُورَ اللَّهِ بِأَفْوَاهِهِمْ وَيَأْبَى اللَّهُ إِلَّا أَنْ يُتِمَّ نُورَهُ وَلَوْ كَرِهَ الْكَافِرُونَ {32}

هُوَ الَّذِي أَرْسَلَ رَسُولَهُ بِالْهُدَىٰ وَدِينِ الْحَقِّ لِيُظْهِرَهُ عَلَى الدِّينِ كُلِّهِ وَلَوْ كَرِهَ الْمُشْرِكُونَ {33}

Wanataka kuzima nuru ya Mwenyezi Mungu kwa vinywa vyao, na Mwenyezi Mungu atakamilisha nuru yake ingawa makafiri watachukia. Yeye ndiye aliyemtuma Mtume wake kwa mwongozo na kwa dini ya haki ili ishinde dini zote ingawa washirikina watachukia”
(Qur’ani; 9:32-33).

Imam al–Sadiq (a.s) amesema: “Kwa sababu ya Qa’im anayetokana na kizazi cha Mtume Muhammad (s.a.w.w) basi atakapotokea Allah (s.w.t.) atamfanya awe juu ya dini zote, mpaka kutakuwa hakuna yeyote aabudi-waye isipokuwa Allah (s.w.t).”17

Al–Mahdi ni neno lenye kubaki: Allah (s.w.t) anasema:

وَجَعَلَهَا كَلِمَةً بَاقِيَةً فِي عَقِبِهِ لَعَلَّهُمْ يَرْجِعُونَ {28}

“Na akalifanya neno liwe lenye kubaki katika kizazi chake ili warejee” (Qur’ani: 43:28).

Imepokewa kutoka kwa Abu Huraira amesema: “Nilimuuliza Mjumbe wa Allah (s.a.w.w) juu ya aya hii. Yeye (s.a.w.w) akasema:

“Uimamu uliwekwa kwenye kizazi cha Al–Husein (a.s). Maimamu Tisa watatokana na kizazi chake, na kutokana na wao atatokea kiongozi - Mahdi (a.s) wa umma huu.”
Kisha akasema: “Kama mtu ataishi baina ya Rukn na Maqam (Huko Makkah al–Mukarrmah) na tena akafa akiwa anawachukia watu wa Nyumba yangu ataingia Motoni.”18

Al – Mahdi (a.s) ndiye mwenye kudhulimiwa: Allah (s.w.t) amesema:

وَنُرِيدُ أَنْ نَمُنَّ عَلَى الَّذِينَ اسْتُضْعِفُوا فِي الْأَرْضِ وَنَجْعَلَهُمْ أَئِمَّةً وَنَجْعَلَهُمُ الْوَارِثِينَ {5}

“Na tunataka kuwafanyia hisani wale waliodhoofishwa katika ardhi na kuwafanya viongozi na kuwafanya warithi” (Qur’ani; 28:5).

Imam Ali (a.s) amesema: “Wao ni watoto wa Muhammad, Allah (s.w.t) atamleta kiongozi Al–Mahdi (a.s) - baada ya jitihada zao, na atawafanya kuwa watukufu, na kuwadhalilisha maadui zao.”19

Al – Mahdi (a.s) ni Kiongozi:Allah (s.w.t) anasema:

وَيَقُولُ الَّذِينَ كَفَرُوا لَوْلَا أُنْزِلَ عَلَيْهِ آيَةٌ مِنْ رَبِّهِ ۗ إِنَّمَا أَنْتَ مُنْذِرٌ ۖ وَلِكُلِّ قَوْمٍ هَادٍ {7}

“Na wanasema wale waliokufuru, mbona hakuteremshiwa dalili kutoka kwa Mola wake? Hakika wewe ni mwonyaji tu, na kila kaumu ina kiongozi.’ (Qur’ani 13:7).

Mtume (s.a.w.w) amesema: “Mimi ni mwonyaji, Ali ni kiongozi, na kwa kila umma kuna kiongozi wa zama zake.”20

Amesema pia (s.a.w.w): “Ewe Jabir kama utakutana na mwanangu al–Baqir, fikisha salaam zangu kwake, kwani yeye ana jina langu, na ni mtu anayefanana mno na mimi.

Elimu yake ndiyo elimu yangu, hukumu yake ndiyo hukumu yangu.

Kati ya watoto wake wa kiume, saba ni watu wenye mamlaka, maasum, na ni Maimam wachamungu. Wa saba ni Kiongozi (Al–Mahdi (a.s)) ambaye ataujaza ulimwengu kwa usawa na haki baada ya kuwa ulikwishajazwa dhulma na ukatili.” (Biharul-Anwar, Jz. 46, uk. 227), na Yanabiul-Mawaddah, uk. 117.

Ndipo Mtume (s.a.w.w) akasoma aya hii:

وَجَعَلْنَاهُمْ أَئِمَّةً يَهْدُونَ بِأَمْرِنَا وَأَوْحَيْنَا إِلَيْهِمْ فِعْلَ الْخَيْرَاتِ وَإِقَامَ الصَّلَاةِ وَإِيتَاءَ الزَّكَاةِ ۖ وَكَانُوا لَنَا عَابِدِينَ {73}

“Na tukawafanya kuwa Maimamu wanaoongoza kwa amri yetu, na tukawapelekea wahyi kuzifanya kheri, na kusimamisha swala na kutoa zaka na walikuwa wanatuabudu Sisi tu.”
(Qur’ ani, 21:73).

Al – Mahdi (a.s) ndiye asiyeonekana:

Yahya ibn Qasim amesema: “Nilimuuliza al-Sadiq (a.s) kuhusu kauli ya Allah (s.w.t) isemayo:

الم {1}

ذَٰلِكَ الْكِتَابُ لَا رَيْبَ ۛ فِيهِ ۛ هُدًى لِلْمُتَّقِينَ {2}

الَّذِينَ يُؤْمِنُونَ بِالْغَيْبِ وَيُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنْفِقُونَ {3}

“Alif, Lam, Miim. Hicho ni Kitabu kisicho shaka ndani yake, ni muongozo kwa wamchao (Mungu). Ambao huyaamini yasiyoonekana na kusimamisha swala na kutoa zaka katika yale tuliyowapa.” (Qur’ani; 2:1 3)

Yeye alisema: Wachamungu ni wafuasi wa Ali (a.s) na asiyeonekana ni Hujjah aliye mafichoni - akimaanisha Imam Al–Mahdi (a.s).

Ushahidi kwa hili ni aya tukufu:

وَيَقُولُونَ لَوْلَا أُنْزِلَ عَلَيْهِ آيَةٌ مِنْ رَبِّهِ ۖ فَقُلْ إِنَّمَا الْغَيْبُ لِلَّهِ فَانْتَظِرُوا إِنِّي مَعَكُمْ مِنَ الْمُنْتَظِرِينَ {20}

“Na wakasema: Kwa nini haukuteremshwa Muujiza juu yake kutoka kwa Mola wake? Basi waambie; Hakika mambo ya ghaibu ni ya Mwenyezi Mungu tu, kwa hiyo ngojeni, kwa hakika mimi ni pamoja nanyi katika wenye kuungojea.”21 (Qur’ani, 10: 20).

Al – Mahdi (a.s) ni katika watu wenye Mamlaka:

Imam al Baqir (a.s) anasema kuhusu usemi huu wa Allah (s.w.t):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنْكُمْ ۖ فَإِنْ تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّهِ وَالرَّسُولِ إِنْ كُنْتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا {59}

“Enyi mlioamini! Mtiini Mwenyezi Mungu na mtiini Mtume na Wenye mamlaka katika ninyi, na kama mkigombana katika jambo lolote basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume ikiwa mnamwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho. Hilo ni bora zaidi na ni lenye mwisho mzuri zaidi.” (Qur’ani, 4:59).

“Wao ni Maimam kutokana na watoto wa Ali na Fatimah (amani iwe juu yao wote mpaka Siku ya Kiyama).”22

Ardhi kamwe haiwezi kumuacha: Allah (s.w.t) amesema:

إِنَّ اللَّهَ يُمْسِكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ أَنْ تَزُولَا ۚ وَلَئِنْ زَالَتَا إِنْ أَمْسَكَهُمَا مِنْ أَحَدٍ مِنْ بَعْدِهِ ۚ إِنَّهُ كَانَ حَلِيمًا غَفُورًا {41}

“Kwa hakika Mwenyezi Mungu huzuia mbingu na ardhi zisiondoke, na kama zikiondoka hakuna yeyote wa kuzizuia baada yake. Bila shaka Yeye ni Mpole, Mwingi wa kusamehe.”
(Qur’ani, 35:41).

Imam Al–Ridha (a.s) anasema: “Sisi ni Hujjat (Mamlaka) za Allah (s.w.t) katika viumbe Vyake, na wawakilishi Wake miongoni mwa waja Wake (viumbe Vyake), na ni walinzi wa siri Zake.

Sisi ni maneno ya uchajimungu na ni kishiko madhubuti. Sisi ni mashahidi wa Allah (s.w.t) na ni alama Zake katika viumbe Vyake.

Kwa ajili yetu, Allah (s.w.t) huzizuia mbingu na ardhi kufikia mwisho wake. Na kwa ajili yetu huifanya mvua inyeshe, na kuisambaza huruma Yake. Ardhi kamwe haitatengana na Mtetezi (Qa’im) anayetokana nasi, awe anaonekana ama awe ghaibu.

Kama dunia ingeachwa kwa siku moja bila ya mwenye mamlaka (hujjah) ingevurugika pamoja na vyote vilivyomo juu yake, kama ambavyo bahari huchafuka pamoja na vilivyomo ndani yake.”23

Yeyote amjuaye hatapata hasara kwa kuchelewa kuja kwake:

Al – Fudhail ibn Yasar amesema kwamba alimuuliza Imam Aba Abdillah al–Sadiq (a.s) kuhusu usemi wa Allah (s.w.t) usemao:

يَوْمَ نَدْعُو كُلَّ أُنَاسٍ بِإِمَامِهِمْ ۖ فَمَنْ أُوتِيَ كِتَابَهُ بِيَمِينِهِ فَأُولَٰئِكَ يَقْرَءُونَ كِتَابَهُمْ وَلَا يُظْلَمُونَ فَتِيلًا {71}

“Siku tutakapowaita kila watu pamoja na Imam wao, basi atakayepe- wa daftari yake mkono wa kulia, basi hao watasoma daftari yao, wala hawatadhulumiwa hata kidogo”. (Qur’ani, 17; 71).

Yeye (a.s) akasema: “Ewe Fudhail, mjue Imam wako, kwani kama utapata kumjua yeye, hutapata hasara kama jambo hili litawahishwa au kucheleweshwa, Yeyote amjuaye huyu Imam, na kisha akafa kabla ya mtekelezaji wa mpango mtukufu (yaani Imam Mahdi (a.s)) kutokea, hatakuwa tu yu katika daraja la wale walio chini ya uongozi wake, bali pia atakuwa katika daraja la wale walio katika jeshi lake.”24

Al–Mahdi na wafuasi wake ndio watu walioahidiwa kuirithi ardhi: Imam al–Baqir (a.s) akifafanua juu ya usemi wa Mwenyezi Mungu:

وَلَقَدْ كَتَبْنَا فِي الزَّبُورِ مِنْ بَعْدِ الذِّكْرِ أَنَّ الْأَرْضَ يَرِثُهَا عِبَادِيَ الصَّالِحُونَ {105}

“Na hakika tuliandika katika Zaburi baada ya ukumbusho kuwa: Ardhi (hii) watairithi waja wangu walio wema.” (Qur’ani, 21:105).

Akasema: “Vitabu vyote (vitukufu) ni maandiko. Na “watairithi waja wangu walio wema” Al–Qa’im (Imam al–Mahdi) na wafuasi wake.”

Imam Al–Sadiq (a.s) juu ya Aya hii ya Qur’ani anasema:

وَعَدَ اللَّهُ الَّذِينَ آمَنُوا مِنْكُمْ وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَيَسْتَخْلِفَنَّهُمْ فِي الْأَرْضِ كَمَا اسْتَخْلَفَ الَّذِينَ مِنْ قَبْلِهِمْ وَلَيُمَكِّنَنَّ لَهُمْ دِينَهُمُ الَّذِي ارْتَضَىٰ لَهُمْ وَلَيُبَدِّلَنَّهُمْ مِنْ بَعْدِ خَوْفِهِمْ أَمْنًا ۚ يَعْبُدُونَنِي لَا يُشْرِكُونَ بِي شَيْئًا ۚ وَمَنْ كَفَرَ بَعْدَ ذَٰلِكَ فَأُولَٰئِكَ هُمُ الْفَاسِقُونَ {55}

“Allah (s.w.t) Mwenyezi Mungu amewaahidi wale walioamini miongoni mwenu na kufanya vitendo vizuri, bila shaka atawafanya makhalifa katika ardhi kama alivyowafanyia makhalifa wake wa kabla yao, na lazima atawaimarishia dini yao aliyowapendelea, na atawabadilishia amani badala ya khofu yao. Wataniabudu, hawatanishirikisha na chochote, na atakayekufuru baada ya hayo, basi hao ndio wenye kuvunja amri”. (Qur’ani, 24:55).

Akasema: “Aya hii imeteremshwa ikimuhusu Imam Al–Mahdi (a.s) na wafuasi wake.”25

Siku ya kutokea kwake ndiyo Siku ya wakati uliowekwa: Allah (s.w.t) amesema:

قَالَ فَإِنَّكَ مِنَ الْمُنْظَرِينَ {37}

إِلَىٰ يَوْمِ الْوَقْتِ الْمَعْلُومِ {38}

“Akasema (Iblis) Mola wangu! Basi nipe nafasi mpaka siku watakayofufuliwa. Akasema (Mwenyezi Mungu) Hakika wewe ni katika wale waliopewa nafasi. Mpaka siku ya wakati uliowekwa” (Qur’ani, 15:36–38).

Imam Ali ibn Musa al–Ridha (a.s) amesema: “Yule ambaye sio mchamungu hana dini, na yule ambaye hana taqiyah (ruhusa ya kuificha imani halisi ya mtu katika hali na mazingira maalum), hana imani. Mtu mbora miongoni mwenu mbele ya Allah (s.w.t) ni yule anayefanya taqiyah.”

Wakamuuliza, Ewe mwana wa Mjumbe wa Allah (s.w.t), mpaka lini? Akajibu: “Mpaka Siku ya wakati uliowekwa, na ndiyo siku ya kutokea kwa Qa’im wetu wa Ahlul Bayt kuonekana.

Yeyote ambaye ataacha taqiyah kabla ya kuonekana kwake si katika wafuasi wetu.”

Wakamuuliza, “Ni nani huyo ambaye ni Qa’im wa Ahlul Bayt?”
Akasema: “Yeye ni wa nne katika kizazi changu, Mwana wa Bibi wa Mabibi. Kupitia kwake Allah (s.w.t) atausafisha ulimwengu kutokana na dhulma, na kuutakasa uwe safi kusiwe na aina yeyote ya ukandamizaji. Yeye ndiye ambaye watu watakuwa na shaka juu ya kuzaliwa kwake kama kweli ameishazaliwa.Yeye ndiye mtu ambaye atakuwa ghaibu kabla hajatokea.

Kama akitokea ulimwengu utang’ara kwa nuru yake aliyonayo, na mizani ya haki itawekwa baina ya watu ili kusiwe na mtu wa kumdhulumu mwengine yeyote.

“Kwa heshima dunia itainama kimiujiza kwa ajili yake. Yeye ndiye mtu ambaye muitaji aitaye toka Mbinguni ambaye watu wote waliopo duniani watamsikia, kuwaeleza watu wamfuate yeye, akisema: “Hakika Hujjah wa Allah (s.w.t) ameshatokeza katika nyumba ya Allah (s.w.t), basi mfuateni yeye kwani ukweli upo pamoja naye na upo ndani yake”.

Hii ni kauli ya Allah (s.w.t):

إِنْ نَشَأْ نُنَزِّلْ عَلَيْهِمْ مِنَ السَّمَاءِ آيَةً فَظَلَّتْ أَعْنَاقُهُمْ لَهَا خَاضِعِينَ {4}

Tungependa tungewateremshia kutoka mbinguni Muujiza, na shingo zao ziwe zenye kuinama”. (Qur’ani, 26:4).

Al Mahdi (a.s) atamuua Iblis (Shetani): Is’haq ibn Ammar amesema: “Nilimuuliza Zain al–‘Abideen (Imam Sajjad) (a.s) kuhusu kuahirishwa kwa adhabu kwa huyu (shetani) na Allah mpaka siku ya wakati uliowekwa ambao Ameutaja katika Kitabu Chake:

قَالَ فَإِنَّكَ مِنَ الْمُنْظَرِينَ {37}

إِلَىٰ يَوْمِ الْوَقْتِ الْمَعْلُومِ {38}

“Hakika wewe ni katika waliopewa nafasi. Mpaka siku ya wakati uliowekwa” (Qur’ani, 15:37 38).

Akasema: “Siku ya wakati uliowekwa ni siku ya kutokea kwa Mtetezi (al–Qa’im). Hivyo Allah (s.w.t) atamleta, na wakati akiwa Kufah, Iblis atakuja huku akiwa amepiga magoti akisema: “Ole wangu mimi kuanzia siku ya leo.” Imam atamkamata utosini na kumpiga shingoni mwake. Hiyo ndiyo siku ya wakati uliowekwa, mwisho wa maisha yake.”26

Vitabu Vinavyozungumzia Juu Ya Imam Al–Mahdi (A.S)

Kuna vitabu vingi ambavyo vimeshughulika katika habari za Imam al–Mahdi (a.s) na kuelezea juu ya maisha yake, anavyoonekana alivyo, kazi yake, na kitakachotokea wakati wa kipindi cha ghaiba yake. Kuna vitabu vingine ambavyo vimeweka majalada maalum au sura maalum kuelezea juu ya Imam Al–Mahdi akiwa miongoni mwa Maimamu wengine, amani iwe juu yao wote hao.

Tumechagua kwa ajili yako vitabu kadhaa vyenye manufaa, ambavyo pia vinaielezea mada hii katika mitazamo mbalimbali na vitabu hivyo ni:

1. Imam Angojewaye, Tegemeo la Maasum Watoharifu (cha Kiarabu)

Mtunzi: Muhammad Ridha Hakini (aliyefariki 1992).

Toleo la; mwanzo; 1995, al–A’lami Organization, Beirut. Ukubwa: kurasa kubwa 680.

Mada: - (a) Imam Mahdi (a.s) katika mtazamo wa Kisunni. (b) Nasaba ya Imam (c) Miujiza ya Imam wakati wa kuzaliwa kwake. (d) Imam al–Mahdi (a.s) ndani ya Qur’ani. (e) Maimam waomba kutokea kwa Kiongozi. (f) Kutajwa kwa wale waliopata bahati ya kuonana naye katika ghaiba yake ndogo na katika ghaiba yake kubwa, na pia waliopata kumuona katika ndoto zao. (g) Idadi ya masahaba zake. (h) Sababu ya kuwa kwake ghaibu. (i) Faida ya kuwepo kwake (wakati akiwa yupo ghaibu). (j) Umri wake mrefu. (k) Dalili zitakazoonekana wakati atakapokuwa karibu kutokea. (l) Mashairi yanayomhusu yeye.
2. Mlengwa Anayengojewa (cha Kiarabu)

Mtunzi: Sheikh Muhammad Mahdi al–Asefi.

Toleo la mwanzo: 1997, Dar al–Ghadeer Publications, Beirut. Ukubwa kurasa za ukubwa wa kati 680.

Mada: - (a) Uhusiano baina ya kungojea na harakati. (b) Sababu kuhusu kuchelewa kutokea kwake. (c) Wale wanaoandaa mazingira mazuri ya kuja kwa Imam Al–Mahdi. (d) Maswahaba zake, idadi ya viongozi wa wafuasi wake. (e) Sifa za maswahaba zake. (f) Ni yupi anayengojea, sisi au ni Imam? (g) Ubora wa kungojea (kwa ajili ya kutokea kwa Imam).

3. Utafiti kuhusu Al Mahdi (a.s) (cha Kiarabu)

Mtunzi: Sayyid Muhammad Baqir al–Sadr, aliyekufa shahidi 1400 A.H.

Toleo la; mwanzo: 1417 A.H, al–Ghadeer Center, Qum. Ukubwa: Kurasa kubwa 143.

Mada:- Shahidi Al–Sadr ameelezea masuala mengi muhimu katika kitabu chake hiki. Baadhi ya hayo ni: (a) Umri wa Imam. (b) Vipi Imam alivyokuwa Kiongozi. (c) Vipi tunaweza kuwa na imani juu ya kuwepo kwa al–Mahdi (a.s). (d) Kwa nini Imam hajatokea. (e) Taratibu za kubadili siku iliyoahidiwa.

4. Historia ya Ghaiba Ndogo (cha Kiarabu)

Mtunzi: Sayyid Muhammad al–Sadr, aliyekufa shahidi 1999.

Toleo la; tatu: 1986, Dar al–Taaruf Publications, Beirut. Ukubwa: Kurasa kubwa 664.

Mada: - (a) Huu ndio mfululizo mzuri wa mwanzo. (b) Encyclopaedia ya Imam al–Mahdi (a.s) iliyoandikwa katika vitabu vikubwa vinne. (c) Historia ya ghaiba ndogo, historia ya ghaiba kubwa, historia baada ya kutokea kwake, na siku ya wakati uliowekwa. (d) Vitabu vya mwanzo vinaelezea masuala mbalimbali, kama vile, wakati wa Imam al–‘Askari. (e) Historia ya Imam al–Mahdi (a.s) wakati wa maisha ya baba yake. (f) Muda unaomalizika ghaiba ndogo; wawakilishi wake wanne; wajibu wa wawakilishi hao; pesa zinazoachwa na Imam.

5. Serikali ya Al–Mahdi (a.s) (cha Kiarabu).

Mtunzi: Sayyid Bassim al–Hashemi.

Toleo la; mwanzo; 1994, Dar al–Haq Publications, Beirut. Ukubwa: Kurasa za ukubwa wa kati 172 .

Mada:- (a) Serikali ya Kweli Iliyokwishapangwa. (b) Al–Sufyani; Al–Yamani. (c) Mauaji ya mtu mwenye roho safi. (d) Kupigwa na kushind- wa jangwani (e) Ukelele utokao mbinguni. (f) Maswahaba wa Imam. (g) Kutokea kwa Imam. (h) Silaha za kupigania vita. (i) Mtazamo wa Imam kwa madhehebu tofauti. (j) Umri wa Imam. (k) Elimu ya kiwango cha juu katika kipindi cha wakati wake. (l) Baada ya Imam.

6. Jua la Magharibi (cha Kiarabu).

Mtunzi: Muhammad Ridha Hakimi Tarjuma: Haidar Aal Haidar

Toleo la, mwanzo: 1408 AH, Dar al–Islamiyah Publications, Beirut. Ukubwa: Kurasa kubwa 357.

Mada: - (a) Kuzaliwa kwa Imam. (b) Maumbile yake. (c) Ghaiba yake. (d) Imam katika maandiko kabla ya kuja kwa Uislam. (e) Imam katika vitabu vya Kisunni. (f) Imam katika vitabu vya Kishi’a (g) Imam ndani ya Qur’ani Tukufu. (h) Imam kulingana na Fikra za Kifalsafa na Nadharia za Kisayansi. (i) Kungojea.

7. Kamal al–Din wa tamam al ni’mah (cha Kiarabu) (Kukamilika kwa dini na neema ya mwisho)

Mtunzi: Shaikh Sadooq (aliyekufa mwaka 381 AH)

Toleo la mwanzo: 1390 AH, Dar al–Kutub al-Islamiyah Publications, Tehran. Ukubwa: Kurasa kubwa 686.

Mada: - Katika kitabu hiki mwandishi ameelezea sana juu ya ghaiba ya Mitume. Amezitaja pia hadithi kutoka kwa Maasum kumi na nne amani iwe juu yao, na barua zilizoandikwa kwa mkono na Imam mwenyewe.

8. Wajibu wa muumini kwa Imam al–Zaman (cha Kiarabu).

Mtunzi: Mehdi Hasan ‘Alaa al–Din.

Toleo la mwanzo: 1999. Ukubwa: Kurasa za ukubwa wa kati 76.

Mada: - Kitabu hiki kinataja mambo 54 ya wajibu wa muumini kwa Imam Al–Zaman (a.s). Mwandishi pia ametoa ushahidi wa kila hadithi mojawapo kati ya hizi kutoka katika hadithi za Ahlul Bayt.

9. Wanaofanya maandalizi kwa ajili ya Al–Mahdi (a.s) (cha Kiarabu).

Mtunzi: Shaikh ‘Ali al–Koorani.

Toleo la pili: 1987. al – Dar al – Islamiyah Publications, Beirut. Ukubwa: Kurasa kubwa 292.

Mada: - (a) Dalili zitakazoonekana itakapokaribia kutokea kwake. (b) Sifa zinazotajwa kuhusu anavyoonekana. (c) Dalili za ki–mbinguni na za ki-duniani. (e) Kushuka kwa Isa (a.s). (f) Shakhsiya za Maimam. (g) Hadithi kuhusu wanaofanya maandalizi kwa ajili ya Al–Mahdi (a.s). (h) Adhabu zilizoahidiwa zitakazotolewa kwa Wayahudi. (i) Watu wa Qum katika hadithi.

10. Kutokea kwa Al–Mahdi (a.s) kwa mtazamo wa Falsafa ya Historia. (cha Kiarabu).

Mtunzi: Shahidi Murtadha Mutahhari (aliyekufa shahidi 1399 AH). Mtarjumi: Muhammad ‘Ali Azarshab.

Toleo la; 1980, Dar al–Tawjih al-Islami Publications. Ukubwa: Kurasa za ukubwa wa kati 90.

Mada: - (a) Kumngojea Muondoshaji wa shida. (b) Aina mbili za Kungojea: Kungojea kwa kuharibu na kungojea kwa kujenga. (c) Msaada usioonekana katika maisha ya mwanadamu.

 • 1. Biharur al–An’war. Juz. 52.
 • 2. Biharul al – An’war. Juz. 27.
 • 3. Biharul al-An’war. Juz. 2.
 • 4. Nuur ath-Thaqalayn. Juz. 2.
 • 5. Dalailun-Nubuwah. Juz. 6.
 • 6. Wasa’il al Shi’a, Juzuu ya 16.
 • 7. Al–Kafiy. Juz. 7.
 • 8. Al–Kafiy. Juz. 8.
 • 9. Biharul al-An’war. Juz. 52.
 • 10. Ikmalud–Diin. Juz. 2.
 • 11. Biharul–An’war. Juz.78.
 • 12. Biharul–An’war. Juz. 10.
 • 13. Biharul–An’war. Juz. 52.
 • 14. Biharul–An’war. Juz. 52.
 • 15. Biharul–An’war. Juz. 51.
 • 16. Biharul–An’war. Juz. 10.
 • 17. Tafsir al–Qummi. Juz. 1.
 • 18. Kifayatal Athar.
 • 19. Kitabu cha Al–Ghaibah. Cha al Toosi.
 • 20. Tafsir al–Ayyashi.
 • 21. Kamalud–Din, Juz. 2.
 • 22. Kamalud–Din, Juz. 1.
 • 23. Kamalud–Din, Juz. 1..
 • 24. Al–Kafiy, Juz. 1
 • 25. Ghaibah cha An–Numani.
 • 26. Biharul-An'war. Juz. 52.