Sala ni nguzo kubwa ya dini. Mtukufu Mtume (s.a.w.) amesema: "Sala ni nguzo ya dini, mwenye kuivunja ameivunja dini, na mwenye kuisimamisha ameisimamisha dini." Mtukufu Mtume ameongeza: "Kila kitu kina uso, na uso wa Uislamu ni sala. Mwenye kuacha kusali ameuchafua uso wa dini." Imam Muhammad Baqir (a.s.) amemnukuu Mtukufu Mtume (s.a.w.) akisema: "Kitu cha kwanza atakachohesabiwa muumini (Siku ya Kiyama) ni Sala. Ikikubaliwa yatakubaliwa matendo mengine, na ikikataliwa yatakataliwa matendo mengine pia."

Kwa ufupi, kuna hadithi nyingi sana kutoka kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.) na Maimamu (a.s.) kuhusu umuhimu wa Sala kiasi kwamba katika hadithi moja, Mtukufu Mtume (s.a.w.) amesema kwamba kitu chenye kutofautisha baina ya Uislamu na ukafiri ni Sala.

Wakati huu tulionao una mitihani mingi sana, vijana wa Kiislamu na wazee pia wamejitumbukiza katika vitendo viovu na vichafu kiasi kwamba mtu hawezi kumtofautisha na mnyama, na pengine hata mnyama ni afadhali. Ili kuishinda mitihani hii na maovu haya, dawa yake ni kushikamana na Sala. Allah 'Azza wa Jalla anasema katika Qur'ani Tukufu: "… Hakika Sala huzuia mambo machafu na maovu, na kwa hakika kumbuko la Allah ni (jambo) kubwa kabisa, na Allah anajua mnayoyatenda." (29:45)