Table of Contents

Sura Ya 10: Kuteuliwa Kwa Yazid Kama Mrithi Wa Mu’awiyah

Mu’awiyah aliutumia uhai wake mrefu katika kufurahia madaraka na mali (utajiri). Kwa muda mrefu alikuwa ameilea tamaa ya kuacha baada ya kufa kwake, mamlaka yake na madaraka yake kwa mwanawe Yazid.

Vitu viwili vilimzuia Mu’awiyah kutoa athari ya kivitendo ya tamaa yake hiyo; (kwanza) mkataba na Hasan ambao ulimnyima haki ya kumteua mrithi wake na (pili) tabia mbaya isiyofaa ya mwanawe, Yazid. Mu’awiyah alikuwa katika namna ya kupendeza sana, amekiuka vipengele vingine vya mkataba, na kuvunjiwa kwa sharti la kukataza uteuzi wa mrithi wake hakukumletea tatizo lolote lile.

Kipingamizi kilichokuwa kizito hasa hasa kwa kulifikia lengo lake kilikuwa katika kutambua kwake kwamba pendekezo la kumteua Yazid kama mrithi wake katika nafasi ya ukhalifa lisingevutia uungwaji mkono mdogo tu bali pia kutapingwa kwa nguvu zote na watu waliokuwa na umuhimu na kuchukiwa na watu kwa ujumla.

Hata hivyo, (Mu’awiyah) alijitahidi kuwaondoa wale watu, kwa kiasi ilivyowezekana, ambao wangekuwa washindani hatari wa Yazid juu ya Ukhalifa. Hivyo aliafanya Abd al-Rahman bin Khalid atiliwe sumu (afe) na akamteua yule muuaji kuwa mkusanyaji wa kodi ya zaka wa sehemu ya Hims.1

Al-Mughira bin Shu’ba alikuwa haendani vyema na Mu’awiyah wakati akifanya kazi kama gavana wa mji wa Kufa. Ili ajipendekeze kwa Yazid alitoa dokezo kwa Yazid afanye atangazwe kama mrithi kwenye kiti cha Ukhalifa.

Mu’awiyah ambaye alikuwa kamwe hajawahi kuchukua matu- maini yoyote ya kupata pendekezo la namna hiyo kutoka kwa mtu yeyote yule mwenye akili, mara moja alimwita al-Mughira kuongea naye juu ya pendekezo lake hili. Al-Mughira alimhakikishia kufuzu kwa mpango huu huko Kufa na akasema kwamba, pamoja na Ziyad kama gavana, Basra nayo pia lazima watayapokea kwa kuyapendelea matakwa hayo ya Mu’awiyah.

Aliporudi Kufa, Mughira aliwaita watu mashuhuri wafahamikao kwa kuyaunga mkono kwao mafunzo ya Bani Umayyah na akawasihi wangojee ujumbe wa Mu’awiyah na wamsisitizie juu yake yeye kuhusu uteuzi wa Yazid kama mrithi wake. Jibu kwa ombi lake lilikuwa la kukatisha tamaa na al-Mughira alitumia fedha kiasi cha dirham elfu thelathini kupata kwa pamoja ujumbe unaokubalika ambao mwanawe Musa aliuongoza kwenda kwa Mu’awiyah, ambaye alikuwa mjanja sana wa kutoweza kudanganywa na mwonekano wa mambo. Baada ya kutoa uhakikisho wa kawaida kwa wajumbe, Mu’awiyah alimuuliza Musa kwa faragha kwamba ni kiasi gani baba yake alichokuwa amelipa kwa kununua imani zao. “Dirham elfu thelathini,” lilikuwa ndiyo jibu.

Kisha Mu’awiyah alimwita Ziyad ambaye alimtangaza kwa kosa kuwa ni ndugu yake kama hatua ya kupatia manufaa ya kisiasa, na akamfahamisha lengo lake hili. Ziyad alikuwa na mashaka makubwa sana kuhusu uhalali wa uteuzi wa mwasherati mwenye shari kama Yazid kwa ajili ya ukhalifa katika kumrithi Mu’awiyah, na akamtaka ushauri Ubayd bin Ka’b al- Numayri ambaye alishauri kwamba Yazid aambiwe arekebishe mwenendo wake kama anapenda kushinda juu ya maoni ya watu kuunga mkono uteuzi wake.

Ziyad alitoa jibu fupi kwa Mu’awiyah akisema kwamba haraka isiyo na mpango itakuwa na madhara kwenye mafanikio ya lengo lao.2

Al-Mughira alifariki dunia mwaka wa 49 A.H. au mwaka mmoja baadaye akiwa na umri wa miaka sabini.3 Ziyad alimrithi kama gavana wa Kufa. Aliwahi kufanywa kuwa gavana wa Basra, Khurasan na Sijistan katika mwaka wa 45 A.H. na Mu’awiyah ambaye baadaye aliongezea Bahrain na Oman kwenye mamlaka yake. Katika Ramadhani ya mwaka wa 53 A.H.

Ziyad pia alifariki dunia, na akitambua kwamba waunga mkono waliobaki pia nao wangekufa hivi karibuni, Mu’awiyah alitangaza urithi wa Yazid kwenye kiti cha Ukhalifa na watawaliwa walilazimishwa kukubaliana na mpango huo………..

Ingeweza kuonekana kwamba al-Mughira alikwisha uandaa uwanja vizuri sana kwa kupata mwitikio wa uhakika kwenye uteuzi wa Yazid kama mrithi wa Mu’awiyah, kwani waunga mkono maarufu wa Bani Umayyah wa Kufa walikwishapatikana, kukubaliana na matakwa ya Khalifa. Ziyad alimfuatia al-Mughira katika ugavana wa Kufa, na wakati akiwa Basra hakushindwa kuendeleza mafanikio ya mpango wa Mu’awiyah ingawa kwa tahadhari kubwa na shauku isiyozuilika.

Hata hivyo, huko Kufa, wote kwa pamoja, Ziyad na mwanawe Ubayd Allah waliwatia watu hofu kubwa kiasi kwamba hakuna hata mtu mmoja aliyethubutu kuzipinga amri zao. Kwa upande wa Syria, ilikuwa ndio ngome kuu ya Bani Umayyah na kama ilivyokwishaelezewa, Abd al-Rahman bin Khalid bin al-Walid, mshindani aliyefaa kwa kiti cha Ukhalifa, alikwishaondolewa kwenye njia ya Yazid.

Sa’id, mwana wa Khalifa aliyeuawa, Uthman, alilalamika dhidi ya uteuzi wa Yazid kwa urithi huo, akidai yeye mwenyewe alikuwa uzao bora, na kumkumbusha Mu’awiyah kwamba mengi ya madaraka yake zaidi yamepatikana kutoka kwa Uthman.

Madai haya yalikubalika, lakini Mu’awiyah alidai kuwa alikuwa ameulipa ukarimu wa Uthman kwake yeye kwa msaada alioutoa kwa Khalifa aliyekufa kwa kulipiza kisasi juu ya wauaji wake na kudai gharama ya fidia ya damu yake. Aliongeza kwamba kama nyumba yake ingekuwa imejaa watu kama Sa’id, wao wote kwa pamoja wasingelingana na Yazid.

Kisha Mu’awiyah alimwandikia Marwan gavana wa Madina, atoe kiapo cha utii kwa Yazid ambaye amemteua kama mrithi wake, na pia apate viapo kama hivyo kutoka kwa watu wa Madina. Hili lilimuudhi na kumkasirisha sana Marwan ambaye alimwona Mu’awiyah huko Damascus na akapinga kwa nguvu sana dhidi ya utenzi wa Yazid kwenye nafasi ya Ukhalifa kama kumpendelea kijana asiye na uzoefu na ujuzi wowote juu ya watu wanaoweza kupatikana wenye uzoefu unaofahamika wa kiutawala. Mu’awiyah alimtuliza kwa kusema kwamba yeye amefanywa kuwa mrithi wa Yazid.

Abd al-Rahman bin Abi Bakr alikuwa amechukizwa sana na uteuzi huu, akieleza kwamba Abu Bakr alikuwa hakuacha wosia wa upendeleo wa kurithi mwanawe, na kwamba Mu’awiyah amefuata njia na taratibu za Makaizar na wafalme wa kidunia. Maoni haya yaliungwa mkono na Imam Husein, Abdallah bin Zubeir, Abdallah bin Umar, Abdallah bin Abbas na Aisha, mjane wa Mtume.

Mu’awiyah lazima atakuwa amejua, kwa wasiswasi wake mkubwa sana, kwamba wapinzani wote hawa juu ya uteuzi wa Yazid kama mrithi wa baba yake katika nafasi hiyo walikuwa na nafasi zenye umuhimu mkubwa katika ulimwengu wa Kiislam.

Inaweza kukumbukwa pia kwamba wale wote ambao, miongoni mwa madhehebu mbalimbali za Kiislamu, waliokuwa wakionekana kana kwamba wameirithi dhamana halisi katika mambo yenye kuhusiana na Waislam, waliungana katika kutokukubaliana kwao juu ya uchaguzi wa Yazid kurithi kama Khalifa wa Uislamu.

Baadhi yao hawa walishikilia msimamo wao na walifanya ujasiri mkubwa kabisa katika matokeo ya baadaye yaliyokuwa mabaya mno, wakati wengine walikubali kulazimishwa kuuacha msimamo wao.

Mu’awiyah alijaribu kuwanyamazisha kwa njia ya vitisho au kuwapata kwa kuwapa mafungu makubwa makubwa ya fedha.

Katika kuitembelea kwake Madina aliongea kwa njia ya dharau sana na Imam Husein, akimwita (Imam) mwanakondoo wa kafara ambaye damu kwa hakika kabisa itakuja kumwagwa tu. Alipokutana na Abdallah bin Zubeir, ambaye alimfananisha na pomboo, alisema kwamba mkia wake ungekamatwa na kunyongwa nyongwa. Alimshutumu Abd al-Rahman bin Abi Bakr kwa kuwa katika hatua ya utu uzima ya uzulufu dhaifu (kipindi cha upungufu wa akili kutokana na uzee). Abdallah bin Umar hakuwa na hali bora zaidi.4

Wakati vitisho vilipothibitika kuwa havisaidii kitu, Mu’awiyyah alitoa vivutio vya mali ili kufanikisha lengo lake. Alipelekea pesa kiasi cha dirham elfu kumi kwa Abd al-Rahman bin Abi Bakr ambaye alikataa kubadilisha imani yake kwa manufaa ya kidunia. Majibu ya Abdallah bin Umar yalikuwa hayo hayo kwa zawadi sawa na hiyo. Imam Husein pia alikataa kupokea zawadi na fungu kubwa la fedha alilopelekewa na Mu’awiyah.

Aisha alichukua nafasi ya mbele katika kuupinga uteuzi wa Yazid kwenye nafasi ya Ukhalifa.
Jalal al-Din al-Suyuti anasimulia kwamba siku moja, akimwona Mu’awiyah akichukua kiapo cha uti kwa Yazid huko Madina, Aisha aliita kwa sauti kubwa akisema, “Nyamazeni! Mnafanya nini? Je, kuna Khalifa yeyote yule wa nyuma aliyepata kiapo cha utii kwa ajili ya mtoto wake?” Papo hapo Mu’awiyah alizifunga shughuli hizo.

Al-Hasan al-Basri anasema: “Mu’awiyah alifanya mambo manne, kila moja lilitosha kwa kuangamia kwake: Aliuchukua Ukhalifa kwa kusaidiwa na wapumbavu wasiojua kitu bila kushauriana na umma wote, ingawaje hata Masahaba wa Mtume walikuwa wanapatikana. Alimteua mtoto wake ambaye alikuwa mlevi na alibakia saa zote akiwa amelewa kuwa mrithi wake, alivaa dhahabu na hariri, na alichezea chombo cha muziki aina ya gitaa.

Tatu, alimtangaza Ziyad kuwa mtoto wa Abu Sufyan dhidi ya hadithi ya Mtume ambayo ilimpa mtoto nasaba au ukoo kutokana na wanandoa (mume na mke) na aliitenga adhabu ya kupigwa mawe mpaka kufa kwa mzinifu. Ya nne, alimuua Hujr na masahaba zake.5

Mu’awiyah alijua kwamba mtu wa kwanza aliye na umuhimu miongoni mwa kundi la watu wakubwa na mashuhuri wanaopinga uteuzi wa Yazid alikuwa Husein na hakupoteza muda katika kumwambia wakati wa ziyara yake mjini Madina kwamba yote ameyapata katika mpango wake isipokuwa watu watano wa kabila la Quraish wakiongozwa na yeye (Husein). Husein alishangaa, na alimuliza Mu’awiyah kama kweli alifikiria watu hawa walikuwa wakiongozwa na yeye.

Vile Mu’awiyah alivyoyarudia madai yake, Husein alipendekeza kwamba awaite hawa, wanaofikiriwa kuwa wafuasi wake, na awatake kuapa kiapo cha utii kwa mtoto wake. Kama wangefanya hivyo, Mu’awiyah hakuhitajia kuhofia hatari yoyote ile kutoka kwa Husein peke yake.
Mpango huu (mbinu) uliahirisha mzozo huo kwa muda huo na Mu’awiyah alirudi (alirejea) Syria.

Hata hivyo, ilionekana wazi kwa Husein, na vivyo hivyo kwa Mu’awiyah, kwamba kugeukia kwenye matumizi ya silaha hakuwezi kukwepeka kwa muda mrefu. Husein, hata hivyo, hakuwa tayari kufungua (kuanzisha) vita kwa misingi ya kawaida na hata vile vile kutokana na mkataba wa amani kati ya Mu’awiyah na Hasan. Mu’awiyah pia aliona siyo wakati muafaka kuanza vita, hivyo hali ya wasiwasi kuhusu amani ilikuwepo kati ya pande zote. Urefu wa kipindi hicho ulifupishwa kutokana na kifo cha Mu’awiyah mnamo mwaka wa 60 A.H.

  • 1. Kitabu: Tabari, Juz. 2, uk. 82
  • 2. Kitabu: Al-kamil, Juz, 3 uk. 418, cha Ibn al-Athir
  • 3. Kitabu: Tabari, uk. 174-175
  • 4. Al-Kamil ya Al-Athir, Juz. 3, uk. 421-424
  • 5. Kitabu: Al-Kamil, cha Ibn al-Athir, Juz. 2, uk. 25