Table of Contents

Sura Ya 11: Kifo Cha Mu’awiyah Na Kupanda Kwa Yazid Kwenye Ufalme

Katika mwaka wa 60 A.H. Mu’awiyah aliugua sana kiasi kwamba hakuweza kurudia afya (yake) njema katika kipindi kirefu cha maradhi yake. Ibn Hajr amesimulia kwamba siku moja Mu’awiyah alianza kulia. Katika kuulizwa sababu (ya kulia), Mu’awiyah alijibu kwamba kama upendo juu ya Yazid usingeshinda kabisa maamuzi yake, angejitafutia mwenyewe njia ya sawa.1

Akifafanua maelezo haya, Ibn Hajar anaandika kwamba Mu’awiyah kwa hiyo alikubali kabisa kwamba upendo kwa Yazid umemtia upofu kwenye njia ya uadilifu na kwamba amewatumbukiza Waislam, baada ya kufa kwake, kwenye mikono ya mtu mwenye dhambi kama Yazid ambaye angewaongoza kwenye kuangamia kabisa.2

Mwanzo wa maradhi yake ambayo yalikatisha uhai wake, Mu’awiyah ali- wahi kumwambia Yazid, “Nimewadhalilisha maadui zako wote, na nimewafanya Waarabu wote wanyenyekee kwenye mamlaka yako na wakubali urithi wako, lakini kuhusu suala la ukhalifa ambao takriban umekamilika, ninahofia kutokea matatizo kutoka kwa watu wanne: Husein bin Ali, Abdallah bin Umar, Abdallah bin Zubeir na Abd al-Rahman bin Abu Bakr.”3

Wakati kifo kilipokuwa kinamkaribia kwa haraka sana, Mu’awiyah aliagizia Yazid aitwe ambaye alikuwa hata hivyo, akijifurahisha kwa uwindaji huko Huwwarin.4

Mu’awiyah, kwa hiyo alimpa al-Dahhak bin Qays al-Fihr, kiongozi wa Shurta yake, kuufikisha kwa Yazid ujumbe huu kama utokavyo kwake, “Watendee watu wa Hijaz kwa heshima inayostahili, wapokee hapo makao makuu kwa wema (ihsani) na heshima, watazame vyema watu wa heshima na maarufu miongoni mwao ambao huja mjini mara kwa mara katika wakati ufaao. Wategemee sana watu wa Syria kama viganja vyako na mikono yako ukichukua tahadhari kwamba hawabakii nje ya nchi ya Syria kwa muda mrefu wasije wakajifunza na kujua tabia za nchi nyingine. Na ujue kwamba ninahofia kukutokea wewe matatizo kuto- ka kwa watu wanne tu, nao ni Husein bin Ali, Abdallah bin Umar, Abd al- Rahman bin Abi Bakr na Abdallah bin Zubeir.5

Mu’awiyah alifariki dunia katika mwezi wa Rajab mwaka wa 60A.H.6 Alikuwa gavana wa Syria akiwa na umri wa miaka 38, akawa Khalifa huru akiwa na umri wa miaka 58 na akafariki dunia akiwa na umri wa miaka 78 au kati ya miaka 73 na 85 kwa mujibu wa baadhi ya wanahistoria.7
Yazid alirudi Damascus baada tu ya baba yake alipokwishazikwa. Alipanda kwenye ufalme na watu wa Syria waliapa kiapo cha utii kwake.

  • 1. Kitabu: Al-Sawa'iq (pembezoni), uk. 56
  • 2. Kitabu: Al-Sawa'iq (pembezoni), uk. 58
  • 3. Kitabu: Tabari, Juz. 2, uk. 196-197
  • 4. Kitabu: Tabari, Juz. 2, uk. 203
  • 5. Kitabu: Tabari, Juz. 2, uk.197
  • 6. Kitabu: Tabari, Juz. 2, uk. 198
  • 7. Kitabu: Tabari, Juz. 2 uk. 19