Table of Contents

Sura Ya 12: Yazid

Mama yake Yazid, Maysum, alikuwa binti wa Bahdal bin Unayf al-Kalbi. Mu’awiyah alimwoa kutokana na uzuri wake wa kipekee. Alimjengea jumba kubwa la kifahari mkabala na Ghuta katika mazingira ya kupendeza na kuvutia sana na kupamba kwa fanicha za fahari ya Kifalme. Alimpatia mke wake huyo vito vya thamani aina mbalimbali na idadi kubwa ya mavazi yaliyotengeneza kwa vitambaa vya kuchaguliwa hasa, vinavyopendeza, na akaajiri vijakazi wengi kumtumkia katika anasa zake binafsi. Anasa zote alizopatiwa kwa matumizi yake na Mu’awiyah zilishindwa kumshawishi mke wake ambaye alikuwa mtoto wa jangwani, aliyezoea kwenye maisha magumu ya ardhi kame na isiyo na manufaa, na akiwa na mapenzi na maisha hayo.
Wakati mmoja kwa hiari yake mwenyewe aliangua kilio, alisema, “Lile hema lisilokingwa dhidi ya dhoruba za upepo wenye nguvu lina thamani kubwa zaidi kwangu kuliko jumba hili la Kifalme. Gauni lile ovyo ovyo la sufu nililokuwa nikivaa lilikuwa lenye thamani zaidi kwangu kuliko nguo hizi nzuri zenye kupendeza. Niliona utamu zaidi kula nyama ya mkate mkavu kwenye pembe ya makazi yangu kuliko kula vipande vya mikate hii mieupe na mizuri na nilikuwa mwenye kupenda zaidi umbo la kijana aliye mwembamba, mrefu na asiyependeza machoni wa ukoo wangu na kabila langu kuliko bonge la mtu, katili mwenye tabia mbaya.”

Mu’awiyah alipoyasikia maneno haya, alikasirika sana, hasa katika utajo wa kushusha heshima ulioelekezwa kwake. Alimtaliki Maysam ambaye alikuwa amekwishakuwa mjamzito.

Alimhamisha kwenda kuishi na jamaa zake katika jangwa la Najd.1 Yazid alizaliwa katika mwaka wa 22 A.H.,2 na alipozipata habari hizi, Mu’awiyah aliagizia aletwe kwake.3

Toka mwanzoni mwa ujana wake Yazid alishikamana na njia za kiovu na aliishi maisha ya kifisadi. Mizaha ambayo kwamba alikuwa anaicheza na wanyama imehifadhiwa katika (kumbukumbu za) historia. Alikuwa mtu wa kwanza kumfanya chui mweusi kupanda farasi. Alifundisha nyani kupanda punda na kushindana katika mashindano ya farasi dhidi ya wapanda farasi wenye sifa kubwa. Yazid alipata kuvuma kwa sifa mbaya kwa mazoea ya ulivi na Abdallah bin al-Zubeir alimpa jina la Sakran, yaani “mlevi.”4

Hakuweza kujizuia na kulewa wakati alipoutembelea mji wa Makka kwenda kutekeleza ibada ya Hijja ili akapate kuungwa mkono na watu kwa ajili ya uteuzi wake kama mrithi wa baba yake.5

Al-Waqid alimnukuu Abdallah bin Hanzala akisema “Wakati wa utawala wa Yazid tulihofia kwamba mawe yangetunyeshea juu yetu kwani hakuwaacha mama zake wa kambo, mabinti na dada zake kutokana na utongozaji wake wa kitamaa. Alikunywa vileo kwa uhuru kabisa na aka- puuza kusimamisha swala.6

Ilikuwa siyo kwamba Yazid alitenda dhambi tu kwa kwenda kinyume na amri za kisheria za Qur’ani na Sunna za Mtume, bali hata mawazo yake pia yalikuwa ya kidhambi vivyo hivyo. Ibara zake, kama zilivyotafsiriwa hapa chini, ambamo ndani yake anazichukulia kwa wepesi amri za kisheria za Qur’ani zinatoa ushuhuda kuhusu ukweli wa maelezo haya: “Sina muda wa kupoteza kutokana na kusikiliza gitaa na matuazi na nikawa nasikiliza adhana (wito) kwa ajili ya kwenda kusimamisha swala na nimechagua mwanamwali mzuri wa kikombe badala ya wanawake wa peponi (Mahurlain)”.

Aliikana pia imani ya kufufuliwa viumbe kama anavyosema katika ibara zilizotafsiriwa hapa chini: “Niimbie kuhusu matendo ya Abu Sufyan kule Uhud wakati alipoziingiza nyumba za maadui zake katika maombolezo.

Msiwe na matumaini ya kukutana kwetu baada ya kuachana ambako kunasababishwa na kifo. Mnaweza kuwa mmesikia kuhusu maisha ya mara ya pili, lakini hizi ni simulizi ndefu ambazo zinapotosha watu.”

Ibara hizi zinaonyesha wazi kabisa kwamba Yazid alitawaliwa na imani za kipindi cha giza cha kabla ya Uislamu, na kwamba alikuwa akiendekeza tamaa ambazo zilisababisha makafiri kupigana dhidi ya Mtume wa Uislamu. Ibara zake alizotoa baada ya kifo cha kishahidi cha Husein, na tena wakati watu wa familia ya Husein walipofika kama watumwa mbele yake kule Damascus zinadhihirisha hisia zile zile za upingaji mabadiliko dhidi ya Uislamu na Mtume wake.

Ilikuwa ni jambo la kinyume sana kwamba mtu kama huyu, sio tu aliweza kuitwaa kazi ya Ukhalifa wa Uislamu bali pia aliweza kukubaliwa kuwa hivyo na idadi kubwa ya Waislam. Matokeo yasiyoepukika yalikuwa kwamba mwelekeo wa jumla wa Waislam kuhusu imani yao uligeuka kuwa wa kutojali, na walibakia tu watazamaji wasiojali wa utafutaji wa starehe uliokuwepo na ukiukwaji wa amri za sheria za Qur’ani na sunna za Mtume.

  • 1. Kitabu: Hayat al-Hayawan, Juz. 2 , uk. 207
  • 2. Kitabu: Tabari, Juz. 4, uk. 259
  • 3. Kitabu: Hayat al-Hayawan, Juz. 2, uk. 207
  • 4. Kitabu: Al-Akhbar al-Tiwal, uk. 265
  • 5. Kitabu: Kamil, Juz. 4 uk. 63
  • 6. Kitabu: Al-Sawaiq, uk. 135