Table of Contents

Sura Ya 18: Mialiko Kutoka Kufa Na Ujumbe Wa Muslim Bin Aqil

Baada ya mafanikio ya Waislamu pale al-Qadisiyya, na katika viwanja vingine vya mapambano ilionekana kuwa ni muhimu kuliweka jeshi la Kiislamu katika makazi ya kudumu ndani ya Iraq. Mji wa Kufa ulichaguliwa kama sehemu ifaayo kwa ajili ya lengo hilo na msikiti na nyumba za kuishi watu zilitayarishwa hapo.1 Katika mwaka wa 17 A.H Sa’d bin Abi Waqqas aliyahamisha makao yake makuu kutoka Madaini kuyapeleka Kufa ambayo kwa kuanzia yalikuwa na idadi ya askari wapatao laki moja.

Wakati Ali alipotawalishwa kuwa khalifa, na Aisha alipochochewa na Talha na al-Zubeir, yeye (Aisha) alisimama kupigana dhidi ya Ali katika yale maasi ya Basra. Alishindwa katika vita vilivyojukana kama ‘Vita vya Ngamia.’ Ilikuwa ni baada ya tukio hili ndipo alipoufanya mji wa Kufa kuwa makao ya serikali yake, katika mwaka wa 36 A.H.

Baadaye katika Vita vya Siffin dhidi ya Mu’awiyah, na katika Vita vya Nahrawan dhidi ya Makhawarij (wale waliojitenga naye), wenyeji wa Kufa kwa sehemu kubwa sana walipigana wakiwa katika upande wa Ali hivyo kwamba walikuja kufahamika kama Shia wa Ali.

Ilikuwa siyo kwamba wote katika wao walikuwa katika imani ya Kishia kwamba hakuna mtu yeyote aliyeingilia katika suala la Ukhalifa kati ya Mtume na Ali, bali wao walipendelea kuitwa Shia (wafuasi) wa Ali kuliko kuitwa Shia wa Bani Umayyah.

Hata hivyo, mara tu Mu’awiyah alipopata udhibiti wa nchi za Kiislamu na Ziyad bin Abihi alipoteuliwa kuwa gavana wa Kufa, enzi ya hofu kubwa ilianzishwa dhidi ya Shi’a; hakukuwa na nafasi kwa ajili yao katika Iraki, na kwa kweli ilionekana kila pumzi waliyoivuta iliwezekana kwao kuwa ni pumzi yao ya mwisho. Na maisha haya ya dhiki kubwa yalidumishwa kwa kipindi ambacho si chini ya miaka ishirini.

Katika hali hizi za mtihani mgumu mno, imani (itikadi) ya Kishia ilikuja kufungika kwa siri ndani ya kikundi kidogo sana cha watu ambacho kilikuwa kinapitisha siku zake katika hatari kubwa sana katika miji mbalimbali ya Iraki na Hijaz katika hali ya kutokuwa na jina kabisa.

Katika mwezi wa Rajab mwaka wa 60 A.H, Mu’awiyah alifariki dunia, na alirithiwa katika nafasi ya Ukhalifa na mwanawe Yazid, ambaye tabia zake za kiuovu, ubobeaji kwenye ulevi, tamaa ya uzinifu, kutojali kabisa makatazo ya dini na staha zake vilikuwa vinafahamika sana miongoni mwa watu. Hisia ya jumla ya chuki kubwa na maudhi iliwashika watu wote, na usakaji wa kutumia akili unaelekea kuwa ulikwishaanza kwa ajili ya mtu ambaye angeweza kuwaokoa waumini kutokana na khalifa huyu wa sifa mbaya na tabia ya kuchukiza.

Msako huu lazima utakukwa umepata mwelekeo wa uhakika kutokana na kile ambacho lazima kingekuwa ni ufahamu wa kawaida kwa wote kwa wakati huo, kwamba mjukuu wa Mtume alikataa kutoa kiapo cha utii kwa Yazid, na alikuwa ameondoka kwenda Makkah.

Ilikuwa ni katika mazingira ya namna hii kwamba baadhi ya marafiki wa Ali, wakiuona mwanga wa matumaini ya nusura yao kutoka kwa madhalimu wao, walikutana katika nyumba ya Suleimani bin Surad, sahaba wa Mtume, mtu mwenye uzoefu mwingi na mkongwe aliyepigana vita vingi akiwa pamoja na Ali.

Akitoa maoni yake kwa mpangilio mzuri sana, alitaja habari za kifo cha Mu’awiyah, na kukataa kwa Husein kutoa kiapo cha utii kwa Yazid kama mrithi wa Mu’awiyah kwenye Ukhalifa. Aliongeza kwamba Husein alikuwa ameondoka kwenda Makkah.

Aliwaambia marafiki zake kwamba kama wangekuwa na uhakika kwamba katika mazingira ya namna yoyote watakayokuwa wasingezembea katika kumsaidia Husein, na katika kupigana dhidi ya maadui zake, wangeweza kuwasiliana naye. Aliwaonya kwamba kama wanatambua ugoigoi wowote wa jitihada au udhaifu wa lengo kwa upande wao, wasije kwa hali yoyote ile, wakahatarisha maisha ya Husein kwa kuzua matumaini ya uwongo.2

Wakati muda ulivyozidi kupita baadhi ya wale waliokuwepo walionekana kukadiria kupita kiasi uwezo wao wa kutenda kwa maneno yao, kwani wote kwa pamoja kwa kauli moja walitamka dhamira yao ya kuwapiga maadui wa Husein mpaka wao wenyewe wawe wamekufa kwa kutoa muhanga maisha yao kwa ajili ya Husein.3 Barua ilipelekwa kwa Husein ikisema:

“Barua hii imeandikwa kwa Husein bin Ali kwa niaba ya Suleiman bin Surad, al-Musayyab bin Najaba, Rifa’a bin Shaddad, na Habib bin Muzahir, na marafiki wengine kutoka miongoni mwa Waislamu na waumini wa Kufa.”

Kisha ilishughulika na kifo cha Mu’awiyah na urithi wa Yazid na ikaendelea kusema; “Hakuna Imam juu yetu. Tafadhali njoo, kwa kupitia kwako Mungu anaweza kutuunganisha kwenye haki.”

Barua hii ilikuwa ya kwanza kupokewa na Husein ambaye aliipata tarehe 10 mwezi wa Ramadhani. Wale ambao kwanza walikuwa wamekutana Kufa nyumbani kwa Suleiman bin Surad ndipo kwa siri walilitangaza vuguvugu lao kiasi kwamba ndani ya siku kadhaa si chini ya maombi ham- sini yaliandikwa. Kila moja lilitiwa sahihi na watu kati ya mmoja hadi wanne.

Mfadhaiko wa kiroho ulioingia kwa wote kwa ujumla, bila kujali dini au madhehebu ambayo mtu alihusika nayo, juu ya urithi wa Yazid kwenye Ukhalifa ulilifanya pendekezo la Suleiman bin Surad na marafiki zake likubalike kwa kila mtu.

Hata wale ambao hawakuwa na itikadi za Kishia waliliunga mkono pendekezo hilo kwa bidii sana, siyo kwa sababu ya imani yoyote ile juu ya uongozi wa Husein, bali kwa sababu ya kuamini kwamba bila shaka yoyote ile yeye (Husein) alikuwa bora zaidi kuliko mtu mlevi kama Yazid.
Al-Dinawar anasimulia kwamba maombi yote haya na barua na wachukuaji wao zilimfikia Husein moja baada ya nyingine ndani ya siku mbili, na baada ya siku chache wingi wa mawasiliamo ya kuandikiana ulizidi sana kiasi cha kujaza mifuko miwili ya shogi.4

Khutba ya Suleimani bin Surad na uchunguzi wa yale yaliyojiri baadaye humfanya mtu kuhitimisha kwamba Husein:

i) Hakukataa kutoa kiapo cha utii kwa Yazid na baadaye akaondoka kwenda Makkah kutokana na vichocheo vyovyote vile kutoka nje au uelewa wa mapema sana ulio wa siri na wakazi wa Kufa;

ii) Alikuwa wala hakufikiria kwenda Kufa wakati alipokuwa anaondoka Madina; na

iii) Hakuanzisha vuguvugu lolote lile kwa ajili yake miongoni mwa wenyeji wa Kufa, na hakufanya mawasiliano na mtu yeyote hapo kueneza maoini yake.

Ni njia ipi Husein angeichukua wakati alipopata idadi kubwa ya maombi kutoka Kufa yakimtaka kwenda kwenye mji ule ili kuwaongoza? Bila shaka kulikuwepo na baadhi ya watu kama Abdalla bin Abbas, ambaye alijaribu kumshawishi asijitolee kufanya safari hiyo ya kwenda Kufa kwa sababu ya kwamba hakuna matumaini yanayoweza kutarajiwa juu ya ahadi zilizofanywa na watu wa Iraq. Husein alikuwa amedhamiria kutotoa kiapo cha utii kwa Yazid. Hili lilihatarisha maisha yake hapo Madina ambapo yeye aliondoka na kwenda Makkah.

Kukaa kwake Makkah kungeweza kumpatia angalau kuahirishwa kwa madhara kwa muda kiasi, kwani Yazid asingeweza kwa njia yoyote ile kutegemewa kuacha kutumia nguvu dhidi yake ndani ya Makkah yenyewe. Aidha, mbali na ukweli kwamba kuondoka kwake kutoka Madina lazima kuwe kumefahamika sana hakupata ahadi yoyote ya kupata msaada, au mwaliko wowote ule kutoka at-Taif au Yemen, Basra au Yamama. Ule mwaliko kutoka Kufa ulichukua umuhimu maalum kwa ajili ya Husein katika wakati huu wa hali ya hatari kwake yeye.

Lilikuwa ni jambo la hiari na limekuja kutoka kwa marafiki na maadui pia na liliungwa mkono na maombi si chini ya hamsini na tano na mifuko miwili ya shogi iliyojaa barua. Lilianzia Kufa, kituo muhimu sana katika eneo lenye kukaliwa na watu wengi mno la Uarabuni, na ombi la kwanza kumfikia yeye lilikuwa na sahihi za akina Habiba bin Muzahir, Suleiman bin Surad na Rifa’a bin Shaddad watu ambao kwao yeye Husein alikuwa na imani thabiti juu yao. Wakazi wa Kufa pia walimsaidia baba yake, Ali, katika Vita vyake.

Katika majibu kwa wale ambao walisisitiza juu ya kutokutegemeka kwa watu wa Kufa ili kumshawishi kuacha kujitolea kufanya safari kwenda Kufa, Husein kamwe hakusema kwamba aliweka matumaini katika ahadi zilifanywa na watu wa Iraq, au kwamba wao kwa hakika wengemsaidia kama angekwenda Kufa. Kwa kawaida alidumisha ukimya juu ya jambo hili.

Wakati mwingine alidokezea kwa uwazi kabisa kwamba hata kama angerefusha ukaaji wake mjini Makkah kwa hakika atakuja kuuawa, na kwamba hapo basi ingekuwa ni kwa sababu yake yeye kwamba Ka’aba ingekuwa imenajisiwa, kama wakati alipomwambia Abdallah bin Zubeir, “Baba yangu aliniambia kwamba kutakujakuwepo na mtu kama kondoo dume ambaye atakuja kusababisha kunajisiwa Ka’aba.

Mimi sipendi kuwa kondoo dume huyo.”5 Katika wakati mwingine alisema, “Naapa kwa Mwenyezi Mungu kwamba inaridhiana nami zaidi kuuawa katika kipimo cha shubiri moja nje kuliko shubiri moja ndani ya eneo la Ka’abah, na Wallahi, kama ningekuwa niishi ndani ya kishimo cha mdudu mharibifu, watu hawa watanitoa ili waweze kunifanyia mimi lile wanalolitaka. Naapa kwa Mwenyezi Mungu kwamba watu watatenda mengi zaidi dhidi yangu kama vile Mayahudi walivyovuka mipaka dhidi ya Sabato.”6
Katika hali ambayo ndani yake mambo kwa sura ya nje yalijidhihirisha yenyewe ilionekana kuwepo nafasi ndogo kwa Husein isipokuwa kukubali maombi yaliyoandikwa kwake na miito iliyotolewa kwake kutoka Kufa, kwa ajili ya lengo lile lile lililosifika la kuwaongoza wakazi wa mji huo kiroho, kimaadili na kidini.

Hata hivyo, hakuonyesha haraka isiyostahili katika kujitolea kuutekeleza ujumbe huu. Alichukua hatua za tahadhari za kumpeleka binamu yake, Muslim bin Aqil, ambaye alikuwa amefuatana naye kutoka Madina, kama mwakilishi wake kuichunguza hali ilivyo7 huko na kumtaarifu makadirio yake mwenyewe kuhusu hilo.

Husein, hata hivyo alipeleka barua kwa wakazi wa Kufa kupitia kwa Hani ibn Hani na Sa’id bin Abdallah, kabla hajatoka kuuendea mji ule. Ilisema; “Hani na Sa’id wameleta barua zenu kwangu, na watu wote wawili hawa waliotumwa nanyi ndiyo wajumbe wenu wa mwisho kuja kwangu. Nimezisoma kwa makini sana na kuelewa yale mliyoniandikia.

Wengi wenu mnaniita nije kwenu mwenyewe kwa vile hamna Imam wa kukuongozeni, ili kwamba Mwenyezi Mungu aweze kuwaunganisheni kupitia kwangu.

Kwa hiyo, ninamtuma kwenu binamu yangu mtoto wa ami yangu, kama mtu ambaye kwake yeye naweka dhamana yangu maalumu ili kuniarifu juu ya masuala yenu. Kama atanitumia neno la kwamba safu zenu na wale walioko kwenye uongozi wa mambo yenu zimeungana kuhusu yale mliyoyasema ndani ya barua zenu, basi nitajiunga nanyi hivi punde …”8

Inaonekana kwamba balaa ilizikumba hata zile hatua za mwanzo za safari ya Muslim kwenda Kufa. Alikuwa amewakodi watu wawili kama waongoza njia wake na walikuwa wameizoea sana njia hiyo ya kwendea Kufa. Wote hawa waliipoteza njia yao, na wakatangatanga ndani ya jangwa na angalau mmoja katika wao,9 kama si wote wawili,10 alikufa kwa kiu.

Ilikuwa ni kwa taabu kubwa kwamba Muslim na sahaba zake walikuta kijito ambapo hapo alielezea bahati yake mbaya kwa Husein, akiongezea kusema kwamba hakuwa na moyo wa kuendelea na safari yake zaidi ya hapo. Hata hivyo, ilibidi aendelee katika safari yake yenye mkosi kwa maelekezo ya Husein. Alipofika Kufa, ilimbidi Muslim akae nyumbani kwa al-Mukhtar bin Abi Ubayd al-Thaqafi11 kwa vile Suleiman bin Surad alikuwa ametoka nje ya mji.

Habari za kuwasili kwa Muslim zilienea na zikapokelewa vizuri kila mahali. Wageni walimiminika kuja kumwona, na Muslim aliisoma barua ya Husein kwenye mkusanyiko wa kundi kubwa la wale ambao walikuja kuonana naye.

Hii ilisababisha kudhihiri kwa ari yenye hamasa nyingi kwa wasikilizaji waliokuwa wakihutubiwa na Abis bin Abi Shabib al- Shakir, Habib bin Muzahir na Sa’id bin Abdallah al-Hanafi. Wazungumzaji, kila mmoja akitoa maoni yake binafsi walimhakikishia Muslim dhamira yao ya kupigana katika upande wake dhidi ya maadui wake, na kushambulia kwa panga zao mpaka wote wawe wamekufa, lengo lao likiwa tu ni kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu. Kisha mkusanyiko huo ulitawanyika.

Mfarakano wa watu na Yazid kutokana na tabia zake za kiovu, umaarufu wa Husein kwa sababu ya utukufu wa familia yake na ubora wake mwenyewe wa tabia na elimu, maarifa na ujuzi, na jina zuri na nafasi yenye mvuto na ushawishi katika jamii ya wanaoendeleza harakati kwa upande wake zilikuwa miongoni mwa sababu kubwa ambazo ziliwavutia wakazi wa Kufa wapatao 12,00012
au 18,00013 ndani ya kipindi cha wiki moja kuja kutoa kiapo cha utii kwake katika mikono ya Muslim.

Je, watu wote hawa walikuwa marafiki wa Ali? Je, idadi kubwa kama hii ya marafiki wa kweli wa Ali wangeweza kubakizwa mjini Kufa wakati wa utawala uliochukuwa zaidi ya miaka ishirini ya Ziyad na kizazi chake wakati watu walikuwa wanauawa kwa upanga bila haya kwa kuonyesha dalili japo ndogo tu za upendo kwa Ali? Jibu lazima liwe la wazi la kukataa kwa nguvu.

Shi’a wa kweli walikuwa wachache kwa idadi hata huko nyuma zaidi na walikuwa takriban wameangamizwa na Mu’awiyah na Ziyad. Wale tu Shi’a wachache kabisa ambao walifanikiwa kujificha wenyewe ndio waliokwepa kufa. Wengine wote ambao walimfanya Ali kama Khalifa wa nne pia walionekana kuwa ni Shi’a kwa maana halisi tu ya neno hilo kwa sababu ya ushirikiano wao naye. Kwa kawaida, uungaji mkono wa watu wa namna hii, na wengineo ambao, wanaweza kuwa wamevutiwa tu na harakati hizi kwa sababu ya kuanzisha kwake jambo mpya, ulikosa umadhubuti.

Haishangazi kwamba wakati waendelezaji wa harakati hizi, waliozaliwa kulelewa mjini Kufa, walishindwa kugundua udhaifu wa msingi ambao juu yake uungaji mkono wa sehemu kubwa ya watu wa mji wao uliegemea, Muslim naye pia alikuwa amechukuliwa na vuguvugu la mapokezi mazuri aliyofanyiwa na watu wote wa mji huo. Viongozi watangazaji wa harakati hizi kwa ajili ya Husein, hata hivyo walisimama imara kwa neno lao la ahadi, na wakalipa kishujaa kwa maisha yao kwa ajili ya kumuunga mkono yeye.

Alipoona kwamba watu wa Kufa walitenda kwa mujibu wa ahadi zao, Muslim alimwandikia Husein akimwomba aharakishe uondokaji wake kuja Kufa.14 Gavana wa mji huo, al-Nu’man bin Bashir, alifanya uvu- milivu na akatangaza kutoka kwenye mimbari kwamba asingechukuwa hatua yoyote mradi tu hapingwi kwa ushari na uchokozi.15

Mshirika mmoja wa Bani Umayyah hakuupenda msimamo huu wa gavana wenye hisani juu ya Muslim, na aliandika kwa Yazid akilalamika dhidi ya ushuhu- likiaji wa kinyonge wa gavana kuhusu hali ya Kufa ambako Muslim bin Aqil alikuwa amefika na wafuasi wake wenye kumuunga mkono wametoa kiapo cha utii kwa Husein. Alipendekeza kwamba al-Nu’man bin Bashir abadilishwe na mtu shupavu mwenye mabavu, kama Yazid alikuwa anataka kuubakiza (mji wa) Kufa katika milki yake.

Umara bin Uqba na Umar bin Sa’d pia waliandika kwa Yazid kuhusu jambo hilo hilo na matokeo yake yakawa kwamba Yazid aiandike barua kwa Ubaydullah bin Ziyad akisema; “................Muslim bin Aqil amefika Kufa na anaunda jeshi ili kuchochea mfarakano na kutokuelewana miongoni mwa Waislamu. Nenda Kufa haraka sana mara tu uipatapo barua hii na ukisha mkamata Muslim, ama umfunge, umkate kichwa au mhamishe.”16

Barua hii ilipelekwa pamoja na amri ya kumteua Ubaydullah bin Ziyad kama gavana wa Kufa. Ubaydullah aliondoka Basra, ambako alikuwa kazini kama gavana akaenda Kufa haraka sana.

Alizifanya nyendo zake kwa hali ya siri sana, ili kwamba kuwasili kwake mjini Kufa kuwe kwa yote mawili; kwa kutotegemewa na kwa ghafla. Ili kuweza kusafiri kupitia jangwani, alikuwa amezungusha kipande cha kitambaa usoni mwake kuulinda na mchanga. Alionekana mwenye kupendeza kiasi, akiwa amepanda juu ya farasi ya Kiarabu, aliyevaa vazi jeusi kichwani la Mwarabu muungwana, na akifuatiwa na msafara.

Kwa vile watu wakati huo walikuwa wanasubiri kuwasili kwa Husein, walifikiri kwamba alikuwa ni mjukuu wa Mtume ambaye alikuwa amewasili mjini hapo, na watu walikuwa wamemiminika kutoka pande zote kuja kumsalimia kwa wingi kama hivyo.
Ubaydullah aliendelea na njia yake bila ya kuitikia salamu hizo. Ummati wa wale ambao walikuja kumkaribisha yule ambaye walikosea wakamdhania ni Husein, walizuia kuendelea mbele kwa Ubaydullah na Muslim bin Amr al-Bahili ambaye alifuatana naye alisema kwa sauti kubwa, “Pisheni njia, yeye ni Ubaydullah bin Ziyad.”

Fazaa ikabadilisha haraka sana ile hali ya furaha ya watu. Kumbukumbu za ukatili wa kinyama wa Ziyad ulioendelea kwa kipindi cha zaidi ya miaka ishirini lazima itakuwa imehuishwa kwa kutokea mtoto wake na mamlaka ya baba yake. Ubaydullah alitangaza kuteuliwa kwake kama gavana wa Kufa mbele ya mkusanyiko wa watu ndani ya msikiti wa Jamaa.

Kisha aliwataka watu wote wenye kuwajibika na sehemu mbalimbali za makazi katika Kufa kumpatia orodha ya wakazi wote wa sehemu zao husika wakitaja na kueleza bayana majina ya wageni na ya wale ambao waliweka tishio kwa serikali ya Syria.

Kama wasingeweza kumpatia orodha hizo kwa maelezo ya kina, basi walitakiwa watoe ahadi kwamba hakuna mtu yeyote katika sehemu yao ya Kufa ambaye angejiingiza katika shughuli yoyote ile ya uchochezi. Endapo utatokea uvunjaji wa ahadi hii, mkuu wa sehemu hiyo ya mji inayohusika atanyongwa mbele ya nyumba yake mwenyewe.17

Hatua hii kali ilileta ndani ya mfuatano wake wingi kupita kiasi wa wapelelezi na watoa habari, na maisha mjini Kufa yakawa hayana usalama kabisa. Watu walikuwa wanaogopa kutoka nje ya nyumba zao na kuwa- tembelea marafiki. Mikutano na majadiliano hata katika vikundi vidogo vidogo sana juu ya suala lolote lile havikuwezekana hata kufikiriwa.

Akiwa ni mwenye wasi wasi juu ya usalama wa maisha yake na kudumu kwa ujumbe wake, Muslim aliacha kuendelea kukaa nyumbani kwa al-Mukhtar bin Abi Ubayd al-Thakafi, ambaye mbali na kuwa nje ya Kufa, hakuwa tena na nguvu kubwa ya ushawishi wa kutosha. Alihamia kwa Hani bin Urwa, mkuu wa kabila lake. Hani alifanya kukaa kwake na Muslim kuwa na ulinzi wa karibu sana na wa siri, akikushirikisha tu na watu wake wanaoaminika sana.

Kwa kuzingatia hatari inayoweza kutokea karibuni ya matumizi ya nguvu dhidi ya Muslim bin Aqil, wasimamizi wa harakati za kumwita Husein kuja Kufa kwa ghafla walibadilisha lengo lao la kutoa msaada wote uwezekanao kwa Muslim ili kupata kutoka kwa watu wa Kufa lile neno lao la ahadi kwa ajili ya Husein ili waweze kuchukua hatua za kumlinda Muslim kutokana na hatari ambayo ilitishia maisha yake. Muslim bin Awsaja aliyejishughulisha katika kupata ahadi kutoka kwa watu kwa ajili ya msaada na ulinzi wa Muslim bin Aqil na Abu Thumama al-Sa’di alichukua wajibu juu yake mwenyewe wa kukusanya silaha na fedha kwa ajili ya lengo hilo.18

Ubaydullah bin Ziyad alikuwa na shauku sana ya kugundua mahali ambapo Muslim bin Aqil alipokuwa amejificha, na akamtuma mtumwa wake, Ma’qil kutafuta mahali gani Muslim alikokwenda kujificha. Ma’qil alikwenda kwenye msikiti wa jamaa kubwa na, kwa bahati nzuri tu, alimwona Muslim bin Awsaja akisali pia.

Kwa vile Muslim bin Awsaja alichukua muda mrefu kumaliza swala zake, Ma’qil alimsubiri, na akamwambia kwamba yeye alikuwa ni Msyria mwenye kuwapenda sana watu wa Nyumba ya Mtume, na amesikia kwamba mtu mmoja atokanaye na familia ya Mtume amewasili mjini hapo na kwamba alikuwa anachukuwa viapo vya utii kwa ajili ya Husein.

Alitoa dirham 3,000 na akasema alipenda kuzitoa pesa hizo kwa mwakilishi wa Husein kama atajua mahali alipokuwa. Yote haya yalisemwa na Ma’qil katika namna ambayo ilipandikiza imani kamili katika unyenyekevu wake na alifanikiwa kumdanganya Muslim bin Awsaja katika kumchukua yeye na kumpeleka kwa Muslim bin Aqil. Ma’qil, katika matembezi yake ya kirefu mara kwa mara kwa Muslim bin Aqil, alikusanya taarifa kamili kuhusu lengo la Muslim bin Aqil kutembelea Kufa. Alizifikisha habari zote alizozikusanya kwa Ubaydullah bin Ziyad.19

Hani bin Urwa kwa muda mrefu alikuwa amezoeana na Ubaydullah bin Ziyad, lakini siku za karibuni alikuwa anakwepa kumwona kwa kisingizio cha ugonjwa isijekuwa Ubaydullah bin Ziyad akapata fununu ya ukaaji wa Muslim bin Aqil pamoja naye. Katika kupata habari hizi kupitia kwa Ma’qil, Ubaydullah aliamua kumwita Hani kuja kwenye kasiri la gavana.

Bila ya kutambua hatari yoyote ile, Hani alikwenda kumwona Ubaidullah akiwa peke yake bila kufuatana na askari wake, na bila ya kumwarifu mtu yeyote yule kuhusu wito wa Ubaydullah.

Aligundua kwamba msimamo wa Ubaydullah kuhusu yeye ulikuwa umebadilika kabisa wakati alipomwambia Hani, “Ni fedheha kiasi gani hii kwamba wewe umeifanya nyumba yako kuwa mahali pa fitna ya njama dhidi ya Khalifa wa wakati huu na dhidi ya Waislam wote.

Umemwita Muslim bin Aqil na umekuwa ukimkirimu nyumbani kwako, ukimkusanyia silaha, ukiandikisha watu kwa ajili ya msaada wake na kuwaweka kwenye nyumba zilizoko kwenye ujirani wako. Je, unafikiri mambo haya yangebakia kufichika kwangu?”20

Hani baada ya hapo mwanzo kuukana ukweli wa madai haya, alitambua, wakati Marqi alipoletwa, kwamba alikuwa akipelelezwa na akasema, “Sasa sikiliza ukweli na uniamini.

Namwomba Mungu awe shahidi yangu kwamba sikumwita Muslim bin Aqil, wala sikuwa nikitambua harakati yoyote ile kwa upande wake, alikuja kwangu kwa uchaguzi wake mwenyewe, na akaelezea hamu ya kukaa nami. Sikuweza kwa heshima kukataa kumkaribisha nyumbani kwangu. Kwa hiyo, mimi nilimpokea kama mgeni kuja kukaa chini ya paa langu.

Hata hivyo, ninaahidi, sitotenda tendo lolote la uchokozi dhidi yako; na nitajiweka chini yako kwa sasa. Hata hivyo, kabla sijafanya hivyo, nataka ruhusa kwako ili nimwambie Muslim atoke nyumbani kwangu na aende popote pale atakapofikiria kwenda, ili kwamba niweze kujitoa kwenye wajibu wangu wa kumpatia hifadhi. Hapo tena nitakuwa sina la kuhusiana naye.”21

Ubaydullah, hata hivyo, alisisitiza kwamba Muslim bin Aqil akabidhiwe kwake na akapendekeza kumtia Hani mbaroni na azuiliwe mpaka wakati huo. Hani alielezea wazi kwamba ilikuwa haiwezekani kwake kumtoa mgeni wake kwenye kifo cha dhahiri. Mabishano kati ya wawili hawa yali- pamba moto kiasi kwamba Ubaydullah alimpiga Hani usoni kwa fimbo, na damu ilitiririka kutoka mahali palipojeruhiwa. Kisha Hani alitupwa gerezani.22

Amr bin Hajjaj, shemeji yake Hani bin Urwa na mkuu wa kabila la Zubayda alilizunguuka jumba la gavana na kundi kubwa lenye kumfuata la wapanda farasi waliposikia uvumi kwamba Hani alikuwa ameuawa. Waliondoka tu pale kadhi Shuraydi alitangaza kwamba Hani alikuwa amewekwa kizuizini kwa muda tu.23

Je, ingekuwa inafaa kwa Muslim bin Aqil kubakia mafichoni hata katika hatua hii, au kuhatarisha zaidi usalama wa rafiki yake mwingine mwamini- fu kwa kutafuta hifadhi kwake? Njia zote mbili hizi zilikuwa hazikubaliki kwa mujibu wa kanuni za uungwana wa Bani Hashim. Tabari ameeleza kwa uwazi kabisa kwamba Muslim alitoka kwenda kupigana na maadui zake bila ya kuwataarifu marafiki zake au bila ya kuwepo hapo mata- yarisho yoyote yale.

Wakati Ubaydullah bin Ziyad alipokuwa anatoa hotuba ya vitisho huko msikitini, watu walimiminika kuingia ndani na kutangaza kwamba Muslim bin Aqil amewasili. Ubaydullah kwa haraka sana aliteremka chini kutoka kwenye mimbari na akajifungia ndani ya kasiri lake.

Akiufikiria mgeuko wa ghafla na usiotegemewa ambao matukio yalichukua hapo Kufa, isingeweza kutumainiwa kwamba watu 18,000 ambao walikuwa wametoa ahadi ya kiapo cha utii kwa Husein mikononi mwa Muslim bin Aqil wangeweza kukusanyika kumzunguuka katika wakati huu wa hatari kubwa ya kutisha. Wafuasi hawa walikuja kutoka sehemu mbalimbali za mji.

Sehemu hizi zilikuwa na umbali kidogo kuto- ka sehemu moja hadi nyingine na habari za yanayotokea katika sehemu moja zilichukua muda kuzifikia zile sehemu za mbali zaidi.

Wengi wa wafuasi hawa walikuwa si watu wenye kufikiri, na walikosa unyofu wa imani na upendo wao kwa watu wa nyumba ya Mtume ulikuwa haujapata mtihani. Katika eneo ambalo ndani yake Muslim bin Aqil amepata hifadhi, watu 4,000 kati ya hawa wenye kuwaonea huruma waliishi, na waliposikia ukelele wa vita wa Mtume walijitokeza. Wakiwa hawakujiandaa na hawakupata mafunzo yoyote hawakuweza kukabiliana na majeshi ya kawaida ya serikali. Wakati Muslim alipowaongoza kushambulia makazi ya gavana alikuwa na watu 300 tu, na kati ya hao hakuna aliyebaki naye alipofika mwisho wa safari yake.

Ubaydullah ibn Ziyad alikuwa tangu asubuhi amewazuilia wakuu (watemi) wa kikabila na watu wengine mashuhuri pamoja naye kama hatua za tahadhari. Alifunga pia vituo vyote vya njia ziingiazo mjini na iendayo kwa Muslim bin Aqil, ili kuzuia msaada kutoka nje kumfikia na kuwaweka wale walioko mjini katika hali ya kushindwa kuungana naye. Msaada wote ulikuwa umekatwa usimfikie ili kwamba hata wale watu watiifu wakuu wenye uthabiti usio na wasiwasi kama vile Habib bin Muzahir, Muslim bin Awsaja na Abu Thumama al-Sa’idi wasiweze kufanya mawasiliano na Muslim bin Aqil katika siku ile ya msiba.

Watemi mbalimbali wa kikabila walipanda juu kwenye mapaa ya makazi ya gavana na wakawasihi wenye kumuunga mkono Muslim bin Aqil kutawanyika, wakitangaza juu ya viapo vyao kwamba jeshi kubwa karibuni lingefika kutoka Syria na lingewasagasaga na kuwaangamiza waunga mkono wote wa Muslim bin Aqil. Matokeo yalikuwa kwamba ni watu 30 tu walibaki na Muslim ulipofika wakati wa jioni. Hata watu hawa walimwacha wakati alipoondoka kwenda kwenye swala ya jioni msikitini.24

Akitangatanga peke yake, na akiwa anatafuta mahali pa kujipatia hifadhi, Muslim alifika baada ya kuingia usiku kwenye nyumba ya Taw’a, kijakazi mwachwa huru wa Muhammad bin al-Ash’ath, ambaye alikuwa na mtoto wa kiume, Bilal. Alimpatia Muslim chumba nyumbani mwake baada ya kuyapata maelezo ya kuhuzunisha. Wakati mtoto wake alipofika wakati wa usiku wa manane, alilazimika bila kupenda kuelezea utambulisho wa Muslim kwake. Alimsihi mwanawe aitunze siri hiyo mwenyewe kwa makini kabisa.

Wakati Ubaydullah bin Ziyad alipoona kwamba hatari imepungua nguvu, alituma itangazwe kwamba kila mtu lazima awepo msikitini, akiongeza kwamba kutoitekeleza amri hii kutaindolea serikali wajibu kwa ajili ya usalama wa mtu anayehusika. Amri hii ilisababisha kujaa sana msikiti hata kabla ya kufika wakati wa swala za usiku (Magharibi na Isha).

Baada ya swala hizo Ubaydulah alitangaza kwamba asingewajibika na usalama wa mtu yeyote yule ambaye nyumbani mwake atakutwa Muslim bin Aqil akiwa amejificha humo, na kisha akaanzisha msako wa kumtafuta Muslim kutoka nyumba hadi nyumba.

Mtoto wa Taw’a, Bilal, alikwenda kumwona Abd al-Rahman, kijana wa Muhamad bin al-Ash’ath wakati wa alfajir na akamwambia kuhusu kuwe- po Muslim nyumbani kwake. Abd al-Rahman aliwasiliana na baba yake na huyo baba yake akazitoa habari hizi kwa Ubaydullah bin Ziyad ambaye alipeleka kikosi chini ya Muhamad bin al-Ash’ath kwenda kumkamata Muslim na kumfanya mateka.

Akiwa anapigana peke yake, Muslim alifanikiwa mara mbili katika kuwatupa askari hao nje ya nyumba ya Taw’a. Katika harakati hizo za kupigana mmoja wa midomo yake ulikatwa na ule mwingine ukajeruhiwa, na meno yake mawili yakang’olewa.

Walipoona kwamba mitindo ya kawaida ya kupigana ilikuwa haina matokeo mazuri, watu walipanda juu ya paa la nyumba na kumtupia mawe Muslim. Walimtupia pia vitita vya matete yaliyowashwa moto kumfanya apate majeraha ya kuungua.

Akishambuliwa kwa njia hii, Muslim alitoka nje ya nyumba kupigana kwa upanga wake. Muhamad bin al-Ash’ath alimwita akisema kwamba angepata ulinzi na usalama na akamtaka aache kupigana. Muslim, hata hivyo hakuisimamisha vita na alisoma beti zinazomaanisha ya kwamba, “Nimekula kiapo nisiuawe kwa upanga isipokuwa nikiwa kama mtu huru. Kifo, kwa kweli, ni kitu kisichopendeza, lakini kwa kila mtu lazima siku moja kitamjia. Nahofia nisije nikaambiwa uwongo na kulaghaiwa.”

Akiwa amechokeshwa na mapigano kama alivyoonekana Muslim aliuliza kama kweli ulinzi na usalama ungeweza kutolewa. Muhamad bin al-Ash’ath na washirika wake wote, isipokuwa mmoja tu ambaye alikataa, walimhakikishia Muslim kwamba alikuwa salama, Muslim aliwaambia tena wakumbuke kwamba alikuwa anaweka upanga wake ndani ya ala yake kwa sababu tu amepewa usalama, vinginevyo asingejitoa mwenyewe kwao. Muslim alipewa farasi wa kumpanda. Kisha askari wakamzunguuka na kumpokonya upanga wake.

Kitendo hiki kilimvunja moyo Muslim kikiwa kama usaliti wa kwanza wa dhamana yake (aliyoahidiwa). Halafu alianza kulia, na alipoulizwa sababu ya kulia alisema, “Naapa kwa Allah, sijililii mimi binafsi, bali moyo wangu unayeyuka kwa ajili ya Husein na sahaba zake ambao watatoka kuja Kufa baada ya kupata barua yangu.”

Kisha alimtaka Muhammad bin al-Ash’ath kumwarifu Husein kwamba Muslim amechukuliwa mateka na maadui zake na alitegemewa kuuawa jioni hiyo, na kumwomba asifikirie juu ya kuja Kufa, na asidanganywe na ahadi zili- zofanywa na wakazi wa mji huo kwani zote zilikuwa za uwongo, na map- atano yao na shughuli zao vyote hivyo vilikuwa siyo vya kutegemewa tena.

Kisha Muhamad bin al-Ash’ath akamwambia Ubaydullah bin Ziyad kwamba ametoa usalama kwa Muslim, lakini Ubaydullah alikataa kuutambua uwezo wa Muahamad bin al-Ash’ath kufanya hivyo. Alimwambia Muslim kwamba angeuawa wakati huo huo. Muslim alijibu kwamba alikuwa tayari kuufikia mwisho huo.

Ombi lake la kuwasilisha matakwa yake ya mwisho kwa mtu fulani aliyekuwapo hapo lilikubaliwa, na Muslim alimchagua Umar bin Sa’d kwa lengo hilo. Alikataa kumlazimisha Muslim ili asije akamkosea Ubaydullah, ambaye alimlaumu Umar bin Sa’ad kwa kutoridhika kwake kuyasikiliza matakwa (maneno) ya mwisho ya Muslim. Kisha Muslim akamwambia kwamba maneno yake ya mwisho yalikuwa kwamba:

(a). Deni la dirmah mia saba (700) alilopata wakati wa kukaa kwake Kufa lilipwe kwa thamani ya upanga wake na deraya. (b). Kwamba mwili wake uzikwe; na (c). Mjumbe atumwe kwa Husein kumjulisha hatma ya Muslim ili kwamba aweze kurudi alikotoka na asidanganywe na ahadi zilizofanywa na wenyeji wa Kufa.

Baada ya kuisikia haja ya mwisho (wosia) ya Muslim, Umar bin Sa’d alik- wenda kwa Ubaydullah bin Ziyad na kumwambia yale yote ambayo Muslim alimwambia. Tabia hii ya kufedhehesha ilimuudhi hata Ubaydullah mwenyewe na aliurudia msemo wa Kiarabu, wenye maana ya kwamba;
“Mtu mwaminifu hawezi kukusaliti lakini wakati mwingine mtu asiyemwaminifu huamimiwa.”25
Halafu alitoa maamuzi mwenyewe juu ya maombi ya Muslim; “Sina haja yoyote katika vitu vyako ambavyo vitauzwa kulipia madeni yako.

Sina lolote la kufanya kuhusiana na Husein, kama hatakuja upande huu. Ninashindwa kutoa ahadi yoyote ile ya kuwa mwenye huruma kuhusu utupaji wa mwili wako kwa vile wewe ulifanya uasi dhidi yangu na uliwatia moyo watu ili kusababisha mfarakano na kutokuelewana miongoni mwao.26
Muslim alijibu shutuma zote hizi na akafichua kabisa uwongo wa madai yaliyoelekezwa dhidi yake. Kisha Ubaydullah bin Ziyad aliamuru Muslim bin Aqil kuchukuliwa juu gorofani mwa kasri lake na auawe hapo. Halafu mwili wake utupwe chini ardhini. Muslim alipanda kwenye gorofani la jumba hilo kwa utulivu mkubwa, huku akimtukuza Mungu na kumwomba baraka Zake.

Bakr bin Humran al-Ahmari ambaye ndiye aliyekuwa amejeruhi midomo ya Muslim na kinywa chake alimnyonga na kuutupa huo mwili wake chini kwenye sakafu ya kasri hilo.27 Muslim alianza mapambano yake hayo tarehe 8 Dhil-Hijja mwaka wa 60 A.H.28 na aliuawa kishahidi katika siku iliyofuatia.

Baada ya tukio hili, hofu iliigubika Kufa, na watu waliacha kutoka nje ya nyumba zao kwa muda mrefu kidogo. Bado tukio jingine kubwa la kusikitisha katika muktadha huo huo ilikuwa ni kwamba Hani ibn Urwa aliburuzwa mpaka sehemu ya sokoni, akiwa amefungwa kamba na akauawa kwa upanga na mtumwa wa ki-Turuki wa Ubaydullah bin Ziyad29 bila ya kuvutia ujulikanaji wake wowote ule makhususi.

 • 1. Tabari, Juz. I, uk. 2389
 • 2. Tabari, Juz. II, uk. 234, Irishad.
 • 3. Ibid
 • 4. Al-Akhbar al-Tiwar, uk. 229.
 • 5. Tabari, Juz. II, uk. 272.
 • 6. Ibid
 • 7. Tabari, Juz. II, uk. 236.
 • 8. Tabari, Juz. II, uk. 235.
 • 9. Tabari, Juz II, uk. 228.
 • 10. Tabari, Juz. II, uk. 237.
 • 11. Ibid
 • 12. Tabari, Juz. II, uk. 220.
 • 13. Tabari, Juz. II, uk. 264.
 • 14. Tabari, Juz. II, uk. 264.
 • 15. Tabari, Juz. II, uk. 228
 • 16. Irishad, uk. 308; Tabari, Juz. II, uk. 240.
 • 17. Tabari, Juz. II, uk. 241.
 • 18. Tabari, Juz. II, uk. 249; Irishad, uk. 311
 • 19. Tabari, Juz. II, uk. 249; Irshad, uk. 311
 • 20. Tabari, Juz. II, uk. 201; Irshad, uk. 312.
 • 21. Tabari, Juz. II, uk. 251-252; al-Irshad, uk. 312-313.
 • 22. Tabari, Juz. II, uk.253; Irshad; 313-314.
 • 23. Tabari, Juz. II, uk. 255; Irshad, uk. 315.
 • 24. Tabari, Juz. II, uk. 258; Irshad, uk. 317.
 • 25. Tabari, Juz. II, uk. 266
 • 26. Ibid
 • 27. Tabari, Juz. II, uk. 267.
 • 28. Tabari, Juz. II, uk. 271.
 • 29. Tabari, Juz. II, uk. 268; Irshad, uk. 325.