Table of Contents

Sura Ya 23: Huduma Ya Maji Kwa Husein Yasimamishwa. Kiu Ya Kupita Kiasi Yaathiri Kundi Lake.

Mpango wa kuzuia maji yasimfikie Husein na watu wa kundi lake pamoja na watoto wadogo lazima ulikuwa unaunda picha hiyo ndani ya fikira za Ubaydullah bin Ziyad kwa kipindi fulani wakati alipoandika barua kwa al-Hurr bin Yazid al-Riyahi ambaye al-Hurr aliipata akiwa Karbala katika siku ya pili ya mwezi wa Muhamrram mwaka wa 61 A.H. Aliagiza katika barua hii kwamba Husein lazima alazimishwe kukaa mahali ambapo huduma ya maji ni haba.

Katika kuafikiana na amri zilizopokelewa na al-Hurr, kambi ya Husein iliwekwa katika kiwanja cha mchanga chenye ardhi isiyo na kivuli iliyoondolewa kutoka kwenye mto, na joto la jua wakati wa mchana lilikuwa ni chanzo cha shida kubwa kwa wote, na hasa zaidi kwa watoto.

Inaonekana kwamba amri za Ubaydullah bin Ziyad zilikuwa kwa ujumla zimefahamika ndani ya jeshi, na baadhi ya watu katika kujaribu kujipendekeza na kujikomba kwa wakuu wao walifanya kazi ya kugawa maji kwa Husein, kuwa ngumu, kama ilivyokuwa na hatari vilevile.

Tarehe 7 Muharam Umar bin Sa’d alipata barua nyingine tena kutoka kwa Ibn Ziyad akimwelekeza asimamishe ugavi wa maji kwa Husein na sahaba zake ili kwamba wasipate hata tone la maji kama alivyonyimwa maji Uthman bin Affan, Khalifa wa tatu.1

Umar bin Sa’d alimdhaminisha Amr bin Hajjaj al-Zubaydi kwa kazi ya kuweka uangalizi mkali sana katika kingo za mto na kulinda lisipatikane hata tone moja la maji kumfikia Husein. Alimpa Amr bin Hajjaj askari 500 kumsaidia katika kuitekeleza kazi hii. Uzuiaji wa ugavi huu wa maji ulisababisha ukali zaidi wa kiu iliyohisiwa na Husein na watu wa kundi lake.

Kuongezea fedheha kwenye jeraha hili, maadui wakati mwingine wakimhutubia Husein, wakisema, “Hapa pana maji, mbwa na nguruwe wanayanywa, punda na hata mbwa mwitu wanayatumia, lakini wewe na wenzio hamtapata hata tone moja la maji hayo.”

Huenda pia kwamba baadhi ya maadui wa Husein angalau wangefikiria kwamba kiu tu yenyewe ingemuua yeye na sahaba zake, na kwamba hatua ya vita iliyokuwa ikiandaliwa kamwe isingefika. Marafiki wa Husein, hata hivyo, wakati mwingine waliweza kuyachota maji kwa ajili ya Husein kutoka kwenye mto kwa kutumia nguvu.

Jaribio la mwisho la namna hiyo lililokuwa na mafanikio lilifanywa na ndugu yake Husein, Abbas, katika usiku kabla ya mwezi 8 Muharam.
Ni mfano wa uaminifu na utii usio na kifani wa idadi kubwa ya watu kwa kiongozi wao, kwamba hata kama baadhi ya ndugu wa Husein na maraf ki wakati mwingine walifaulu kuufikia mto, hakuna hata mmoja katika wao alijali hata kuilowesha tu midomo yake kwa maji ambayo yalikuwa hayapatikani kwa ajili ya kukata kiu ya Husein.

Husein hakutumia nguvu ili aweze kuyapata maji. Alijaribu katika siku zote tatu alizokaa akiwa amenyimwa maji kuziamsha dhamira za maadui zake ili kwamba waweze kukubaliana na ombi lake la mara kwa mara la kupewa maji. Aliwaruhusu marafiki zake pia wafanye maombi kama hayo.

Burayr al-Hamadani alikutana na Umar bin Sad na akasema; “Wewe ni mwislamu wa namna gani uliyejiandaa kukichinja kizazi cha Mtume na pia unalikuza zaidi kosa kwa kumzuia Husein, na watu wa familia yake na marafiki zake, wanaokufa sasa kwa kiu, (unawazuia) kuyapata maji ya Mto Furat kwa matumizi yao, ambayo yananywewa bure na kwa uhuru kabisa na mbwa na nguruwe?”

Umari bin Sa’d alikiri udhaifu wake vinginevyo mpaka labda auachie uongozi wake wa eneo la Rayy, jambo ambalo hangeweza kulifanya kwa hali yoyote na kwa gharama yoyote ile.

Katika tarehe 10 Muharam wakati al-Hurr alipolitelekeza jeshi la Umar bin Sa’d, na kwenda kujiunga na kundi la Husein alielezea majuto makubwa pamoja na mambo mengine, kwa kusababisha Husein kuwekwa kambi yake mbali na mto.

Ni lazima awe ameteswa na kumbukumbu za tabia ya ukarimu ambayo Husein hapo nyuma kidogo alimfariji nayo kwa kumtuliza yeye na watu waliokuwa chini yake na farasi wao kutokana na kiu yao iliyowazidi nguvu na yenye kudhikisha.

Baada ya kujasiria shida kubwa ya kiu kali kwa muda wa siku tatu, na kutekeleza wajibu wao
wa kupigana vita takatifu kwa ujasiri mkubwa, Husein na sahaba zake walikutana na vifo vyao
vya kishahidi.

  • 1. Tabari, cha II, uk. 312.