Table of Contents

Sura Ya 24: Jaribio La Mwisho La Kuleta Amani Na Jinsi Lilivyofikia Mwisho.

Ili kuepusha vita na kuwazuia Waislamu kujiingiza katika umwagaji damu kwa pande zote, Husein alijaribu kufungua mazungumzo kwa ajili ya kuwepo amani na Umar bin Sa’d hapo Karbala na akamwalika Umar bin Sa’d kwa kumtumia Quraza bin Ka’b al-Ansar kukutana naye katika ardhi ambayo iko katikati ya sehemu zenye majeshi yao. Mazungumzo yalirefushwa mpaka ukaingia usiku. Kisha washiriki (katika mazungumzo hayo) wakarudi kwenye kambi zao.1

Uendeshaji wa mkutano ule ulikuwa ni siri, lakini ilitangaa kuhusu Husein kuwa alikuwa amejiandaa kuondoka Iraq, na hata kuihama Bara Arabu yote na kwenda sehemu ya mbali sana katika ulimwengu huu.2 Kwa ukweli hili nalo pia lilikuwa sawa na ufanikishaji wa lengo la Husein ambalo kwalo ameyatoa maisha yake, nalo ni kutotoa kiapo cha utii kwa Yazid kama khalifa.

Tabia za Husein zilikuwa ni za upole sana na za kiungwana zenye kutoa fursa kiasi kwamba Umar bin Sa’d mara moja alikiri kwamba alitaka kupita katika njia ya amani na kwa kweli alikuwa anachukizwa sana na kujiingiza katika vurugu.

Alimjulisha Ubaydullah bin Ziyad juu ya masharti ya amani yaliyokubaliwa na Husein, na akasema, “Mungu atukuzwe na kushukuriwa kwamba moto wa fitina umezimishwa, ule uwezekano wa Waislamu kubakia wameshikamana pamoja umejitokeza na mambo ya wafuasi wa Uislamu yako katika mwelekeo wa kuboreka.” Aliongeza kusema kwamba hakuna sababu nyingine zaidi iliyobakia kuleta mzozo, na kwamba jambo hili sasa lingeweza kufungwa.3

Imeelezewa kwamba Ibn Ziyad alielekea kukubaliana na rai ya Umar bin Sa’d ambayo ilikuwa ikipingwa kwa nguvu sana na Shimr4 ambaye alihoji kwamba ikiwa Husein angeruhusiwa kutoroka wakati huo, angedai kwa haki kabisa madaraka na heshima. Kuyakubali mapendekezo ya Husein kulikuwa machoni ni alama ya unyonge ambayo ingeleta aibu tupu na fedheha.

Alishauri kwamba Husein lazima aambiwe asalimishe silaha zake bila ya masharti yoyote, na akubali kumtii Ibn Ziyad, ambaye angeweza wakati huo kumuua Husein kwa upanga jambo ambalo lingekuwa halali kabisa, au kumpa msamaha. Alilalamika dhidi ya Umar bin Sa’d, akisema kwamba alitumia mikesha mizima kwa kuongea na Husein.

Kwa maneno haya, ambayo mara ni yenye kutisha na mara ni yenye kusifu sana, Ibnu Ziyad alivutiwa sana na akamwona Shimr kuwa mshauri wake mwaminifu na mwenye kumtakia mema. Alitilia shaka juu ya uaminifu wa Umar bin Sa’d ambaye kwake aliandika barua akisema, “Sikukupeleka wewe kwa Husein, ukamsikilize na kuzingatia maneno yake, au kurefusha sana mazungumzo yenu au kumpa matumaini ya kuishi au kufanya mapendekezo kwangu yenye manufaa kwake.

Angalia kwa makini sana kwamba kama Husein na marafiki zake (wafuasi) watanyenyekea kwangu na watataka huruma yangu, basi walete kwangu upesi sana, na kama wakikataa kufanya hivyo, waue, na wakate vipande vipande kwani haya ndiyo wanayoyastahili kuyapata.”

Kwa aibu yake ya milele aliongeza kusema, “Kama Husein atauawa, kifua chake na mgongo vikanyagwe chini ya kwato za farasi kwa sababu yeye ni muasi ninaongeza hili kwa sababu nimesema kwamba ningemshugulikia Husein katika namna hii kama ningempata kwa kuuawa kwa upanga. Kama utatekeleza maagizo hayo utalipwa ipasavyo. Kama hupendi kufanya kama ulivyoamriwa hapa, kabidhi madaraka yako kwa Shimr.”

Ubaydullah bin Ziyad baada ya hapo alimpa Shimr barua na akamuambia kwa mdomo kwamba kama Umar bin Sa’d hakutekeleza maagizo yake haraka vya kutosha, lazima achukuliwe kwamba ameondolewa katika wadhifa wake na kwamba Shimr angefanywa kuwa mrithi wake. Kisha alimwambia Shimr kupigana na Husein, amue Umar bin Sa’d na apeleke kwake kichwa chake pia.5

Umar bin Sa’d alikuwa na uhakika kabisa kwamba Husein kamwe asingetoa kiapo cha utii kwa Yazid, wala kujisalimisha yeye na sahaba zake bila ya masharti yoyote kwa Ibn Ziyad, lakini kuwepo kwa Shimr ubavuni pake kulifanya tishio katika kuendelea katika wadhifa wake wa juu, na hatari kwa maisha yake kuwa karibu sana, kiasi kwamba aliagiza maandalizi yafanywe juu ya kumshambulia Husein mara tu baada ya kupata barua ya Ibnu Ziyad.

Ilikuwa tarerhe 9 Muharam kabla ya jioni ambapo mashambulizi kwa kweli yalielekezwa dhidi ya Husein bila ya kumtangulizia taarifa kabla. Husein alikuwa amekaa karibu na mlango wa hema lake, wakati alipotiwa wasiwasi na vishindo vya majeshi yanayokuja, dada yake, Zainab, alimtahadharisha juu ya mvumo huo. Husein alimwambia dada yake katika kumjibu kwamba aliota ndoto Mtume anamwambia kwamba wangeonana naye muda mfupi baadaye.

Wakati huo huo Abbas alimletea Husein habari za mashambulizi, na habari za maagizo kutoka kwa Ubaydullah bin Ziyad. Husein alipendekeza kwamnba adui aombwe kuakhirisha vita kwa usiku ule ili kwamba aweze kuutumia katika du’a na maombi kwa Mwenyezi Mungu, kusoma Qur’an Tukufu, kuomba msamaha Wake na kumwomba Yeye rehema Zake.

Umar bin Sa’d alihisi haja ya kuchukua tahadhari katika uamuzi juu ya ombi la Husein kwa vile Shimr alikuwa yupo pale, alimtaka maoni yake juu ya jambo hili.

Shimr hakutaka kumlazimisha, akasema kwamba kwa vile yeye (Umar) alikuwa katika madaraka, ilikuwa ni juu yake kuliamulia jambo hilo. Kisha aligeukia kwa maafisa wengine kwa maoni yao.
Amr bin Hajjaj al-Zubaydi alisema, “Hata kama watu hawa wangetoka makabila ya Turk na Dailan, kisha wangeomba tahafifu hiyo ndogo, ungepaswa kulikubali hilo.”6 Angalau vita viliakhirishwa kwa usiku huo.

  • 1. Tabari, cha II, uk. 313-314.
  • 2. Ibid.
  • 3. Tabari, cha II, uk. 315 Irshad uk. 343.
  • 4. Jina la Shirm lilikuwa Shurahbil bin Amr bin Muawiya, wa uzao wa al- Walid wa kabila la Bani Amr, kutoka kitabu; al-Akhbar al-Tiwal, uk. wa 267.
  • 5. Tabari, II uk. 315-316 Irshad, 344.
  • 6. Tabari, II uk. 319-320.