Table of Contents

Sura Ya 26: Kumalizika Kwa Mazungumzo Na Kuanza Kwa Vita.

Wakati wa asubuhi na mapema katika siku ya 10 Muharam, 61 A.H, Husein aliongoza idadi ndogo ya wafuasi wake waliokusanyika kwa Sala ya jamaa.

Waliliona lile jeshi kubwa la Umar bin Sa’d, likiwa bila upungufu japo kidogo, kwa maana ya mahitaji ya kimaada, likija kukabiliana na kikundi chao kidogo, kilichoteseka kwa kiu kali kupindukia. Nyuso zao, hata hivyo, hazikuonyesha ishara za kuvunjika moyo, sembuze za kukata tamaa. Kinyume chake, ule uhakika wa kukutana kwao na mauti karibuni sana kulizifanya nyuso zao zikichangamka kwa furaha.

Kwa kweli, mmoja wao, Burayr bin Hudayr al-Hamadan, alikengeuka kwenye umakini wa kawaida wa uzungumzaji wake na alielekea kupamba maneno yake kwa ucheshi wenye mahoka kidogo. Wakati upinzani ulipoingia juu ya mwelekeo usio wa wakati muafaka wa mazungumzo yake alisema, “Naapa kwa jina la Mwenyezi Mungu, kitu ambacho kinatutenganisha kutokana na furaha kuu ya milele hasa ni kutokana na kuchelewa ambako maadui wanakufanya katika kutushambulia kwa panga zao. Kwa kweli naitamani hiyo saa wakati panga zao zitakapoanza kutupiga.”1

Wakati huo huo Umar bin Sa’d alilipanga jeshi lake, lenye askari wapatao karibu 20,000 katika uwanja wa vita. Kwenye kikosi cha Amr bin Hajjaj al-Zubayd alipangiwa kusimamia upande wa kulia wa jeshi na Shimr alipangiwa kuongoza upande wa kushoto wa jeshi. Azra bin Qays al-Ahmasi aliwekwa kuliuongoza jeshi la askari waendao kwa miguu na Shabath bin Ribii alikuwa aongoze jeshi la askari wapandao farasi. Durayd, mtumwa wa Umar bin Sa’d, alipewa bendera ya jeshi.2

Husein pia naye aliongoza jeshi lake dogo kwenye uwanja wa vita. Lilikuwa limekadiriwa kuwa na watu 72, askari 32 wakiwa ni wapanda farasi na 40 ni askari waendao kwa miguu.3 Ni kwa sababu hii kwamba idadi ya wale ambao walijitolea mhanga maisha yao hapo Karbala kwa kawaida inachukuliwa kuwa ni 72.

Kutokana na vyanzo mbalimbali ambavyo vinapatikana, inaonekana kwamba idadi ya wale ambao walipigana upande wa Husein walikuwa kati ya mia moja na mia mbili.
Katika wakati wa kuingia kwenye uwanja wa vita, Husein aliomba dua kwa Mwenyezi Mungu ambayo maneno yake yanaonyesha imani thabiti isiyotikisika katika kumtegemea na kumtumainia Mwenyezi Mungu.

Kwa dua hii maneno ya Yesu Kristo pale Msalabani (kama wanavyodai wakristo kwamba kasulubiwa); “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeni- acha (umenitelekeza)?” Kama ilivyotajwa katika Agano Jipya, yasingekuwa na ulinganisho hata kidogo. Katika upeo wa mateso yake Husein aliomba, “Ee Mwenyezi Mungu, hakika Wewe ndio msaidizi wangu katika dhiki na shida zote, na Kwako Wewe ndio nageukia kwa matumaini katika matatizo yangu yote …”

Husein kisha alilipanga jeshi lake dogo akiukabidhi upande wa kulia wa jeshi hilo kwa Zuhayr bin Qayn, na kwa upande wake wa kushoto ukawekwa chini ya maamrisho ya Habib bin Muzahir na bendera ya jeshi akaikabidhi kwa ndugu yake, Abbas.4

Bani Umayyah walieneza kwa utaratibu maalum, propaganda katika nchi ambazo zilikuwa chini ya mamlaka yao kwamba wao ndio waliokuwa warithi pekee wa Mtume ambaye alikufa bila ya kuwa na watoto.

Kwa hiyo, ilikuwa ni muhimu kwa Husein kwamba afanye jina lake, majina ya mahenga (mababu) wake, sifa njema za familia yake na hadithi za Mtume juu ya tabia njema kumhusu yeye mwenyewe zifahamike kwa mapana sana na bila makosa kiasi kwamba kusingekuwa na hata mtu mmoja aliyebaki kuwa na nafasi yoyote ile ya kudai kutojua ukweli kuhusu yeye, familia yake, na hadithi zilizopo katika Uislam kuhusu yeye.

Kufanya hivi kulikuwa na umuhimu mkubwa ili kuufanya uovu na ukatili wa wakandamizaji wake kujidhihirisha wenyewe kwa kila mtu.

Ilikuwa ni pamoja na lengo lililotajwa katika ibara iliyotangulia kwamba kabla ya kuanza kwa vita, Husein alimpanda ngamia, akaiweka Qur’an mbele yake5 na akiwahutubia wakuu wa jeshi la Umar bin Sa’d, alitoa hotuba akasema, “… msiwe na haraka, Acheni nitekeleze wajibu wa kuku- peni onyo na mwongozo nilio na deni kwenu, na kukuwekeeni mbele yenu ule ukweli wote kuhusu kuja kwangu kwenu ninyi.

Kama mtayaamini maneno yangu na mkanitendea haki mimi, itakuwa hiyo ni bahati kwenu, na mtatambua na kujua kwamba hamuwezi kuwa na sababu ya kunipinga mimi. Kama hamtaamini yale ambayo nitayasema kwenu, na mkaacha kunitendea kwa haki, basi mnakaribishwa kukusanya majeshi yenu… na kuukomesha uhai wangu… Muumba wangu ananitosha …

Fikirini sana kuhusu jina langu na jadi yangu, na jaribuni kuelewa na kutambua mimi ni nani na jaribuni kuwa na haya. Fikirieni kama ni halali kwenu kuimwaga damu yangu au kulishusha daraja langu la juu. Je, mimi siyo mjukuu wa Mtume wenu Muhammad, na mtoto wa binamu yake ambaye alikuwa ndiye mtekelezaji wa wosia wake, aliyekuwa wa kwanza kuukubali, kuuamimi na kula kiapo kwa ajili ya Uislamu?

Je, hamkuisikia ile hadith maarufu sana ya Mtume kumhusu ndugu yangu (Hasan) na mimi kwamba sisi ni mabwana wa vijana wa peponi? Je, Hamza hakuwa kiongozi wa mashahidi, ami yake baba yangu, na Ja’far al-Tayyar ami yangu mwenyewe?

Kama mkikubali ninayokuelezeni kuwa ni kweli, na bila shaka hii ni kweli, kwa vile kamwe sijatamka au sijaongea uwongo, hakuna kinachobakia kwangu cha kuongeza au kueleza. Hata hivyo, kama mngeyafanya maele- zo haya kuwa ya uwongo, bado kuna watu wanaoweza kupatikana ambao watakuelezeni ukweli huu kama mtawauliza. Waulizeni Jabir bin Abdillah al-Ansar, Zayd bin Arqam na Anas bin Malik. Je sasa basi haitoshi hii kukuzuieni kuimwaga damu yangu.”

Baaada ya kukatishwa na baadhi ya watu, aliendela na hotuba yake akisema, “Kama mnatia shaka juu ya ukweli na usahihi wa hadithi hizi za Mtume kunihusu mimi, je mnafanya namna yoyote ya mashaka kuhusu mimi kuwa mjukuu wake? Naapa kwa Allah, kamwe katika Magharibi wala katika Mashariki, hakuna mjukuu wa Mtume zaidi yangu mimi anaishi, kamwe siyo miongoni mwenu nyinyi wala katika kabila lingine lolote lile. Mimi ni Mjukuu wa Mtume wenu Muhammad. Niambieni mumeniinamia mnataka kuniua? Je, mnataka kulipa kisasi cha mauaji ya yeyote yule miongoni mwenu ambaye kwake yeye huyo labda nimeyafanya? Je, mnataka malipo ya mali yenu yoyote ile ambayo labda nimeyasababisha kwa yeyote yule kati yenu?”

Kimya kizito kuligubika jeshi lote la maadui wa Husein, na hakuna hata mtu mmoja aliyethubutu kujibu. Husein kisha akaanza kutaja majina ya maafisa wale wa jeshi la Umar bin Sa’d, Shabath bin Ribii, Hajjaj bin Abjar, Qais bin al-Ash’ath na Yazid bin al-Harith, ambao walitia sahihi zao kwenye barua zilizo na mwaliko wa yeye kuja Kufa, na akawauliza kama wao hawakufanya hivyo (kutia sahihi). Kila mmoja katika watu hawa aliongoza askari si chini ya 500, na unafiki wao wa undumilakuwili ulikuwa sasa unafichuliwa, na uhai wao wote wa baadaye ukawa uko hatarini.

Kwa hiyo walikana kufanya mawasiliano ya kuandikiana na Husein ambaye aliwashutumu kwa kukana kwao ukweli bila haya.

Kisha alihoji kwamba kama kweli hawakutaka yeye aende huko Kufa, wangemruhusu kwenda mahali pengine kwenda kutumia maisha yake huko katika hali ya amani na Usalama. Qays bin al-Ash’ath, ndugu wa Ju’da, yule mwanamke ambaye alimpa sumu al-Imam Hasan mume wake, na pia ni ndugu wa Muhammad bin al-Ash’ath, ambaye alihusika na kukamatwa mateka Muslim bin Aqil, alisema, “Kwa nini ewe Husein hutoi kiapo cha utii kwa Yazid?”

Husein alijibu, “Kwa kweli kabisa wewe ungependekeza hivi. Je, huoni kama inakutosha kungojwa na kujibu juu ya kuuawa kwa Muslim bin Aqil? Sitajitosa mwenyewe katika mikono yenu kwa aibu na fedheha, wala nisingekukimbieni kama mtumwa ili kuyaokoa maisha yangu.” Kisha Husein alimalizia hotuba yake, na akashuka chini kutoka juu ya ngamia wake.6

Wengi wa watu katika jeshi la Umar bin Sa’d walikuwa watu wa Kufa na hutuba zilizotolewa kwao na watu wao mashuhuri zilibeba uzito mkubwa kwao. Zuhayr bin al-Qays alikuwa na fursa ya kuwa mwenye kumuunga mkono Uthman, mpaka kabla ya kutoa kiapo cha utii kwa Husein, kama ilivyokuwa kwa watu wengi wa Kufa.

Uaminifu wake kwa Husein ukiwa umeanza hivi karibuni tu, alikuwa mwenye kukubalika zaidi kwa watu mjini mwake kuliko Habib bin Muzahir, aliyefahamika kwa muda mrefu sana kama mmoja wa wafuasi (shia) wa Ali, na mmoja wa wale ambao walianza kumwita Husein kuja Kufa. Akilihutubia jeshi la maadui, al- Zuhayr alisema, “Enyi watu wa Kufa, ogopeni ghadhabu ya Mwenyezi Mungu…

Amekuwekeni nyinyi na sisi katika mtihani kupitia kwa dhuria (kizazi) wa Mtume Wake, Muhammad, aliyechaguliwa ili kwamba aone ni kwa jinsi gani mtashughulika nao na mtatenda vipi kuhusu wao.

Nakuombeni nyinyi nyote kuwasaidia wao kuondoa utii wenu kwa Ubaydullah bin Ziyad. Kamwe hamtatendewa mema na Yazid na Ibn Ziyad katika kipindi chao chote cha utawala. Wataendelea kukupofueni na kukutoeni macho yenu, watakukateni mikono yenu na kuwanyonga na kuwauwa watu wema kama vile Hujr bin Adi, washirika wake, ambao waliijua Qur’ani kwa moyo, na Hani bin Urwa.”7

Khutuba ya Zuhayr ilikuwa mara nyingi ikikatishwa katishwa na watu wanaojikomba na kujipendekeza wa Ibnu Ziyad. Kisha Shimr akatupa mshale kuuelekeza kwa Zuhayr huku akipiga kelele, “Nyamaza. Mwenyezi Mungu aunyamazishe ulimi wako.”

Zuhayr, hata hivyo aliendelea kuongea na alikatishwa tena na Shimr ambaye alisema, “Hivi karibuni utamuona kiongozi wako na nyinyi nyote mkiuliwa.” Zuhayr alitoa jibu la kijasiri, akasema, “Je, unanitishia kifo? Naapa kwa Mwenyezi Mungu hivyo ndivyo nipendavyo zaidi mimi kufa pamoja nao kuliko kubakia hai nanyi daima.” Kisha aliendelea na hotuba na akawasihi, “Enyi watu, msikubali kupotoshwa na watumwa wa mali kama hawa.

Naapa kwa Mwenyezi Mungu uombezi wa Mtume hautapatikana kwao kwa vile wanamwaga damu ya dhuria wake na ambao wanawaua wasaidizi wao.” Alipoona kwamba maneno yaliyozungumzwa kutoka upande wake yanaleta mishale kama majibu, na kwamba hoja kamili zilikuwa zimetolewa kwa maadui ili waachane na udhalimu wao, Husein alimtaka Zuhayr kuhitimisha hutuba yake.8

Ilikuja kuwa wazi, wakati muda kidogo baadaye katika siku hiyo al-Hurr aliondoka kutoka kwenye jeshi la maadui kwenda kujiunga na Husein, kwamba nia ya Husein ya kurekebisha maadui kwa ukweli wake maelezo na maelekezo ya kuadilisha yote yalifanikiwa katika kuwashawishi wao na kujipatia marafiki kutoka miongoni mwao, mafanikio yake siyo ya kupimwa kwa kuangalia idadi ya watu waliogeukia kwenye fikra zake, bali kwa mazingira ambayo kwayo ameyapata mafanikio hayo, katika mitihani isiyo na kifani, ambayo alikuwa akikutana nayo katika wakati ule pamoja na uhakika wa kuchinjwa yeye mwenyewe, na hatari ya kifo kwa maisha ya wale walioingia upande wa Husein.

Tokea pale ugavi wa maji uliposimamishwa, na kiu ikawatesa sana wafuasi wa Husein, pamoja na watoto wadogo, al-Hurr alikuwa amechanganyikiwa sana kiakili kwani alijichukilia yeye mwenyewe kuhusika katika kubakia kwa Husein kwenye ardhi ya Karbala na kumfanya apige hema zake katika sehemu mbali na mto.

Kumbukumbu za namna ya ukarimu mno ambao kwamba Husein aliwagawia maji al-Hurr, watu wake na wanyama pia katika wakati ambao walikuwa wamedhikika sana kwa sababu ya kiu lazima zitakuwa bado ziko katika fikra zake. Aligundua kwamba Umar bin Sa’d alitamani kuwepo amani na Husein, na alikuwa amefikiria kwamba vita visingepiganwa dhidi ya Husein ambaye khutba yake siku ya 10 Muharram ilileta athari kubwa kwa al-Hurr lakini mapokezi yake ya baridi yalizuia matumaini yake. Alimuona Umar bin Sa’d na akamuuliza kama kweli angepigana na Husein.

Umar akasema ndio atapigana, al-Hurr alimuuliza kama hakukuwa hata sharti moja katika yale yaliyopendekezwa na al-Husein kwa ajili ya kurudisha amani ambalo linakubalika. Umar bin Sa’d alijibu, “Kwa jina la Allah kama uamuzi ungekuwa kwangu basi kwa hakika ningeyakubali mapendekezo ya Husein. Nitafanya nini, wakati mtawala wako hakubali.”9

Al-Hurr hakuwa na cha kungojea, na hatua ilikuwa imefika haswa kwa maamuzi ambayo alikuwa ameyafikia akilini mwake, baada ya kuchunguza undani wa makusudio ya moyo wake kwa kiasi kikubwa, na kuyapatia picha ya kivitendo.

Al-Hurr alichukua uzito mkubwa wa kuyaficha makusudio yake mpaka wakati wa mwisho, kwa hofu ya kuchukuliwa mateka hata kama shaka ndogo sana ya utovu wake wa uaminifu ingelifahamika. Hata hivyo, wasiwasi wake wakati alipokuwa anaondoka kwenda kambini kwa Husein ulikuwa ulionwa na al-Muhajir bin Aws, mtu wa kabila lake, ambaye alimuuliza, “Ewe al-Hurr ni nini makusudio yako? Je, unataka kuanzisha mashambulizi?” Al-Hurr alinyamaza kimya, lakini mtetemeko mdogo ulimpata mwilini mwake.

Al-Muhajir mara moja aliliona hilo na akamuuliza, “Je, unajionaje, ewe al-Hurr? Kamwe sijawahi kukuona ukiwa katika hali hii. Wakati nilipokuwa nikiulizwa kutaja jina la mtu aliye shujaa sana kuliko wote wa mji wa Kufa, jina lako lilikuwa linajitokeza katika midomo yangu. Ni kitu gani kiko nyuma ya mabadiliko haya katika tabia?” Al-Hurr alijibu, “Mbele yangu nina uchaguzi wa kuchagua kati ya pepo na moto kwa saa hivi, na sitapendelea kitu kingine chochote kile kisi- chokuwa pepo, hata kama nichanwe vipande vipande na kuingizwa motoni.” Alipokwisha sema hivi, alimpiga farasi wake na akavuka kwenda kwenye kambi ya Husein.
Alijikabidhi mwenyewe kwa al- Husein, akisema, “Ewe mwana wa Mtume, maisha yangu yawe ni fidia kwako. Mimi ndiye mwenye hatia ambaye nimekuzuia katika njia yako, nikazifuatilia karibu sana hatua zako wakati wa safari yako na nikakufanya upige kambi hapa (katika ardhi ya Karbala).

Naapa kwa Mwenyezi Mungu, kamwe sikuwazia hata kwa fikra ndogo kwamba watu hawa wangeyakataa masharti yako yote ya amani, na kwamba mambo yangekuja kuwa katika hali hii, vinginevyo nisingejishughulisha mimi mwenyewe kutenda dhidi yako kama ambavyo nimefanya.

Sasa mimi niko hapa (mbele yako) nikijionea aibu kabisa mimi mwenyewe, na ninaomba msamaha wa Mola wangu ili kwamba niweze kushiriki kwa moyo wangu wote na nafsi yangu yote katika mitihani yako yote mpaka niwe nimejitoa mhanga maisha yangu chini ya miguu yako.” Husein alimhakikishia kwamba toba yake itakubaliwa na Mwenyezi Mungu.

Alipokwisha hakikishiwa hivyo, na pia baada ya kupata msamaha kutoka kwa Husein, al-Hurr alifikiria kwamba angeelezea maneno machache ya ushauri na nasaha vile vile kwa askari wa jeshi la Umar bin Sa’d.

Aliwahutubia yeye mwenyewe wanajeshi wa Kufa, akisema, “Enyi ndugu zangu kwa nini hamkubali (hata) moja ya masharti yaliyotolewa na Husein, ili kuzuia vita dhidi yake.”

Askari hao walipendekeza jambo hilo lirejeshwe kwa Umar bin Sa’d. Lakini Umar bin Sa’d alisema kwamba uamuzi wa kifanyike nini katika suala hili hauko mikononi mwake vinginevyo angefanya kama ambavyo imependekezwa (kukubali masharti hayo ya amani).

Maelezo haya yalimpandisha al-Hurr hasira kali, ambaye alifoka kwa kusema, “Enyi watu wa Kufa, Mwenyezi Mungu akuangamizeni! Mlimwita hapa mtu huyu mtukuka wa heshima kuu, na katika kuwasili kwake mkamtoa kwa adui yake. Mlikuwa mmetanguliza mbele ahadi yenu ya kutoa mhanga uhai wenu kwa ajali yake, na mumefanya isiwezekane kwake kupumua kwa uhuru, na sasa mumedhamiria kumkaba koo.

Mmemzunguuka na mumemzuia kwenda popote pale ambapo angechagua kwenda katika ardhi hii pana ya Mwenyezi Mungu, na sasa amekuwa kama mfungwa katika mikono yenu. Ameachwa bila msaada, na mmemzuilia yeye, wanawake alionao na watoto, yale maji yatembeayo ya mto Furati ambayo uhuru wa kuyatumia uko wazi kwa Mayahudi, kwa waabudu moto na Wakristo, na ambamo nguruwe na mbwa wa Iraq hugaagaa.

Ni Husein tu na kundi lake ambao wamefikishwa kwenye milango ya mauti kwa sababu ya kiu. Ni jambo la kulaumika kwa kweli, kwa kitendo hiki ambacho mmekifanya kwa dhuria ya Muhammad baada yake. Namwomba Mwenyezi Mungu asiikate kiu yenu katika Siku ya Hukumu wakati haja kubwa sana ya kuhitaji maji itakapowashika.

Kama hamtaki kujilaumu wenyewe kwa matendo yenu mnayoyatenda, na kufungua ukurasa mpya na kubadilika hapa na sasa hivi. Al-Hurr aliitikiwa kwa salaam ya mishale iliyotupwa kumlenga yeye, na akaondoka kurudi kwa Husein.10

Muda ulikuwa umesogea mbele sana siku hiyo wakati Umar bin Sa’d alipomwita Durayd, mshika bendera wa jeshi lake, na akaurusha mshale wa kwanza kuelekea kwenye jeshi la Husein na kuyataka majeshi ya Yazid yashuhudie kwamba yeye (Umar bin Sa’d) amekuwa mtu wa kwanza kushambulia katika vita kwa kurusha mshale kuuelekeza kwa adui.11

Mbali na kutangazwa kuanza kwa vita, mishale iliyotupwa na adui haikusababisha hasara kubwa na wafuasi wa Husein walijibu kwa kutupa mishale mingi kuelekea kwa adui.

 • 1. Tabari, cha II, uk. 326.
 • 2. Tabari, cha II, uk. 327.
 • 3. Tabari, cha II, uk. 325- 326
 • 4. Tabari, cha II, uk. 326; Irishad, uk. 350..
 • 5. Tabari, cha II, uk. 329-330.
 • 6. Tabari, cha II, uk. 330-331; Irishad, 352.
 • 7. Tabari, cha II, uk. 321-322.
 • 8. Tabari, cha II, uk. 232.
 • 9. Tabari, cha II, uk. 332-333
 • 10. Tabari, cha II, uk. 334-335; Irishad, 353-254.
 • 11. Tabari, cha II, uk. 335; Irishad 354