Table of Contents

Sura Ya 27: Masahaba Wa Husein Na Mihanga Yao Ya Kushangaza

Imependekezwa kutoa katika ibara zifuatazo, pamoja na maelezo ya maendeleo ya vita vya Karbala, mukhtasari wa maisha na sifa bainifu za masa- haba wa Husein:

1. Abdallah bin Umayr al-Kalbi, aliyekuwa sahaba wa Ali ibn Abi Talib, alikuwa shujaa sana na raia mtukufu wa Kufa. Alikuwa amemwoa Umm Wahb, binti ya Abd. Baada ya Muslim bin Aqil kuuawa kishahidi, wakati majeshi yalipokuwa yanakaguliwa kule Nukhayla kabla ya kupelekwa Karbala, Abdallah, ambaye nyumba yake haikuwa mbali aligundua kwam- ba walikuwa wanakusudia kwenda kumpiga vita Husein.

Alikuwa siku zote akitamani kupigana dhidi ya washirikina, na akiwafikiria wale ambao wamefanya vita dhidi ya Husein kuwa hawana tafauti na waabudu sanamu, aliamua kuwapiga vita makafiri kama hao. Mke wake alikubaliana naye na akafuatana naye kwenda Karbala kujiunga na Husein.1

Abdallah bin Umayr alikuwa wa kwanza miongoni mwa wafuasi wa Husein kuingia katika uwanja wa vita ambako Yasir na Salim, watumishi wa Ziyad na mtoto wake Ubaidullah, wametoa changamoto kupigana na yeyote yule ambaye angethubutu kupigana nao. Walikataa kupigana na Abdallah bin Umayr, ambaye walisema walikuwa hawamfahamu.

Akikasirishwa na hili, Abdallah aliwaua wote wawili; lakini katika mapambano hayo dhidi ya Salim, vidole vya mkono wake wa kushoto vilikatwa. Akiwa amejeruhiwa lakini (pia) akiwa amefanikiwa, Abdallah alikariri (alisoma) beti zikiweka sifa zake mbele, na kwa kuonya aliongeza kusema,

“Ewe Umm Wahb, naahidi ningerudia rudia kusonga mbele na kuchoma kwa nguvu na mkuki wangu na kutoa mapigo kwa upanga wangu kama vile achepukavyo mbele kijana ambaye humwamini Mwenyezi Mungu.”

Alipokwisha msikia Abdallah bin Umayr akisema haya, Umm Wahb, mke wake, alijitumbukiza katika uwanja wa vita, akisema kwa sauti kubwa, “Wazazi wangu wawe fidia kwako, usiache hata jitihada moja katika kuwasaidia dhuria wa Mtume.”

Akiwa na wivu kwa ajili ya heshima yake, Abdallah bin Umayr alijaribu kumshawishi mke wake arudi hemani kwake haraka sana bila kuchelewa, lakini hakuwa katika hali ya kukubali na alisema, “Sitaweza kukuacha peke yako katika uwanja wa vita, sio kabla ya mimi nami niuawe.”

Kisha aliitwa na Husein ambaye alimwambia kwamba wanawake wameondolewa kwenye wajibu wa kupigana vita vya Jihad. Basi alirudia kwa wanawake wa familia ya Husein. Abdallah bin Umar pia alirudi kutoka kwenye uwanja wa vita.2Alijiunga tena kwenye vita katika kipindi cha baadaye na aliuawa kishahidi baada ya Muslim bin Awsaja (kuuawa kishahidi pia).

2. Al-Hurr bin Yazid al-Riyahi alitoka kwenye familia kongwe na tukufu. Attab, wa ngazi ya nne kutoka kwa al-Hurr katika mpangilio wa kupanda wa nasaba yake, alikuwa mmoja wa watumishi maalum wa Nu’man bin al-Muudhir, mfalme wa Hira. Mmoja wa watoto wake, Qays, alipanda akashika madaraka makubwa baada yake. Mjukuu wa Qays, Zayd bin Umar ibn Qays alikuwa mshairi na Sahaba wa Mtume. Alikuwa ami yake al-Hurr, akiwa binamu wa baba yake, Yazid.

Akiwa mmoja wa watu watukufu wa Kufa, al-Hurr alikuwa afisa katika jeshi la Ubaydullah bin Ziyad aliyetumwa katika eneo la al-Qadasiyya kuweka uangalizi mkali katika barabara.

Baadaye aliamriwa kumwinglia kati Husein ili kumzuia asiifikie Kufa. Kama ilivyokwisha sema, al-Hurr alikuwa na uzoefu binafsi wa utukufu wa tabia ya Husein na ukarimu wake wa wazi usio na kupendelea, wakati ambapo, ili kuwatuliza al-Hurr, watu wake na farasi wao kutokana na kiu kubwa ya maji isiyovumilika, Husein aliwapatia wote maji. Baadaye al-Hurr alimlazimisha Husein kuuacha mpango wake wa kwenda al-Kufa na kupiga kambi hapo Karbala katika sehemu iliyo mbali kutoka mtoni. Katika siku ya 10 ya Muharram al-Hurr aliondoka na kulikimbia jeshi la Umar bin Sa’d na kujiunga na sahaba wa Husein.

Al-Hurr alimwomba Husein aruhusiwe kujitoa mhanga maisha yake kabla ya wengine wote, kwani alikuwa yeye ndiye ambaye aliyempa upinzani wa mwanzo. Alipokwisha pata ruhusa ya Husein, al-Hurr aliingia katika uwanja wa vita na akawashambulia maadui kwa juhudi kubwa na uhodari. Hapo mapema, wakati al-Hurr alipokimbia toka jeshi la Umar bin Sa’d, Yazid bin Sufyan al-Tamimi, askari mmoja katika jeshi, alisema kwamba angempatia al-Hurr mchomo mmoja tu wa mkuki wake kama angegundua kutoroka kwake.

Wakati al-Hurr alipokuwa akiutumia upanga wake kwa mafanikio makubwa, afisa mmoja katika jeshi alimkumbusha Yazid bin Sufyani kuhusu nia yake ya kumuua al-Hurr na kwa hilo mtu huyo alimtaka al-Hurr kukubali kupigana naye. Hili likiwa limekwishakubaliwa al-Hurr mara moja alimuua adui yake.3 Tukio hili liliamsha woga fulani katika nyoyo za adui kiasi kwamba hakuna mtu aliyethubutu kuamka kupigana na al-Hurr ambaye baadaye alitoka kwenye uwanja wa vita. Alikutana na kifo chake baadaye na maelezo mengi kuhusu hilo yatatolewa hivi punde.

3. Muslim bin Awsaja al-Asadi alikuwa ni mfuasi maarufu wa Husein. Mswalihina, aliyependa sana kusimamisha sala za usiku, yeye alimwona Mtume. Alikuwa mpanda farasi mashuhuri na alijipatia sifa kubwa katika vita zilizopita, kama vile katika vita vya kuivamia Azerbayjan nchini Iran katika mwaka wa 20 A.H. Anahesabiwa yeye kuwa chanzo cha kutegemeka cha hadith. Alikuwa ametukuzwa sana katika Uarabu yote.

Baada ya Ubaydullah bin Ziyad kuwa ameteuliwa kuwa gavana wa Kufa, Muslim bin Aqil alikaa na Hani bin Urwa na akachukua jukumu la kuwakusanya wale ambao walitoa kiapo cha utii kwa Husein. Muslim bin Awsaja sasa alishughulika kama mwakilishi maalumu wa kuchukua viapo vya utii na ahadi ya kuwaunga mkono watu wa nyumba ya Mtume. Inabakia bado ni jambo lisiloeleweka vizuri mahali alipokwenda baada ya kifo cha kishahidi cha Muslim bin Aqil na kwa namna gani alivyopanga kwa ustadi hata kuweza kufika Karbala, akiwa tena na umri uliosonga mbele sana kwa miaka.

Baada ya Abdallah bin Umayr na al-Hurr, Nafi bin Hilal al-Jamali alijiunga katika vita, na akamwuua Muzahim bin al-Harith. Hasara waliyoipata jeshi la Ibnu Ziyad mikononi mwa wafuasi wa Husein ilimtia wasi wasi mkubwa mno Amr bin Al-Hajjaj, na aliwaonya watu wa jeshi lake dhidi ya kukutana na wapiganaji wa Husein katika mapigano ya mmoja kwa mmoja, kwani wanajeshi hawa wa Husein ndiyo askari wapanda farasi walio bora kabisa katika nchi kuliko wengine wote ambao walikuwa wanapigana ili kuokoa maisha yao.

Kisha alilishambulia jeshi la Husein kwa kutumia kikosi chote cha jeshi cha upande wa kulia kikiwa chini yake. Shambulio lilipingwa kwa ushupavu mkubwa kiasi kwamba lilibidi liondolewe, lakini lilimwacha Muslim bin Awsaja akigaagaa chini ardhini ndani ya dimbwi la damu yake. Habib bin Muzahir alimuuliza kama alikuwa na matakwa yoyote yale ya mwisho ayaseme. Muslim alinyoosha kidole kwa Husein kuwa jibu lake na akasema, “Matakwa yoyote ya mwisho niliyo nayo yanamhusu yeye tu (Husein).”

Hivyo alikufa akiwa mfuasi wa kwanza katika wafuasi wa Husein katika kuyatoa mhanga maisha yake kwa ajili ya mjukuu wa Mtume.

Wakati habari za kifo cha Muslim bin Awsaja zilipokuwa zinapokelewa kwa shangwe kubwa katika safu za vikosi vya adui, Shabath bin Ribii, ambaye aliongoza kikosi cha askari wa miguu katika jeshi la Umar bin Sa’d alitokea mbele kwa ghafla akisema, “Fedheha gani hii! Mtu kama Muslim bin Awsaja ameuawa na ninyi mnashangalia kifo chake.4
Naapa kwa Mwenyezi Mungu nimeshuhudia matendo makubwa ya kijasiri na yaliyo magumu mno aliyoyafanya kwa ajili ya Uislamu.” Kifo cha Muslim bin Awsaja kilitia nguvu ari ya kupigana ya askari wa adui.

Kwa hiyo, Shimr bin Dhi Jawshan, alishambulia kikosi cha upande wa kushoto cha jeshi la Husein na alipingwa kwa nguvu nyingi sana. Abdallah bin Umayr ambaye kwamba utajo wa ujasiri umekwisha fanywa alijitahidi tena kwa juhudi kubwa na akawaua askari wawili wa jeshi la adui. Kisha naye akashambuliwa na Hani bin Thubayth al-Hadrami na Bukayr bin Hayy na akauawa, akiwa msaidizi wa pili wa Husein kukutana na mwisho wake.5

Mke wa Abdallah bin Umayr, aliposikia kifo cha mume wake aliingia kwenye uwanja wa mapambano kuona maiti yake na akikaa karibu yake alianza kuondoa vumbi na damu kutoka usoni mwake, akisema, “Pokea hongera zangu kwa kufanikiwa kuipata pepo.” Hata hivyo ukatili uliozidi nguvu, ulimshawishi na kumchochea Shimr kumfanya mama huyu asiye na ulinzi kuuawa.6

4. Burayr bin Hudayr al-Hamadan alikuwa mtu wa Kufa na alikuwa sahaba mtu mzima (mzee) wa Ali bin Abi Talib, mtiifu aliyependa sana kusali. Aiijua Qur’ani kwa moyo na alikuwa akiwaelekeza watu na kuwafundisha Qur’an ndani ya msikiti wa Kufa na aliitwa kiongozi wa wale watu ambao waliijua Qur’an kwa moyo. Alijiunga na Husein mahali fulani katika njia ya safari yake kwenda Karbala.

Maelezo ya hotuba yake katika kuijibu hotuba ya Husein, na maelezo yake kuonyesha moyo wake mchangamfu wakati ni masaa machache tu yaliyokuwa yamemtenganisha na kifo yamekwishatolewa.

Wakati Yazid bin Maqil alijotokeza mbele kutoka jeshi la Umar bin Sa’d kutoa changmoto kwa sahaba wa Husein kwa mapambano ya mtu mmoja mmoja alimwita Burayr ambaye alimfahamu kwa muda mrefu. Pia walikuwa wamezoea kuhojiana wenyewe kwa wenyewe kuhusu uhalali na uthabiti wa kidini wa misimamo iliyochukuliwa na Ali na Mu’awiyah. Yazid bin Maqil alilirejea suala hilo tena, na iliamuliwa kwamba wote wawili lazima wamwombe Mungu amlaani mwongo katika wawili hao na auawe kwa upanga na yule ambaye yuko katika haki na sawa.

Hapa walianza kupigana hao wawili. Yazid alipiga dharuba la kwanza ambalo lilisababisha majeraha fulani tu ya juu juu, lakini Burayr ambaye alipiga dharuba la pili, liliikata kofia ya chuma ya Yazid, na upanga wake ulipenya ukaingia kichwani mwake. Yazid alianguka chini kutoka juu ya farasi wake.

Wakati Burayr alipokuwa anachomoa upanga wake Radi bin Munwidhi alimshambulia. Akimwangusha chini ardhini, Burayr alimrukia kifuani mwake. Makelele yake yalimleta Ka’b bin Jabir bin Amr al’Asadi kuja kumsaidia. Alimshambulia Burayr, lakini askari mwingine wa jeshi la Umar bin Sa’d alimsihi asifanye hivyo kwani Burayr aliijua Qur’an kwa moyo na aliwafundisha wengine namna ya kuikariri. hata hivyo Ka’ab bin Jabir, alimuua Burayr.7

5. Munhij bin Sahm alikuwa mtoto wa mjakazi wa Husein, aliyeitwa Husayniyya. Alikuwa ameolewa na Sahm, na alimtumikia Ali bin Husein ambaye alifuatana na mwanae katika safari ya Husein huko Karbala. Munhij aliuawa mwanzoni kabisa mwa vita.

6. Umar bin Khalid alikuwa ametoka miongoni mwa watu watukufu wa Kufa na alikuwa mtu mtiifu na mnyenyekevu kwa watu wa nyumba ya Mtume. Hapo mwanzoni alimuunga mkono na kumsaidia Muslim bin Aqil, lakini watu wengi katika wakazi wa Kufa walipomkimbia, na matumaini yote ya kufaulu kwa njia yake hiyo ilibidi yaachwe, Umar bin Khalid alikimbilia mafichoni.

Alipozisikia habari kwamba Husein alikuwa amefika Hajir akielekea Kufa, Umar bin Khalid mawla wake, Sa’d, Mujammi bin Abdalah, mtoto wake, Aidh, na Jabir bin al-Harith al-Salmani walijiunga na Husein sehemu iitwayo Udhayb al-Hijanat.

Wakati huo huo al- Hurr alifika hapo kumzuia Husein asiendelee na mwendo wa safari yake, na alipinga kuingizwa kwa Umar bin Khalid na washirika wake katika kundi la Husein. Kwa msisitizo wa Husein, pingamizi hilo liliondolewa.

Katika siku ya 10 ya Muharram, Umar bin Khalid na ndugu zake wanne waliyashambulia majeshi ya adui kwa pamoja na panga zao. Askari wa adui waliwazunguuka watu hawa kuwatenga kutoka sahaba wengine waliobakia wa Husein.

Husein alimpeleka ndugu yake, Abbas kwenda kuwanusuru. Peke yake, Abbas aliwafukuza maadui, na akawafanya watu hawa majasiri watembee juu ya farasi wao mbele yake ili kuhakikisha usalama wao. Hata hivyo, mara tu walipowaona maadui wanawafuata, walikasirishwa kiasi kikubwa kwamba walifuata wafukizaji wao, wakiwashambulia kwa nguvu zao zote, mpaka kila mmoja wao akafa akipigana katika sehemu hiyo hiyo.8

Maelezo ya Sa’d, Mujammi, A’idh bin Mujammi na Jabir bin al-Harith yanatokea chini ya majina yao yaliyo orodheshwa (7) mpaka kumi (10).

7. Sa’d, mawla Umar bin Khalid aliuawa kishahidi kama ambavyo imewisha kuelezwa.

8. Mujammi bin Abdallah alizaliwa wakati Mtume bado alikuwa anaishi. Baba yake alikuwa sahaba wa Mtume na yeye mwenyewe alikuwa sahaba wa Ali ambaye ubavuni mwake alipigana vita huko Siffin. Alimwambia Husein kwamba watu maarufu wa Kufa wamehongwa na wameuza uaminifu wao kwa serikali, na kwa hiyo, wote walikuwa dhidi yake. Nyoyo za watu wa kawaida zilikuwa, kwa mujibu wake, zinapendelea upande wa Husein, lakini katika wakati wa vita, panga zao zingegeuzwa kuwa dhidi yake. Aliuawa kishahidi kama ilivyokwishaelezwa.

9. A’idh bin Mujammi alikuwa mtoto wa Mujammi bin Abdallah na aliuawa kishahidi kama ilivyokwisha elezwa.

10. Jabir bin al-Harith al-Salmaani, mtu mashuhuri katika Shi’a wa Kufa alizaliwa wakati wa uhai wa Mtume na alipigana upande wa Ali katika vita vya Siffin. Alitoa kiapo cha utii kwa Husein kwa kupitia mkono wa Muslim bin Aqil, na alishiriki katika vita ambavyo Muslim bin Aqil alivipanga. Hata hivyo, mambo yaligeukia kwenye maangamizi kwa upande wa Muslim bin Aqil na Jabir akajificha. Alikipata kifo cha kishahi- di kama ambavyo imekwishaelezwa.

11. Jundub bin Hujr al-Kindi alikuwa mtu mwenye kujulikana sana, maarufu wa kundi la Shia wa Kufa na sahaba wa Ali bin Abi Talib. Aliongoza vikosi vya Kinda na Azd katika vita vya Siffin. Alikutana na Husein katika safari yake ya kwenda Kufa kabla ya kufika kwa al-Hurr kudhibiti maendeleo yake kuelekea Kufa. Alikufa akipigana kwa ajili ya Husein katika hatua za mwanzo za vita vya tarehe 10 Muharram hapo Karbala

12. Yazid bin Ziyad ibn Muhaasir al-Kindi alikuwa askari shujaa kutoka kwa Shi’a wa Kufa. Alijiunga na Husein kabla ya kuwasili kwa al-Hurr, na alibakia naye Husein katika safari yake. Wakati wa kukaribia Karbala, mjumbe wa Ibnu Ziyad alimletea Hurr barua ikimwelekeza kumlazimisha Husein avunje safari yake haraka sana mara tu al-Hurr atakapoipata barua hii, Yazid bin Ziyad alimtambua mjumbe kuwa mtu atokanaye na ukoo wake mwenyewe wa Kindi. Kwa hiyo, yeye alimkaripia sana na kumlaumu kweli kweli kwa kuleta ujumbe wa kimakosa, wenye dhambi.9

Alikuwa bingwa wa kupiga mishale, na katika tarehe 10 ya Muharram (61 A.H) alipiga mishale mia moja, ilikuwa ni mitano tu ambayo ilikosa sehe- mu zao zilizokusudiwa kupiga. Alipofikia mwisho wa mishale yake, aliingia kwenye uwanja wa vita ambako aliuawa mwanzoni tu wa vita hivyo.10

Shambulio La Kwanza La Jumla

Haishangazi sana zaidi ya inavyokumbukwa kwamba kundi la wafuasi wa Husein wasiozidi watu 150 kwa nje, wakiwa wamechakazwa na kiu ya siku tatu, wangeweza sio tu kulizuia jeshi la Umar bin Sa’d lililokuwa na watu wasiopungua 30,000, bali pia wangefanya mashambulio ya mara kwa mara na yenye mafanikio, ndani ya jeshi la adui wapanda farasi na kulifanya kuwa mchafukoge (vurugika).

Mapigano haya yasiyolingana yaliendelea hivyo hivyo kuanzia asubuhi mpaka karibu ya mchana, na maafisa wa jeshi la adui waliona ugumu kuamua juu ya njia ya utendaji hatua iliyokadiriwa vizuri mno kwa kuleta mwisho wenye kufaa na wa mapema sana.

Baada ya mabishano fulani kati ya makamanda wa majeshi ya wapanda farasi na wa askari wa miguu, Husein bin Tamin alielekezwa aende na jeshi lililowekwa eneo la al-Qadisiyya kufunga njia zote za kuingia na kutoka za Kufa. Pia alipewa wapiga mishale 500 kupiga mishale kwenye kambi ya Husein bin Ali.11

Mvua ya hakika ya vyuma vyenye ncha lazima vitakuwa viliwaangukia Husein na sahaba zake ambao walikabiliana na shambulio hili kishujaa, wakitumia panga zao kama ngao zao, na wakafanya shambulizi kubwa la dhamira juu ya adui, shambulio hili kubwa ambalo lilishuhudia mapigano makali sana linaitwa shambulio la kwanza la jumla na lilifanywa saa moja kabla ya kuingia adhuhuri. Wakati wafuasi wa Husein walipowarudisha nyuma adui, walipata hasara kubwa sana. Watu hamsini kati ya idadi yao ndogo waliuawa na kadhalika farasi wao wote.

Haiwezekani kutambua mpangilio ambao ndani yake watu hawa hamsini wafuasi wa Husein waliuawa lakini majina yao yametolewa moja moja au katika makundi kama ilivyoonyeshwa hapo chini na maelezo mafupi ya maisha yao pia yametolewa pale ilipowezekana:

Al-Harith bin Banhaan
Shabib bin Abdallah al-Nahshali
Qarib bin Abdallah
Nasir bin Nayzar.

Hawa walifuatana na Husein kutoka Madina. Al-Harith alimtumikia Ali, na kisha Hasan na kisha akafuatana pamoja na Husein katika safari yake. Shabib alipigana upande wa Ali kwenye vita vya Ngamia (Jamal), Siffin na Nahrawan. Mama yake Qarib, aitwaye Fakiha alimtumikia mama yake Sakina, mke wa Husein. Baba yake Nasr alikuwa na nasaba ya kifalme na alifundishwa na Mtume. Nasr alitumia ujana wake akiwa katika kundi la Ali, na kisha akabakia katika kuambatana na watoto wake.

Janada bin Ka’b al-Ansar,
Abd al-Rahman bin Abd Rabb al-Ansar alijiunga na Husein mjini Makkah, Jabir bin Hajjaj al-Taymi,
Jabla bin Ali al-Shaybani,
Hubab bin Amir bin Ka’b al-Taymi, na
Zarghama bin Malik al-Taghlabi.

Hawa hapo mwanzo walimuunga mkono Muslim bin Aqil, lakini wakati Ubaydullah bin
Ziyad alipofanikiwa kuwageuzia mbali watu katika kumuunga mkono na kumsaidia, walikimbia
kwenda kujificha, na baadaye walipoisikia safari ya Husein ya kwenda Kufa, walipanga kuungana naye hapo Karbala.

Al-Harith bin Imru al-Qays bin Abis al-Kindi,
Juwayn bin Malik bin Qays al-Taymi,
Halas bin Amr al-Azd,
Ndugu yake al-Nu’man,
Zuhayr bin Salim bin Amr al-Azdi,
Mas’ud bin al-Hajjaj al-Taymi,
Abd al-Rahman bin Mas’ud,
Abdallah bin Bishr al-Khath’ami,
Amr bin Zabi’a bin Qays al-Taymi,
Qasim bin Habib bin Abi Bishr al-Azdi.

Hawa waliwasili Karbala na jeshi la Umar bin Sa’d. Abd al-Rahman bin Mas’ud na Masud bin Hajjaj walikwenda kwa Husein tarehe 7 Muharram kutoa heshima zao kwake na kamwe hawakurudi tena kwenye uhudumu wao wa kijeshi. Watu watano wa kwanza katika kundi hili walivuka na kwenda kwa Husein wakati mapendekezo yote ya kuleta amani yaliy- ofanywa naye yalipokataliwa, na vita ikawa haikwepeki. Wale wengine watatu pia waliobakia walikwenda kwake katika nyakati zisizojatwa maalum.

Shi’a wa Basra walikuwa wakikutana katika nyumba ya mama mmoja, aliyeitwa Mariyya, bint ya Munqidh, ambaye alikuwa kipenzi cha watu wa nyumba ya Mtume. Wakati habari zilipofika Basra kuhusu safari iliyokusudiwa ya Husein kwenda Kufa, na kufungwa kwa barabara zielekeazo katika mji huo na gavana wa Basra, Yazid bin Nubayt alionyesha nia yake ya kwenda kumsaidia Husein. Kwa vile mpango huo ulikuwa wa hatari, watu wengi hawakuungana na shauku hiyo ya Yazid. Hata hivyo, aliondoka kwenda safari hii ya hatari pamoja na watoto wake wawili:

Abdallah, na Ubaydullah,12
Adham bin Umayyah,
Sayf bin Malik al-Abdi,
Amir bin Muslim al-A’bdi al-Basri,
Salim, mtumwa wa Amir bin Muslim.

Walikutana na Husein sehemu iitwayo al-Abtah ndani ya mipaka ya Makkah, na wakafuatana naye kwenda Karbala.

Mtumwa mwaminifu wa Hasan, kwa jina aliitwa Salim, aliuawa pia kishahidi katika shambulio hili. Inaonekana kwamba katika mwendo wa safari yake, Waarabu wengi walivutiwa na msafara wa Husein kwa matu- maini yasiyo na msingi, na kwamba walimwacha mara tu walipoutambua ukweli. Lakini wengine waliambatana naye na waliuawa katika mapigano ya mwanzoni. Hao walikuwa ni:

Abd bin Muhajir al-Juhani,
Uqba bin Salat al-Juhami,
Mujammi bin Ziyad bin Amr al-Juhani,
Qasit bin Zuhair bin al-Harith al-Taghlabi,
Muqsit, pia ndugu wa Qasit,
Kardus, pia ni ndugu wa Qasit.

Ndugu hawa walikuwa masahaba wa Ali. Kisha waliungana na kundi la Husein mpaka alipoondoka kwenda Madina. Baada ya hapo ndugu hawa walifanya makazi hapo Kufa na kwa kufika kwa Husein hapo Karbala waliweza kuungana naye.

Umayyah bin Sa’d bin Zayd al-Tai alikuwa mkongwe aliyebobea ambaye alipigana katika vita vya Siffin akiwa katika upande wa Ali. Alifika Karbala wakati Husein alikuwa anafanya mazungumzo ya kupatikana amani na Umar bin Sa’d.

Zahir bin Amr al-Kind alikuwa Sahaba wa Mtume. Alishiriki katika vita vya Khaybar, na alifahamika sana kwa ushujaa wake, na alikuwa na mapenzi makubwa na Ahlul-l’Bait. Wakati Ziyad alipokuwa gavana wa Kufa na Amr bin Hamiq al-Khuzai akasimama kuwa dhidi yake, Zahir alijiunga naye. Hata hivyo, alifanikiwa kujificha na akakwepa kukamatwa.
Aliitekeleza ibada ya Hijja katika mwaka wa 60 A.H. na akakutana na Husein, na aliungana na vikosi vya kijeshi vya sahaba wake alibakia pamoja naye na akafuatana naye kwenda Karbala.

Suwar bin Abi Umayr al-Nahmi alikuwa msimulizi wa hadith ambaye alifika Karbala baada ya Husein akiwa amefungua mazungumzo ya amani. Tarehe 10 ya Muharram alishiriki katika Jihad hiyo, alijeruhiwa na akakamatwa na akapelekwa kwa Umar bin Sa’d ambaye alitaka kumuua.

Askari watokanao na kabila lake walilipinga hili na wakamwondoa. Hata hivyo, alikufa kutokana na majeraha.

Shabib ibn Abdallah alikuwa mtu wa Kufa na alikuwa mawla wa al-Harith bin Sari al-Hamadani, na Sahaba Mtume. Alishiriki katika vita vya Ngamia (Jamal), Siffin na Nahrawan akiwa upande wa Ali na akafika Karbala akiwa pamoja na Sayf na Malik, watoto wa bwana wake.

Abd al-Rahman bin Abdillah bin Kadan al-Arhabi alikuwa mmoja kati ya ujumbe wa pili wa watu wa Kufa ambao uliomwona Husein. Baada ya kuuawa kwa Muslim bin Aqil na kufika kwa Husein hapo Karbala aliweza kuungana na Husein.

Ammar bin Abi Salama al-Dulani alipigana upande wa Ali katika vita vya Ngamia (Jamal), Siffin, na Nahrawan.

Ammar bin Hasan al-Ta’ai alikuwa Shia maarufu sana. Baba yake aliuawa katika vita vya Siffin, akiwa sahaba wa Ali. Ammar alifuatana na al-Husain kutoka Makkah hadi Karbala.

Kinana bin Atiq al-Taghlabi alikuwa mtu wa Kufa, na alikuwa maarufu kwa ujasiri wake. Alikuwa msimamishaji Sala na aliijua Qur’an kwa moyo. Alijiunga na Husein hapo Karbala kabla ya vita havijapiganwa.

Muslim bin Qasir al-Azdi alifanywa kuwa mlemavu wakati akipigana kati- ka Vita vya Ngamia (Jamal). Alitokea Kufa kumsaidia Husein.

Na’im ibn Ajlan al-Ansari na ndugu zake, Nasr na al-Nu’man, walikuwa masahaba wa Ali. Kaka yake alimtangulia kufa. Wakati Husein alipowasili Iraq, Na’im aliweza kuungana naye Karbala akitokea Kufa.

Habsha bin Qays al-Nahmi alikuwa mjukuu wa sahaba wa Mtume, na yeye mwenyewe alikuwa msimulizi wa hadith.

Hajjaj bin Zayd al-Taymi alikuwa mtu wa Basra. Wakati akiondoka Makkah, Husein alipeleka barua kwa watu mashuhuri wa Basra, pamoja na Mas’ud bin Amr al-Azd. Mas’ud alikusanya watu wa koo za kabila lake za Bani Tamimi, Bani Hanzala, Bani Sa’d na Bani Amir na aliwasihi na kuwashawishi kwenda kumpa msaada Husein, na kundi moja la watu miongoni mwao liliahidi kufanya hivyo.

Mas’ud aliandika barua katika kujibu na aliikabidhi kwa al-Hajjaj ili aifikishe kwa Husein. Mjumbe ali- itoa barua na pia alijitoa mhanga maisha yake kwa ajili ya Husein.

Habab bin al-Harith
Hanzal bin Umar al-Shaybani
Zuhayr bin Busr al-Khath’ami
Imran bin Ka’b al-Ashjai
Maani‘ bin Ziyad

Hakuna lolote linalojulikana kuhusu watu hawa.

Mashambulizi Katika Kambi Ya Husein

Wakitiwa moyo (wa kupigana) kutokana na askari wengi waliouawa kutoka kwenye kikundi kidogo cha Husein chenye askari waaminifu, na mashujaa, jeshi la Umar bin Sa’d lilianzisha mashambulizi katika kambi ya Husein. Lengo lao lilikuwa kufika nyuma ya kambi ya Husein, na kuwazunguka watu wake kwa nyuma ambako kulisimama safu za mahema ya watu wa Husein yaliyofungwa kwa kukamatana moja moja kwa kamba kwa umadhubuti na uimara kiasi kwamba yaliyoonekana kama ukuta imara au ngome.

Alipoona hivi, Umar bin Sa’d aliamuru kamba zikatwe. Wanajeshi wa Husein hapo walirudi kwenye mahema na wakawashitukiza na kuwaua wavamizi wale. Kwa kushindwa huku kwa jaribio lake la kutaka kuwazunguuka wapiganaji wa Husein, Umar bin Sa’d aliamuru mahema yachomwe moto. Kuungua kwa mahema yenyewe kulilishinda lengo na kusudio la adui, na katika kukasirika Shimr alitaka kulichoma hema la Husein moto ili kuwaua watu wote waliokuwemo ndani yake.

Shabath bin Rib’ii, kamanda (kiongozi) wa kikosi cha miguu katika jeshi la Umar bin Sa’d alimwambia Shimr, “Bado mpaka sasa sijawahi kusikia jambo lenye dhambi kubwa zaidi ya hili likitamkwa.” Hakuruhusiwa kutekeleza mipango yake ya kikatili na upinzani uliotolewa na watu wa kundi lake mwenyewe. Wakati huo huo Zuhayr bin al-Qayn alifanya shambulio kali kwa adui kwa msaada wa marafiki zake kumi, na kumrudisha sana nyuma Shimr, akaua mmoja wa watu wake mashuhuri. Tukio hili liliwakasirisha maadui na wakafanya shambulizi kali la nguvu la kujibu, na kusababisha umwagaji mwingi wa damu. Adui alishindwa tena.

Wafuasi wawili tu wa Husein ndio walipoteza maisha yao. Walikuwa ni: Bakr bin Hayy al-Taymi ambaye alijiunga na Husein baada ya kuja Karbala na majeshi ya Umar bin Sa’d.

Amr bin Janaada bin Ka’b al-Khazraji, kijana aliyekuwa mdogo wa karibu miaka kumi ambaye alifuatana na wazazi wake kuja Karbala. Baada ya baba yake kufa kishahidi hapo Karbala katika shambulio kubwa la kwan- za la adui, mama yake alimwelekeza apigane kwa ajili ya al-Husein. Amr alimuomba Husein ruhusa afanye hivyo, lakini ruhusa haikutolewa.

Amr aliomba kwa kusihi kwamba mama yake mwenyewe alimwagiza kupigana kwa ajili ya Husein. Basi alipata ruhusa ya kwenda kupigana. Aliingia kwenye uwanja wa vita na askari wa upande wa adui walimkata kichwa. Kwa hili mama yake akasema kwa sauti kubwa, “Vizuri sana, mwanangu! Umeufariji mno moyo wangu katika kuyatoa maisha yako mhanga kwa ajili ya Husein.” Adui walimtupia mama yule kichwa cha mwanawe, laki- ni aliwarudishia kichwa hicho, na akiokota rungu la chuma alikwenda kupambana na maadui yeye mwenyewe. Alikatazwa na Husein asifanye hivyo kwani wanawake wamesamehewa katika kupigana Jihad.

Mashambulizi Wakati Wa Sala Za Mchana

Wakati huo saa ya sala za mchana ikaingia. Abu Thumaama Amr bin Abdallah al-Saa’id alimwelezea Imam Husein kwamba maadui walikuwa wamemsogelea karibu sana, na akaonyesha haja ya kusimamisha Sala za mchana na Husein kwani zingekuwa ni za mwisho katika uhai wake ambazo angezifanya na Imam. Husein alimtaka awaombe watu wa upande wa adui kusimamisha mapigano katika kipindi chote cha Sala. Husein bin Tamim alitokea ndani ya vikosi vya jeshi na alisema, “Sala zenu hazi- takubaliwa.”

Habib bin Muzahir alirudia tena, “Hazitakubaliwa? Je, unad- hania kwamba Sala za mtoto wa Mtume hazikubaliwi, na za kwenu ndiyo zinakubaliwa?” Hili lilipelekea Husein bin Tamin kumshambulia Habib, na mapambano ya watu wawili hawa yakafuatia, na Husein bin Tamim alishindwa vibaya sana katika mapambano hayo, lakini aliondolewa akapelekwa kwenye usalama.

Habib bin Muzahir sasa aliingia katika orodha. Alikuwa miongoni mwa masahaba mashuhuri wa Ali kama Mitham al-Tammaar na Rashid al-Hijrii na pia mmoja katika sahaba zake na sahaba wa Hasan na Husein.
Itakumbukwa kwamba alikuwa amechukua nafasi muhimu katika kuzifadhili harakati za kumwita Husein kuja Kufa na kwamba barua ya kwanza aliyoandikiwa na shia wa Kufa ilikuwa ina sahihi zake. Pia, katika kufika kwake Kufa,

Muslim bin Aqil aliahidiwa kila aina ya msaada kutoka kwake. Katika mahala pengine mbali mbali, Habib alijaribu kuhojiana na maadui wa Husein juu ya njia zao za kiuovu. Katika mkesha wa tarehe 10 ya Muharam, alikuwa amepata idadi ya juu ya watu wa ukoo wa Bani Asad ambao walikuwa wanaishi katika maeneo ya Karbala kumuunga mkono Husein. Umar bin Sa’d, hata hivyo, alitishika na ujumbe wa Habib, na alipeleka askari mia tano (500) waliopanda farasi ili kuwazuia Bani Asad wasimfuate Habib.

Habib alikuwa kamanda wa kikosi cha kushoto cha jeshi la Husein, na alipigana kwa ujasiri mkubwa na alimuua askari mmoja wa Bani Tamimi kwa pigo moja la upanga wake. Askari mwingine wa upande wa adui alimshambulia kwa mkuki, na Habib akaanguka chini kutoka juu ya farasi wake na adui yake ambaye hapo kwanza alikuwa amemshinda, Husein bin Tamim alimpiga kichwani kwa upanga wake na Habib akaanguka chini akiwa amekufa. Kifo cha kishahidi cha Habib kwa uwazi kabisa kilimwathiri Husein.

Mwisho wa Jihad ya al-Hurr sasa inabakia kuelezewa. Farasi wake alikuwa amekwishauawa. Baada ya kifo cha Habib, al-Hurr aliamua kujitoa mhanga mwenyewe. Alianza kupigana sambamba na Zuhayr bin al-Qayn lakini mpango huu ulivunjika kutokana na shinikizo la jeshi la miguu ambalo lilimtenganisha na kumzunguuka al-Hurr. Al-Hurr kwa matokeo ya hali hii alipigwa akaanguka chini.

Wakati mwili wa al-Hurr ulipokuwa unarudishwa kutoka uwanja wa vita, Husein mwenyewe aliondoa vumbi na damu kutoka kwenye uso na akasema, “Al-Hurr, wewe uko huru katika dunia hii na pia katika ulimwengu ujao.”

Abu Thumaama al-Saa’idi, mpanda farasi hodari sana nchini Uarabuni mtu maarufu sana katika Shi’a wa Ali ambaye aliambatana naye katika vita vyote alivyopigana (Ali), akaufanya mji wa Kufa makao yake baada ya Hasan kuondoka mjini pale. Alimuunga mkono na kumsaidia Muslim bin Aqil kwa nguvu zote baada ya yeye (Muslim bin Aqil) kuwasili Kufa.

Wakati hali ilipokuwa ni ya hatari, Muslim bin Aqil akamkabidhi Abu Thumama mafungu ya pesa na kazi ya kumkusanyia silaha. Baada ya kifo cha kishahidi cha Muslim bin Aqil, Abu Thumama aliondoka Kufa na Naafii bin Hilal na akajiunga na Husein katika safari yake ya kwenda Iraq.

Katika siku ya 10 ya Muharram alielezea kwa Husein haja yake ya kujiunga kwenye Sala zitakazoongozwa naye (Husein) kabla ya kwenda kukutana na Mola wake. Husein alimbariki Abu Thumama kwa kukumbuka kusimamisha Sala katika wakati kama huu wa hatari. Pia alimtuma kwam- ba watu wa upande wa adui waombwe kusimamisha vita katika kipindi chote cha kusimamisha Sala. Hili lilisababisha mlipuko wa vurugu na ghasia ambazo ndani yake Abu Thumama alikuwa miongoni mwa wale ambao waliuawa.

Sala Ya Adhuhuri

Mapigano hayakusimamishwa. Katika nyakati za hatari na hofu muundo wa Sala fupi umeelekezwa, unaoitwa “salat al-Khawf,’ yaani Sala ya hofu. Akiwa na imani kamili katika uthabiti na ushujaa wa sahaba zake, Husein alimwelekeza Sa’id ibn Abdallah al-Hanafi na Zuhayr bin al-Qayn kusimama mbele yake ili kwamba aweze kuswali Sala ya mchana (ya adhuhuri).

Wote sahaba wawili hawa wajitoleao mhanga nafsi zao wenyewe walisonga mbele pamoja na karibu nusu ya wafuasi wote wa Husein, na wakisimama mbele yake, walimkinga kama alivyoelekeza.

Sa’id bin Abdallah al-Hanafi alikuwa mtu maarufu miongoni mwa Shi’a wa Kufa na alifahamika kwa ujasiri na uchamungu wake. Alikuwa ameahidi msaada wa uaminifu kwa Muslim bin Aqil pindi atakapowasili Kufa.
Alithibitisha ukweli wa maneno haya fasaha ambayo kwayo, mnamo usiku wa mwezi 10 ya Muharram, yeye aliahidi kuyatoa mhanga maisha yake kwa ajili ya Husein, kwa kusimama pamoja na Zuhayr bin al-Quyn mbele ya Husein kumkinga asipatwe na mishale wakati akisimamisha Sala zake za mchana.

Si chini ya mishale kumi na tatu ilimwingia mwilini mwake kabla ya kumalizika kwa Sala. Kisha alianguka chini akafariki.

Zuhayr bin al-Qayn bin Qays al-Bajali alikuwa mtu wa Kufa na alikuwa miongoni mwa watu wa daraja kubwa kidogo wa Uarabuni. Alipigana kati- ka vita nyingi, alihesabika kwa ujumla kuwa miongoni mwa wale ambao wakidai ulipizaji kisasi kwa ajili ya Uthman, wafahamikao kama wa Uthmaniyya kama watofautishwavyo kutoka Alawiyya, ambao walikuwa wafuasi wa Ali.

Tayari ilikwishaelezewa kwa kurudia jinsi gani katika kurudi kwake baada ya kufanya ibada ya Hija mwaka ule, alikutana na Husein sehemu iitwayo Zarud na jinsi gani kwa haraka na kwa ukamilifu alivyobadilishwa kuingia katika itikadi za Husein.

Aliwekwa kukiongoza kikosi cha majeshi ya Husein. Kuonyesha huruma na upendo, kwa maneno na vitendo, juu ya utiifu wake wa kudumu kwa Husein pia vimekwisha tajwa. Alipewa jukumu la kusimama na Sa’id bin Abdallah al-Hanafi mbele ya Husein kumkinga kutokana na mishale wakati wa kusimamisha Sala zake za mchana. Sa’id alikufa kutokana na majeraha yaliyosababishwa na mishale na Zuhayr pia alikuwa amejeruhiwa vibaya sana. Wakati alipoona kwamba maadui walikuwa kwa hatari sana wako karibu na Husein alifanya shambulizi lake la mwisho na akafa akipigana.

Salman bin Muzarib bin Qays al-Bajali, binamu yake Zuhayr bin al-Qayn alifuatana na Zuhayr na aliuawa kishahidi wakati wa mchana ule.

Amr bin Quraaza bin Ka’b al-Ansaar alikuwa mtoto wa Sahaba wa Mtume na alikuwa mtu wa Kufa. Alifika Karbala katika mwezi wa Muharram mwaka wa 61 A.H. na alitumwa na Husein kwa Umar bin Sa’d apendekeze kwake kufungua mazungumzo ya amani. Wakati wa mchana wa mwezi 10 ya Muharram, Amr alingia katika vita na baada ya kufanya mapigano kiasi fulani alirudi kwa Husein kwenda kumlinda kutokana na mishale, akiutumia mwili wake mwenyewe kama ngao mpaka akauawa kishahidi.

Nafi’ bin Hilal al-Jamali alikuwa mkubwa wa kabila lake na aliijua Qur’an kwa moyo. Alipigana katika upande wa Ali katika vita vya Ngamia (Jamal), Siffin na vya Nahrawan na akajiunga na Husein katika safari yake akienda Iraq. Wakati adui alipoanza kuzuia maji yasimfikie Husein, alienda na Abbas na watu wengine ishirini kuchukua maji kwa nguvu.

Waliwasukuma nyuma walinzi waliowekwa hapo mtoni na wakafanikiwa kuleta kiasi cha maji kwenye kambi ya Husein. Nafi’ alikuwa bingwa wa kutumia upinde na katika mchana wa tarehe 10 ya Muharram aliwaua watu kumi na mbili wa maadui mbali na kuwajeruhi wengine wengi kwa mishale yake. Alikamatwa na maadui na mikono yake yote miwili ilivunjwa. Alichukuliwa akapelekwa kwa Umar bin Sa’d ambako Shimr alimuua wakati ambapo Nafi’ alimshukuru Mwenyezi Mungu kwamba alikuwa anakufa mikononi mwa viumbe Vyake walio wabaya mno kuliko viumbe vingine vyote.

Shawdhab bin Abdallah alikuwa mtumwa wa Abis bin Abi Shabib al- Shakri na alifuatana na bwana wake kwenda Makkah. Huyu Abis bin Abi Shabib al-Shakri alimletea Husein barua moja kutoka Kufa iliyoandikwa na Muslim bin Aqil.

Wote wawili bwana na mtumwa walifuatana na Husein katika safari yake ya kwenda Karbala. Wakati alipoulizwa na bwana wake siku ile ya tarehe 10 ya Muharam kuhusu kipi amepangilia cha kukifanya, Shawdhab mara moja alijibu kwamba alikuwa hana nia nyingine yoyote ile isipokuwa kupigana kwa ajili ya Husein na kuuawa. Shawdhab kisha alitoa heshima zake za mwisho kwa Husein na alitoka kwenda kupigana na akafa kifo cha kishahidi.

Abis bin Abi Shabib al-Shakhri alikuwa miongoni mwa viongozi wa Shi’a wa Kufa, ni mzungumzaji wa busara, msalihina sana, na aliyezoea kukesha wakati wa usiku. Wakati Muslim bin Aqil alipoisoma barua ya Husein kwenye mkusanyiko wa watu wa Kufa, yeye Abis alitoa hotuba yenye ushawishi mkubwa na alimhakikishia Muslim msaada wake kwa kipindi atakachoishi.

Baada ya watu 18,000 walipokwishatoa kiapo cha utii kwa Husein, Muslim aliandika barua kwa Husein, akiipeleka kwa kumtumia Abis ambaye alikwenda pamoja na mtumwa wake Shawdhab, na walitoa barua hiyo kwa Husein huko Makkah. Abis na mtumwa wake kisha walisafiri pamojna na Husein kutoka Makkah kwenda Karbala. Baada ya Shawdhab kujitoa mhanga maisha yake, Abis alimwomba Husein kumruhusu kuingia katika uwanja wa mapambano.

Akiipokea ruhusa hiyo, Abis aliziendea safu jeshi la upinzani (adui), na akatoa changamoto kwa mtu yeyote katika majeshi ya adui atoke kupam- bana naye katika mapambano ya ana kwa ana. Hata hivyo, hilo ni tishio alilolitoa yeye kiasi kwamba hakuna hata mtu mmoja aliyethubutu kuikubali changamoto yake hiyo. Umar bin Sa’d aliamuru kwamba Abis apigwe mawe mpaka afe.

Kwa hiyo mawe yalianza kummiminikia Abis kutoka pande zote. Katika mapigano ya namna ya woga wa namna hii, Abis aliondoa kofia yake ya chuma na akawashambulia maadui, akipepea upanga wake, na kuwaswaga mamia ya askari mbele yake. Kisha idadi kubwa ya maaskari walimzunguka na wakamuua.

Abdallah na Abd al-Rahman bin Urwa walikuwa wajukuu wa Haraaq al-Ghiffar, sahaba wa Ali. Walifika Karbala wote pamoja na wakajitoa mhanga maisha yao kwa ajili ya Husein katika mchana wa mwezi 10 ya Muharram.

Hanzala bin Asad al-Shaybaani alikuwa mtu maarufu katika Shi’a wa Kufa, na alikuwa mzungumzaji mzuri. Aliijua Qur’ani kwa moyo. Alijiunga na Husein hapo Karbala, na tarehe 10 ya Muharram wakati wa mchana, baada ya wafuasi (wapenzi) wengi wa Husein walipokuwa wamekwishauawa, aliwahutubia maadui, akiwaonya kwa ukali kuhusu njia mbaya na ya dhambi walioichukua. Aliwataka waogope ghadhabu na hasira za Mwenyezi Mungu katika Siku ya Hukumu, na wajizuie kumuua Husein. Kisha alienda kupigana, na baada ya muda kidogo, aliuawa.

Saif bin al-Harith bin Sari na Malik bin Abd bin Sari bin Jabir al-Hamadani walikuwa mabinamu wa kwanza. Walijiunga na Husein hapo Karbala wakati majadiliano ya kuleta amani yalikuwa bado yanaendelea kati ya Husein na Umar Sa’d. Wote wawili walikufa wakipigana kwa ajili ya Husein.

Jawn, Mhabeshi, alikuwa mtumwa wa Fadhl bin Abbas bin Abdul Muttalib ambaye alimuuza kwa Ali. Ali alimtoa zawadi kwa Abu Dharr. Baada ya kifo cha Abu Dharr, Jawn alirejea Madina kumtumikia Ali, Hasan na Husein kwa mfuatano wa mmoja baada ya mwingine. Tarehe 10 ya Muharram, alisisitiza juu ya kujitoa mhanga maisha yake kwa ajili ya Husein ili kuweza kuipata pepo. Aliona haiwezekani kabisa kumtelekeza Husein katika wakati wa dhiki na taabu zake. Alikwenda kupigana na baada ya muda fulani aliuawa.

Mtumwa wa Kituruki alitolewa kwa Husein na mwanawe, Ali Zainul- Abidiin. Aliihifadhi Qur’ani kwa moyo. Alipokwishapata ruhusa ya kupigana, aliingia katika uwanja wa vita, na baada ya kuawa askari wengi wa upande wa maadui alianguka chini akiwa amejeruhiwa vibaya sana. Husein alimwendea, na akaweka mikono yake kuzunguka shingo yake, wakati uso wake ukiwa umegusana na uso wa mtumwa anayekufa, aka- fungua macho yake, akatabasamu na (kisha) akafariki dunia.

Anas bin al-Harith al-Asadi alikuwa miongoni mwa Masahaba wa Mtume na alisimulia hadith zake. Alimsikia Mtume akitabiri mhanga utakaotole- wa na Husein, na akawa ametamani kuwa katika upande wake (Husein), kama tukio hilo lingetokea katika uhai wake.

Anas alikuwa mzee sana wakati wa Vita vya Karbala vilipopiganwa. Alifika Karbala akiwa na Husein na alipopata ruhusa ya kupigana, aliziamsha nyusi zake za macho zilizolegea kwa kuzikaza kwa kitamba, na alijifunga kiunoni barabara kwa kilemba chake, na akafa akipigana kwa ajili ya Husein.
Hajjaj bin Masruq al-Jufi alikuwa ni Shi’a wa Kufa aliyeheshimiwa sana, na sahaba wa Ali. Alijiunga na Husein kule Makkah na alikuwa ndiye mwadhini wa Sala zilizoongozwa na Husein. Alipigana na aliua watu wengi wa upande wa maadui. Hatimaye aliuawa kishahidi.

Ziyad bin Arib al-Hamdani alikuwa mwenye kufanya ibada (kusimamisha Sala), mwenye kujihini
na alikuwa akitukuzwa kwa ushujaa wake. Alifanya mashambulizi ya ari kubwa na hatimaye
aliuawa kishahidi.

Salim bin Amr bin Abdallah alikuwa mtumwa wa ukoo wa Bani Kalb wa Madina. Aliungana na Muslim bin Aqil wakati Musilm bin Aqil alipopigana kwa kuokoa maisha yake. Baada ya Muslim kujitoa mhanga maisha yake Salim alikamatwa, lakini alifanikiwa kutoroka na kujificha. Wakati aliposikia habari za kuwasili kwa Husein hapo Karbala, aliungana naye na akauawa kishahidi siku ile ya mwezi 10 ya Muharram.

Sa’d bin al-Harith alikuwa mtumwa wa Ali ambaye alifuatana na Husein kutoka Madina hadi Karbala ambako aliuawa kishahidi.

Umar bin Jundab al-Hadrami alikuwa mmoja wa Shi’a wa Kufa, na alipi- gana katika upande wa Ali katika Vita vya Jamal (ngamia) na Siffin. Katika mwaka wa 51 A.H., wakati Hujr bin Adi alipokosana na serikali ya Bani Umayyah, aliungana na wafuasi wa Hujr, lakini wakati Hujr alipokamatwa na kupelekwa Syria Umar alijificha. Alikuwa mmoja wa watu waliomuunga mkono Muslim bin Aqil na kwa siri wakaungana na Husein baada ya kifo cha kishahidi cha Muslim bin Aqil na yeye aliuawa kishahidi tarehe 10 ya Muharram 61 A.H.

Qa‘nab bin Amr al-Numari alikuwa mtu wa Basra, na aliipata shahada siku ya mwezi 10 Muharram pale Karbala. Yazid ibn Thubayt al-Abdi alikuwa mtu wa Basra. Mazingira ambayo kwamba alikiongoza kikundi cha wakazi wa Basra kwenda kwa Imam Husein na akakutana naye pale al-Abtah karibu na Makkah, habari zake zimekwisha simuliwa tayari kwenye maelezo ya kujitoa mhanga maisha ya watoto wake, Abdallah na Ubaydullah. Alikwenda kupigana Siku ya tarehe 10 ya Muharam baada ya watoto wake walipokwishauawa na yeye alili- pata taji la kishahidi.

Yazid bin Mughfil al-Ju’fi alikuwa mmoja wa masahaba wa Ali, na alikuwa ameteuliwa kukiongoza kikosi cha kulia cha jeshi lililopelekwa kuzima maasi ya Ahwaz. Alipigana katika vita vya Siffin katika upande wa Ali. Tarehe 10 ya Muharram alipigana na maadui wa Husein na akapata shahada (akauawa kishahidi).

Rafi bin Abdallah alikuwa mtumwa wa Muslim ibn Qasir, yuke aliyekuwa mlemavu. Baada ya kufika Karbala na bwana wake, alipigana kwa ajili ya Husein na aliipata shahada siku ya tarehe 10
ya Muharram.

Bishr bin Amr al-Hadrami al-Kindi kwa asili alitokea Hadhramaut, lakini aliifanya Kufa kuwa maskani yake. Mmoja wa watoto wake alikamatwa ndani ya mipaka ya Rayy, lakini alimpeleka mmoja wa watoto wake wengine kupanga namna ya kuachiliwa ndugu yake, akipendelea kukaa katika kundi la Husein ambalo alijiunga nalo wakati majadiliano ya kupatikana amani yalipokuwa yakifanywa hapo Karbala. Mwishowe aliji- toa mhanga maisha yake kwa ajili ya Husein tarehe 10 ya Muharam.

Suwayd bin Abi al-Mataa‘ al-Khath’ami alikuwa amesonga mbele katika umri, aliyetawaliwa na Sala, na kujinyima, ambaye ametenda matendo ya kuonekana wazi katika vita vingi. Baada ya kupigana na adui, alianguka chini akiwa amejeruhiwa sana kiasi kwamba walimkatia tamaa.

Hata hivyo, alikuwa na uhai kiasi aliobakia nao, na aliposikia kwamba Husein ameuawa kishahidi, alijinyanyua kwa mhemuko usiozuilika, na akaanza kuwashambulia maadui walio karibu yake kwa kisu kikubwa ambacho bado alikuwa amebaki nacho. Kisha alishambuliwa na maadui na kuuawa.

Walikuwa ni nani watu hawa wote ambao waliungana kumsaidia Husein mbele ya matatizo mengi yasiyoelezeka na uhakika wa kufikwa na mauti?
Jambo moja linajitoeza dhahiri, nalo ni, kwamba wengi wa watu hawa walikuwa hawaeleweki vizuri au walikuwa watu wasiokuwa maarufu. Nane kati yao walikuwa Masahaba wa Mtume, nao walikuwa ni:

• Muslim bin Awsajah,

• Zahir bin Amr al-Aslami al-Kindi,

• Shabib bin Abdallah,

• Abd al-Rahman bin Abd Rabb bin al-Ansar,

• Ammar bin Abi Salama al-Dulani

• Muslim bin Qasir al-Sadafi,

• Habib bin Muzahir,

• Anas bin al-Harith al-Asadi.

Vita vya Karbala vilitokea miaka hamsini baada ya kifo cha Mtume, na wale katika Masahaba zake ambao walikuwa hai katika mwaka wa 61 A.H. lazima watakuwa wamepita zaidi ya miaka 50 ya umri wakati wa vita vya Karbala. Baadhi yao lazima watakuwa wamezeeka zaidi ya hapo, kama vile, 1. Muslim bin Awsaja, 2. Abd al-Rahman bin Abd Rabb bin al-Ansari, 3. Habib bin Muzahir, 4. Anas bin al-Harith na 5. Suwayd bin Amr al- Khath’ami. Watu wa kundi la umri huu hawakubali wenyewe kujiingiza katika vita kwa msingi tu wa mihemko ya ghafla na hisia kali za muda.

Miongoni mwa wale ambao walijitoa mhanga mkubwa kwa ajili ya Husein, wafuatao walikuwa sahaba wa Ali, na kwa hiyo, wanawekwa kicheo kwa hadhi ya kuwa tu chini kuliko sahaba wa Mtume:

• Abdallah bin Umar al-Kalbi,

• Mujammi bin Abdallah al-Muzhiji

• Janada bin al-Harith al Salmaani

• Jundab bin Hujr al-Kindi

• Umayyah bin Sa’d al-Ta’i

• Al-Harith bin Bahban

• Shabib bin Abdallah al-Nahshadi

• Na’im bin Aljan al-Ansaari

• Hulas bin Umar al-Azdi

• Al-Nu’man bin Umar Azd

• Qasit bin Zuhayr al-Taghlabi

• Jabala bin Ali al-Shaybani

• Karduus bin Zuhayr al-Taghlabi

• Miqsat bin Zuhayr al-Taghlabi

• Abu Thumaama al-Sa’idi

• Shazib bin Abdallah

• Jawn, mtumwa wa Abu Dharr al-Ghiffari,

• Hajjaj bin Masruq

• Sa’d bin al-Harith

Amr bin Jundab al-Hadrami, na Yazid bin Mughfil al-Ju’fi. Wengi katika wao walipigana katika upande wa Ali katika vita vya Ngamia, vya Siffin na vya Nahrawan, na baadhi yao walikuwa wafuasi wake.

Kwa mashahidi, ni wachache sana katika wao walioihifadhi Qur’an kwa moyo. Walikuwa:
1) Burayr bin Hudayr al-Hamdaani, (2) Abd al-Rahman bin Abd Rabb al- Ansaari. (3) Nafi’ bin Hilaal al-Jamali (4) Hanzala bin Asad al-Shaybani, (5) Kinaana bin Atiq al-Taghlabi, na mtumwa mmoja wa Kituruki.

Wafuatao miongoni mwa mashahidi walikuwa ni watu wasomi na vyanzo vya hadithi nao ni:

• Muslim bin Awsaja,

• Habsha bin Qays al-Nahmi

• Zahir bin Amr al-Aslami

• Suwar bin Abi Umayr al-Nahmi,

• Abd al-Rahman bin Abd Rabb al-Ansaari,

• Habib bin Muzahir,

• Nafi bin Hilal al-Jamali

• Shuwayb bin Abdallah na Anas bin al-Harith.

Wapiganaji hodari na wale wanaotambulika kwa vipaji na mafanikio yao ya kivita pia waliwakilishwa miongoni mwa sahaba za Husein ambao kwamba shahada zao tayari tumekwishaziandika. Hawa walikuwa ni:

• Al-Hurr ibn Yazid al-Riyahi,

• Muslim bin Awsaja,

• Al-Harith bin Imru al-Qays al-Kindi;

• Abd al-Rahman bin Abdallah bin Kadan al- Arhabi,

• Mas’ud bin Hajjaj al-Taymi,

• Sa’id bin Abdallah al-Hanafi,

• Zuhayr bin al-Qayn al-Bajali,

• Aabis bin Abi Shabib al-Shakri,

• Ziyad bin Arib al-Hamdan, na

• Suwayd bin Amr bin Abi al-Mataa’ al- Khath’ami.

Wengi wa wale ambao majina yao hutokea katika makundi mbalimbali katika ibara zilizopita walikuwa wanafahamika sana kwa usimamishaji wa Sala, kujihini kwao, uchamungu wao na watu hawa walikuwa ni heshima kwa nyakati zao na njia zao mbalimbali. Maisha yao yalikuwa mifano ya kuigwa katika hali zao zote na waloitoa mifano ya maisha ya maadili na tabia za Kiislamu. Ilikuwa ni kutokana na hawa kuliko watu wa kawaida waendeshayo watu kwamba Husein alipenda kuungwa mkono na kusaidi- wa katika vita yake na Yazid.

Husein angeweza kuchagua watu bora wachamungu, waswalihina, wenye kujihini wa wakati wake kuwa masahaba zake, kuwa na watu wachache, waliosogea mbele sana katika umri, walio tayari kuyatoa maisha yao, ili kwamba kule kutokea kwao tu katika uwanja wa vita peke yake kungefungua macho ya Waislamu na kuwalazimisha kuitafakari hali mbaya ambamo Uislam ulikuwa umetumbukia ndani yake.

Historia imeandika hadithi fupi fupi kuhusu vitendo vya jeshi la Umar bin Sa’d wakati baadhi ya masahaba wa Husein walipokuja kuhuzunika. Vitendo hivi ni vyenye kutoa heshima sana, na viliandikwa na wale ambao wasingeweza kuwa na uhodari wa kumsifu Husein na sahaba zake.

Wala wasingeweza kupenda kusaidia katika kuandika hadithi zote kama hizo. Heshima kubwa ambazo kwazo baadhi ya masahaba wa Husein walikuwa wamezipata kwa watu kwa ujumla inafananishwa na heshima kama aliyopewa Muslim bin Awsaja na kamanda (kiongozi) wa jeshi la Umar bin Sa’d, Shabath bin Ribii, wakati alipowaona watu wa jeshi lake wakifurahia kifo cha yule sahaba wa Husein alisema;

“Inasikitisha kiasi gani! Mtu kama Muslim bin Awsaja amekufa na nyinyi mnajihusisha katika kuonyesha furaha! Mimi mwenyewe binafsi nimeona matendo makubwa na ya ajabu ambayo ameyatenda kwa sababu ya Uislamu.”

Kama Husein angekwenda Karbala na watu wa familia yake tu pekee, ingeweza kusemwa, kama kwa hakika ilivyo hata sasa hivi baadhi ya watu wanajaribu kuhoji kwamba vita hivyo vilikuwa ni ugomvi mkubwa wa tangu miaka mingi kati ya matawi mawili ya familia moja - ukoo wa Bani Hashim na ukoo wa Bani Umayyah - ambao walidumu katika vita wenyewe kwa wenyewe. Lakini Husein alikuwa pamoja naye, watu maarufu na mashuhuri waliopatikana karibu kutoka kabila zote na sehemu zote za Bara Arabu na kitu chenye kuwaunganisha kati yao si kingine ila ile heshima ya zile kanuni na kuwepo kwa lengo maalum - ambalo ni - utekelezaji na kutimiza wajibu wa kidini.
Umuhimu wa mikataba hii (viunganisho) ambayo iliunganisha wafuasi wake hapo Karbala, kwa Husein ulikuwa ni msisitizo mkali wa ukweli kwamba Husein alimsihi sana kila mtu katika wafuasi wake katika nyakati mbali mbali, na hata baada ya kuingia giza la usiku wa mwezi 9 Muharram, kuondoka na kumwacha pekee akabiliane na adui. Ilikuwa ni sehemu ya mbinu na mpango wa Husein kuwafanya watu wafikiri wao wenyewe, kuchukua maamuzi kwa mujibu wa sauti ya dhamira zao wenyewe, ziziso shawishika kabisa kwa hali za kutoka nje na kuchukua wajibu kamili kwa vitendo vyao.

Siku ya tarehe 10 Muharram, ilikuwa siyo kwamba Husein aliwaleta wafuasi wake wengi ili kuweza kulifikia lengo lake, bali tu ni kwamba kila mmoja wa wafuasi wake, kwa hiari yake mwenyewe, alijitoa mhanga maisha yake kwa malengo ambayo Husein alikuwa nayo katika fikra.

Kichocheo cha matendo yao, kwa mtu mmoja mmoja au kwa pamoja, kilitolewa au kilipatikana kwa sauti ya dhamira ya kila mmoja katika wao, na hii ndiyo ilikuwa sababu kubwa kwa uthabiti wao na makusudio yao.

 • 1. Tabari, cha II, uk. 335
 • 2. Tabari, cha II, uk. 335-337.
 • 3. Tabari, cha II, uk. 342.
 • 4. Tabari, cha II, uk. 343.
 • 5. Tabari, cha II, uk. 344.
 • 6. Tabari, cha II, uk. 346.
 • 7. Tabari, cha II, uk. 338-339.
 • 8. Tabari, cha II, uk. 356
 • 9. Tabari, cha II, uk. 307.
 • 10. Tabari, cha II, uk. 355-356.
 • 11. Tabari, cha II, uk. 345.
 • 12. Tabari, cha II, uk. 235-236.