Table of Contents

Sura Ya 29 : Jihad Ya Mwisho Na Kifo Cha Kishahidi Cha Husein.

Baada ya kifo cha Ali al-Asghar ni dhahiri kwamba jambo moja pekee lililobakia kwa Husein kufanya lilikuwa ni kufa. Lengo hili lingeweza kutekelezwa kwa urahisi kwa kuweka upinzani hafifu kwa maadui na kukiruhusu kichwa chake kikatwe kutoka mwilini mwake kufuatia mapigano madogo tu. Majibu yake ya kisilika juu ya hali yake lazima iwe kwamba yalikuwa tofauti sana. Vipi angeweza kuwa ameyasahau mafanikio ya kishujaa ya Hamza, Ja’far na Ali na ujasiri usio kifani ambao uliweka chapa katika vita vya Badr, Uhud, Khandaq na Siffin.

Husein alikwenda hemani kwake kupata pumziko lake la mwisho kabla ya kwenda kupigana, na akachana shuka iliyotengenezwa Yemen, sehemu nyingi mbalimbali juu yake, na akaivaa chini ya nguo zake nyingine zote, inawezekana akitegemea kwamba nguo hii iliyorarukararuka, ingeweza kuachwa mwilini mwake baada ya kuuawa kwake, mwili wake utakapokuwa umeporwa nguo nyingine zote.1

Akiwa mwenye huzuni, amevunjika moyo, na mwenye kiu isiyovumilika kama alivyokuwa wakati alipowakabili maadui akiwa peke yake kabisa, upanga mkononi, Husein alitia hisia za woga hivyo katika nyoyo za maadui wake kiasi kwamba hakukua na hata adui mmoja aliyekuwa na ujasiri wa kumkabili. Akigundua kuvunjika moyo huku kwa maadui, Shimr alijaribu kuwatia moyo.

Akizipanga upya safu za maaskari aliliweka jeshi la watembeao kwa miguu mbele ya jeshi la wapanda farasi na akawaamuru wapiga pinde wamimine mishale kwa Husein. Hivyo kwa wingi sana mishale ilitupwa kwake, kiasi kwamba mwili wa Husein ulifanana na mwili wa mnyama aitwaye nungunungu!2

Kisha Shimr alitoa amri kwa sauti kubwa kwa askari wake kumuua Husein. Jeshi lenye askari wengi sana la Umar bin Sa’d lilifanya tena mashambulizi juu ya al Husein kutoka pande zote, na panga zao, mikuki na mishale ilitumika kwa uhuru kabisa dhidi yake. Farasi wake lazima alikuwa amejeruhiwa mno kiasi kwamba Husein alishuka chini.

Hata ingawa alikuwa chini, aliendelea kushambulia maadui zake, na mara alipolifanya jeshi lote kukimbia alikwenda mtoni. Akitambua kwamba Husein angekunywa kiasi fulani cha maji kukata kiu yake, Husein bin Tamim alimtupia mshale ambao uliupiga mdomo wa Husein bin Ali ambamo humo damu nyingi ilimtoka. Husein alichukua damu iliyojaa kiganya chake na akairusha juu angani, na kumshukuru Mwenyezi Mungu.3

Wakati huohuo Shimr alisogea mbele na kikosi kimoja cha jeshi kwenda kwenye mahema ya wanawake wa kundi la Husein ili wakawapore na kuwanyang’anya vitu vyao. Husein aliwaonya, akiwataka kuzingatia kwa kiasi fulani kanuni za ungwana na wasifanye makosa dhidi ya wanawake wa nyumba yake. Shimr alirudi nyuma, akijionea haya kwa yale ambayo ameyafanya.4

Kisha Shimr alimzunguuka Husein, akiwa na askari wake wa miguu ambao walisukumwa nyuma na kufukuzwa kila wakati Husein alipopambana nao. Askari mmoja wa jeshi la adui alizungumzia kumhusu Husein akisema, “Sijamwona mtu yeyote yule ambaye alikuwa amejeruhiwa, ambaye kizazi chake, jamaa zake na wapenzi wake wote wakiwa wameuawa kwa panga, lakini bado yeye akatokea kuwa imara na aliyetulia na ambaye akashambulia maadui zake kwa ushujaa wa waziwazi kabisa kama Husein.

Watu wa kikosi cha askari wa miguu walimzunguuka Husein kutoka pansde zote, lakini kila alipowashambulia kwa upanga wake, walikuwa wanakimbia kwenda upande wa kulia na kushoto kama kondoo wafanyavyo wanapotimuliwa na mbwa mwitu anayeshambulia.”5

Wakati huohuo Husein alikuwa akirudiarudia maneno ambayo yalilengwa kutoa mwongozo kwa maadui na pia kuonyesha alama za matokeo ya vita. Kisha Husein alishambuliwa kwa nguvu sana na kwa kurudiwarudiwa. Alianguka chini, akiwa na majeraha mengi sana na akashindwa kusimama kutokana na udhaifu.

Mtoto wa Hasan, mdogo kuliko ndugu yake, al-Qasim, aliyeitwa Abdallah bin Hasan, akimwona ami yake Husein, anasujudu juu ardhini, alikwenda akimkimbilia wakati Bahr bin Ka’b bin Ubaydullah al-Taymi alikuwa anakwenda kumshambulia Husein kwa upanga. Abdallah alimlaumu, lakini Bahr alimkata mmoja wa mikono yake kwa upanga wake, na Harmala aliachia mshale kuelekea kwake, ukamchoma na ukamuua.

Husein alibakia bado anasujudu juu ya ardhi, akiwa ameumizwa sana na kuchoka, kwa kipindi kirefu kidogo kwa sababu kila mtu alikuwa anajaribu kukwepa kushiriki katika kosa hili kubwa na baya sana na ovu la kumuua (Husein).

Hatimaye Shimr akawakemea watu wake akisema; “Sasa mnangojea nini nyinyi?” Kwa swali hili al-Malik bin Nasr al-Baddi alisogea mbele, na akampiga Husein kwenye kichwa kwa upanga ambao ulichoma ngozi yake ya kichwa,6 na mwishowe upanga wa Zuraa bin Sharik,7 mkuki wa Sinan bin Anas,8 na sime (hanjari) ya Shimr viliyamalizia maisha ya mtu yule aliyekuwa mfano mzuri wa uadilifu. Hapo kichwa cha shahidi wa haki, cha shahidi katika njia ya Allah, kilinyanyuliwa juu kwenye ncha ya mkuki.

Ilikuwa ni siku ya Ijumaa, mwezi 10 Muharram mwaka wa 61 A.H. ambapo tukio hili la kuhuzunisha lilipofanyika.

  • 1. Tabari juz. 6 uk. 240.
  • 2. Al-Irshad, juz. 6, uk. 257.
  • 3. Tabari juz. 6 uk. 250
  • 4. Tabari juz. 6 uk. 253.
  • 5. Al-Irshad, uk. 257/ Al-Akhbar al-tawal, uk. 255
  • 6. Tabari juz. 6 uk. 257; Al-Irshad al-Tawal, uk. 255.
  • 7. Al-Akhbar al-Tawal, uk. 255.
  • 8. Tabari juz. 6 uk. 260; Al-Akhbar al-Tawal uk.256.