Table of Contents

Sura Ya 3: Uislamu Na Ujumbe Wake

Kipindi cha kabla ya Uislamu cha historia ya Uarabuni kinaitwa “kipindi cha zama za ujahilia” au “zama za giza”. Isije ikamaanisha kwamba Waarabu walikuwa hawazitambui sanaa na njia za maisha ya kijamii. Karne nyingi kabla ya kudhihiri Uislamu, Arabuni ya Kusini iliendeleza ustaarabu uliostawi na ilijishughulisha na biashara zenye kustawi.

Tungo zao za kishairi zikiwa na baadhi ya vielelezo bora kabisa vya fasihi ya Kiarabu, zinaonyesha kwamba Waarabu walikuwa wana viwango vya hali ya juu kabisa vya ujasiri, ukarimu, ukaribishaji, uaminifu, upendo wa kindugu na upendo wa ndoa. Wakati ambapo walikuwa wanashughulika zaidi na ibada ya sanamu, hawakuwa kwamba hawatambui kabisa kuwepo kwa Mungu Mmoja.

Walikusanyika kila mwaka mjini Makka kwa ajili ya kutekeleza Hijja, lakini walikuwa hawajui kabisa umuhimu halisi wa mikusanyiko hii. Dini nyingine zilizofuatwa katika nchi hiyo zilikuwa Uyahudi wa kuabudu moto na Ukristo. Waarabu walifanya misafara ya biashara kwenda Hijaz, Iraq na Syria. Hata hivyo hali ya jumla ya matatizo na ufukara ndani ya jangwa iliwafanya wawe mabahili, na wakajiingiza katika vita vya kulipiza kisasi, mara nyingi vikienea na kuendelea kwa miaka mingi. Dhana zilizoeleweka vibaya (visivyo) za kujistahi mara nyingi ziliwasababishia kuwauwa watoto wa kike walio wachanga.

Wazo la usawa wa binaadamu lilipuuzwa kabisa katika jamii ambamo ndani yake mlikuwa na ushindani binafsi, wivu wa kivikundi na chuki ya kikabila.

Ilikuwa ni katika mazingira haya kwamba Muhammad bin Abdallah aliyechaguliwa na Mwenyezi Mungu alitokea kueneza ujumbe wa Uislamu. Alikabiliana na kazi ya sulubu. Ingekuwa ni rahisi zaidi kwake kuwarudisha washenzi, watu wasiostaarabika, wanaoishi katika hali ya asili kuliko kuirudisha tena kwenye mwenendo mzuri ule utaratibu wa jamii wenye maradhi.

Ilibidi afundishe uvumilivu, unyenyekevu na msamaha kwa wale ambao kwao sifa hizi zilionekana kuwa dalili za unyonge. Ilibidi afundishe usawa wa binadamu na udugu kwa wale ambao walijivunia nasaba zao. Uislamu pia, umeharamisha matumizi ya pombe (ulevi) matendo ya uchezaji kamari na michezo ya bahati nasibu na kutoa au kupokea riba - yote haya yakiwa maarufu sana miongoni mwa waarabu. Pia ulichukia sana matendo mengine yote maovu.

Uislamu ulileta ujumbe wa uhuru kwa kila mtu kutoka kwenye pingu za ukasisi, kutoka kwenye udhalimu wa wenye ukwasi (utajiri) ambao waliyatumia vibaya matunda yaliyotokana na kazi ngumu za wengine, na kutokana na ukatili wa mabwana kwa wafungwa wao. Pia Uislamu ulitoa faraja kwa wanawake ambao walikuwa wamenyimwa hata zile haki za kibinadamu za kimsingi. Uislamu ulifundisha uhuru, undugu na usawa na kwa mara ya kwanza katika historia ya mwanadamu ulitoa kwa watu wote haki kamili za kiraia na kibinaadamu, ukiamsha matumaini mapya katika nyoyo za waliodhulumiwa na mafukara.

Uislamu ulibashiri kutokuwezekana kupata usawa wa nje wakati watu wakiwa wamejigawa katika makabila mbalimbali na mataifa.

Lengo la Uislamu, kwa hiyo, lingeweza kupatikana kwa mapinduzi ya kisomi, na ulijaribu kuvuta uzingativu wa watu kwenye mamlaka mamoja pekee, kuutengeneza mwishilizio wake bila ya kuingiliwa na vitu vya kimaada.

Njia pekee ya kupata kukubalika kwa jumla kwa ajili ya usawa wa watu wote na undugu ni kuanzisha uhusiano wa moja kwa moja kati ya wingi wa vikundi na umoja mkuu. Kwani ina maana kwamba sehemu za huo wingi zingekuwa baadae zinalingana.

Lakini umoja mkuu ambao wanaadamu wote lazima wauelekee inabidi kwa lazima uwe si wa kimaada kwani vile vyote ambavyo ni vya kimaada vitakuwa ni vyenye kutegemea mipaka mbalimbali kama ile ya umbali, nafasi na idadi. Kwa hiyo, ilikuwa jambo lenye umuhimu sana kwamba mawazo ya mwanadamu yangelenga kwenye ule uwezo usiokuwa wa kimaada, uliozidi ule wa mwanadamu, ambao, kwa kutofungwa na ile mipaka ya nafasi, vipimo na viwango, ungebeba uhusiano kwa kila mtu, na ambao kila mtu alihusika nao. Uwezo huu ni yule Mungu mmoja aliyedhihirishwa na Uislamu kwa kufanyiwa ibada na watu wote, Muumba wa vitu vyote.

Kutambua kwamba wanadamu wote ni viumbe vya Mwenyezi Mungu kumefanya ujenzi wa hali ya usawa na undugu miongoni mwa watu kuwa mwepesi vya kutosha. Baadhi ya dini zimemfanya Mungu kuwa ni wao pekee, na wafuasi wao wanadai kuwa ni watoto Wake. Uislamu umekanusha madai kama haya na kuwafundisha Waislamu kutamka kwamba: “Yeye (Allah) ni mlinzi wetu na mlinzi wenu.” Wakati uki- wafanya wanadamu wote kuwa ni sawa, ulifanya uwezo na ubora kuwa ni sifa ambazo zinaamriwa pekee na tabia za mtu mwenyewe.

Utekelezaji tu wa wajibu wa mtu kama mwanadamu ndio ulivutia ubora wa hali ya juu kabisa. Hivyo tabia za asili zilikataliwa katika kuyachukua mamlaka kwa nguvu za idadi ya watu uongozi na mambo mengine kama hayo. Ubora wa tabia na usafi wa maadili vilisisitizwa sana. Mtume aliutangaza ujumbe wake kwenye kuwaendeleza wanaadamu na ukamilifu wa tabia njema.

Mwislam ameelezewa kuwa ni yule mtu ambaye amejisalimisha kabisa kwa Mwenyezi Mungu. Usawa kwa wote, kimaumbile na kiasili ulitangazwa katika Aya ya Qur’ani, “Amekuumbeni kutokana na nafsi moja.”1 Waarabu waliambiwa kwamba nafasi ya kipaumbele haitokani na utaifa; Mquraishi kwa asili hakuwa mbora juu ya asiyekuwa Mquraishi. Matendo yalifuata maagizo mwongozo na maadili ya Mtume. Alimteua Bilal, mtumwa wa Kihabeshi, kuwa mwadhini wake, na wakati mtu mmoja alipolizungumzia jambo hili kwa dharau, Aya ya Qur’ani iliteremshwa ikisema, “Enyi watu kwa hakika sisi tumekuumbeni (nyote) kutokana na mwanamume na mwanamke,”2 hivyo kwamba wanadamu wote ni sawa.

Uislamu kwa kweli kabisa unataka kusimamisha serikali ya Mungu. Serikali ya Mungu inasimama moja kwa moja katika uadilifu na usawa. Qur’ani inawaelekeza Waislam, “...Na mnapohukumu baina ya watu, hukumuni kwa uadilifu,”3 na tena inasema Wala kuchukiana na watu kusikufanyeni kutotenda uadilifu. Fanyeni uadilifu. Hivyo ndio kuwa karibu mno na uchamungu. Na mcheni Mwenyezi Mungu.”4. Kwa sababu hiyo Mtume alitangaza, “Hakuna mtu aliye mbora juu ya mwingine isipokuwa tu kwa sababu ya imani yake na ucha-Mungu.” Hata hivyo ingawa alikuwa hodari kuendesha mamlaka yasiyofungwa juu ya wafuasi wake, Mtume kamwe hakujiita yeye mwenye, au kufikiria kwamba yeye alikuwa mfalme.

  • 1. Qur’an; 4:1
  • 2. Qur’an; 49:13
  • 3. Qur’an; 4:58
  • 4. Qur’an; 5:9