Table of Contents

Sura Ya 31: Mazingatio Ya Kina Juu Ya Umateka Wa Wanawake Wa Familia Ya Husein

Lengo la Yazid halikuwa ni kumuua Husein tu kwa kisingizio cha kukataa kwa Husein kutoa kiapo cha utii kwake, bali pia na kuangamiza kitovu (kituo kikuu) cha kiroho ambacho kwa kuwa mlezi wa mafundisho ya Uislamu, hakiweza kushirikiana na yeyote yule katika zoezi la kuendesha utawala usio halali, Mfululizo wa matukio yote ambayo yalianza na uonyeshaji wa ukaaji wa Husein mjini Madina kuwa ni chanzo cha hatari kwa maisha yake, safari yake kutoka Makkah chini ya mazingira yenye kufanana na hayo, na yale mauaji makubwa ya Karbala na matokeo ya kufungwa na kutembezwa kwa wanawake wa familia ya Husein kutoka sehemu moja kwenda nyingine, katika hali ya umateka, yote haya yali- chochewa bila namna yoyote ile ya shaka, na maelekezo ya Yazid.

Kama Ubaydullah bin Ziyad asingewapeleka wanawake hao Damascus katika hali ya umateka kwa agizo la Yazid, na kama Yazid hakuwa amenuia kweli kuwadhalilisha, basi wangepelekwa moja kwa moja Madina.

Badala ya kuwapokea kwa busara na mema, Yazid aliamuru waletwe kwake kwenye ukumbi wa mikutano mbele ya wajumbe wake wa baraza na akaonyesha dhihaka juu ya kichwa cha Husein mbele yao wote. Ilikuwa tu baada ya muda mrefu kupita ambapo Yazid akatoa nyumba kwa ajili ya makazi ya wanawake hao wa familia ya Husein. Wanawake wa baadhi ya familia zilizochaguliwa za mjini Damascus baadaye waliwatembelea wanawake wa familia ya Husein ili kutoa rambirambi zao kwa vifo vya mashahidi hao.
Husein alikuwa ameshauriwa asiwachukue wanawake na watoto pamoja naye wakati alipoanza safari yake kutoka Makkah kwenda Kufa. Hata hivyo, alishikilia uamuzi wake huo, wakati mwingine akisema kwamba huu ulikuwa ni uamuzi wa Mwenyezi Mungu kwamba wapaswe kufanywa wafungwa, au pengine angesema kwamba lolote lile ambalo limeamuliwa na Mwenyezi Mungu kuwa, lazima lije kutokea.

Msimamo huo huonyesha kwamba akizijua vyema kabisa hatari zote hizi na vipingamizi vyote ambavyo viliandamana na kuweko kwa wanawake hawa pamoja naye katika safari yake, Husein alichagua kuwachukua pamoja naye. Je, yalikuwa ni mawazo ya Husein kwamba kuwepo kwa wanawake pamoja naye katika safari hiyo kungesaidia jambo moja muhimu katika kulifikia lengo lake?

Husein kamwe hakukusudia kupigana kwa kutumia rasilimali za kimaada (silaha na vitu vinginevyo) ili kupata maslahi ya kidunia. Alikataa kutoa kiapo cha utii kwa Yazid ili kuisalimisha haki na uadillifu. Yeye aliamua kushikilia msimamo wa kukataa kwake mpaka pumzi ya mwisho ya uhai wake, ili kwamba haki iweze kuwepoiliyo wazi kabisa na isiyofichika kwa watu kuweza kuiona - na pia ili kwamba mtu yeyote asije akapotezwa kabisa katika kushikilia kwamba kitendo na mwenendo wa tabia ya Yazid vilibeba ridhaa ya Uislamu au vilihusiana kwa namna yoyote ile na Uislamu. Ilikuwa ni katika umuhimu wa juu sana kwa kulitimiza lengo lake kwamba maadui zake wapaswe kuona ni vigumu kutafsiri chochote kati ya vitendo vyake.

Lengo hili lilifaulu kwa mafanikio makubwa sana kwa kuwepo wanawake wa nyumba yake pamoja naye pale Karbala, na kuwa na haki kwake, na uonevu mwingi na makosa mengi yasiyo na idadi ambayo aliyavumilia yaling’ara kwa mwanga mng’avu sana kiasi kwamba hakuna kiwango chochote cha upotoshaji kingeweza kuleta dalili japo kidogo za shaka au wasiwasi juu ya hayo.

Utawala wa Bani Umayyah ulitumia dhidi ya Bani Hashim mkakati mujarabu wenye sanaa ya kumfanya Uthman bin Affan kama Khalifa aliyedhulimiwa na kuuwawa, wakiwashikilia Bani Hashim kwa ujumla, na hususan Ali, kuhusika na mauaji yake.

Ili kuongeza hoja na nguvu kwenye propaganda hii, shati la Uthman lililotapakaa damu na vidole vya mke wake Naila vilivyokatwa, vyote vilionyeshwa kwa watu kwenye mikutano iliyofanywa mara kwa mara kuomboleza mauaji ya Uthman ndani ya msikiti mkuu mjini Damascus. Umati mkubwa wa watu walishughulishwa katika kulia na kupiga vichwa vyao na vifua katika kuomboleza juu ya Khalifa huyo aliyefariki.

Watu wa Bani Umayyah walifanikiwa kupata kuonewa huruma kwa kujifanya kama wao ndiyo warithi wa Uthman na wakadai kulipiza kisasi kwa damu yake. Matokeo mabaya ya propaganda hii ya uwongo yasingeweza kusitishwa isipokuwa mpaka dhuria ya Mtume ipatwe na msiba kama huo mikononi mwa warithi wa Abu Sufyani.

Kwa kumuua Husein, adui bila ya kujua walifanikisha kuleta mapinduzi katika nyoyo za watu na kusababisha mabadiliko ya hisia za watu katika kuunga mkono familia ya Mtume. Wakiwa wamelewa ushindi, Bani Umayyah walizorota kuufahamu mgeuko huu kamili na usiotazamiwa wa hisia za umma. Mpaka mwezi 10 ya Muharram walikuwa wakirejelea kwenye kumbukumbu ya mauaji ya Uthman katika kuhalalisha matendo yao. Kuzuiwa kwa ugavi wa maji kwa Husein na sahaba zake kulichukuli- wa na wao kama ni kulipiza kisasi kwa kukataliwa ugavi wa maji kwa Uthman, ingawa hakukuwa na Bani Hashim yeyote aliyehusika chochote na jambo hilo.

Maovu yaliyokithiri yaliyofanywa hapo Karbala, kuanzia na kuuawa bila huruma masahaba na ndugu wa Husein, pamoja na mtoto wake mchanga, na mauaji yake mwenyewe, kukanyagwa kanyagwa maiti yake chini ya kwato za farasi, kuporwa na kuchomwa moto mahema yaliyokuwa yakikaliwa na wanawake wa familia ya Husein, kunyanyuliwa juu kwa kichwa kilichokatwa cha Husein kwenye mkuki na taabu nyingi zisizoelezeka na ufidhuli, ambayo yote haya watu wa Husein waliosalia katika vita waliyapata, yalikuwa kwa namna ya ukatili wa kuchukiza sana kiasi kwamba marafiki wa Bani Umayyah walinyamazishwa kabisa na wakaepuka kuongea masaibu ya Uthman katika mazingira ya matukio ya Karbala na matokeo yake yaliyofuatia mara tu baada ya hapo.
Inashangaza kuona kwamba wakati shati la Uthman lililotapakaa damu na vidole vya mke wake Naila vilionyeshwa kwa watu ambao walitokana na kundi la Khalifa aliyekufa (Uthman), na walikuwa hawana ushahidi wa kuwatambulisha wale ambao walilitenda jinai hiyo, vichwa vilivyokatwa vya mashahidi wa Karbala vikiwa vimenyanyuliwa juu kwenye mikuki, na mateka wa familia ya Husein, wakiandamana pamoja na kichwa cha Husein mwenyewe, waliongozwa huku na huko na wauaji hao wenyewe, wakifanya uchunguzi wowote wa kuchukua muda kwa ajili ya kuwahakiki wahalifu wenyewe, au kuwatambua, kuwa hauna umuhimu kabisa. Matokeo yalikuwa kwamba hata huruma za wale ambao, kwa sababu ya upendeleo wao kwa Uthman, waliwapendelea Bani Umayyah, walitengwa nazo na zikahamishwa kwa Bani Hashim.

Kama Husein asingewachukua wanawake wa familia yake pamoja naye, ingeweza kuwa ni vigumu kwamba msiba wa Karbala uweze kutangazika kwa mapana sana na kwa athari kubwa katika kipindi kifupi sana kama hicho, na upotofu wa Bani Umayyah ukadhihirika kwa nguvu na kwa haraka sana kwa watu.

Ni muhimu sana kwamba haki ilikuja kufahamika na kutambulika kwa mfano huu, kwani masula sio machache katika nchi za Kiislamu, kama kwa hakika ilivyo katika sehemu nyingine pia, ambamo humo mwanga wa haki kuhusu kadhia za namna hii huwa umezimwa, na hakuna mtu yeyote ambaye amefanikiwa katika kuufikia ukweli kupitia utusitusi uliotanda. Hasan bin Ali alitiliwa sumu na hata sasa hivi utambu- lisho wa mtu yule ambaye anahusika kimsingi kwa kutenda jinai hiyo bado limewekwa kuwa ni lenye kutiliwa mashaka.

Kama watu 72 au 125, idadi iliyokisiwa ya wale ambao walijitolea mhanga maisha yao kwa ajili ya al-Husein na misingi yake, waliuawa hapo Karbala, wakizungukwa na pazia za silaha za makundi ya Yazid, wakiwa wametengwa kabisa na dunia yote iliyobakia, kiasi kwamba, bila kutaja uwezekano wa kuwafikiwa na mwanadamu, hata kuwapelekea habari lilifanywa kuwa jambo lisilowezekana, ingekuwa ni rahisi sana kwa Yazid na vibaraka wake kutoa upindishaji wowote ule kwenye maelezo ya tukio hili, kama ikibidi lazima kutoa maelezo yoyote yale.

Kwani wangekuwa ni hao wauaji tu ndiyo wangekuwa mashahidi wa tukio hilo na wangeweza kulipa mapambo ya rangi yoyote ambayo ingewafaa kwa lengo lao.

Ni nani wangekuwa pale kama mashahidi wa matukio yote kuweza kuukanusha moja kwa moja ule uwongo ambao ungetolewa na maadui wa Husein? Wangeweza vizuri kabisa kuelezea tabia ya Husein katika namna tofauti kabisa.

Kwa mfano, angeweza kushutumiwa na ukaidi wa wazi wa kuidharau mamlaka iliyokuwa madarakani. Au wasiwasi pia ungeweza kuletwa juu ya nia na mwenendo wa Husein, mbali na mihanga yake yote hiyo mikubwa na isiyo na kifani iliyochukuliwa kuongoza katika mwamko wa wema na uadilifu. Katika kurasa za historia, Yazid angeweza kuibuka kama mtetezi wa Uislamu, na Husein angekuwa kama mwasi na mueneza fitina.

Hakuna mbadala kwa ajili ya wale wanawake wasio na marafiki na walio watoharifu wa familia yake, walioongozwa na kupelekwa toka mji mmoja kwenda mji mwingine kama wafungwa, nyoyo zao zikiwaka moto kwa huzuni na hisia kali, damu ya Ali na Fatimah ikitiririka ndani ya mishipa yao, ndimi zao zikitoa matamshi kwenye khutuba zenye kugusa sana, zikikumbusha ufasaha wa lugha wa Mtume na ya Ali, ungeweza kupatikana kwa Husein kwa ajili ya uenezaji baada yake wa falsafa ya Shahada (mihanga) na uenezaji wa uadilifu na haki.