Table of Contents

Sura Ya 35:Wenye Hatia Wajisikia Aibu.

Majeshi yaliyokuwa chini ya mamlaka ya Husein yalikuwa yamezidiwa sana kwa idadi na yale ya Yazid hapo Karbala kiasi kwamba, ingeweza kutabiriwa kwa urahisi kwamba licha ya upinzani mkali sana uliotegemewa kuwekwa, majeshi ya Yazid mwishoni lazima yashinde. Ama kuhusu Husein, alikuwa hana shaka kwamba vita vingeishia kwa maafa upande wake.

Hata hivyo, yeye alishikamana na njia aliokwisha jichagulia mwenyewe, na siyo yeye wala mtu yeyote kati ya wale ambao walikufa pamoja naye wala mtu yeyote kati ya wale walionusurika vitani ambaye alijutia kabisa kile alichokitenda au matokeo yake. Kinyume chake, siyo tu maadui zake na wauaji wake, bali pia wale ambao walishindwa kumsaidia walikuwa wamepatwa na aibu kubwa sana.

Al-Hurr bin Yazid al-Riyahi, afisa katika jeshi la adui alikitelekeza cheo chake na akajiunga na Husein katika siku ya 10 ya Muharram kwa kulipa au kufidia kosa la matatizo aliyoyasababisha kwa Husein kwa kumzuia asiendelee na safari yake ya kwenda al-Kufa na kumfanya aweke kambi yake hapo Karbala katika sehemu ambayo si rahisi kuufikia mto.

Hali ya hatia ilihisiwa na wenyeji wale wa Kufa ambao walikuwa wameahidi kutoa msaada wao kwa Husein kupitia kwa Muslim bin Aqil lakini ambao hawakuweza kwenda Karbala kumsaidia Husein au hawaku- fanya jaribio lolote la kuungana naye pale. Unyofu wa majuto yao ulionyeshwa pale muda mfupi tu baada ya masaibu ya Karbala, wao walipokuja kuitwa, “Wenye kutubia” kwa zile juhudi zao za kulipiza kisasi cha mauaji ya Husein.

Miongoni mwa wale ambao walichelewa kutoa msaada kwa Husein alikuwa Abdallah bin al-Hurr al-Ju’fi. Akiwa njiani kwenda Kufa, Husein mwenyewe alimtaka ampe msaada lakini Abdallah hakutimiza ombi hilo ili kwamba asije akahatarisha maisha yake.1

Aibu ilimuandama katika uhai wake wote na alionyesha kujuta na kutubia kwake katika ibara zenye maana, “Nitaendela kujisikitikia kwamba Husein aliomba msaada wangu, na sikuzipata baraka za kukubali na kutekeleza haja zake.”2 Baada ya matukio hayo ya kuhuzunisha ya Karbala, wakati Ubaydullah bin Ziyad alipolalamika kwa Abdallah kuhusu kupuuzia kumwona kwa muda mrefu na kutokwenda kupigana dhidi ya Husein, na akadokezea juu ya dhana ya kuwaonea huruma maadui zake, hisia za Abdallah zililipuka katika mashairi yenye maana, “Mtawala ambaye ni bwana wa zamani katika udanganyifu ananiuliza kwa nini sikujiunga katika vita dhidi ya mwana wa Fatimah, wakati mimi nimepatwa na aibu kwa kukosa kumsaidia Husein. Kwa kweli, yule ambaye hachagui njia ya haki lazima ajisikie aibu.” Kisha aliondoka Kufa. 3

Qurra bin Qays ambaye alikuwa mjumbe wa Umar bin Sa’d kwa Husein alikuwa akisema baadaye katika uhai wake kwamba kwa hakika angefu- atana na al-Hurr kujiunga na kundi la Husein kama al-Hurr angemwarifu juu ya nia yake ya kuondoka kwenye utumishi wa Yazid. 4
Radii bin Munqidh al-Abdii ambaye alimuua Burayr al-Hamdan kwa kusaidiwa na Ka’b bin Amr al-Abdi alikuwa akitumia kuelezea aibu yake kwa maneno yafuatayo, “Kama isingekuwa imejaaliwa hivyo, mimi nisingejiunga na vita hivi nikapata kushuhudiwa na Ibn Jabir… napenda ningekuwa nimekufa na kuzikwa kabla ya kuuliwa kwa Burayr na vita dhidi ya Husein. 5

Shabath bin Ribi’i, mmoja wa makamanda muhimu wa jeshi la Umar bin Sa’d alisikiwa akisema, “Mungu hatafanya wema kwa watu wa nchi hii. Ni uovu ulioje huu kwamba kwa kipindi cha miaka mitano tumepigana dhidi ya kizazi cha Abu Sufyan tukiwa upande wa Ali bin Abi Twalib na mwanawe, Hasan, kisha tulijiunga na kizazi cha Mu’awiyah na Ziyad katika kufanya mashambulizi dhidi ya Husein ambaye, kwa mafanikio binafsi, alikuwa bora mno kuliko mtu yeyote hapa ulimwenguni. Huu ulikuwa ni mkengeuko ambao unabakia bila kusawazika. 6

Mkubwa zaidi kuliko watu hawa katika jinai lake alikuwa ni Umar bin Sa’d, kamanda wa majeshi ya Yazid hapo Karbala. Mmoja wa marafiki zake, Humayd bin Muslim, ameelezea kwamba, wakati wa kurudi kwake kutoka Karbala, pale alipoulizwa juu ya matokeo ya hapo (Karbala), Umar bin Sa’d alisema, “Usiniulize juu ya jambo lolote. Hakuna msafiri atakayefikia mwisho wa safari yake akiuendea mwisho mbaya namna hii kama ilivyo kuwa kwangu mimi. Nilifanya ukaribu wa uhusiano wenye matokeo yenye nguvu kidogo sana na nimetenda jinai mbaya sana.”7

Makosa ya Ubaydulah bin Ziyad, gavana wa Kufa yalikuwa mabaya zaidi. Alipeleka majeshi yote Karbala chini ya uangalizi wake mwenyewe na akamwamuru Umar bin Sa’d kumuua Husein na marafiki zake. Wakati Yazid alipokufa, maasia yalitokea katika nchi yote ya Iraq na ilimbidi Ibn Ziyad akimbie kutoka Basra.

Alimchukua pamoja naye mtu wa kumwongoza. Katikati ya safari hiyo alimwambia mtu huyo kwamba kwa vile Husein bin Ali alimpinga mtawala, basi mtawala huyo alimwamuru yeye (Ibn Ziyad) kumwua Husein. Kwa hiyo, yeye alishikilia kwamba uajibikaji na mauaji ya Husein lazima uwe juu ya Yazid na siyo juu yake yeye.8

Maelezo haya yasiyo na maana yoyote ni jaribio tu la kuhamisha jukumu lake hilo kwa Yazid na linachipuka kutoka kwenye hali ya kujuta kwa kuchukua sehemu muhimu katika mauaji ya Husein. Vinginevyo wakati Yazid alipomtaka Ibn Ziyad kuishambulia Hijaz na jeshi na kumpiga Abdallah bin al-Zubeir, kwa nini asingemkatalia Yazid kwa kusema, “Nimemwua mjukuu wa Mtume kwa amri ya mtu huyu mwovu, na sasa siwezi kuishambulia Ka’abah.”9

Mtu mhalifu kabisa kuliko wote alikuwa Yazid bin Mu’awiyah. Hili linathibitishwa na maelezo ya Ibn Ziyad yaliyokwishanukuliwa. Alipotambua kwamba Husein alikusudia kwenda Kufa, alimfanya Ibn Ziyad gavana wa hapo kuhakikisha kwamba hatua kali kabisa kuliko zote zinachukuliwa dhidi ya Husein. Ilikuwa ni baada ya kupata ruhusa yake kwamba, baada ya vita vya Karbala, kichwa cha Husein na vichwa vya mashahidi wengine wa Karbala pamoja na watu wa Husein waliokoka vitani walipelekwa na Ibn Ziyad mpaka Damascus. Kwa kweli yeye mwenyewe binafsi alikitendea kichwa cha Husein utovu mkubwa wa adabu.

Baada ya kujulishwa ukatili wote ambao Husein na sahaba zake waliupata, na baada ya kifo chake, ukatili waliofanyiwa watu wa Husein waliopona vita, Yazid hakuonyesha dalili yoyote ile ya kumchukia Ibn Ziyad. Bali kinyume chake alimruhusu aendelee na ugavana wa Kufa. Mmoja wa ndugu zake, Abd al-Rahman, ambaye alikuwa gavana wa Khurasan tangu mwaka wa 58 A.H alikwenda Damascus aliposikia kifo cha kishahidi cha Husein na alipata mkopo 10 wa crore dirham mbili (ambazo kwa sasa ni takriban dirham 36,500,000) kutoka hazina ya Khurasan ambako, kwa mujibu wa mapatano naye, kiasi hicho kilibakia kikiwa kimehifadhiwa.
Baada ya Abd al-Rahman ugavana wa Kurasan alipewa ndugu yake, Salm bin Ziyad. 11

Hapo mwanzoni Yazid alifurahia sana kifo cha Husein. Hata hivyo, wakati ilipoonekana kwamba mapinduzi yalikuwa yanasukwa, macho ya Yazid yalifunguka na alikuwa akilalama, “Ole wangu! Kwa kumuua Husein bin Ali, Ubaydullah bin Ziyad amenifedhehesha na kunifanya mlengwa wa chuki mbele ya macho ya Waislamu, Amepandikiza mbegu ya uadui na kinyongo dhidi yangu katika nyoyo zao. Watu wema na wabaya pia miongoni mwa Waislamu wanayaona mauaji ya al-Husein kama kosa la uovu mkubwa kabisa na wananichukia sana na kuniondoa kinyaa kwenye utu. Ubaya gani mtoto wa Marjana ameufanya! Namwomba Mungu Amlaani.”12

 • 1. Irshad, uk. 237.
 • 2. Al-Akhbar al-Tawal, uk. 258.
 • 3. Tabari, Juz. 6, uk. 270.
 • 4. Irshad, uk. 249/ Tabari, uk. 244.
 • 5. Tabari, juz. 6, uk. 248
 • 6. Tabari, juz. 6, uk. 250.
 • 7. Al-Akhbar al-Tawal 257
 • 8. Tabari, juz. 6, uk. 250.
 • 9. Tabari, juz. 6, uk. 6.
 • 10. Al-Wuzara wa al-Kuttab, uk. 18.
 • 11. Al-Wuzara wa al-Kuttab, uk. 19 na Kitabu tabari, juz. 6, uk. 271-272.
 • 12. Tabari, juz. 7, uk. 19.