Table of Contents

Sura Ya 36 : Hisia Za Ulimwengu Wa Kiislamu

Wakati maelezo kamili ya ukatili wa kinyama ambao Husein na wapenzi wake na ndugu zake waliyotendewa hapo Karbala yalipokuja kufahamika, kila moyo wa Mwislam ulitupwa kwenye wimbi la huzuni na ghadhabu kali. Wahalifu wa jinai hizi walichukiza mno, na hayo mauaji ya Husein yaliwatia fedheha tele.

Kwa vile watu wa Kufa walionekana kuhusika sana juu ya masaibu hayo makubwa, walijipatia wenyewe jina baya sana, hivyo kwamba iliwachukua karne nyingi kuweza kusahau fedheha hiyo. Abu Uthman al-Nahdi, Sahaba wa Mtume, aliyaacha makazi yake ya Kufa, akikataa kuishi sehemu ambayo mtoto wa Mtume ameuawa. Fedheha hiyo itokanayo na msiba huo ilienea katika maeneo yote ya Iraq.

Baadhi ya wale ambao wamewaua mashahadi wa Karbala walikuwa wamekasirikiwa mno na ndugu zao wa karibu. Mke au dada yake Ka’b bin Jabir ambaye alimuua Burayr al-Hamadani alikataa kuongea naye kwani alipigana dhidi ya mtoto wa Fatimah, na akamuua Burayr al-Hamadan.1

Margana, mama yake Ubaydullah bin Ziyad, alimlaani kwa kupigana dhidi ya al-Husein na kusababisha auawe.2

Hata kabla Yazid hajaanza kuhamisha lawama ya mauaji ya Husein kwa Ibn Ziyad na kumzungumzia vibaya, baadhi ya washauri wake tayari walikwishaanza kufanya rejea zenye dharau kwa Sumayyah, bibi (nyanya) yake Ibn Ziyad na Yazid alilazimika kuzisikia kashfa hizi akiwa kimya,

Yahya bin al-Hakam alisoma mashairi yenye maana, ‘Vichwa vilivyokat- wa kutoka kwenye miili yao katika bonde la Karbala vilikuwa na uhusiano wa karibu zaidi na sisi, kuliko na Ibn Ziyad, aliyezaliwa na mtumwa akichipukia kwenye shina la kudharaulika. Tazama! Kizazi cha Sumayyah kimeongezeka kama mchanga, na kizazi cha binti ya Mtume kimefutiliwa mbali.

Siyo tu watu walioishi wakati mmoja na Yazid waliomchukia, bali pia baadhi ya kizazi chake cha baadaye waliyajua na kuyachukia matendo yake maovu. Mtoto wake, Mu’awiyah bin Yazid aliyakiri hadharani makosa madogo madogo ya udhaifu wa baba yake na akakataa kukikalia kiti kilichoachwa wazi na baba yake. Umar bin Abdul-Aziz, Khalifa wa Bani Umayyah katika karne ya pili ya hijiriya aliamuru kuchapwa viboko ishirini kwa mtu ambaye atatanguliza kuweka maneno, Amir al-Muuminin (kiongozi wa waumini) kwenye jina la Yazid.

Mauaji ya Husein, na Ukhalifa wa Yazid vilichukuliwa kama matukio ya kuaibisha Waislamu wenyewe wakati mwanafalsafa maarufu na mshairi, Abu al-Ala al-Ma’arri, akiandika katika karne ya 4 ya hijiriya, alisema, “Mabadiliko ya wakati huniletea maono yaliyo ya ajabu na mageni kiasi kwamba nimepoteza shauku yote ya kuyashuhudia.
Kwa nini! Je, Maquraishi wenu hawakumuua Husein, na je, mtu mwovu kama Yazid hakupanda kwenye kiti cha Ukhalifa wenu?”

Ni dhahiri kabisa chuki iliyohisiwa kwa undani na jumla na watu wote dhidi ya utawala unaohusika na mauaji ya Husein ulikuwa ni mwanzo wa (kufanyika) mapinduzi.

  • 1. Tabari, juz. 6, uk. 247.
  • 2. Tabari, juz. 7, uk. 7.