Table of Contents

Sura Ya 37: Dalili Za Mapinduzi

Dalili za mapinduzi yaliyokuwa yanakaribia kutokea yalikuwa yaonekane wazi tangu kwa watu wa Husein waliopona vita, wakiwemo zaidi wanawake, watoto wadogo kadhaa, na mwanawe mkubwa, lakini akiwa dhaifu sana na asiyejisikia vizuri walipoanza kutembezwa kama wafungwa katika mitaa ya Kufa. Wafungwa hawa hawakuruhusiwa kulia na ingawa ilikuwa imepangwa kwamba tukio hili litekelezwe kwa kusherehekea, vilio vya maombolezo viliamshwa na watazamaji walipowaona watu wa Husein waliopona vitani wenye huzuni na katika kuzisikia hotuba nzito zenye nguvu za Zainab, Umm Kulthumu na Ali bin Husein.

Maafisa wa Yazid hawakuruhusiwa kuingia kwenye vitongoji vingi au maeneo ya humo njiani kutoka Kufa kwenda Damascus wakati walipokuwa wanawaongoza watu wa Husein waliopona vita kwenda Syria. Katika sehemu nyingi watu walitoa upinzani wa silaha, na nguvu kwa kweli ilitumika katika sehemu chache zikaliwazo na watu.

Madina na Makkah ilikuwa ndio vitovu vya usimamizi vya ulimwengu wa Kiislamu. Madina lilikuwa Jiji la Bani Hashim, wengi wao walikuwa wametokana na Abu Talib, na waliutoka mji pamoja na Husein. Watu wengine wa familia hiyo wote walikuwa Madina.

Abd al-Malik bin Abi al-Harith al-Sulami ambaye alizichukua habari za kuuliwa kwa Husein na kuzipeleka Madina anasema kwamba wakati zilipotangazwa, mara sauti kubwa za vilio vya kuomboleza na kusikitikia vilisikika vikitoka kwenye nyumba za Bani Hashim ambavyo kwamba kamwe hajawahi kusikia mfano wake kabla ya hapo.

Vyovyote vile ambavyo watu wa Madina wangeweza kutojali wao wasingeweza kubakia bila uchangamfu wa kutojihusisha na hali ya huzuni ya kuvunja moyo ya roho nyingi zilizoteseka sana kwa muda mrefu kiasi hicho.

Kwa sababu hiyo, watu wa Madina waliona kwamba ilikuwa ni laz- ima kupeleleza na kujua mapema zaidi kiasi iwezekanavyo, juu ya tabia za Yazid. Katika mwaka wa 62 A.H, tume iliundwa yenye baadhi ya watu mashuhuri wa Madina, akiwemo Abdallah bin Hanzala, waliondoka na kwenda Syria kuchunguza tabia ya Yazid.

Ingawaje wao walipewa fedha nyingi sana kama hongo, wajumbe hao, katika kurudi kwao kutoka Syria walitaarifu hivi, “Tumerudi kutoka kwa mtu ambaye hafuati dini, yeye anakunywa pombe, anacheza dufu, anasikiliza muziki wa waimbaji wanawake, anacheza na majibwa na anatumia muda wake na walevi na mafisadi katika kupiga porojo na maongezi yasiyo na maana. Kwa hivyo sisi tunaachana na kiapo cha utii tulichokitoa kwake.1

Jalal al-Din Suyuti ameandika katika kitabu kiitwacho Tarikh al-Khulafai kwamba wajumbe wa tume hiyo walieleza hivi, “Sisi tumechagua kumpinga Yazid wakati tulipotambua kwamba adhabu ya Mwenyezi Mungu ingechukua umbo la mawe yakituangukia kutoka mbinguni kwani ni mtu ambaye aliona ni halali kulala na wajakazi ambao wamechangia kitanda na baba yake, na binti zake na dada zake, anakunywa pombe na anaacha kusimamisha Sala zake.”

Mjumbe wa tume hiyo, al-Mundhir bin al-Zubeir alisema, “Yazid amenipa hongo ya dirham mia moja elfu (laki moja) ambazo zisingenizuia kukufa- hamisheni habari zenye ukweli.

Nakuelezeni wazi kwamba yeye (Yazid) anakunywa sana pombe kiasi ambacho anashindwa na kuacha kusimamisha Sala zake.” Pia alikubaliana na yale maelezo ambayo wajumbe wengine wa tume hiyo walisema kuhusu Yazid.

Tabia ya Yazid iliwatenganisha wenyeji wa Madina na yeye kiasi kwamba mwanzoni mwa mwaka wa 62 A.H, watu wa Madina walimwondoa gavana wao, Uthman bin Muhammad bin Abi Sufyan, binamu yake Yazid, na wakaweka mzingiro (karantini) kwa Bani Umayyah wapatao karibu elfu moja ambao waliishi Madina.

Hii ilisababisha kuchukuliwa hatua za kukandamiza kulipiza kisasi na Yazid, ikifuatiwa na maandamano ya kuchukiwa kwao kukubwa na kinyongo cha Waislam. Yazid alipeleka jeshi chini ya uongozi wa Muslim bin Uqba kuuzima uasi huo hapo Madina.

Akiunguzwa na ghadhabu kali, aliamuru kwamba Madina ifanyiwe uporaji na mauaji kwa muda wa siku tatu bila kupumzika na kwamba jeshi lingeweza kutwaa chochote kile ambacho wangekiteka, pamoja na wafungwa wa vita.

Mateka wa Madina lazima watakuwa wamewajumuisha wanawake na watoto wa familia za masahaba wa Mtume na wafuasi wao. Maagizo ya Yazid yalikuwa ya wazi kwamba wangegawanywa miongoni mwa askari wa jeshi hilo. Raia wengine wa Madina waliobaki walitoa baia (kiapo cha utii) kwa Yazid kama watumwa wake, wakimpa mamlaka isiyo na mipaka kamili juu ya maisha yao, mali zao na watu wanaowategemea.

Wakati Yazid bin Abdallah bin Rabi’a bin Aswad, mtoto wa binti ya Umm Salama, mjane wa Mtume, alikataa kula kiapo cha utii kwa Yazid katika sura hii, aliuawa mara moja. Wakati Yazid alipoyasikia maelezo kamili juu ya matukuo haya, alisoma mashairi ambayo kwamba kidokezo kikubwa kilikuwa kwamba shambulio juu ya Madina lilikuwa ni kulipiza kisasi kutokana na kushindwa kwa ndugu zake katika vita vya Badr.

Mambo hapo Makkah napo pia yalikuwa yamebadilika. Wakati Abdallah bin al-Zubeir, ambaye kwa muda mrefu alitamani kupata wadhifa wa kuwa khalifa, aliliona wimbi la jumla la hasira kubwa miongoni mwa watu dhidi ya Yazid kwa kusababisha kuuliwa kwa Husein hapo Karbala, aliiona kama ni nafasi inayofaa sana kuendeleza maslahi yake binafsi, na akatoa hotuba nzito yenye nguvu akiwashutumu vikali wenyeji wa Kufa kwa kigeugeu chao, akimsifia sana Husein na akaelezea wazi makosa ya Yazid. Kama matokeo ya hotuba hizo, wakazi wa Makkah, kwa ujumla, walikubali kula kiapo cha utii kwa Abdallah bin Zubeir.

Haya yalikuwa maendeleo yasiyopendeza na yalisababisha wasi asi mkub- wa sana kwa Yazid. Alijitahidi kuwapata watu wengi maarufu wa Makkah kwa kiasi alichoweza kukipata, lakini kosa la kumfanya Husein auawe lilikuwa baya la uovu mkubwa mno kiasi kwamba, ingawa baadhi ya watu hawakupenda kutoa kiapo cha utii kwa Abdallah bin al-Zubeir, walishikil- ia kumchukia Yazid. Abdallah bin Abbas alikuwa mmoja wa watu kama hao. Alikuwa ni mtoto wa ami yake Mtume, aitwaye Abbas.

Yazid alimwandikia barua Abdallah bin Abbas, akimsifu kwa kutokula kiapo cha utii kwa Abdallah bin al-Zubeir, na akataka kufanya ionekane kama dalili ya uaminifu kwake yeye. Aliahidi kumtumia zawadi inayostahiki katika muda wa karibuni sana. Siku iliyofuata Abdallah bin Abbas alimpa Yazid jibu lenye kuchoma sana moyo ambalo ndani yake alizielezea hatua zote kwa urefu ambazo Yazid alikuwa amezichukua kumzuia al-Husein kuondoka Madina na Makkah na ukatili aliokuwa amemfanyia hapo Karbala.

Alisema kwamba hata baada ya vifo vyao, Husein na sahaba zake walikuwa bado hawajazikwa, kwamba wanawake wa familia yake walinyang’anywa nguo za kujifunika vichwa vyao na wakatembezwa kutoka Iraq mpaka Syria kama wafungwa. Alieleza matu- maini kwamba Mwenyezi Mungu angemtesa Yazid kwa ghadhabu Yake, na alitupilia mbali (alilikataa kabisa) pendekezo la kuzawadiwa alilokuwa ameahidiwa na Yazid.

Aliongeza kusema kwamba kwa kuuawa wahenga (mababu) wake makafiri, walio na dhambi na wachafu katika vita vya Badr, Yazid alikuwa analipiza kisasi kwenye kizazi cha Mtume.

Katika kuisoma barua hii yenye kumfedhehesha, hasira ya Yazid haikujua mipaka, na alifikiria juu ya kumuua Abdullah bin Abbas, lakini kwa vile alikuwa ameshughulishwa katika uadui na Abdallah bin Zubeir, hakuweza kuendelea na jambo lolote dhidi yake.

Baada ya kushambuliwa na kuangamizwa kwa wakazi wa Madina, Muslim bin Utba alisonga mbele kuelekea Makkah kama alivyoelekezwa na Yazid, lakini alifariki dunia katika mwezi wa Muharram mwaka wa 64 A.H. Hata hivyo, alimteua Husein bin Numayr kuwa kiongozi wa jeshi kama alivyoelekezwa na Yazid. Husein alivamia Makkah na akaizingira Ka’bah, na katika mwezi 3 wa Rabi I, mwaka 64 A.H. siyo mawe tu bali hata moto uwakao pia ulimiminwa kwenye Nyumba ya Mwenyezi Mungu ambayo ilishika moto.2

Haya yalikuwa mafaniko ya mwisho ya Yazid. Alifariki dunia mnamo mwezi 14 Rabiul-Awwal,
mwaka wa 64 A.H. Kwa kifo chake hicho, ugomvi na vita vilikwisha, na Husein bin Numayr akarudi.

Al-Fakhri anasema kwamba jumla ya kipindi cha utawala wa Yazid kilikuwa miaka mitatu na nusu. Katika mwaka wa kwanza wa utawala wake alimuua Husein bin Ali, katika mwaka wa pili aliuvamia mji wa Madina na akauacha uporwe mali na kutekwa nyara kwa muda wa siku tatu, na katika mwaka wa tatu alipeleka kikosi maalum dhidi ya Makkah ambacho kiliichoma moto Ka’abah. Kwa jinai hizi tatu mbaya na za uovu mkubwa mno, masaibu ya Karbala yalitoa mshtiko mkubwa wa kutisha kwa ulimwengu wa Kiislamu kiasi kwamba hakukuwa na mtu mwenye akili timamu ambaye aliyajua maelezo ya tukio hili la kusikitisha sana kwa undani zaidi aliyeweza kujizuia asiathirike kwalo.

Tendo hili la Yazid halikuwa la dhambi na kosa la jinai tu, bali pia lilikuwa ni kosa la kijinga la kisiasa la dhahiri ambalo kwa sababu yake, Yazid na washauri wake wa kudharaulika kama vile Ubaydullah bin Ziyad na Shimr waliwafanyia uadui hata wale ambao, licha ya imani yao juu ya ukuu wa Mtume wa Mwenyezi Mungu na kushikamana kwao na dini ya Uislamu, walitaka kushikilia mpaka mwisho, sera yao ya kutokuingilia kati, na kuivumilia serikali ya Bani Umayyah, ingawa hawakuwa na hisia za kushikamana nayo au utii kwayo.

Baada ya kifo cha Yazid katika mwaka wa 64 A.H hisia za chuki zilizokuwa zimefichika za watu wa Iraq dhidi ya Ubaydullah bin Ziyad zilijionyesha kwa nguvu kiasi kwamba ilibidi (Ibn Ziyad) akimbie kutoka Basra bila kusindikizwa.3Na asingeweza kujiamini wakati akiwa safarini alipomsikia mpanda ngamia mmoja akisoma beti zenye maana, “Ewe Mwenyezi Mungu! Mlaani Ziyad na kizazi chake, ambaye amewaua, bila hatia au kosa lolote lile Waislamu wengi ambao walikuwa wakisimamisha Sala wakati wote, wakikaa macho usiku (kwa ajili ya kusali na kuomba dua) na walikuwa wacha –Mungu na wenye kujizuia.”

Hali ya hisia hapo Kufa katika maeneo ambayo Ibn Ziyad mwenyewe alihusika nayo inaweza kukadiriwa kwa ukweli kwamba baada ya kifo cha Yazid, vuguvugu lilianzishwa kwamba Ibn Ziyad atambuliwe kama mtawala, Yazid bin al-Harith al-Shaybani, askari na mjumbe katika jeshi la Yazid aliipinga rai hiyo, akisema, “Tunatamani kuachana na mtoto wa Sumayyah. Kwa kweli hatuwezi kuukubali utawaka wake.”4

Kilele katika kuonyesha kukerwa na Yazid kilikuwa kimefikiwa wakati mtoto wake na mrithi, Mu’awiyah bin Yazid, alipopanda mimbari na akasema, “Enyi watu! Taasi ya Ukhalifa ilikuwa ndiyo kamba ya Mwenyezi Mungu yenye nguvu, lakini babu yangu, Mu’awiyah bin Abu Sufyan, alibishania haki ya kuhusika nayo pamoja na Ali bin Abi Talib ambaye, kwa ukweli halisi kabisa, alikuwa ndiye mwenye haki na cheo hicho, na akachukua njia zote za kulaumiwa ama kushutumika ambazo nyinyi nyote mnazifahamu.
Kwa vyovyote, yeye amelifikia kaburi lake likiwa limezunguukwa na madhambi yake. Kisha kiti hicho cha Ukhalifa kikaenda kwa baba yangu, ambaye naye pia hakukistahili kabisa kabisa. Yeye amemua Husein, mtoto wa binti ya Mtume. Mwishowe na yeye pia aliufikia mwisho wa siku zake na kaburi lake, akiwa amenaswa kwenye madhambi yake.”

Kisha alikatisha na kulia, “Msiba mkubwa sana kwetu sisi ni ile hisia iliyoko ndani yetu sisi kwamba alifikia mwisho wenye kufedhehesha kwani alikiua kizazi cha Mtume, akaruhusu kunywa ulevi (pombe) na akakufurisha utakatifu wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu. Sasa, kwa vile mimi nimekuwa mgeni kwenye starehe za Ukhalifa mpaka sasa, kwa nini basi nionje uchungu wake?

Shughulikieni mambo yenu wenyewe. Mimi sihusiki lolote na masuala ya Ukhalifa. Hata kama dunia ni yenye kupen- deza na ni neema, tumekwishapata kiasi cha kutosha na kama kwa kweli ni isiyofaa, chochote kile ambacho tumekipata kama fungu letu kutokana nayo (basi) hilo ni zaidi kuliko chenye kutosheleza.”

Kisha akajitenga ndani ya kasri, na alifariki dunia siku arobaini baadaye. Halafu ghasia (zahama) zililipuka mjini Khurasan na magavana wa ki-Bani Umayyah waliopelekwa pale waliondolewa. Watu walijiingiza kwenye mapigano mpaka mwishowe wadhifa wa Ukhalifa ukatoweka kwenye kizazi cha Abu Sufyan moja kwa moja, na mzee Marwan bin al-Hakam alikubaliwa kuwa khalifa nchini Syria, na cheo cha Ukhalifa kilishikiliwa na kizazi chake kwa muda mrefu.

  • 1. Tabari, juz. 7, uk. 6-7.
  • 2. Sahih Muslim, juz. 1, uk. 420; na Tabari, juz. 7, uk. 14.
  • 3. Al-Akhbar al-tiwal, uk. 276-277.
  • 4. Tabari, juz. 7, uk. 28.