Table of Contents

Sura Ya 38: Wenye Kutubia

Wakati Ubaydullah bin Ziyad alipokuwa amerejea Kufa kutoka makao makuu ya jeshi lake pale Nukhayla baada ya mauaji ya halaiki pale Karbala Shi’a wa Ali walishikwa na aibu kwa kuzembea kwao kutokwenda kumsaidia Husein. Walijichukulia wenyewe kuwa ni wenye kuwajibika kwa yale mazingira ya kuvunja moyo sana ambamo Husein aliuliwa, kwani ilikuwa ni kutokana na mialiko yao na ahadi zao za kumsaidia walizompa ndipo yeye alitoka Makkah kuja Kufa.

Waliamua kwamba lile kosa la jinai kubwa la kutokuwa na msimamo, na kutokuwa wakweli kwenye ahadi yao na matokeo yake yakawa ni kumfikisha Husein kwenye mauti yake, lilitia doa jina lao kiasi kwamba hawakuweza kuwa na matumaini ya kusafisha na kurudisha heshima yao isipokuwa kwa kuwaua wale wote ambao wametia mikono yao katika mauaji ya Husein na wapenzi wake na kama ikibidi, kuyatoa mhanga maisha yao katika kulifikia lengo hili.

Kwa hiyo, waliwasiliana na watu watano watiifu wakubwa wa watu wa nyumba ya Mtume, Suleimana bin Surad al-Khuzaa’i, sahaba wa Mtume, al-Musayyab bin Najaba, sahaba mashuhuri sana wa Ali bin Abi Talib, Abdallah bin Sa’d bin Nufayl al-Asadi, Abdullah ibn Waalin al-Taymii na Rifa’a ibn Shaddad al-Bajali. Wao na wengine wengi walikutana kwenye nyumba ya Suleiman bin Surad.

Al-Musayyab bin Najaba kisha akatoa hotuba yenye kuwalaumu vikali ndugu zake wa mji kwa kosa la kumwita Husein kuja Kufa na kumpa ahadi za kumsaidia, na wasiende kumpa msaada huo hapo Karbala ambapo, baada ya kupatwa na ukikatili usioelezeka, akauawa. Aliwaambia kwamba fedheha ambayo kwamba wamejigubika nayo ingeweza kutulizwa kama watawaua wale ambao wameshiriki katika mauaji ya Husein, au kuyatoa maisha yao (kufa) katika kulijaribu hili. Rifaa bin Shaddad alifuata kwa kutoa hotuba yenye kumuunga mkono al-Musayyab.

Wazungumzaji wengine pia walielezea maoni kama hayo hayo, na Suleiman bin Surad al- Khuzai alichaguliwa kwa uamuzi wa pamoja kuwa kiongozi wa kundi hilo. Kisha Suleiman bin Surad alisimama na akatoa hotuba iliyojaa huzuni na hamasa sana. Baadhi ya dondoo kutoka kwenye hotuba yake zaweza pia kutolewa hapa.

Yeye alisema, “Tulisubiri kwa hamu kubwa kufika kwa watu wa Nyumba ya Mtume, lakini walipofika tulionyesha kutojihusisha na kuwa wazembe kiasi kwamba katika nchi yetu na siyo mbali kutoka tulipo sisi mtoto wa Mtume akauawa.
Aliponyanyua kwa nguvu sauti yake katika kuomba uadilifu na msaada, hakukuwepo mtu yeyote yule wa kumwitikia. Watu wenye dhambi walimgeuza kuwa shabaha ya mishale yao na mikuki yao na wakamuua. Hawakukomea kwenye hili tu, bali walimvua nguo zake baada ya kifo chake.

Sasa kama mnataka kufanya jambo lolote lile, basi amkeni sasa. Ghadhabu na hasira ya Mwenyezi Mungu imekwishaguswa. Amueni hapa na tena sasa hivi, msirejee kwa wake zenu na watoto wenu mpaka muwe mumechukua hatua ili kupata radhi za Mwenyezi Mungu.

Naapa Wallahi, nafikiri Mungu hatakuwa radhi nanyi maadamu hamjawatendea waovu kama walivyokutendeeni nyinyi au hamjajitoa mhanga maisha yenu katika jitihada hii. Hebu kuweni wenye kuonyeka kabla. Msikiogope kifo, kwani yeyote yule aogopaye kufa, hupoteza heshima.”

Mfumuko mkubwa wa mhemuko uliushika mkusanyiko ule baada ya kusikia hotuba hii yenye mguso. Abdullah bin Walin al-Taymii aliteuliwa kuwa mweka hazina wa kundi hili. Suleiman bin Surad aliandika barua kwa Sa’d bin Hudhayfa bin Yamaan wa Madaain na kwa wengine pia kuwafahamisha mantiki na malengo ya vuguvugu lililofadhiliwa na kundi hilo lililisimamiwa na yeye. Barua hizo kwa ujumla zilikariri yale aliyoyasema katika hotuba ambayo kwamba dondoo yake imekwishatolewa.

Sa’d aliisoma barua ya Suleiman kwa Shi’a wa Mada’in, na wote walikubali kuwasaidia wale wote ambao waliamua kuwapiga maadui wa watu wa nyumba ya Mtume. Sa’d alipeleka jibu kwa Suleiman bin Surad kama ilivyostahili.

Hali kadhalika hilo lilikuwa ndio jibu lililotolewa na wale wengine pia. Harakati zote hizi zilifanyika katika usiri mkali, na idadi kubwa ya watu ilijiunga katika harakati hizi zilizoshauriwa, lakini hakukuwa na hatua zozote zilizoweza kuchukuliwa kuyapa sura ya kivitendo malengo haya mpaka baada ya kifo cha Yazid mnamo mwezi wa Rabul-Awwal ya mwaka wa 64 A.H. Harakati hiyo ilipata nguvu sana baada ya kifo cha Yazid kiasi kwamba iliweza kuenezwa kwa uwaziwazi.

Ilifika Misri pia, na shauku kubwa ilipatikana hapo kwa kutokana na mfululizo wa hotuba za mara kwa mara juu ya jambo hili zilizotolewa na Ubaydullah ibn Abdillah, ambaye aliongelea kuhusu mauaji ya Husein kwa maneno yenye mguso wa kusisimua sana.

Kama ilivyoamuliwa hapo awali, watu wote waliojitolea kwenye harakati hii walikusanyika hapo Nukhayla mwezi mosi ya Rabiul-Thani, mwaka wa 65 A.H. Hata hivyo, kati ya watu 10,000 ambao waliahidi kujitokeza ni watu 4,000 tu waliojitokeza kwa kushiriki katika harakati hii.1

Pendekezo la Suleiman bin Surad kwamba mhalifu mkubwa kabisa aliyepo kuhusiana na mauaji ya Husein alikuwa Ubaydullah bin Ziyad, na kwamba yeye lazima awe mtu wa kwanza kabisa kuuawa lilikubaliwa.2

Tarehe 5 ya mwezi wa Rabiul-Thani mwaka wa 65 A.H. watu hawa watafutao kulipa kisasi kwa mauaji ya Husein waliondoka kwenda Syria.3

Kwanza kabisa walilitembelea kaburi la Husein ambako waliutumia mchana mmoja na usiku katika maombelezo na Sala. Hotuba za Suleiman bin Surad na wengineo zilihimiza shauku na hamasa ya wasikilizaji kwenye msisimko.

Mashujaa hawa walijiweka katika mpango wa kivita hapo Ayn al-Warda. Majeshi ya Syria chini ya uongozi wa Ibn Dhi al-Tila na Husein bin Numayr yalifika baada ya siku tano kuja kupigana nao vita. Baada ya kufanya maandalizi yake ya mwisho, Suleiman bin Surad alitangaza kwamba kitokeapo kifo chake basi atarithiwa katika uongozi na al- Musayyab bin Najab, Sa’d bin Nufayl, Abdallah bin Walin na Rifaa bin Shaddad kwa mfuatano wa mpango wa majina yao yalivyotolewa.
Tarehe 8 mwezi Jamadul-Awwal, mapigano ya kwanza yalitokea, na watubiaji ambao idadi yao ilifikia watu 4000 tu waliwashinda adui ambao walikuwa 10,000 kwa idadi yao, lakini siku iliyofuata nguvu mpya ya wanajeshi 8000 ilipokelewa kutoka kwa Ubaydullah bin Ziyad. Idadi hii iligeuza kabisa mizani dhidi ya watubiaji, ambao walipigana vikali sana mpaka upevu wa usiku lakini walipata majeruhi wengi.

Siku iliyofuatia hali yao ikawa mbaya zaidi, na Suleiman bin Surad aliuawa. Al-Musayyab bin Najaba alichukua nafasi yake akawa kiongozi na akapigana kwa ushu- jaa mkubwa sana. Na yeye pia aliuawa.

Abdallah bin Nufayl kisha naye akauchukua uongozi wa wenye kutubia wakati habari zilipowafikia kwamba msaada kutoka Madain na Basra ungewafikia watubiaJi punde. Hata hivyo, ilionekana kwamba kusingekuwa na matumanini juu ya kufika kwao wakati wa uhai wa wale wanaopigana katika vita. Wakati huo huo Abdallah bin Sa’d na Abdallah bin Walin wakawa pia wameuawa.

Kwa vile jioni ilikwishaingia, vita vilisimamishwa. Kati ya watu watano waliochaguliwa kuwa viongozi wa watubiao, alikuwa ni Rifaa bin Shaddad tu alibaki na watu mamia wachache tu, wengi wao wakiwa wamejeruhiwa au wameachwa hawafai kwa kupigana. Katika hali isiyofaa ya namna hiyo, watubiaji walijitoa (katika mapigano) wakati wa usiku. Hivyo ndivyo lilivyokwisha jaribio la kwanza la kulipiza kisasi cha mauaji ya Husein.

  • 1. Tabari, juz. 7, uk. 67.
  • 2. Tabari, juz. 7, uk. 69.
  • 3. Tabari, juz. 7, uk. 74.