Table of Contents

Sura Ya 39: Umwagaji Damu Usio Haki Walipizwa.

Watubiaji hawakufaulu katika jaribio lao la kutaka kulipiza kisasi kwa wale waliohusika na mauaji ya Husein kutokana tu ya idadi kubwa ya jeshi la maadui. Si muda mrefu baadae alipotokea al-Mukhtar bin Abi Ubaud al- Thaqafi ambaye alikusudia kutoa adhabu inayostahili kwa wale wote ambao walishiriki katika kumuua Husein.

Baba yake al-Mukhtar alikuwa amejitambulisha katika vita vilivyopigwa wakati wa utekaji wa Uajemi (Iran) na majeshi ya Uislamu. Miongoni mwa Shi’a wa Kufa, al-Mukhtari alikuwa akifahamika sana na mapenzi yake makubwa kwa watu wa nyumba ya Mtume, na Muslim bin Aqil aliwahi kukaa nyumbani kwake kwa muda fulani, lakini al-Muktar alikuwa ameondoka Kufa kwa shughuli zake binafsi kabla ya hatua za matokeo ya kimsiba kuhusu Muslim bin Aqil kuanza kuonekana.

Alirudi Kufa baada tu ya Muslim bin Aqil na Hani bin Urwa wote wawili walipokuwa wamek- wishauawa, na akaona kwamba Amr bin Hurayth amesimamisha bendera kuhakikisha usalama wa maisha na mali za wale ambao walichukuliwa hifadhi chini yake. Alipochukulia kwamba ni jambo lenye kufaa kufanya hivyo, al-Mukhtar alichukua hifadhi chini ya bendera hiyo.

Hata hivyo, yeye alikataliwa usalama wa mtu na mali, na Ubaydullah ibn Ziyad alimpiga kwa fimbo na kumsababishia maumivu makali sana kwenye moja ya macho yake. Kisha alitupwa gerezani, na alikuwa ndani ya gereza wakati masaibu ya Karbala yalipotokea.

Dada yake alikuwa mke wa Abdallah bin Umar, na kwa vile Yazid haku- penda kumuudhi Abdallah bin Umar, aliamuru kuachiliwa huru mara moja kwa al-Mukhtar kwa ombi lake. Bin Ziyad, hata hivyo, alimwachia al-Mukhtar kwa sharti kwamba kama hakuondoka Kufa ndani ya siku tatu, kuuawa kwake kungekuwa halali. Matokeo yake, al-Mukhtar aliondoka Kufa kama ambavyo ilikuwa imeamuliwa.1

Kwa zaidi ya mwaka mmoja, al-Mukhtar alisafiri kutoka mahali fulani na kwenda mahali pengine nchini Hijaz, wakati wote akielezea nia yake ya kulipiza kisasi mauaji ya al-Husein, na asipumzike mpaka amefanya hivyo.2

Al-Mukhtar alikuwa Makkah wakati jeshi la Syria chini ya Husein bin Numayr liliposonga mbele dhidi ya Abdallah bin al-Zubeir na kuuzingira mji wa Makkah. Wakati ambapo katika tarehe 3 Rabiul al-Awal, mwaka wa 64 A.H, Ka’abah ilipochomwa moto, na majeshi ya Husein bin Numayr yalipoingia Makkah, al-Mukhtar alipigana dhidi ya majeshi ya watu wa Syria kwa ujasiri mkubwa na wavamizi walishindwa. Wakati huo huo, kifo cha Yazid kilitangazwa, na uvamizi ukasimamishwa. Al-Mukhtar, hata hivyo alibakia kukaa na Abdilah bin Zubair kwa zaidi ya miezi mitano.

Katika kipindi kirefu hiki cha mpito, mapinduzi yalitokea huko Kufa, na naibu wa Ubaydullah bin Ziyad, aliyeitwa Amr bin Hurrayth alikuwa ameondolewa na wakazi wa Kufa. Walimfanya Amr bin Mas’ud kuwa gavana wa Kufa na alitoa kiapo cha utii kwa Abdallah bin Zubeir na kuwafanya watu wa Kufa wamkubali kuwa khalifa wao.

Hali hii ya kutotulia ilichukuliwa na al-Mukhtar kuwa yenye kufaa kwa utekelezaji wa mipan- go ya kulipiza kisasi kwa wauaji wa Husein, na hivyo aliondoka kwenda Kufa.3 Watu mashuhuri wa Shi’a wa Kufa walikubaliana na rai zake.4 Wakati watu waliobaki wa kundi la watubiaji liliporudi pamoja na Rifa’a bin Shaddad baada ya kushindwa, al-Mukhtar alikuwa yuko kifungoni.5

Ilikuwa tena ni kwa msaada wa Abdallah bin Umar ambao aliandika kwa wote wawili Abdallah bin Zubeir na Ibrahim bin Muhammad bin Talha, gavana wa Kufa, kwamba al-Mukhtar alipata uhuru wake tena.

Watu mashuhuri na mashujaa pamoja na Ibrahim ibn Malik al-Ashtar wal- iungana na al-Mukhtar katika kuendeleza zaidi lengo la kulipiza kisasi kwa umwagaji wa damu ya Husein. Iliamuliwa kwamba tarehe 14 mwezi Rabiul-Awal mwaka wa 66 A.H, hatua lazima zichukuliwe kuanza kufanya kile ambacho kikundi kimelenga kukifanya. 6

Wauaji wa Husein walikuwa ndani ya Kufa yenyewe. Walikuwa wakilip- wa na serikali ya Syria na kuwiwa utii wao kwa watawala wa nchi hiyo. Walikuwa pia wakazi wa Kufa ambayo ilikuwa chini ya msukosuko wa Abdallah bin Zubeir. Tendo lolote litakalochukuliwa na al-Mukhtar dhidi ya wakazi waovu kama hawa wa Kufa lingemuingiza katika matata na Abdallah bin Zubeir. Kama tatizo hili lilikuwa ni la kuamuliwa, kwa nini basi lisijaribu kutatuliwa hapa mwanzoni.

Kwa hiyo, al-Mukhtar, alifanikiwa kumwondoa madarakani gavana wa Kufa aliyeteuliwa na Ibn Zubeir, siyo kwa kutumia nguvu moja kwa moja, bali ilikuwa ni kuweka shinikizo dhidi yake hivyo kwamba gavana huyo alikimbia kuitoka Kufa. Al-Mukhtar aliweka serikali yake mwenyewe hapo. Alitekeleza kazi yake na katika kufanya hivyo alikumbana na hali fulani fulani zilizokuwa ngumu.

Ubaydullah bin Ziyad aliivamia Mosul akiwa na jeshi la Syria na al-Mukhtar alimpeleka Yazid bin Anas na watu 3,000 kupigana naye. Adui alishindwa, lakini wakati Yazid bin Anas, ambaye alikuwa hajisikii vyema alipofariki, Warqa bin Azid aliamua kuakhirisha mapigano mpaka kufika kwa nguvu mpya kutoka Kufa kwa kuzingatia idadi kubwa ya jeshi la adui. Alipozipata habari juu ya hali hii, al-Mukhtar alipeleka watu 7000 chini ya Ibrahim bin al-Malik al-Ashtar kumsaidia Warqa.

Mkubwa wa majeshi ya adui alipoona kwamba al-Mukhtar ameachwa takriban pekee kabisa, kwani Ibrahim alikuwa amepelekwa Mosul, alifikiria kuwa hii ni fursa nzuri sana ya kufanya uasi dhidi ya al-Mukhtar, na hivyo walifanya shambulio dhidi yake. Waliokuwa maarufu miongoni mwa wakubwa hawa walikuwa Shabath bin Ribi’i, Shimr bin Dhi al-Jawshan, Muhammad bin al Ash’ath, Zahr bin Qays, Hajjar bin al-Abjar, Yazid bin al-Harith al-Shaybani na Amr bin al-Hajjaj al-Zubaydi.

Al-Mukhtar aliendeleza mapigano na adui, na akapeleka ujumbe kwa Ibrahim bin al-Malik al-Ashtar kurudi Kufa mara moja. Alirudi katika siku tatu.

Wakati sasa ulikuwa umeshawadia kwa kutoa adhabu ya maadui wa dhuria ya Mtume na kuwakamata kwao kukaanza kufanyika.

Wakati kundi la kwanza la watu mia tano waliokamatwa kuhusiana na jambo hili walipoletwa kwa al-Mukhtar, yeye alitangaza kwamba wale waliokuwepo Karbala katika wakati wa kuuliwa Husein ni lazima waonyeshwe kwake kwani hatawaacha wabakie hai. Wengine wote waliachiliwa huru baada ya kuchukua kutoka kwao kiapo cha utiifu.7

Mnamo mwezi 24 ya Dhul Hijja mwaka wa 66 A.H. ilitangazwa kwamba mtu yeyote yule atakayefunga mlango wa nyumba yake na akabakia ndani yake angepata usalama labda kama alishiriki katika mauaji ya dhuriya wa Mtume.8

Kwa vile wauaji wa Husein walikuwa pia wamejificha pia majumbani mwao, Abu Amra Kaysaan, kiongozi wa Shurta (polisi), ambaye ndiye aliyekuwa anawatambua wote, aliamriwa aende na wafanyakazi elfu moja na kuzibomoa nyumba za wale wote ambao walishiriki katika matendo ya kinyama hapo Karbala. Nyumba nyingi zilibomolewa na maadui wengi wa Ahlul Bait waliuawa.

Maarufu miongoni mwa wauaji wa Husein ambao waliuawa walikuwa ni: Shimr bin Dhi al-Jawshan, Abdallah bin Asad, al-Malik bin Nasr al-Badii, Haml bin Maalik al-Muharabii, Ziyad bin Maalik, Imraan bin Khalid, Abd al-Rahman bin Abi Khushkara al-Bajali, Abd al-Rahman bin Qays al- Khawlaani, Abdallah bin Salkhab, Abdul-Rahman ibn Salkhab, Abdallah bin Wahb, Uthman ibn Khalid al-Juhani, Bushr ibn Saat, Qubayz Khawtii, Yazid al-Asbahii, Umar bin Sa’d, Hukaym bin Tufayl al-Taai, Zayd bin Rifaad al-Juhani, Harmala bin Kaahil al-Asad, Amr bin Sabiih al-Sa‘di na Qays bin al-Ash’ath.

Baada ya kukamilisha kazi yake hapo Kufa, al-Mukhtar alimpeleka Ibrahim al-Malik al-Ashtar tena kwenda kupigana na Ibn Ziyad. Baada ya mapigano makali sana jeshi la Syria lilishindwa katika sehemu iitwayo Khaazir na Ubaydulah bin Ziyad aliuawa. Husein bin Numayr al-Sakuni na Sharhabiil bin Dhi al-Kalaa pia waliuawa.

Ibrahimn alikata kichwa cha Ubaydullah bin Ziyad, na akakipeleka kwa al-Mukhtar ambaye alikitoa kwa Muhammad bin Hanafiyya.9

Ibrahim kisha aliitiisha Mosul na nchi zinazoizunguka kuwa chini yake. Kisha akaenda kukaa Nisibin na al- Mukhtar akabaki peke yake hapo al-Kufa.

Uadui ulikuwa umekwishaibuka kati ya al-Mukhtar na Abdullah bin Zubeir ambaye alikuwa bado anaimiliki Basra nchini Iraq, na alikuwa amembadilisha gavana wa Basra kwa kumweka ndugu yake mwenyewe aliyeitwa Mus’ab ibn Zubeir.

Wauaji wa Husein ambao walifanikiwa kukikwepa kifo mikononi mwa al-Mukhtar kama vile Shabath bin Ribi’i, Muhammad bin Ash’ath, Murra bin Munqidh al-Abdi, Sinan bin Anas na Abdallah bin Urwa al-Khath’ami walikimbia kutoka Kufa na wakaenda moja kwa moja mpaka kwa Abdallah bin Zubeir huko Barsra.10

Walimshinikiza kupigana na al- Mukhtar. Pole pole kiasi cha wakazi 10,000 wa Kufa waliondoka na kwen- da Basra, na wakiongozwa na Muhammad bin al-Ash’ath walimhakikishia Ibn Zubeir kupata ushindi dhidi ya al-Mukhtar.

Wakati huo huo, Abdallah bin Zubeir alikuwa amemtupa gerezani Muhammad bin Hanafiyya, pamoja na watu wake wanaomtegemea na wale wenyeji wa Kufa ambao walikuwa Makkah, akionyesha mwisho wa wakati ambao ndani yake walitakiwa watoe kiapo cha utii kwake, na kushindwa kufanya hivyo angewachoma moto wakiwa hai.
Muhammad bin al-Hanafiyya alimwarifu al-Mukhtar kuhusu balaa hili na al-Mukhtar alipeleka jeshi kutoka Kufa ambalo liliwaweka huru mateka na lilikuwa tayari pia kumuua Abdallah bin Zubeir. Muhammad bin al-Hanafiyya alilikataza hili kwani ilikuwa sawa na kuinajisi Ka’abah.

Mwishowe, labda kabisa kwa kukubaliana na matakwa ya ndugu yake mkubwa, Mus’ab bin Zubeir aliivamia Kufa akiliongoza jeshi kubwa sana. Ibrahim alikuwa Nisibin, na al-Mukhtar peke yake alipambana naye. Alipigana kishujaa sana kwa siku kadhaa akiwapoteza baadhi ya watu muhimu katika jeshi lake kama vile Ahmar bin Shumayt na Abdallah bin Kaamil. Mmoja wa maadui wakubwa wa dhuriya ya Mtume, Muhammad bin al-Ash’ath, aliuawa pia katika vita hivi.11

Mwishowe wakati wenzi wake wote waaminifu walipokwisha kuuawa na watu wakatupwa katika hali ya kuchanganyikiwa, al-Mukhtar alijikuta amezingirwa katika ngome. Kisha al-Mukhtar alitoka nje akiwa na wasaidizi wake wachache waliobakia na akapigana vita vyake vya mwisho kwa ushujaa mkubwa na alikufa akiwa katika kupigana siku ya mwezi 14 Ramadhani mwaka wa 67 A.H, akiwa na umri wa miaka 67. 12

Uadui na usugu wa adui zake ulishuka kwenye viwango vya chini kabisa vya ubaya wakati mke wa al-Mukhtar alipouawa hadharani kwa kukataa kwake kumlaani mume wake marehemu.13

 • 1. Tabari, juz. 7, uk. 59.
 • 2. Tabari, juz. 7, uk. 62.
 • 3. Tabari, juz. 7, uk. 63.
 • 4. Tabari, juz. 7, uk. 64.
 • 5. Tabari, juz. 7, uk. 80
 • 6. Tabari, juz. 7, uk. 100.
 • 7. Tabari, juz. 7, uk. 121.
 • 8. Tabari, juz. 7, uk. 121.
 • 9. Al-Akhbar al-Tiwal, uk. 288.
 • 10. Tabari, juz. 7, uk. 124, 128-130, 146.
 • 11. Tabari, juz. 7, uk. 151.
 • 12. Tabari, juz. 7, uk. 155, 161.
 • 13. Tabari, juz. 7, uk. 158.