Table of Contents

Sura Ya 5: Kuzaliwa Kwa Husein Na Maisha Yake Ya Utotoni

Mtoto wa pili wa Ali bin Talib na Fatima, binti ya Mtume alizaliwa mwezi wa 5 Shabaan mwaka wa 3 A.H., na aliitwa kwa jina la Husein na Mtume.

Baba yake alijibainisha mwenyewe kama askari asiyeshindika wa Kiislam, aliyekuwa tayari kuzichukua zile kazi zenye hatari sana katika kuulinda Uislamu. Mama yake alionyesha mfano wa tabia mzuri sana kwa wanawake na akaongezea nguvu mafundisho ya baba yake kwao kwa kuwapa maonyesho ya vitendo.

Husein na kaka yake mkubwa walikabidhiwa wote kwenye malezi ya mapenzi na upendo mkubwa wa mwalimu mtukufu kama huyu mjumbe mkuu wa Mwenyezi Mungu, ambaye lengo lake pekee lilikuwa ni kuzitakasa roho.1 Watoto waliokuzwa katika hali na mazingira ya kimungu mara walipata ubora wa kupigiwa mfano wa tabia na ukamilifu wa maadili.

Tabia nzuri za wajukuu wake ziliwafanya kuwa vipenzi wakuzidi mno kwa Mtume. Aliwataka watu wengine kushiriki katika upendo wake huu na akatangaza, akasema: “Mtu yeyote yule awapendaye hawa, huyo amenipenda mimi na yeyote ambaye atawafanyia uadui huyo ni adui yangu.2

Alimwomba Mwenyezi Mungu kuwa shahidi kwamba yeye aliwapenda sana sana wote wawili.3 Husein alijua, hata hivyo, kwamba Mtume alijizatiti na kujitoa kwa ajili ya mafanikio na utukufu wa Uislamu, na kwamba asingesita kumtoa mhanga kwa ajili ya hilo, kama uhifadhi wa Uislamu ungetaka hivyo.

Mtume alitoa changamoto kwa Wakristo wa Najran nchini Yemen kwa ajili ya shindano la kiroho (mubahila) ambalo ndani yake washindani walikuwa waombe laana ya Mwenyezi Mungu ianguke juu ya kundi amba- lo madai yao yalikuwa ya uwongo. Mtume aliwataka waje na watoto wao, wanawake wao na nafsi zao wenyewe. Yeye (mtume) alimchukua pamoja naye Hasan, Husein, Fatima na Ali.
Wakristo walifadhaishwa sana kwa kutokea kwa kundi la Mtume kiasi kwamba walikataa kushindana na wakalipa jizya (kodi) kwake.4

Tukio hili limepata kutajwa katika Qur’ani,5 na miongoni mwa malengo lililoyatumikia ilikuwa kuwafunza watu wa Nyumba ya Mtume kubeba majukumu mazito, na kuwaonyesha watu kwamba ni wao tu pekee wangeweza kutegemewa katika kuulinda Uislamu, na kwamba Uislamu ulimtegemea kila mtu – mwanamume, mwanamke na mtoto – kutoa mchango wake kwa ajili ya usalama wake (Uislamu).

Mtume alieleza wafuasi wake mara nyingi sana kuwafuata Ahlul Bayt wake. Wakati fulani aliwaambia (watu) kwamba anaacha nyuma yake (anawaachia) vitu viwili vizito mno: Kitabu cha Mungu (Qur’ani) na watu wa nyumbani kwake na kivifuata viwili hivyo kungewazuia watu kupotea. Alisisitiza kwamba Hasan na Husein walikuwa ndio viongozi wa vijana wa peponi.

Alibainisha umuhimu wa maana sana wa Husein wakati aliposema “Kama vile maisha ya Husein yanavyotokana na mimi ndivyo uhai wangu unavyotokana na Husein,”6 akiwa na maana yake kwamba ujumbe wake ungehuishwa na Hussein.

Husein alikuwa hajafikia umri wa miaka 7 wakati Mtume alipofariki dunia katika mwezi wa Rabiul- Awwal, mwaka wa 11 A.H.

  • 1. Qur’an; 2; 129 na 151
  • 2. Ibn Maja, Sunan, Juz. 1 uk. 33
  • 3. Sahih Muslim, Juz. 2 uk. 282
  • 4. Irshad, Kur. 116-119
  • 5. Qur’an; 3:131
  • 6. Ibn Maja, Sunan, Juz. 1 uk. 33