Table of Contents

Sura Ya 6: Awamu Ya Pili Ya Maisha Ya Husein

Tangu Kifo Cha Mtume Mpaka Kuuawa Kwa Ali. ( 11 A.H. Mpaka 40 A.H.)

Kifo cha Mtume kiliwaingiza watu wa familia yake kwenye maombolezo makubwa. Miongoni mwa wale ambao walihuzunika sana hasa walikuwa ni binti yake Fatima na wajukuu zake, Hasan na Husein. Huzuni ya Fatima ilikuwa hailiwaziki kabisa kiasi kwamba alilia kilio cha kumwombeleza baba yake mchana na usiku bila kupumzika kiasi kwamba watu waliona haiwezikani kula chakula chao au kuweza kupumzika katika mji wa Madina.

Baada ya malalamiko mengi ya kukaririwa yaliyofanywa kwake kuhusu namna gani maombolezo yake yalivyovuruga maisha ya kawaida mjini Madina, alikubali kwenda kwenye uwanja wa makaburi ya Al-Baqi ili aweze hapo kujishughulisha na uombolezaji wake bila kuzuiliwa juu ya pengo lake lisilozibika.

Ama kuhusu wajukuu zake, Hasan na Husein kifo cha Mtume kilileta mateso yasiyoelezeka. Alitoa upendo mwingi sana juu yao na akawalea kwa uangalifu mkubwa na mapenzi katika njia za Uislamu.

Alichukua hatua za kuwaonyesha wafuasi wake kulikuwa na umuhimu kiasi gani kwao katika kuwapenda wajuu zake, na kuwa kuzembea kidogo kabisa katika jambo hili kulimuudhi sana Mtume kutokana na kuwa katika kitovu cha mambo ya Uislamu. (Vijana waliona kwamba watu wa nyumba ya Mtume, ahlul bayt wake walikuwa wamenyimwa madaraka yote, na kwa nje walikuwa wakionekena hawana mamlaka).

Husein lazima atakuwa ameona kwamba baba yake Ali bin Abi Talib alikuwa amejitoa kutoka mambo ya kidunia ili kujizamisha zaidi tu katika kuikusanya Qur’ani katika utaratibu wa uteremsho (wahyi) wake. Somo la kwamba hata katika hali na mazingira yaliyokuwa magumu kiasi gani watu wa nyumba ya Mtume hawakuweza kuacha kuutumikia Uislam, na kwamba kama Qur’ani ilivyokuwa iwe pamoja nao wakati wote, ni lazima wai- hifadhi na kuilinda, lisingeweza kumpotea Husein.

Katika saa hii ya mtihani, Husein aliona kwamba baadhi ya marafiki kama vile ami yake Mtume, Abbas bin Abdul-Mutallib na washirika wasio waaminifu kama Abu Sufyan bin Harb, mkuu (chifu) wa ukoo wa Bani Umayyah, walimshauri Ali kujaribu kuchukua udhibiti wa dola ya Kiislamu yeye mwenyewe.

Abu Sufyan alimchochea Ali, akisema kwamba ilikuwa siyo sawa kwamba moja ya familia zilizo za chini mno ichukue udhibiti juu yake, na kwamba angempatia askari wa farasi kumsaidia. Ali alimpa jibu la mkato akimwambia, “Naapa kwa jina la Mwenyezi Mungu, wewe bado ni adui wa Uislamu.”1

Hii ilidhihirisha jinsi Ali alivyokuwa imara katika kuyaweka maslahi ya jumla ya jamii mbele zaidi kuliko maslahi yake mwenyewe, na pia kutokuaminika kwa uingiaji wa Abu Sufyan katika Uislamu, na ikawa kama onyo dhidi ya unafiki ambao kwa sura ya marafiki wa uwongo na maadui wenye kudhuru, ni wenye kuleta madhara makubwa zaidi kuliko wawezavyo kufanya maadui wenye kujitangaza kwa dhahiri.

Miezi michache baada ya kifo cha Mtume, Husein alimpoteza mama yake pia. Kutoka kwenye umri mdogo wa miaka saba mpaka kufikia umri wa ujanadume wa miaka thelathini na nane, Husein aliishi chini ya uongozi wa baba yake aliyejaaliwa kipaji, mwenye elimu, mwenye busara na mwadilifu, na lazima atakuwa amepata picha ya ushirikiano huu mpaka mwisho wa siku zake.

Lazima atakuwa amefahamu kwamba, wakati alipohitajika, baba yake bila ya kinyongo aliyatatua matatizo yaliyowakabili Waislamu, na alitoa ushauri wake kuhusu mipango muhimu na safari zenye nia maalum bila kusita, na ingawaje alisikitishwa sana na uzimwaji wa madai yake juu ya ukhalifa.

Fursa ilijitokeza yenyewe kwa Ali kupata kusimikwa kuwa khalifa wakati wajumbe wote wa baraza la ushauri walioteuliwa na Umar wakati wa kifo chake kuchagua mrithi wake walipokubali kumteua Ali kwa nafasi hiyo iwapo kwa nyongeza ya kufuata sheria za Qur’ani, hadithi na mwendo (sunna) wa Mtume, atakubali pia kufuata hadithi na mienendo ya watawala wawili waliomtangulia yeye. Ali alikataa kukubaliana na ahadi hizi mbili za mwisho na akatupilia mbali ahadi hiyo ya ukhalifa.

Kutokana na mwenendo wa baba yake, Husein alijifunza utumiaji wa kivitendo wa somo muhimu ambalo juu ya hilo, hapo baadaye tabia na mwenendo wake mwenyewe ulitegemea. Aliona kwamba mfumo wa sheria za Kiislam na matendo ya watawala wa Kiislam kwa dhahiri kabisa yalikuwa mambo mawili tofauti na kwamba njia za watawala hazikuweza kutafsiriwa kuwa, au kulinganishwa na mwenendo chini ya mfumo wa sheria ya Uislamu.

Kwa kweli ulikuwa mfumo huu ambao ulikuwa uwafunge watawala wa Kiislam kwa daraja lile lile la ulazimishaji kama ulivyowafunga Waislam wote kwa ujumla. Na wakati mtawala yeyote anapofuata njia zilizo tofauti na kanuni za Uislamu, ilikuwa ni jukumu la Waislam kuilinda dini (imani) na kutoona muhanga wowote kwa ajili ya lengo hilo kuwa na thamani sana.

Katika mwaka wa 31A.H. mabinti wa Yazdigard Mfalme wa Uajemi (Iran), waliletwa Madina kama wafungwa baada ya kuuawa kwake. Ali na Husein waliwaokoa kutokana na makundi ya wadhalilishaji, na Husein akamuoa mmoja wao, aliyeitwa Shahrbanawayh.

Katika kukaribia mwisho wa miaka ya utawala wa Uthman, khalifa wa tatu, watu walianza kujihisi kutoridhika kabisa na utawala wake, na hata wakaishia kwenye kufanya matendo ya vurugu. Ali aliingilia kati mara nyingi sana ili kuleta amani na akafanya baadhi ya malalamiko kuweza kurekebishwa. Aliwashauri wafanyaghasia kutawanyika na warudi walikotoka.2 Lakini Marwan, mkwe na katibu wa khalifa alionyesha ukatili sana kiasi kwamba jitihada za Ali katika kuleta amani zilishindwa, na waasi wakayazingira makazi ya khalifa ambaye maombi yake ya mdomo ya kupatiwa maji yalisikiwa na Ali.

Ali aliwaagiza wanawe, Hasan na Husein, kupeleka maji kwa Uthman katika hali ya hatari kubwa sana kwa maisha yao binafsi. Khalifa huyo hata hivyo, aliuawa na kundi lililokuwa na vurugu nyingi.

Inastaajabisha kwamba ingawaje khalifa alibakia kushambuliwa hapo Madina kwa siku 49,3 hakuna hata mkazi mmoja wa mji huo alijitokeza kuja kumwokoa, na kwamba alibakia bila kuzikwa kwa muda wa siku tatu na kwamba hatimaye mabaki ya mwili wake hayakupata nafasi katika eneo la makaburi ya Waislam.4

Baada ya ghasia kutulia Waislam waliamua kumweka Ali kama khalifa wao. Katika matukio yote ya nyuma ya uchaguzi wa khalifa, Ali alikuwa amehoji kwa nguvu sana kuhusu ubora wa madai yake juu kazi hiyo, lakini sasa hakuwa tayari kabisa kuukubali (ukhalifa), kwani aliona kwamba katika miaka iliyoingilia kati, serikali ya Kiislam ilichukua sura na ari ya falme za kikoo, ambayo ilikuwa na urahisi usio rasmi usiyopatana na moyo wa kupenda usawa wa Uislamu.

Ali asingeweza kuvumilia uozo uliokuwepo katika utawala uendelee, na alijua kwamba katika kujaribu kuusimamisha angezusha wimbi la upinzani usiodhibitika ambao ungechukua muda mrefu kuudhibiti, na kwamba kwa wakati huohuo angejiweka kwenye hali ya kuitwa mtawala asiyefaa. Hata hivyo Waislamu walisisitiza kwamba aukubali tu ukhalifa, na Ali kwa shingo upande sana alikubali kufanya hivyo. Katika mwezi wa Dhil-Hijja mwaka wa 35 A.H. Waislam walitoa kiapo cha utii kwa Ali kama khalifa wao.

Baada ya Ali kuchukua madaraka, wasiwasi wake uligeuka kuwa kweli. Watu hawakuwa na mwelekeo wa kutekeleza maelekezo (maagizo) yake. Baadhi ya Waislam mashuhuri kama vile Usamah bin Zayd, Hasan bin Thabit, Abdallah bin Umar na Sa‘d bin Abi Waqqas walijizuia kutoka kiapo cha utii kwake. Ali, hata hivyo hakuchukua hatua yoyote dhidi yao kwa vile katika Uislamu “hakuna kulazimishana katika dini.”

Kushikilia Syria kwa Mu’awiyah kulitiwa nguvu na kile kipindi kirefu cha ugavana wake wa nchi hiyo, na Ali alishauriwa ambakishe yeye pamoja na maofisa wote walioteuliwa na Uthman katika nafasi zao za kazi, kama hatua ya uangalifu mpaka watakapokuwa wamejinyenyekesha wenyewe kwenye udhibiti wake.

Ali alikataa kukikubali kipande hiki cha ushauri ambacho kingekuwa na maana ya kuunga mkono udhalimu na uharibifu wa watendaji hawa, na kwa kweli ni kama kushiriki kwenye maovu haya. Ali alimwandikia Mu’awiyah barua akimwambia alivyoikubali kwa shingo upande kazi ya ukhalifa na akamtaka apate viapo vya utii kutoka kwa watu wa nchi yake kwa ajili ya khalifa mpya.

Pia alimtaka Mu’awiyah aje yeye mwenyewe pamoja na ujumbe wa watu wa Syria.5 Mu’awiyah hakutekeleza lolote katika maelekezo haya, na uadui wa toka zamani ulimshawishi kuzua shitaka la uwongo la mauaji ya Uthman dhidi ya Ali dhidi ya yule ambaye hata yeye pia alimwasi. Mwanazuoni mkubwa wa Kisunni, Ibn Hajr amemnukuu Marwan bin al-Hakam akiwa amekiri kwamba hakuna aliyekuwa na msaada mkubwa zaidi kwa Uthman kuliko Ali, na kama alivyokuwa amesema kwamba matumizi ya lugha chafu dhidi ya Ali yalifanywa kwa sababu, kwani bila kufanya hivyo Bani Umayyah wasingeweza kusimamisha mamlaka yao.6

Mu’awiyah alichukua hatua za aina mbalimbali kuwachochea watu wa Syria dhidi ya Ali. Mikutano iliyohudhuriwa na watu wengi ilifanyiwa mara kwa mara katika msikiti wa swala za jamaa wa Damascus kuomboleza mauaji ya Uthman ambamo shati lake lililolowa damu na vidole vilivyokatwa vya mke wa khalifa (Uthman) vilionyeshwa kwa makundi makubwa ya watu ambao walipandisha sauti za maombolezo, na katika mfadhaiko huu wa huzuni walishawishiwa kulipizia kisasi mauaji yake.7

Wakati maendeleo haya kiuchochezi yalipokuwa yanafanyika nchini Syria, Talha na al-Zubeir waliweka upinzani mkubwa kwa Ali, wakiungwa mkono na Aisha, mjane wa Mtume na binti ya Abu Bakr, khalifa wa kwanza.

Ali alikwishakuwa mtu mzima na kwa kipindi kirefu aliishi maisha ya faragha. Hata hivyo, alijiandaa kwenda vitani na kupigana dhidi ya Aisha kuzilinda sheria na kanuni za Uislamu na za haki kwa nguvu zake za kawaida kwani jukumu la ulinzi wao ulikuwa hasa juu yake yeye. Kampeni hii ilikomea katika kutokea vita ya Ngamia, kwani Aisha aliliongoza jeshi lake kutoka kwenye kiti chake juu ya ngamia, na kushindwa kwake kabisa mnamo mwezi 10 Rabiul Thaaniya mwaka wa 36 A.H.

Katika wakati wa ushindi wake Ali alimtendea Aisha kwa uungwana na ukarimu usio na kifani na alimpeleka Madina kwa heshima kubwa akisindikizwa na askari ambao wote walikuwa wanawake waliojifanya kama wanaume.

Huko Syria vurugu na uchochezi wa ghasia viliendelea bila kupungua nguvu. Maombolezo kwa ajili ya Uthman yaliendelea kufanywa kwa mwaka mzima kamili na watu wengi wa Syria walichukua nadhiri ya kujiepusha na raha za kidunia mpaka wawe wamewaua wale wote ambao walimuua Uthman, hivyo Mu’awiyah akafanikiwa kuiamsha nchi yake dhidi ya Ali mpaka mwishowe vita vya Siffin vilikuja kupiganwa kati yake na Ali.

Ni lazima itajwe kwamba mpaka wakati wa mwisho kabisa kabla ya kuanza kwa vita Ali alijitahidi kwa kusisitiza kuwashauri wapinzani wake kutenda kwa busara na uadilifui na kutafuta kuungana na wanaodhaniwa kuwa ni maadui zao. Hata hivyo ushauri wake wa usuluhishi ulikataliwa na damu ya Waislam ikamwagika kwa wingi sana.

Kama kawaida, Ali aliliagiza jeshi lake lisianze mashambulizi, wakiliachia jeshi la maadui kuanza vita. Pia alikataza ufukuziaji wa adui aliyeshindwa, kumuua adui aliyejeruhiwa, kuukatakata mwili wa mtu aliyekwishakufa, alikataza kulazimisha kuingia katika hema bila ya kuruhusiwa, kupora mali ya adui na kusababisha madhara kwa wanawake hata katika hali ya kuchokozwa.

Wakati wa vita, majeshi ya Mu’awiyah yalitwaa udhibiti wa mto Furati (Euphrates) na yakasimamisha hudumu ya ugavi maji kwa jeshi la Ali ambalo liligeukia katika kutumia nguvu na hatimaye wakapata tena udhibiti juu ya mto huo. Ali alikataa kulipiza kisasi kwa kusimamisha huduma za kulipatia maji jeshi la Mu’awiyah, na akajishusha mwenyewe kufikia kiwango cha maadui zake.

Ali alipata uchungu sana kuona damu nyingi ya waislamu inamwagika katika vita vya Siffin, na akamwambia Mu’awiyah kwamba kwa vile vita halisi ilikuwa kati yao wawili, ingekuwa ni unyofu juu yao (Ali na Mu’awiyah) kuliamulia jambo hili kwa kukutana wao wawili katika pambano la watu wawili tu. Mu’awiyah hakutoa jibu, akiogopa kwamba asingeweza kunusurika katika pambano kama hilo. Kwa hiyo, yeye alishikilia tu kuwatoa muhanga wengine kwa malengo yake binafsi.

Mu’awiyah, alitembelea uwanja wa vita kwa nadra, wakati Ali alikuwa akionekana kila mahali ndani yake akiliongoza jeshi lake, wakati mwingine akilielekeza na zaidi sana yeye mwenyewe akiwa katikati ya vita vyenyewe. Alitamani kupata shahada na akaapa kwamba mapigo elfu moja ya upanga kwenye kichwa cha mtu yalikuwa yanastahimilika zaidi kuliko kifo cha kuteseka muda mrefu kitandani mwake mtu.8

Mwenendo wake sasa ulifuata mkondo uleule wa kutokusita kujihatarishia kifo kwa ajili ya Uislamu kama ulivyofuatilia hapo mapema katika maisha yake wakati alipolala katika kitanda cha Mtume usiku, Mtume alipotorokea Madina.

Husein na ndugu zake walihusika kikamilifu katika vita hivyo na wakamtumikia baba yao kwa uimara mkubwa katika nyakati za hatari kubwa kabisa.

Wasingeweza kutenda kinyume kabisa kwani walikuwa watoto wa Ali ambaye alikuwa amemwambia Husein wakati wa vita hivi kwamba ilikukwa haina tofauti muhimu kama ni kifo kimwangukie au ni yeye akiangukie kifo.9

Siku moja wakati vita ambapo vilipokuwa vimepamba moto, Ali alionekana akiliangalia jua ili kuhakikisha kama wakati wa swala ya mchana umekwishaingia. Alipoulizwa kama huo ulikuwa ni wakati wa kuswali katikati kabisa ya vita, Ali alijibu, “Ni kitu gani tunachokipigania basi?” Alifundisha kwamba swala ni lazima zisimamishwe katika wakati wake makhsusi iwe inamiminika mishale au moto.

Ili kuifupisha vita, siku moja Ali alifanya shambulio kubwa kabisa juu ya maadui, akiendeleza mashambulizi hadi usiku mzima uliofuatia. Wakati kulipopambazuka, watu wa Syria walikuwa wameshindwa vibaya sana na idadi yao kubwa walikuwa wameuawa na wengine kujeruhiwa.

Ilionekana kwamba wasingeweza kukwepa kushindwa kwa muda mrefu. Amr bin Aas, mshauri wa Mu’awiyah, alikimbilia kwenye hila ya kunyanyua nakala za Qur’ani Tukufu juu zikiwa zimechomekwa kwenye ncha za mikuki na kupandisha sauti zao juu wakidai kwamba tofauti kati ya pande husika zirejeshwe kwenye Kitabu cha Mwenyezi Mungu (Qur’ani) kwa ajili ya uamuzi.

Ali alikwisha ng’amua mtego wa hila hii na akawashauri wafuasi wake dhidi ya kuangukia katika mtego huu uliowekwa na watu wale ambao kamwe hawakuamini Uislamu wala hawakuwa na heshima yoyote juu ya Qur’ani. Aliwakumbusha pia kwamba ombi kama hilo alilokuwa amelitoa yeye kabla ya kuanza kwa vita lilikuwa limekataliwa.

Lakini watu wengi wa jeshi la Ali walikuwa wamepotoka katika kukataa maagizo yake na wakageuka dhidi yake, na hata kumtishia maisha yake. Wakati utovu wa nidhamu kamili ulipozidi ndani ya jeshi lake, Ali alisitisha mapigano. Masuala kati ya pande mbili hizi zenye kushindana yalipelekwa kwa wasuluhishi wawili, Amr bin al-Aas na Abu Musa al-Ash’ari.

Amr bin al-Aas alimwakilisha Mu’awiyah na watu wa Syria na Abu Musa al-Ash’ari alilazimishwa juu ya Ali kuwa kama mwakilishi wake, kinyume kabisa na alivyotaka mwenyewe, na akawa kama mwakilishi wa wakazi wa Kufa. Tabia ya Abu Musa huko nyuma ilikuwa imeonyesha mwelekeo wake usiopendeza kumhusu Ali ambaye alikubali kuchaguliwa kwake kwa ajili tu ya kukwepesha umwagaji wa damu ndani ya kundi lake.

Makundi hayo mawili yalikubaliana kutii uamuzi wa Mwenyezi Mungu na Kitabu Chake na sio kitu kingine kile. Wasuluhishi walikuwa chini ya masharti ya kuiweka Qur’ani wakati wote katika mazingatio na kuifanyia kazi, na kama hawakupata mwongozo kutoka humo, ilikuwa watende kwa mujibu wa matendo na kanuni za Mtume zisizotiliwa shaka. Ali alichukua tahadhari kuwasisitizia kwamba hawakupewa mamlaka yoyote yale ya kuamua kwa kulingana na fikra zao binafsi. Mkataba huu ulifanyika mwezi 13 Safar, 37 A.H.

Makubaliano haya yalikuwa hata bado hayajaanza kutekelezwa wakati fitna mpya ilipoinua kichwa chake kibaya katika sura ya makhariji ambao walinyanyua ndani ya jeshi la Ali ule wito wa makelele kwamba hakuna hukumu isipokuwa ya Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo, wao waliuchukulia ule uteuzi wa hivi karibuni wa wasuluhishi kuwa ni wenye makosa na wakamshinikiza Ali kupigana na Mu’awiyah na wakaahidi kumsaidia. Ali alikataa kuwakubalia akisema kwamba Qur’ani inaagiza kwamba neno lililowekewa ahadi lazima liheshimiwe. Ma-Khariji wakageuka kuwa wasaliti kutoka kwenye Uislamu na wakaunda kundi lao tofauti.

Wasuluhishi wakapuuza kabisa masharti yote ya chombo cha usuhulishi na wakadharau sheria za Qur’ani. Amr bin al-Aas alikuwa bingwa mkubwa katika hila na akamfanya Abu Musa al-Ash’ar kuwa mjinga kabisa. Alimmvutia Abu Musa al-Ash’ari kwa tabia yake ya kiheshima kwamba kwa kweli yeye alimheshimu sana Abu Musa kuwa ni mkubwa na mbora kwake, na kwa hiari kabisa akamkubalia kutangulia.
Kati yao wenyewe, walitokea kuamua kuwatangaza wote wawili Mu’awiyah na Ali kuwa hawafia kushika wadhifa wa ukhalifa na (wakaamua) kuwapa Waislam haki ya kuchagua khalifa mwingine.

Wakati muda ulioteuliwa wa kutoa tangazo la uamuzi wa wasuluhishi ulipofika, Abu Musa al al-Ash’ari aliombwa na Amr bin al-Aas kutangaza uamuzi huo, ambao akautangaza kama walivyokubaliana kati yake na Amr bin al-Aas.

Kisha Amr bin al- Aas alisimama kusema kwamba kwa vile Abu Musa anamwakilisha Ali, alikubaliana na uamuzi wake wa kumuuzulu Ali kutoka kwenye ukhalifa. Akaongoza kwamba akiwa kama mwakilishi wa Mu’awiyah, yeye anausimika ukhalifa juu yake.

Uamuzi huu usio wa udanganyifu ulisababisha vurugu na miongoni mwa wale waliokuwepo, na wasuluhishi wakafanyiwa fujo. Uamuzi ukakataliwa na pande zote. Ushindani kati ya pande zote ukabakia bila kufumbuliwa. Tukio hili liliimarisha ile rabsha ya mgawanyiko katika safu za kundi la Ali na liliwapa Makhariji muda wa kujiweka sawa ili kuweza kumpinga Ali kwa upinzani mkali katika vita vya Nahrawan ambayo vilifuata.

Hata baada ya vita vya Nahrawan ambamo Makhawarij walipata kipigo na kushindwa kabisa, bado utovu wa nidhamu, vurugu na uchochezi wa maasi ulikuwa bado haujang’olewa kabisa ndani ya jeshi la Ali. Alikuwa kwa kweli katika masaibu yasiyopendeka. Alikuwa na mzigo wa wafuasi wasio waaminifu waliogawanywa na kutoelewana na mfarakano. Makhawarij ambao walikuwa hawakupigana au walitoroka kule Nahrawan walichochea hisia za kufanya uasi dhidi yake miongoni kwa watu. Mu’awiyah aliitumia nafasi hiyo ya kukosekana umoja uliokuwepo Kufa.

Aliyatumia majeshi yake kuchochea ghasia katika nchi za Kiislam na alikimbilia matendo kama hayo kama ya kuwaondolea wapinzani, kama vile Malik al- Ashtar,10 kwa kuwafanya watiliwe sumu au kwa njia nyingine za kudanganyifu, kama katika suala la Muhammad bin Abu Bakr, ambaye alikuwa amelelewa na Ali na alikuwa mmoja wa wafuasi wake watiifu mno.

Alipelekwa na Ali kuwa gavana wa Misri na kwa ombi la Mu’awiyah, Amr bin al-Aas aliongoza jeshi dhidi yake kwa ushirikiano kabambe na kikosi cha wahaini wa Kimisri11. Hili liliishia katika kushindwa kwa Muhammad bin Abu Bakr na kuuawa kwake. Mabaki ya mwili wake kisha yalichomwa moto.12

Alipoona kwamba ilikuwa vigumu kumshinda Ali katika vita vya viwanja vya wazi, Mu’awiyah alitumia mbinu vita vya msituni kama njia ifaayo ya kuiweka dola ya Kiislam katika hali ya hofu, fujo na ghasia wakati wote.

Idadi ya mashambulizi kama hayo ya ghafla na kukimbia yalifanywa na wafuasi wa Mu’awiyah, na baadhi walizuiliwa kwa nguvu na kurudishwa nyuma. Shambulizi la kikatili sana la namna hiyo liliongozwa na Busr bin Abi Artat dhidi ya Hijaz, tukio ambamo alilazimisha viapo vyao vya utii kwa Mu’awiyah kutoka kwa wakazi wa Makkah na Madina, na akawachinja watoto wawili wa kiume wa Ubaydullah bin Abbas nchini Yemen.

Ali alikuwa anajishughulisha katika kujiandaa kupambana na tishio hili, lakini katika wakati ule ule Ibn Muljam al-Muradi alimpiga dhoruba kichwani kwa upanga uliotiwa sumu wakati akiwa yuko katika kusujudu mbele ya Mwenyezi Mungu ndani ya msikiti wakati wa swala ya asubuhi (alfajiri) ya siku ya mwezi 19 Ramadhani mwaka wa 40 A.H. Siku tatu baadaye, Ali akawa hayupo tena katika ulimwengu huu (akafariki dunia).

 • 1. Irshad, uk. 136, Tabari, Juz.1, uk. 1827-8
 • 2. Tabari, Juz. 1 uk. 2969 na 2971
 • 3. Tabari, Juz.1 uk. 3009
 • 4. Tabari, Juz.1 uk. 3008
 • 5. Nahjul-Balaghah, Juz. 2, uk. 140
 • 6. Ibn Hajr, al-Sawaaiq, uk. 33
 • 7. Tabari, Juz. 1, uk. 3091
 • 8. Irshad, uk. 177
 • 9. Tabari, Juz. 1, uk. 3294
 • 10. Tabari, Juz. 1, uk. 3401
 • 11. Tabari, Juz. 1, uk. 3404
 • 12. Tabari, Juz. 1, uk.3406