Table of Contents

Sura Ya 7: Uwezo Wa Bani Umayyah Na Namna Zake Za Utaratibu Wa Kisiasa

Bani Umayyah walilazimika kuukubali Uislamu ili kuyaokoa maisha yao, na siyo kwa imani yoyote ile kuhusu ubora wa ujumbe wake. Matokeo yake waliendelea kuendekeza, katika nyoyo zao hisia za chuki na uadui juu ya dini (imani) yao mpya waliyoipata, na walisubiri kwa shauku kubwa kuipata fursa ya kuuangamiza mwenendo wake, kwani waliona kwamba ilikuwa nje ya uwezo wao kufanya jaribio la wazi la maangamizi yake ya mara moja.

Walifikiria mpango unaofaa sana wa kiutendaji kuziharibu na kuzichafua tabia na sifa pambanuzi za Uislamu ambazo zilivunjilia mbali uwezo wao. Ilikuwa ni kutumia kivuli cha Uislamu wenyewe kuidhuru imani yake, na kuufagilia njia ufufuaji upya wa maadili na fursa zilizokuwepo kabla ya kudhihiri Uislamu.

Kwa ufupi, walikuwa wanafiki. Madhara kidogo sana yaliyopatikana au kutegemewa kuwapata Waislam yalileta furaha ya kiuovu iliyofichika kwa Bani Umayyah.

Hivyo katika vita vya Uhud, pale watu wote walipokimbia isipokuwa Waislamu wachache waaminifu, Abu Sufyan alionyesha furaha yake kwa lile alilolifikiria kuwa ni ushindi wa sanamu la kipagani liitwalo al-Uzza.1

Hadithi kuhusu namna gani Ali alivyozuia jaribio la kwanza la Abu Sufyan la kutaka kuvuruga Uislamu kwa kukataa kuukubali msaada wa kijeshi alioupewa na yeye Abu Sufyan wakati Abu Bakr alipowekwa kuwa Khalifa kuliko madai yake Ali ambayo yamekwishasimuliwa.

Ali mara moja alikwishauona mchezo huu wa Abu Sufyan na akamwambia kwamba yeye (Abu Sufyan) alikuwa ni adui wa Uislamu na Waislamu.

Abu Sufyan bila kusita alibadilika, na kwa mafanikio makubwa akajadiliana masharti ya ushirikiano na wapinzani wa Ali. Khalifa wa kwanza alipeleka jeshi kubwa kuivamia nchi ya Syria katika mwaka wa 13 A.H., na miongoni mwa wale ambao waliongoza jesi hili walikuwamo watoto wawili wa Abu Sufyan, Yazid (bin Abu Sufyan) na Mu’awiyah.

Abu Sufyan mwenyewe alishughulika kama msimuliaji wa hekaya kwa ajili ya burudani ya viongozi wa vita,2 na binti yake na mkwewe pia walishiriki katika vita hii. Baada ya ushindi wa Syria, Yazid bin Abu Sufyan aliteuliwa kuwa gavana wa nchi hiyo. Alipokufa alirithiwa na ndugu, yake, Mu’awiyah.3

Wakati wa kipindi cha ugavana wa watoto wao, Abu Sufyan na Hind, ambaye alikuwa ameachika, walipata manufaa mengi za kiuchumi. Hind alitanguliziwa fedha kiasi cha dirham 4,000 kutoka kwenye Hazina ya taifa ambazo aliziwekeza katika biashara yenye faida kubwa sana.

Abu Sufyan alilipwa dinari mia moja kama gharama za kujikimu wakati alipotembelea Damascus,4 ingawaje bado alikuwa na nia mbaya dhidi ya Uislamu kwani yeye hakuweza kuzishinda hisia za huruma alizozichukua kwa ajili ya wa-Byzantine, waliokuwa kwa wakati huo wakipigana huko Yarmuk dhidi ya Waislamu.

Uthman alikuwa Khalifa mnamo mwaka wa 23 A.H. na Abu Sufyan akamshauri kuimarisha mamlaka yake kwa msaada wa ndugu zake, Bani Umayyah. Aliongeza kwamba ni mamlaka ya kidunia tu ndiyo yenye maana, kwani hakuweza kuelewa imma pepo au jahannam.

Abu Sufyan na watu wa familia yake waliugeuza ukhalifa wa Uthman kwa manufaa kamilifu kabisa. Sehemu za Hims, Qinnasrin na Palestina ziliongezewa kwenye milki ya Mu’awiyah na akawa mtawala wa Syria yote.5

Inaelekea kwamba ushauri wa Abu Sufyan ulipelekea kwenye uharibifu wa Uthman na hatimaye kuuawa kwake. Katika mahojiano yake ya kwanza na Uthman kuhusu marekebisho ya kufanywa katika utawala, Ali alimwonya akisema, “Unatoa tahafifu zisizo za kawaida na upendeleo kwa ndugu zako, unapuuzia makosa yao, hata Mu’awiyah humwonyi wakati anapofanya mambo bila ya idhini yako, na humshutumu wakati anapotangaza kwa uwongo kwamba matendo yake yana kibali chako.”

Madaraka makubwa kama hayo yalikuja kutumiwa na Mu’awiyah kiasi kwamba ikaanza kusemwa waziwazi kwamba angekuja kumrithi Uthman kwenye Ukhalifa. Akihisi mustakabali wake kuwa salama kabisa, Mu’awiyah alipuuzia kwenda Madina kumsaidia Uthman dhidi ya waasi ingawa alikuwa amefika karibu na mji ule. Alipendelea kuwa mtazamaji tu katika masaibu ya Khalifa huyo mzee kutoka kwenye umbali ulio salama. Mshauri wake mkuu na muungaji mkono, Amr bin al-Aas kwa wazi kabisa alichochea vurugu na uasi dhidi ya Uthman na akarudi Palestina kungojea kusikia matokeo ya jitihada zake.

Bani Umayyah walitwaa njia zote za wafalme baada ya kujiimarisha wenyewe katika madaraka. Katika utukufu na fahari iliyoingizwa katika maisha kwenye makasiri yao, ule utulivu, usawa na undugu wa Uislamu ulikuwa hauna nafasi yoyote ile, ukiwa mahali pao pamechukuliwa kabisa na ustaarabu wa kidunia.

Pombe ilianza kutumika kwa uhuru kabisa hususan na watu matajiri, na pale mmoja wa masahaba wa Mtume alipofungua mifuko iliyojazwa na vileo, Mu’awiyah aliudhika sana na akifikiria kwamba yuko kwenye umri wa kupungukiwa na akili. Kuvuka mipaka dhidi ya sheria na kanuni za Qur’ani na hadithi na mwenendo wa Mtume uliongezeka sana na Masahaba wazee wa Mtume walizidi kutengewa na Mu’awiyah.

Inaelekea kwamba kikubwa zaidi kilikuwa ni mamlaka ya Mu’awiyah, kilichokuwa chini zaidi ni makubaliano yake na kanuni na sheria za Uislamu na utamaduni wake halisi. Matokeo yake, vigezo vya tabia na sifa pambanuzi za desturi zilizoagizwa na Uislamu kwa ajili ya maisha ya jamii ya kawaida zilikuwa zimepuuzwa kabisa, kama mfano ulionyeshwa wa kuhamishwa kwa Abu Dharr kulikoamriwa na Uthman kwa kuombwa na Mu’awiyah.

Abu Dharr alikuwa sahaba wa Mtume aliyeheshimiwa sana, lakini alizungumza wazi wazi ilipokuja nafasi ya kusema kweli. Alishutumu kwa ujasiri mkubwa kuhusu kuhodhi mali na isitumiwe kuwasaidia wenye njaa na dhiki. Alikuwa akizunguuka kwenye mitaa mjini Damascus akikariri Aya ya Qur’ani, yenye maana, Wale ambao wanakusanya fedha na dhahabu katika masanduku ya hazina zao na hawautumii utajiri katika njia Mwenyezi Mungu, basi wangojee wakati utakapofika vipaji vya nyuso zao vitakapobabuliwa kwa moto wa Jahannam.”6

Abu Dharr alifukuziwa sehemu yenye kuhuzunisha wasiokaa watu na ali- poshindwa kuvumilia taabu za maisha hapo, akafariki dunia katika mwaka wa 33 A.H. Mke wake na binti yake walikuwa pamoja naye, na kwa matataizo makubwa waliweza kuuosha mwili wake na kuuvisha sanda. Kwa tukio la bahati ya pekee, Abdallah bin Mas’ud, sahaba wa Mtume alifika hapo na akaomboleza kifo na misiba ya Abu Dharr, na akauzika mwili wake.

  • 1. Tabari, Juz. 1, uk. 1418
  • 2. Tabari, Juz. 1, uk. 2095
  • 3. Tabari, Juz. 1, uk. 2860
  • 4. Tabari, Juz. 1, uk. 2766 na 2767
  • 5. Tabari, Juz. 1, ukarasa 2866
  • 6. Tabari, Juz. 1, uk. 2859