Table of Contents

Sura Ya 8: Mgogoro Kati Ya Watetezi Halisi Wa Uislamu Na Wahusika Wakuu Wa Syria Baada Ya Mtume

Baada ya kifo cha Mtume, walikuwa ni Ahlul al-Bayt wake ambao ndiyo walidumisha uhai wa kanuni kuu za Uislamu na kuyahifadhi yale maadili aliyokuwa akitafuta kuyasimamisha.
Katika makao ya serikali za Waislam, hali za maisha zilishindana kwa ubora na fahari kwa kutumia pesa zilizopatikana kutokana na utekaji nyara au, kutozwa kama ushuru kwenye nchi zilizowekwa chini ya utii. Dhuria ya Mtume, hata hivyo, iliendelea kuishi maisha ya kawaida, ya kutojishaufu, na kupitia matumizi yao binafsi, wakitumia kila walichokiweza kuwasaidia mayatima wajane na masikini kwa ujumla.

Tofauti kali ambazo zilitenganisha mtindo wao wa maisha kutokana na ule wa maisha ya hali ya juu wa wale ambao lengo lao lilikuwa kutwaa mamlaka na starehe zake nyingi kwa kawaida ziliishia katika migogoro. Vita kati ya Mu’awiyah na Ali havikuwezekana kuzuilika.

Dhuria ya Mtume, kama wafuasi halisi wa Uislamu, walisimama kwa ajili ya kuziondoa tofauti zote miongoni mwa Waislam, na kusimamisha usawa na undugu, kuhifadhi utoaji wa stahili kwa ubora wa tabia na ukamilifu katika utekelezaji wa wajibu wake mtu kama mwanadamu.

Ulimbikizaji wa mali (utajiri) katika hazina ya serikali kwa ugawaji wa baadaye kama msaada maalum au hiba binafsi ziliashiria dalili ya upendeleo na ulielekea kutia nguvu ushindani miongoni mwa wapokeaji wake, Ali aliisimamisha desturi hii. Alitumia ugawaji wa kila siku, kwa mazingatio makali ya uadil- ifu kila kitu kilichokuwa kimeingizwa katika hazina.

Watu ambao walifaidika na vitendo hivi vya upendeleo kabla ya Ali kuwekwa kama Khalifa lazima watakuwa wameathiriwa vibaya sana na mpango wa Ali wa ugawaji wa fedha ya serikali miongoni mwa Waislam.

Bani Umayyah walikuwa hawana wasiwasi katika kutumia fedha ya umma kama ilivyofaa kwenye lengo lao la kupata uungwaji mkono na watu, na walifanikiwa katika hilo, wakabakisha idadi ndogo tu ya watu kumfuata Ali. Matokeo haya haya ya ifuatia kutokana na mazingira magumu ambamo kwa ujumla Ali aliendesha maisha yake.

Watu kwa kawaida huwafuata watu ambao kiuchumi hawajambo na ambao wanaweza kuwasaidia wakati wa haja. Kwa hiyo, wale ambao walikuwa macho yao wameyakazia katika bahati hiyo kubwa, walipendelea kwenda kwa Mu’awiyah zaidi kuliko kumfuata Ali. Bani Umayyah pia walipendelea madai ya waarabu kama taifa, kuwa bora zaidi kuliko wasiokuwa Waarabu. Hili lilikuwa likipingana moja kwa moja na mafundisho ya Uislamu, na Hadith na Sunnah (mwenendo) wa Mtume wake.

Ubaguzi wa Bani Umayyah ulisababisha mlipuko wa tatizo la Waarabu dhidi ya wasiokuwa Waarabu. Kama watetezi halisi wa kanuni na misingi ya Uislamu na utekelezaji wake, Bani Hashim hawakuweza kuyakubali madai ya Waarabu kuwa wao wawe bora zaidi kuliko wasiokuwa Waarabu. Fikra hii inapata kuungwa mkono kutokana na ukweli kwamba Bani Abbas ambao walikuwa wanatokana na Bani Hashim, katika chagamoto yao kwa utawala wa Bani Umayyah waliwapata waungaji mkono wengi kutokana na watu wasiokuwa Waarabu wa Iran.

Kutokana na sababu zilizotajwa katika ibara zilizotangulia na kwa sababu ya uadui ambao Bani Umayyah na makabila mengine walikuwa nao juu yao, dhuria ya Mtume kwa kawaida walipata uungwaji mkono mdogo zaidi wa watu wa nchi yao kuliko walivyoungwa mkono Bani Umayyah.