Table of Contents

Sura Ya 9: Mkataba Wa Hasan Na Mu’awiyah Na Matokeo Yake Yasiopendeza.

Kabla ya kuutoka ulimwengu, Ali alifanya wasia akiwaagiza watoto wake, Hasan na Husein, hasa kuhusu wajibu wao kwa Mwenyezi Mungu, Kitabu Chake, kwa masikini na wanyonge, na mambo mengine kama hayo.1 Aliwaelekeza kuhakikisha kwamba ni muuaji wake tu ndio auawe kulipiza kuuawa kwake.2

Baada ya kifo cha Ali, Hasan alikubaliwa kwa pamoja na Waislam kama khalifa wao kama ilivyopendekezwa na Abdullah bin Abbas, wakati watu wote ambao walikusanyika kwa ajili ya maziko hayo walipojiunga na Hasan katika kuomboleza juu ya kifo cha baba yake mashuhuri huyu. Kisha Waislam kwa hiari yao walitoa kiapo cha utii kwa Hasan kama ilivyopendekezwa na Ibn Abbas.

Katika wakati huu muhimu, Hasan aliwataka watu kukubali kumfuata yeye aidha akiwa amechagua kwenda vitani au kuishi katika amani. Hii ilikuwa mwezi 21 Ramadhan, 40 A.H.3

Wakati ambapo nchi bado iko katika maombolezo na Hasan alikuwa hajap- ata muda wa kutosha kukamilisha mipango yake kwa ajili ya utawala unaofaa kwa nchi za Kiislam, Mu’awiyah alianza tena mchezo wake aupendao sana wa kuamsha hisia za kutoridhika miongoni mwa wakazi wa nchi za Waislamu. Aliwaweka wapelelezi na mawakala wachochezi wa ghasia katika sehemu ambazo zina maovu mengi na fitna kama vile miji ya Kufa na Basra kuchochea vurugu na utovu wa nidhamu.

Hasan alikerwa sana na udukizi huu wa Mu’awiyah katika maeneo yaliyo chini ya utawala wake na akamwandikia kwa kulenga kuvuta mazingatio yake kuhusu kuingilia huku kusiko na sababu.

Alilalamika pia kwa Mu’awiyah kwamba yeye Mu’awiyah amewahi kuripotiwa kuwa amemtukana Ali mwenye kuheshika ambaye wakati huo alikuwa amekwishakufa, na akamwambia kwamba hilo lilikuwa tendo lisilofaa kabisa. Aliongeza kusema kwamba kama Mu’awiyah alitaka vita, basi anaweza kujiandaa nayo. Mabadilishano zaidi ya mawasiliano na Mu’awiyah yalisaidia tu kuweka wazi kwamba alikuwa na hisia za uadui usiozimika dhidi ya Ali ambao hata kifo chake Ali pia hakikusaidia hata kidogo kupunguza uadui huo.

Kwa kupita muda, shughuli za kutotulia za wapelelezi na watoa habari wa Mu’awiyah zilianza kupata nguvu zaidi na ukamilifu. Hata hivyo, Hasan alikuwa amejiandaa zaidi kupigana vita na Mu’awiyah kuliko kuhatarisha misingi ya haki na uadilifu.

Hata hivyo, hali ya mambo haikuonekana kuwa ya uhakika moja kwa moja, kwani mbali na njama mbaya za kiovu za Mu’awiyah, watu walikuwa wameanikwa kwenye vishawishi vya kichochezi vya mabaki ya kikundi cha Khawariji ambacho kilikuwa kimeshindwa vita lakini kilikuwa hakikuangamizwa kabisa na kutoweka katika jamii kiasi cha kukosa wapenzi wa kukionea huruma kikundi chao kilichoshindwa.

Ali mwenyewe alionyesha kukirihika na kuudhika kwa kukosekana umoja na kuwepo utovu wa nidhamu ambao sasa ulipenya na kuingia katika jeshi lake na katika wakati fulani alienda hata kufikia hatua ya kupenda Mu’awiyah angekubali kubadilisha mfuasi wake mmoja kwa watu wawili wa Ali kama kubadilisha dhahabu kwa fedha.

Hao ndio aina ya watu ambao Hasan alikuwa afanye nao kazi. Aliwajua fika kama Mu’awiyah alivyojua kwa kupitia majasusi na watoa habari wake. Akitiwa moyo kwa hali ya mambo iliyokuwepo wakati huo, Mu’awiyah bila kutegemewa aliishambulia Iraki. Hujr bin Adi alizunguka huku na huko kuandikisha askari wa kumsaidia Hasan, lakini alikutana na majibu yasiyoridhisha. Miongoni mwa wale ambao walijitokeza kuja kusaidia walikuwa watu duni waliokuwa wanataka tu kupora, baadhi yao ambao walikuwa wameshinikizwa kufanya hivyo na watemi wao wa kikabila, Khawariji ambao kwa hali yoyote walitaka kupigana na Mu’awiyah, na watu mmoja mmoja walio watiifu wa madhehebu ya shia.4

Hasan alimpeleka Qays bin Sa’d bin Ubada al-Ansar akiliongoza jeshi la watu 20,000 na yeye mwenyewe akabakia huko Sabat. Alipoushuhudia uadui wa kisaliti wa wafuasi wake alisimama kuwapa nasaha za ubora wa kutenda mambo kwa makubaliano na umoja. Alikuwa hata bado hajamaliza hotuba yake wakati Khawariji walipoleta fujo, wakisema, “Ametoka kwenye Uislam na kuwa mwasi”5.
Hasan alifanyiwa shambulizi la ghafla, lakini makabila tiifu (kwa Hassan) ya Rabi‘a na Hamadan yalimwokoa, na kuwatawanya washambuliaji wake.

Hasan aliondoka kwenda Mada’in ambako huko Khawarij mmoja alimjeruhi kwa sime. Jeraha hilo lilichukua muda mrefu sana kupona. Kisha Hasan alianza tena maandalizi ya kupigana na Mu’awiyah, ambaye hata hivyo, kwa upande mmoja alitoa pendekezo la amani kwa masharti yoyote yale ambayo Hasan angeyaona yanakubalika. Mu’awiyah pia alimpelekea Hasan barua za wale viongozi wa jeshi la Hassan ambao walimkaribisha kuishambulia nchi yao na hata pia kumwahidi kumtoa Hasan kama mateka wake, au kumuua.6

Katika mazingira haya, ilikuwa haifai kurefusha hali ya vita na kwa mujibu wa yale ambayo Mtume na Ali wameyafanya katika matukio yafananayo na hili, Hasan alikubali kufanya mkataba wa amani na Mu’awiyah. Masharti ya mkataba ambayo yalianza kutumika katika mwezi Rabiul Awwal au Jamadil Awwal, mwaka wa 41 A.H.7 yalikuwa:

(1) Mu’awiyah angetawala nchi za Kiislamu kwa mujibu wa Kitabu cha Mwenyezi Mungu, Sunna za Mtume na Makhalifa wake waadilifu;

(2) Mu’awiyah atakuwa hana haki ya kuteua mrithi wake kwenye nafasi ya Ukhalifa;

(3) Wakazi wa nchi zote za Kiislam kama vile Syria, Iraki, Hijaz na Yemen watalindwa;

(4) Maisha, mali na heshima za mashia wote wa Ali, popote pale watakapokuwa wanaishi lazima walindwe kwa usalama;

(5) Mu’awiyah asingefanya jaribio lolote lile, la wazi au la siri, juu ya maisha ya Hasan na Husein au ya yeyote yule mwingine ahusikanaye na familia ya Mtume, wala vinginevyo, kumfanyia ukatili, kumtisha au kumdhuru yeyote yule katika wao.

Ugomvi wa Hasan na Mu’awiyah uliibuka hasa kutokana na matakwa ya Hasan kutaka kuilinda misingi na kanuni za sharia na za imani. Sharti la kwanza la mkataba liliufanya kuwa wajibu kwa Mu’awiyah kutenda kwa mujibu wa sheria za Qur’ani na Sunna za Mtume na makhalifa wake waadilifu.

Halikuthibitisha tu bali lilimtaka Mu’awiyah akubali kwamba kabla ya kutiwa sahihi kwa mkataba huo utawala wa Syria ulikwishakosea dhidi ya sheria za Qur’ani na sunna za Mtume na makhalifa wake waadilifu. Lilithibitisha pia kwamba misingi na kanuni za sheria na imani ziko mbali kabisa na zile sheria za serikali za kidunia na matendo ya watawala wa kidunia.

Kifungu cha pili cha mkataba huu kilimzuia Mu’awiyah kuteua mrithi wake ili kudhibiti ile hali ya kufuata njia za wafalme ambao waliwataja warithi wao bila ya kuzingatia sifa na pia kumvua madaraka ya kumteua kama mrithi wake yule ambaye mwenendo wake usingepatana na amri za sheria za Qur’ani, na sunna za Mtume na za Makhalifa wake waadilifu.

Hitimisho la mkataba lilileta ufidhuli usiostahili kabisa juu ya Hasan kutoka kwa wafuasi wake wadanganyifu na wasaliti na ongezeko kubwa la nchi zake kuwa chini ya utawala wa Mu’awiyah. Muda mfupi tu baaada ya amani kurudishwa, Mu’awiyah aliuambia mkusanyiko wa Waislam karibu ya mji wa Kufa kwamba lengo na kusudio lake pekee la kwenda kupigana vita lilikuwa ni ili yeye akubalike kama mtawala mkuu wa Iraki na nchi nyingine za Waislamu, na kwamba utimilizwaji wa masharti ya mkataba na Hasan yalitegemea juu yake yeye tu.8

Kuteka madaraka kulikofanywa na Mu’awiyah kulimpa hamasa ya kumtukana Ali mbele ya watoto wake, Hasan na Husein. Hasan alitoa majibu mafupi lakini yenye kueleweka vizuri sana.
Husein aliuchunguza mwelekeo wa malengo ya serikali ya wakati huo kwa ukaribu zaidi, na akatambua kwamba mtihani wa mwisho ulikuwa ungojewe katika hali ya ukimya.

Hasan aliitoka mji wa Kufa na kwenda Madina ambako Husein pia aliungana naye. Ili kuleta mgawanyiko kati ya ndugu wawili hawa Bani Umayyah walieneza uvumi wa uwongo kwamba Hasan na Husein walikuwa na maoni tofauti kuhusu mkataba wa amani na Mu’awiyah. Uvumi huo ulipotea kwa haraka sana, kwani ndugu hawa wawili walikuwa pamoja kabisa.

Husein alijua kwamba Hasan aliamua kuyaacha madaraka ya kidunia ili tu kuondoa uwezekano wa vita ingawa alikuwa hajaamua kabisa kuikimbilia silaha kama hatua ya mwisho kumaliza mzozo huu. Ukiashiria kwa uwazi kabisa utendaji wa kina wa akili yake, ulikuwa ni ule ukweli kwamba Hasan alikuwa akisikika mara kwa mara akiyakariri mashairi yenye maana ya kwamba: “Yeyote yule aufanyaye upanga kuwa kinga yake huzawadiwa kwa amani ya pekee na uhuru kutokana na matatizo: imma kuutoka ulimwengu huu upesi sana, au kubakia ndani yake katika kufurahia faraja adilifu”.

“Kamwe usitafute urahisi, ni tabia isiyofaa kabisa. Huwezi kuipata heshi- ma ila kwa kupitia kupata taabu na matatizo”9

Kwa kuhitimishwa mkataba huo, Bani Umayyah walijiona wenyewe kuwa huru kutenda lolote walilolitaka, na walipuuza kuyaheshimu masharti ya mkataba.

Kama Mu’awiyah angetimiza sharti la kwanza la mkataba kutenda kwa mujibu wa amri za kisheria za Qur’ani na sunna za Mtume na makhalifa waongofu, angekuwa amehesabiwa kuwa mmoja kati yao. Lakini hata Waislam wa madhehebu ya Sunni hawatoi madai yoyote kama hayo kwake. Wanashikilia kwamba ukhalifa wa haki ulidumu kwa miaka thelathini tu baada ya kifo cha Mtume, na kipindi hiki kilimalizika wakati wa hitimisho la mkataba kati ya Hasan na Mu’awiyah.

Kulikuwepo na mifano mingi ambayo ndani yake mahitaji ya umuhimu wa sharti la kwanza la mkataba yamevunjwa. Inaonyesha kwamba manufaa ya kisiasa yalimshawishi Mu’awiyah kumtangaza Ziyad, mwana wa Sumayyah, kuwa ni ndugu yake. Hekeya hii si ya bure tu bila maslahi na ingefaa kuelezewa hapa kwa ufupi.

Mama yake Ziyad, aitwaye Sumayyah, alikuwa kijakazi aliyeachwa huru. Aliolewa na Ubayd ambaye alikuwa mtumwa wa mtu mmoja wa ukoo wa Bani Thaqif na akamzaa Ziyad ambaye alilelewa na kukuzwa na al-Mughira bin Shu’ba, na alikua na akawa kijana mwenye akili na aliyesoma sana. Umar alimfanya kuwa gavana wa Basra, na baadaye Ali alimteua kuwa gavana wa Fars (Uajemi).

Baada ya kuuawa Ali, Ziyad mwanzoni alikasirika vibaya sana kutokana na vitisho vya Mu’awiyah, lakini katika mwaka wa 44 A.H., Mu’awiyah alimtangaza kuwa ndugu yake,10 kwa vile Abu Sufyan alifahamika kuupi- tisha usiku katika urafiki haramu na Sumayyah. Kuanzishwa kwa uhusiano huu wa undugu kati ya Ziyad na Mu’awiyah kulileta mtikisiko miongoni mwa Waislam kwa ujumla na hususan miongoni mwa masahaba wa Mtume, kwa sababu ilikuwa kinyume na hadithi ya Mtume aliyokuwa akiitamka mara kwa mara kwamba mtoto atahusishwa na wazazi walio wanandoa, ila mawe ndio majaaliwa ya mtu mzimifu.

Mu’awiyah hakujali hasira za watu kwa ujumla kwa sababu kulikuwa na manufaa kwake kule kuununua utiifu wa Ziyad na dhuria wake kwa ajili ya malengo yake.

Mu’awiyah alianzisha na kuingiza matendo mengi yaliyopingana na sheria na kanuni za Kiislam. Hivyo alipunguza kiwango cha zaka kitolewacho kwenye sikukuu ya Id-el-Fitr kutoka kiwango cha pishi moja hadi kufikia vibaba viwili tu kwa kila mtu. Alivaa mapambo ya dhahabu, nguo zili- zotengenezwa kwa ngozi za wanyama wenye kula nyama wawindaji, ingawa alikuwa anatambua sana kwamba matendo hayo yalikatazwa au kuharamishwa na Mtume.
Katika siku ya Arafa wakati wa ibada za Hija utaratibu wa “talbiya” umaanishao “Ee Allah, mimi niko hapa nikiitekeleza ibada Yako. Wewe huna mshirika”, iliyokuwa ikitamkwa kwa kukaririwa kama sehemu ya matendo muhimu. Mu’awiyah alilikataza tendo hili. Abdallah bin Abbas, mtu aliye na elimu sana, alikanusha ukatazaji huu wa talbiya katika nyakati nyingi.

Mu’awiyah alikuwa akitumia kumimina fadhila zake kwa waimbaji ingawaje Uislamu unachukia muziki. Sa’id Khathir, mtu aliyejishughulisha sana katika kufuatilia mambo maovu aliimba na kujipatia mafanikio makubwa katika baraza la Mu’awiyah. Ibn al-Faqih, mwanachuo maarufu, ameandika kwamba Mu’awiyah alikuwa mtu wa kwanza kuweka vituo vya ulinzi vya polisi, kuwahanithisha (kuwahasi) wanaume kuwafanya matowashi na kuhifadhi fedha katika hazina za taifa. Mu’awiyah aliazisha utaratibu wa kupokea, kama wafalme, zawadi katika nyakati za sherehe za Waajemi za Nauruz (mwaka mpya) na Mihrajan ambazo katika miaka fulani fulani zilimpatia dirham milioni kumi.

Kaida za Kiislamu ziliangukia katika kupuzwa kabisa. Bukhari anaandika kwamba wakati fulani Abu Darda, sahaba wa Mtume alionekana kuwa katika hali ya kukasirika sana kwa vile hakuona katika watu dalili yoyote ile ya kumfuata kwao Mtume, isipokuwa tu kwamba walitekeleza swala za jamaa. Malik amesimulia kwamba isipokuwa kwa wito wa kwenda kusimamisha sala (adhana) hakuna hata moja kati ya matendo ya Kiislam ya miaka ya nyuma lililoweza kuonekana.

Mu’awiyah hakulitaja hata jina la Mtume kwa heshima inayostahili, na mtu mmoja mzee ambaye Mu’awiyah alimhoji alimnyanyua kwa nguvu wakati mzee huyo alipomwuliza Mu’awiyah kuhusu Mtume, akimtaja kirahisi tu kama “Muhammad.” Mzee huyo alimuuliza Mu’awiyah kwa nini yeye hakulitaja jina hilo kwa heshima inalolistahili na kumwita Mtume wa Mungu Muhammad tu, basi!

Wakati fulani, ili kuzuia werevu muovu wa Amr bin Aas wa kumdhalilisha yeye mbele ya macho ya watu wa Misri, aliwafanya watu wa ujumbe wao wawe na nidhamu ya kuogopa kiasi kwamba wote walimwita Mu’awiyah kama Mtume wa Mungu. Mu’awiyah hakujali kuaadhibu, au hata pia kuwaonya tu dhidi ya kufuru hii.

Watu wanawafuata watawala wao katika dini kama vile wanavyowafuata katika kila kitu kingine. Wakati mtendaji mwenye mamlaka makuu alipokuwa hajali sana katika utekelezaji wa kanuni na matendo ya Uislamu, watu (wengi) lazima watakuwa bado wana mwelekeo mdogo wa kuzifuata. Kwa kweli, dini ilikuja kuwa kitu cha kuuzwa kwa mnada.

Wakati fulani Hatat bin Yazid na watu wengine watatu walikwenda kum- wona Mu’awiyah ambaye alimpa Hatat dirham elfu sabini (70,000) wakati wale wengine watatu walipata kila mmoja dirham laki moja. Hatat alilalamika dhidi ya utendewaji huu wa kibaguzi na Mu’awiyah akamwambia kwamba kile kiwango kikubwa zaidi kiliwakilisha bei ya imani ya wenye kupokea. Hatat mara moja alijitoa kuiuza imani yake kwa kiwango hicho.11

Waislam wachache wacha-Mungu, ambao walikuwa bado wangali hai walichoshwa na maisha. Al-Hakam bin Amr akiongoza kampeni kwa upande wa Mashariki alikataa kukubaliana na amri ya Mu’awiyah ya kupeleka kwenye hazina ya serikali ngawira za vita katika mwaka wa 50 A.H. badala ya kuzigawa ngawira hizo miongoni mwa askari kwa mujibu wa desturi ya zamani.

Hata hivyo, alishikwa kwa vitisho vikubwa mno kiasi kwamba alikiombea kifo chake na alifariki muda mfupi tu baadaye.12

Ili kufuta kumbukumbu za Bani Hashim, Mu’awiyah alijaribu kuiondoa mimbari ya Mtume kwa nia ya kuisafirisha kwenda Syria. Hata hivyo, aliacha kutekeleza mpango wake huo na alipatwa na ugonjwa wa kupooza uso katika mwaka huo huo.13

Tukiacha ukiukwaji wa sharti la pili la mkataba kwa ajili ya kuja kuelezea baadaye, tungeweza kushughulika na uvunjwaji wa sharti la tatu ambalo lilieleza kwamba nchini Syria, Iraki, Hijaz na Yemen ulinzi ungetolewa kwa watu bila ya kuangalia sehemu za nchi walizotokana nazo.

Chakusikitisha hasa ni ule ukiukwaji wa sharti hili. Ziyad bin Sumayyah alifungulia ulafi wa umwagaji damu ambao shabaha yake kuu ilikuwa ni wakazi wa Iraki. Adhabu zilikuwa zikitolewa bila makosa ya aina yoyote ile kutendeka, watu walikuwa wanafungwa jela bila kufanywa uchunguzi na kutia watu vilema na kuua kwa kutumia visingizio vidogo sana ikawa ni kawaida ya kila siku.

Wakati Samura bin Jundab alipochukua nafasi ya Ziyad huko Basra alitokea kuwa dhalimu aliyekuwa na kiu ya kumwaga damu zaidi kuliko hata mtangulizi wake na alifanya watu wasiopungua elfu nane (8,000) kuuliwa kwa upanga ndani ya miezi sita tu.

Aliwaua watu 47 ambao waliihifadhi Qur’ani kwa moyo. Samura aliwaamuru watu wasijizoeshe kutembea tembea kwenye mitaa ya jamaa baada ya usiku wa manane. Mtu mmoja aliwasili hapo kutoka sehemu za shamba na alitiwa mbaroni kwenye mtaa wa jamaa wakati wa masaa yaliyopigwa marufuku kutembea. Samura alikubali kwamba mtu huyo alikuwa hatambui kuhusu amri zake hizo lakini hata hivyo alimuua kwa “manufaa ya Umma”. Mtu mwingine alilipa zaka kwa Samura na alikuwa akiswali msikitini wakati mtu mwingine alifika hapo na kumuua. Mifano mingi ya ukatili wa namna hiyo iliweza kuzidishwa sana.

Sharti la nne la mkataba kwamba maisha, mali na heshima za wafuasi (Shi’a) wa Ali lazima zilindwe kutokana na madhara lilikiukwa kwa ufisadi kabisa. Taabu iliyokuwa ndogo sana ambayo shi’a wa mjini Kufa na Basra waliipata ilikuwa kwamba walilazimishwa kuziacha nyumba zao ili kuwapa nafasi wafuasi wa Mu’awiyah na (wao) walipelekwa Qinsrin, sehemu isiyokaliwa na watu nchini Syria, kwenda kuishi huko katika kambi ya kijeshi.

Hujr bin Adi na masahaba zake waliitwa kwenda Syria na waliuawa ingawa walitamka wazi kwamba walikuwa ni Waislam, na kwamba wal- ishikilia neno lao hilo la ahadi na hawakuwa waasi. Kosa lao tu na ambalo halikuweza kusameheka kabisa lilikuwa ni kule kukataa kwao kumtukana Ali.

Sayfi bin Faysal al-Shaybani, mmoja wa watu maarufu sana miongoni mwa marafiki wa Hujr alipigwa bila huruma wakati alipomwambia Ziyad kwamba alimchukulia Ali kwa heshima kubwa kabisa. Mateso yaliendelezwa na kisha Sayfi aliulizwa tena kuhusu alivyojihisi kumhusu Ali.

Sayfi alirudisha jibu kama lile lile la mwanzo tena kwa nguvu ya nyongeza na hoja. Alikuwa miongoni mwa watu kumi na mbili pamoja na Hujr bin Adi ambao walipelekwa Syria. Wengine wawili waliungana nao baadaye. Katika watu hawa kumi na nne, saba waliachiwa huru kwa mapendekezo yaliyofanywa kwa ajili yao, watu sita waliuawa kwa upanga, na mmoja aliyeitwa Abd al-Rahman bin Hassan al-Anaz alichaguliwa kwa ajili ya adhabu ya mfano, akiwa mfuasi mtiifu zaidi kwenye njia ya Shi’a. Ziyad alimzika mtu huyu akiwa angali hai.14

Hujr bin Adi alikuwa miongoni mwa watu wale ambao waliuawa. Alikuwa ni mtu aliyetukuzwa sana katika ulimwengu wote wa Kiislam. Mauaji yake yaliombolezwa kwa kina sana na Waislam wote, Shi’a wa mjini Kufa wakichukulia kuwa ni msiba mkubwa mno.

Wakati Aisha, mjane wa Mtume, aliposikia kwamba Ziyad ameandaa taarifa dhidi ya Hujr, yeye alimpelekea ujumbe kupitia kwa Abd al-Rahman bin Harith bin Hisham kumwogopa Mwenyezi Mungu. Mjumbe alikuwa amechelewa sana kumfikia Ziyad na Hujr alikuwa amekwisha uawa. Wakati Aisha aliposikia mwisho wa kuhuzunisha wa Hujr, alizungumzia kwamba kama Mu’awiyah asingejua kwamba wakazi wa Makka walikuwa wameachwa na dalili yoyote ile ya ujasiri, asingekuwa na ujasiri wa kumwita Hujr na masahaba wake wakiwa wamefungwa minyororo kwenda Syria na kumuua. Aliongeza kusema kwamba mtoto wa mwanamke ambaye alikula ini la Hamza alijua kwamba ujanadume ulikoma kuwepo.

Alithibitisha kwamba kwa elimu yao na mafanikio yao watu hawa wangefaa kuonekana kama kichwa na akili ya Uarabuni.

Wakati Mu’awiyah alipokuja Madina na akamtembelea Aisha, anaonekana alimshambulia vikali kuhusu kifo cha Hujr kiasi kwamba Mu’awiyah aliu- funga mjadala akisema, “Tuache mimi na Hujr peke yetu. Suala hili litachambuliwa mbele ya Mwenyezi Mungu.”

Wakati Abdallah bin Umar mtoto wa Khalifa wa pili aliposikia kuuawa kwa Hujr katika sehemu ya sokoni alisimama na akaomboleza kwa kun- yanyua sauti kubwa.

Rabi bin Ziyad al-Harith gavana wa Khurasan, alipatwa huzuni sana kwa kuuawa kwa Hujr na utepetevu wa jumla wa Waislam kiasi kwamba anyanyua mikono yake juu mbinguni kuomba, akiwaomba Waislam ambao walikuwa wamejikusanya pamoja kwa ajili ya swala ya Ijumaa waitike kwa kusema “Amin.” Aliomba, (akisema), “Ee Mwenyezi Mungu! Kama kuna lolote lile zuri kwa (mja wako) Rabi’i, (basi) muondolee uhai.” Dua yake ilikubaliwa, na baada ya kuutoka msikiti, hakuwa amekwenda mbali sana wakati alipoanguka na akafariki.

Inaonyesha kwamba Mu’awiyah mwenyewe baadaye alitambua kwamba Hujr bin Adi aliuawa kwa makosa. Alisikika akijisemea kichini chini, “Ee, Hujr itanibidi nije kukutana na siku ndefu kwa mauaji yako,” wakati alipoona mwisho wake unakaribia haraka.

Amr bin al-Hamiq al-Khuzai alikuwa anaheshimiwa sana kama Mtume alivyopeleka salaam zake kwake. Yeye pia aliuawa kwa maelekezo yaliyotolewa na Mu’awiyah.

Matukio haya yaliwahuzunisha vikubwa Shi’a wa Ali. Aliposikia kwamba malalamiko mengi yamepelekwa kwa Husein dhidi ya kuuawa kwa Hujr, na Husein mwenyewe alikuwa amehuzunishwa sana na tukio hili na akihofia kwamba Husein angesimama kufanya uasi dhidi yake, Mu’awiyah alimwandikia barua iliyojaa vitisho.

Husein alimpelekea jibu, na akiuweka kando unyamavu wake wa kawaida, alisimulia, moja baada ya lingine, matukio yote ambayo ndani yake masharti ya mkataba na Hasan yalikuwa yamekiukwa, na akatoa maelezo ya kumbukumbu yenye kugusa kuhusu kifo cha Hujr, na akamwambia kwamba hakuna kilichosababisha huzuni kubwa zaidi kuliko ukhalifa na utawala wake.

Sharti la tano la mkataba lilimwajibisha Mu’awiyah asifanye jaribio la wazi au la siri, kuleta madhara kwa Hasan na Husein au yeyote yule mwingine ahusikaye na familia ya Mtume, Sharti hili lilikiukwa vibaya sana, ingawa pia dhuria wa Mtume wenyewe walijitoa kabisa kwenye shughuli za nchi.

Hasan alitendewa utovu wa heshima mbaya wa kificho na maafisa wa serikali. Hata wakati mwingine pia walitumia lugha chafu dhidi yake, nia ikiwa ni kuwachockoza na kuwatumbukiza Bani Hashim kwenye matendo ya vurugu, ili kwamba Mu’awiyah aweze kupata kisingizio cha kumwaga damu yao, lakini uvumilivu mkubwa wa Hasan ukalizuia tukio la ghafla kama hilo kufanyika.

Bani Umayyah kisha wakageukia kwenye hatua za siri ili kulipata lengo lao, na walitumia hongo na sumu katika kumwondoa duniani Hasan. Mu’awiyah alimkodi Ju’da, mke wa Hasan, kwa malipo ya dirham mia moja elfu na kumwaahidi baadaye kuolewa na mwanawe, Yazid.

Hasan alikufa, kwa kutiliwa sumu na Ju’da (mkewe), mnamo mwezi 28 Safar, mwaka wa 50 A.H. Alikuwa ametoa ombi la kuzikwa kando ya kaburi la Mtume, lakini akitarajia kutokea matatizo, aliamuru kwamba kama maziko yake karibu na kaburi la Mtume yatapingwa basi azikwe karibu na kaburi la nyanya (bibi) yake mzaa baba, Fatima, binti Asad katika eneo la makaburi ya al-Baqi.

Husein aliuchukua mwili wa ndugu yake kuelekea kwenye kaburi la Mtume, lakini alizuiwa kumzika hapo na Bani Umayyah ambao walion- gozwa na Marwan. Husein alikasirishwa sana na uingiliwaji kati huu, lakini kwa kustahi matakwa ya Hasan (ndugu yake) alimzika katika eneo la al- Baqi15.
Kifo cha Hasan kilikuwa ni msiba mkubwa kwa watu wa Bani Hashim ambao waliendelea kumwombelezea kwa kipindi cha mwezi mzima. Husein aliendelea kufuata njia ya amani kama vile (alivyofanya) ndugu yake.

Wakati Shi’a wa Irak walipomtaka akubali viapo vyao vya utii kwake, Husein aliwaambia kwamba isingekuwa sawa kuukana mkataba uliofanywa na Hasan kwani wao walifungwa na mkataba huo. Alipendekeza kwamba suala lote zima lingeangaliwa upya baada ya kufa Mu’awiyah.

 • 1. Abu al-Faraj al-Isfahani, Kitabu. Maqatil, uk. 38-40
 • 2. Kitabu: Maqatil, uk. 36
 • 3. Kitabu: Irshad, uk. 280 - 281
 • 4. Kitabu: Irshad, uk. 282
 • 5. Kitabu: Irshad, uk. 283
 • 6. Kitabu: Irshad, uk. 28
 • 7. Kitabu: Sawa'iq, uku. 81
 • 8. Kitabu: Irshad, uk. 286
 • 9. Kitabu: Kitab al-Baladan, uk. 53 cha Bin al-Faqih al-Hamadan
 • 10. Kitabu: Tabari, uk. 69-70
 • 11. Kitabu: Tabari, Juz. 2, uk. 96 - 97
 • 12. Kitabu: Tabari, Juz. 2, uk. 110-110
 • 13. Kitabu: Tabari, Juz. 2, uk. 92
 • 14. Kitabu: Tabari, Juz. 2, uk. 142
 • 15. Kitabu: Irshad, uk. 287 - 288