read

(10) Wanavyosema Wapinga Maulidi Na Majibu Yetu

Wiki iliyopita tuliona kwamba wapinga maulidi, wanaposoma vitabu vya maulidi, wakaona kuwa Mtume (s.a.w.w.) amesifiwa kwa neno alilosifiwa Mwenyezi Mungu, au kitendo chake kimetajwa kwa neno ambalo, kwa kawaida, hunasibishwa nalo Mwenyezi Mungu -- wanapoona hayo, moja kwa moja husema ni shirki, kwa sababu hivyo ndivyo wanavyoielewa wao shirki, na hali hivyo sivyo.

Neno lililotumiwa kumsifia Mwenyezi Mungu, linapotumiwa kumsifia Mtume (s.a.w.w.), halimfanyi Mtume kuwa ni Mungu (kwa hivyo si shirki) kama ambavyo, vile vile, neno lililotumiwa kuelezea kitendo cha Mtume (s.a.w.w.), halimfanyi Mtume kuwa ni Mungu. Kwa kutolielewa hili ndipo wapinga maulidi -- wao na viongozi wao -- walipokosea na kudai kuwa vitabu vya maulidi vina shirki!

Kuthubutisha kosa lao hilo, hapa chini tunayataja mifano michache tu (sio yote) kutoka katika Qur'ani Tukufu:

1. Tunaposoma Sura 2:143, tunamuona Mwenyezi Mungu anavyojisifu kuwa Yeye ni rauufun (Mpole) na rahiimun (Mwenye kurehemu). Na tunaposoma Sura 9:128, tunamuona Mwenyezi Mungu, Yeye Mwenyewe, anamsifu Mtume Wake (s.a.w.w.) kwa sifa zizo hizo za rauufun rahiimun! Jee, kwa kufanana matamko ya sifa hizo, Mwenyezi Mungu alikusudia kumfanya Mtume Wake ni Mungu kama Yeye? Jee, sisi tunapomsifu Mtume kwa sifa hizo, huwa tumefanya shirki kwa sababu tu matamko yaliyotumiwa yanafanana?

Jawabu ni: La! Isipokuwa kama tutaamini kuwa uraufu na urahimu wa Mtume (s.a.w.w.) ni sawa na ule wa Mwenyezi Mungu! Na hilo, sisi watu wa maulidi, hatulisemi wala hatuliamini. Tunaloliamini sisi ni kwamba uraufu na urahimu wa Mwenyezi Mungu ni Wake Mwenyewe kwa asili (bil aswaala / independently); wa Mtume (s.a.w.w.) ni wa kupawa na Yeye, Mola wake. Kama kumsifu Mtume kwa sifa hizo ni shirki kwa sababu tu zimefanana na za Mwenyezi Mungu, basi na wapinga maulidi nao pia ni mushrikina kwa sababu hatuamini kwamba wanapoifikia aya hiyo (Sura 9:128), kama Waislamu, huiruka wakaacha kuisoma, au huibadilisha maneno yake.

2. Tunaposoma Sura 16:70, tunaona kwamba Mwenyezi Mungu ndiye aliyetuumba na ndiye anayetufisha / anayetuuwa (yatawaffaakum); na tunapoisoma Sura 32:11, tunaona kwamba atakayetufisha (yatawaffaakum) sisi ni "malaika wa mauti". Sasa tushike lipi hapo, maana neno lililotumiwa kuelezea kitendo hicho cha kutoa roho ni lilo hilo moja: yatawaffaakum? Afishaye ni Mwenyezi Mungu, au ni huyo malaika?

Tukisema ni Mwenyezi Mungu peke Yake, tutakuwa tunaikanusha Qur'ani kwa sababu Qur'ani yiyo hiyo imetwambia kuwa na malaika huyo naye huifanya kazi hiyo. Na tukisema ni malaika peke yake, tutakuwa vile vile tunaikanusha Qur'ani kwa sababu Qur'ani yiyo hiyo imetwambia kuwa Mwenyezi Mungu naye huifanya kazi hiyo. Sasa ni nani basi? Ni wote wawili?

Jawabu ni: Ndiyo! Ni wote wawili; lakini pana tafauti. Japokuwa maneno (yatawaffaakum) yaliyotumiwa yanafanana, tawaffaa ya Mwenyezi Mungu si sawa na ya malaika. Ya Mwenyezi Mungu ni ya uweza Wake alionao Yeye Mwenyewe kwa asili. Ile ya malaika si hivyo. Yake ni ya "kuwakilishwa" (alladhii wukkila bikum) na Mwenyezi Mungu, kama aya yake (Sura 32:11) inavyofafanua. Kwa hivyo, ukiamini hivyo; hiyo si shirki. Lakini ukiamini kuwa uweza wa kufisha alionao malaika ni sawa na ule alionao Mwenyezi Mungu; hiyo, bila shaka yoyote, itakuwa ni shirki. Na ni Mwislamu gani anayeamini hivyo?

3. Tunaposoma Sura 22:6, tunaona kwamba Mwenyezi Mungu ndiye anayefufua (yuhyii) wafu; na tunaposoma Sura 3:49, tunamuona Nabii Isa (a.s), mtume wa Mwenyezi Mungu, anasema kuwa yeye naye anafufua (uhyii) wafu! Sasa basi, kwa kusema hivyo, Nabii Isa hapo alijifanya ni Mungu? Au sisi, tunapoisoma aya hiyo katika Qur'ani, huwa tunamshirikisha Nabii Isa na Mwenyezi Mungu? Jawabu ni: Ndiyo, kama tutaamini kuwa Nabii Isa (a.s) alikuwa nao uweza huo yeye mwenyewe. Lakini kama tutaamini, kama alivyoeleza yeye mwenyewe Nabii Isa katika aya yiyo hiyo, kuwa aliweza kufanya hilo "kwa idhini ya Mwenyezi Mungu" (bi idhnillaahi), hapo hatutakuwa tumemshirkisha na Mwenyezi Mungu japokuwa neno lililotumiwa kwa wote wawili -- yuhyii na uhyii -- ni lilo hilo moja.

4. Tunaposoma Sura 25:2, tunaona kuwa Mwenyezi Mungu ndiye aliyeumba kila kitu. Sisi binadamu (Sura 32:7) alituumba (khalaqa) kwa udongo, kisha (Sura 32:9) akatuvivia / akatupulizia (nafakha fiihi) roho Yake, tukawa. Hali kadhaalika Nabii Isa (a.s); kwa mujibu wa Sura 3:49 anasema, "…Ninawaumbia nyinyi (akhluqu lakum) kwa udongo, kama sura ya ndege, kisha nampuliza (anfukhu fiihi), mara anakuwa ndege …"

Jee, Nabii Isa hapo alikuwa Mungu? Au sisi Waislamu -- tunaosoma maulidi na tunaoyapinga -- tunapoisoma aya hiyo, pamoja na kuwa ametumia maneno yale yale (akhluqu lakum na anfukhu fiihi) yaliyotumiwa na Mwenyezi Mungu, humfikiria Nabii Isa (a.s) kuwa ni Mungu? Hasha! Kwa nini? Kwa sababu, katika aya hiyo hiyo, amesema kuwa ameweza kulifanya hilo "kwa idhini ya Mwenyezi Mungu" (bi idhnillaahi); si kwa uweza wake yeye mwenyewe.

Kwa mifano mine hiyo tuliyoitaja hapo juu, tumeona kwamba linalozingatiwa katika kuhukumu jambo kuwa ni shirki au la, si maneno yanayotumiliwa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake kufanana; hasha! Linalozingatiwa ni hilo tunalomnasibisha nalo Mtume, au kiumbe yoyote, linatokana na uweza alionao yeye mwenyewe kwa asili au aliopawa na Mwenyezi Mungu? Tukiamini hilo la kwanza,, itakuwa ni shirki. Tukiamini hilo la pili, itakuwa si shirki. Na hili ndilo aliloliamini Buswiri na wanaoyakubali ya Burdah: kwamba uweza alionao Mtume (s.a.w.w.) wa kutoa msaada ni wa kupawa na Mwenyezi Mungu; si wake mwenyewe kwa asili.

Inshallah wiki ijayo tutayajibu ya "Wakereketwa wa sunnah Malindi".

ABDILAHI NASSIR
P.O. BOX 84603
MOMBASA

22 Jamaadal Uulaa, 1423
2 Agosti, 2002