read

(11) Wanavyosema Wapinga Maulidi Na Majibu Yetu

Leo tunaanza kuyajibu yaliyochapishwa na "Wakereketwa wa Sunnah Malindi" kwa jina la "Majibu ya Abdillah Nassir". Makala tunayoyajibu leo ni yale ya "chapa ya kwanza". Sijui kama, baada ya hiyo, wametoa chapa nyengine kwa sababu mimi sijaziona. Kama wamezitoa, basi naomba waniletee kwa anwani yangu iliyomo humu ili niweze kuzishughulikia.

Katika makala yao hayo, walianza kwa kusema: "Tunashindwa kukuelewa tukueke wapi …"

MAJIBU: Tunalolijadili ni maulidi ni bid'a au ni haramu, au si bid'a wala si haramu? Sijadiliwi mimi niwekwe wapi. Kwani "wakereketwa" wakishajua pa kuniweka, ndio watajua hukumu ya maulidi ni ipi; ni bid'a / haramu au si bid'a / haramu?

Kisha wakasema: "… Sifa za mwanzo ilikuwa sunna, ukawa mstari wa mbele kwa kuamrisha, kufanya, kukataza lolote la uzushi au haliambatani na sheria ya Mwenyezi Mungu na Sunna ya Mtume S.A.W."

MAJIBU: Hilo ni kweli; na mpaka hii leo msimamo wangu ungali huo huo. Tafauti iliyoko hapa, baina ya "wakereketwa" na mimi, ni kwamba baadhi ya mambo wanayoyaona wao kuwa ni "uzushi", mimi siyaoni hivyo kwa sababu bid'a wanavyoielewa wao sivyo ninavyoielewa mimi. Kwa ajili hii, katika uhai wangu wote mpaka hapa nilipofika, sijapata kupinga maulidi hata siku moja. Kinyume cha hilo, nimekuwa nikihudhuria maulidini, na wakati mwengine kutoa khutba -- si hapa Mombasa tu, bali Afrika ya Mashariki nzima na hata ng'ambo, kuanzia 1955 (nilipoanza kutoa khutba hadharani) hadi hii leo. Kama uko ushahidi wa mimi kupinga maulidi, nawaomba "wakereketwa" watutolee.

Wakasema tena: "PILI: Ukawa kadiani ukapinga kwamba Mtume S.A.W siyo Mtume wa mwisho ikawa Gulam Ahmed ndiye wa mwisho kuambatana na safari yako isiyoeleweka, ukapinga kabisa thibitisho la Kuran Mtume Muhammad S.A.W kwamba ndiyo wa mwisho".

MAJIBU: Astaghfirullah! Watu hawa hawamchi Mola wao? Hayo yote ni uwongo! Kama "wakereketwa" wadai hivyo, ninawaomba wawatolee Waislamu ushahidi wao. Wangu mimi, mbali na ninayoyasema katika darasa zangu, ni kijitabu changu kiitwacho Hakika ya Ukadiani ambacho, miaka isiyopungua thalathini iliyopita, kilichapishwa na kuenezwa na National Union of Kenya Muslims wakishirikiana na Ansaar Muslim Mission ya Mombasa. Humo nilieleza uwongo wa Mirza Ghulam Ahmad na ukafiri wa Ukadiani.

Vile vile, miezi michache inayokuja inshallah, nina azma ya kuchapisha tafsiri ya Kiswahili ya Sura Al-Ahzaab ambamo ndani yake nimetoa ushahidi mwingi sana, ambao haujapatapo kuchapishwa kwa urefu hivyo kwa lugha ya Kiswahili hadi hii sasa, kuthubutisha kuwa Muhammad (s.a.w.w.) ni Mtume wa Mwisho, na kuwa hakuna mtume mwengine baada yake. Pia nimejibu kwa tafsili upotofu wote ambao Makadiani wameuandika katika maelezo yao ya Sura 33:40 katika tafsiri yao ya Kiswahili ya Qur'ani Tukufu.

Wakaendelea kusema: "TATU: Ukawa Shia, ukamkadhibisha Mwenyezi Mungu pamoja na Mtume wake S.A.W. na kwamba Jibril alifanya hiana, kwamba Qur'ani ina kasoro ukawatukana wake za Mtume S.A.W. pamoja na maswahaba zake radhia allahu anhum …"

MAJIBU: Ni kweli mimi ni Shia Ithnaashari. Hilo silifichi wala silionei aibu kwa sababu ninaamini kwamba kuwa Shia si kuwa kafiri. Nguzo tano zinazokubaliwa na Waislamu wote, mashia vile vile wanazikubali. Hali kadhaalika nguzo za imani.

Kuwa Shia "wanamkadhibisha Mwenyezi Mungu pamoja na Mtume wake S.A.W."; huo ni uwongo ulio wazi. Kwa Shia, yoyote anayefanya hivyo huwa ni kafiri wa kutiwa Motoni. Hilo ndilo lililomo katika vitabu vyao.

"Kwamba Jibril alifanya hiana"; hilo nalo pia ni uwongo. Ukisoma vitabu vya fiqhi vya madhihabi ya Shia utaona kwamba anayeamini hivyo si kafiri tu, bali ni najisi kamwe! Ngozi ya mwili wako ikigusana na ngozi ya mwili wake lazima yako uioshe. Haya! Ikiwa hiyo ndiyo imani yao, vipi watu hao watarudi waseme wao kuwa "Jibril alifanya hiana"?!

"Kwamba Qur'ani ina kasoro"; hilo pia ni uwongo. Imani ya Shia ni kama ile ya Waislamu wote: kuwa hii Qur'ani tuliyonayo sasa ndiyo ile ile iliyokuwako wakati wa Mtume Muhammad (s.a.w.w.) shilingi kwa ya pili. Haikubadilika hata kitone. Kwa maelezo zaidi juu ya jambo hili, kwa anayetaka kujua msimamo wa Shia, ninamshauri asome kitabu changu kiitwacho Shia na Qur'ani : Majibu na Maelezo, kinachoweza kupatikana bure kutoka ofisi yoyote ya Bilal Muslim Mission ya Mombasa (S.L.P. 82508) au ya Dar es Salaam (S.L.P. 20033). Humo utaona majibu ya Shia juu ya tuhuma zote juu ya Qur'ani Tukufu zinazotolewa na watu kama kina "wakereketwa".

Kuwa nimewatukana "wake za Mtume (s.a.w.w.) pamoja na maswahaba zake radhia allahu anhum"; hilo pia ni uwongo. Nimewatukana wapi? Ninawaomba "wakereketwa" watoe ushahidi wa nilipofanya hivyo.

Imani yangu mimi, na imani ya Shia wote, juu ya maswahaba nimeieleza katika kitabu changu chengine kiitwacho Shia na Sahaba : Majibu na Maelezo ambacho, vile vile, unaweza kukipata kutoka Bilal Muslim Mission. Humo nimechapisha kwa Kiarabu, pamoja na tafsiri yake ya Kiswahili, dua ya kuwaombea Mwenyezi Mungu maswahaba ambayo Shia huisoma. Kwa wale wasiolijua hilo, dua kama hiyo haipatikani katika madhihabi yoyote mengine ya Kiislamu isipokuwa ya Shia. Basi vipi watawaombea Mungu na hapo hapo wawatukane?

Inshallah yaliyobakia tutaendelea nayo wiki ijayo.

ABDILAHI NASSIR
P.O. BOX 84603
MOMBASA

29 Jamaadal Uulaa, 1423
9 Agosti, 2002