read

(2) Wanavyosema Wapinga Maulidi Na Majibu Yetu

Katika makala yetu kabla ya haya, tulijibu hujja ya kwanza ya wanaopinga maulidi. Leo tunaendelea na hujja yao ya pili.

Katika hujja yao ya pili wanasema: Maulidi hayakusomwa na maswahaba wala waandamizi wao (taabi'in). kama kweli yangelikuwa ni sawa kuyasoma, bila shaka mabwana wakubwa hao wangelikuwa ni wa mbele kufanya hivyo.

MAJIBU YETU: Hakuna Mwislamu yoyote anayekataa kuwa maswahaba ni watu watukufu. Wala hakuna anayekataa kuwa wao ndio kiungo chetu sisi na Bwana Mtume (s.a.w.w.). Lakini, pamoja na utukufu wote huo, wao walikuwa ni binadamu; hawakuwa ni ma'asumin. Walikiweza kufanya jambo, wakaswibu (wakapata); kama ambavyo walikiweza kufanya jambo, wakakosea. Na mifano ya yote mawili hayo ni mingi katika historia yao.

Kwa hivyo, kuwa tu jambo fulani halikufanywa na maswahaba, haliwi ni hujja sahihi ya kuwazuilia Waislamu kulifanya jambo hilo. Hujja ya pekee iliyo sahihi ni iwapo lile ambalo hawakulifanya wao, waliacha kulifanya kwa sababu ndivyo alivyoamrisha Mwenyezi Mungu na Mtume Wake (s.a.w.w.), au waliacha kulifanya kwa sababu linapingana na maamrisho ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake (s.a.w.w.). Ikiwa walifanya hivyo ndipo jambo hilo litakapokuwa ni hujja; lakini si kwa sababu ya kuwa halikufanywa na maswahaba, bali ni kwa sababu tu ya kuwa ndivyo alivyoamrisha Mwenyezi Mungu na Mtume Wake (s.a.w.w.), au ni kwa sababu tu ya kuwa linapingana na mafunzo ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake (s.a.w.w.) -- na hivyo ndivyo Kiislamu.

Kwa hivyo si sawa kuyapinga maulidi kwa sababu tu hayakusomwa na maswahaba na waandamizi wao. La sawa ni kuyapinga kwa sababu tu yamekatazwa na Mwenyezi Mungu au Mtume Wake (s.a.w.w.), au yanapingana na maamrisho yao. Na hilo, mpaka hivi sasa, wapinzani wa maulidi hawajaweza kulithubutisha.

Tunasema hivyo kwa sababu, mmoja kati ya misingi muhimu ya sharia ya Kiislamu, inyaokubaliwa na wanazuoni wa wanaosoma maulidi na wale wa wanaopinga maulidi, ni kwamba -- tunapokuja kwenye mambo kama ya maulidi, ujenzi wa msikiti, mavazi, na kadhaalika -- kila kitu ni halali mpaka kithubutishwe kuwa ni haramu. Kwa hivyo, kwa msingi huu, uharamu wa maulidi haitaki uthubutishwe na wanaoyasoma, bali inataka uthubutishwe na wanaoyapinga. Wala wasilithubutishe hilo kwa vichwa vyao (Sura 16:116), bali kwa kutoa ushahidi wa maneno ya Mwenyezi Mungu au Mtume Wake s.a.w.w. (Sura 4:59). Na hilo pia, mpaka dakika hii, wapinzani wa maulidi hawajaweza kulifanya.

Mwanzo mwanzo wa kuzuka madhihabi haya ya kupinga maulidi, wafuasi wake waliyapinga mambo mengi yaliyozuka katika zama zao. Kati ya mambo hayo ni kuvuta sigara, kupiga simu ya mdomo (telephone), kujiwekea kashida mbele ya mtu anaposwali, kumwamkia mtu kwa: "Umeamkaje?", kupana mikono baada ya swala, kutandika busati misikitini, na hata kuvaa nguo yenye thamani inayozidi dirhamu 100 (mia)!

Yote hayo waliyapinga kwa hujja ya kuwa hayakuwako zama za Mtume (s.a.w.w.), na kwamba hayakufanywa na maswahaba na waandamizi wao! Lakini, baada ya kutambua walikosea wapi, walirudi nyuma, wakayakubali yote hayo. Kwa maneno mengine, yakawa sio bid'a tena!

Leo, kwa hujja hizo hizo, waandamizi wao wameanza kusema vibula vivunjwe! Kesho watasema na minara nayo ivunjwe! Kesho kutwa watasema mimbari za mbao au za mawe, nazo pia ziondolewe, zirudishwe zile za vigogo vya mtende; hata vya mnazi havitafaa! Baada ya hapo ni nini kitakachowazuia wasitwambie tuondoe banka (panka) misikitini, turudi kujipepea kwa nguo zetu kama ilivyokuwa zama za Bwana Mtume (s.a.w.w.)? Au twende hijja kwa ngamia au farasi badali ya ndege? Au ni lipi litakalowazuia kutuamrisha kuisoma Qur'ani katika ngozi na mbao, kama ilivyokuwa zama za Bwana Mtume (s.a.w.w.) na maswahaba, badali ya hii miswahafu mizuri mizuri tuliyonayo?

Ni matumaini yetu kwamba, kama ambavyo watangulizi wao walirudi nyuma na kuyakubali yale waliyoyafanya ni bid'a mwanzo, wao nao watafuata nyayo zao, wayaone maulidi, na mengine kama maulidi, kuwa sio bid'a iliyokatazwa na Mtume Muhammad (s.a.w.w.). Alhamdulillaah, baadhi yao wameanza kuona hivyo na kufanya sherehe za mazazi ya Bwana Mtume (s.a.w.w.). Lakini badali ya kuyaita maulidi, huyaita seera!

Inshallah, katika makala yanayofuatia, tutazijadili hujja zao nyengine.

ABDILAHI NASSIR
P.O. BOX 84603
MOMBASA

25 Rabiul Awwal, 1423
7 Juni, 2002