read

(5) Wanavyosema Wapinga Maulidi Na Majibu Yetu

Tunaendelea na hujja za wanaopinga maulidi na majibu yetu.

Katika hujja yao ya tano wanasema: Hakuna ushahidi wowote, wa Qur'ani wala Hadithi za Mtume Muhammad (s.a.w.w.), unaothubutisha usawa wa kuyasoma maulidi, sikwambii kuyatilia nguvu.

MAJIBU YETU: Katika majibu yetu ya hujja yao ya pili, tulieleza kwamba -- kwa mujibu wa msingi mmoja kati ya misingi muhimu ya sharia ya Kiislamu -- anayetakikana kuthubutisha kuwa maulidi hayafai kusomwa si anayesema yasomwe; ni anayesema yasisomwe. Kwa hivyo ushahidi wa Qur'ani na Hadithi unaotakikana si wa kutolewa na sisi tunaosema ni sawa kusoma maulidi, bali ni wa kutolewa na wao wanaoyakataza. Jee, wanao ushahidi huo? Kama wanao, twaukaribisha.

Hata hivyo, kama ushahidi wanaoutaka wapinga maulidi, wa Qur'ani na Hadithi, ni unaosema kwa kutasua (nassun qat'iyy / categorically), "Enyi mlioamini! Someni maulidi"; basi ushahidi huo hakuna. Lakini tunauliza, kwa sharia ya Kiislamu, ni lazima jambo litasuliwe katika Qur'ani au Hadithi ya Bwana Mtume (s.a.w.w.) ndipo liruhusiwe kufanywa? Jee, hakuna mambo ambayo Waislamu -- wakiwamo wanaopinga maulidi -- huyafanya pamoja na kuwa hawana ushahidi wa Qur'ani wala Hadithi zilizoyataja mambo hayo?

Kwa mfano, ni nani kati ya wanaopinga maulidi anayeweza kututolea ushahidi wa kutasua -- wa Qur'ani au Hadithi ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.) -- wa Waislamu kuruhusiwa kujenga vyuo (colleges) na vyuo vikuu? Au kutoa digrii? Au kujenga hospitali na zahanati? Au kujenga nyumba za mayatima (orphanages)? Au kuunda vyama vya ushirika? Au kuweka mashindano ya kusoma Qur'ani na kuyatolea zawadi, na mengine mengi kama hayo? Jibu ni: hakuna! Kama uko, tunaomba tutolewe. Jee, kwa kuwa hauko, ndio watakuwa Waislamu wote -- wakiwamo wanaosoma maulidi -- wanakosea kwa kuyafanya mambo hayo kwa sababu tu hakuna aya au Hadithi inayoyataja? Kama ni hivyo, basi kwa nini wao wanayafanya? Kama sio hivyo, basi kwa nini wanatukataza kuyasoma maulidi kwa sababu hiyo hiyo?

Katika Qur'ani na Hadithi kuna mambo ambayo uhalali wake umetasuliwa (specified). Mfano wa hayo ni kumpwekesha Mwenyezi Mungu, kuswali, kufunga (saumu), kutoa zaka, kuhiji, kuowa, kufanya biashara, kufanya uadilifu, na kadhaalika. Kuna na ambayo uharamu wake pia umetasuliwa; kama kumshirikisha Mwenyezi Mungu, kuzini, kula riba, kuiba, kudhulumu, kusema uwongo, kusengenya, na kadhaalika. Yote hayo ni mambo ambayo ushahidi wake -- wa kuyatasua khaswa -- unaweza kutolewa katika Qur'ani na / au Hadithi za Bwana Mtume (s.a.w.w.).

Kuna na ambayo hayakutasuliwa isipokuwa yametajwa kwa jumla (generally) tu. Hayo, kinyume na yale yaliyotasuliwa tuliyoyataja hapo juu, yana uwanja mkubwa wa jinsi ya kuyatekeleza maadamu hayatachanganywa na ya haramu. Hebu tuangalie mifano miwili mitatu:

1. Mayatima: Tunaposoma Qur'ani na / au Hadithi, tunaona kwamba tunahimizwa kwa jumla tuwatizame, tusiwatupe; tuwahurumie, tusiwatese. Vipi? Hilo hatukutajiwa tafsili zake isipokuwa tumeachiwa sisi, bora tu tusitie la haramu. Kwa sababu hii ndio ukaona hakuna aliyezuia kujengwa nyumba za mayatima (orphanages) japokuwa hazikutajwa kwa jina katika Qur'ani wala Hadithi za Mtume Muhammad (s.a.w.w.)!

2. Ilimu: Tunaposoma Qur'ani na / au Hadithi, tunaona jinsi tunavyohimizwa, bali kufaradhiwa, kusoma na kuitafuta ilimu popote ilipo. Hatukupawa tafsili ya namna ya kulitekeleza hilo. Kwa hivyo, maadamu hatulitii la haramu, tuko huru kusoma kwa ubao, kitabu, tepu, video, redio, runinga, mtandao, na kadhaalika; kama ambavyo tuko huru kusoma madrasa, nyumbani, msikitini, chuoni (college) au kwenye vyuo vikuu; na kama ambavyo tuko huru kukaa majamvini, vitini au madeskini. Hakuna hata mmoja wa mashekhe wa wanaopinga maulidi anayewazuia watu kuyafanya hayo, na tuliyoyataja hapo juu yanayohusu mayatima, kwa sababu tu hayakutajwa kwa jina katika Qur'ani wala Hadithi za Mtume Muhammad (s.a.w.w.)!

Basi kwa nini kuyapinga maulidi?

Inshallah, katika makala yanayofuatia haya, tutazidondoa aya za Qur'ani na Hadithi za Bwana Mtume (s.a.w.w.) ambazo, japokuwa hazikutaja maulidi kwa jina, zinaunga kwa jumla yale yanayofanywa na yanayofanyika maulidini.

ABDILAHI NASSIR
P.O. BOX 84603
MOMBASA

16 Rabiuth Thani, 1423
28 Juni, 2002