read

(6) Wanavyosema Wapinga Maulidi Na Majibu Yetu

Kama tulivyoeleza katika makala yetu ya wiki iliyopita, sio kila kitu kimetajwa kinaga ubaga katika Qur'ani na / au Hadithi. Kuna yaliyotajwa hivyo; kuna na yaliyotajwa kwa jumla, kama maulidi. Lau Waislamu (wanazuoni wao) wangekataa kila jambo ambalo halikutajwa kwa jina katika Qur'ani na / au Hadithi, wangelibaki nyuma kwa karne 14, na wasingekuwa na maendeleo yoyote.

Sasa tuje kwenye maulidi.

Japokuwa -- kama tulivyoeleza katika makala yetu ya wiki iliyopita -- maulidi hayakutajwa kwa jina katika Qur'ani wala Hadithi, lakini yamekusanya mengi yaliyoamrishwa au yaliyopendekezwa na Qur'ani na / au Hadithi. Hapa chini tutayataja baadhi yake tu:

1. Kusoma na kusikiliza Qur'ani: Tunaposoma Qur'ani (k.m. Sura 73:4 na 20), tunaona jinsi Mwenyezi Mungu anavyotuamrisha tuisome. Na tunapokuja kwenye Hadithi zake, tunaelezwa kwamba Bwana Mtume (s.a.w.w.) alikuwa akipenda sana mtu amsomee yeye Qur'ani, na yeye akisikiliza.

Jee, pale tunapoyafungua maulidi yetu kwa mmoja wetu kuisoma Qur'ani, na wengine tukawa tunamsikiliza, huwa -- kama hatukufanya la sunna -- tumefanya lipi la bid'a?

2. Kumswalia Mtume (s.a.w.w.): Katika Qur'ani Tukufu (Sura 33:56), Mwenyezi Mungu anatuamrisha tumswalie Mtume Wake (s.a.w.w.) baada ya kutwambia kuwa Yeye na Malaika Wake hufanya hivyo pia. Isitoshe! Na kila Ijumaa, khatibu hutukumbusha juu ya mimbari, kwa kututajia Hadithi ya Mtume (s.a.w.w.), kuwa yoyote atakayemswalia yeye mara moja, Mwenyezi Mungu atamswalia (atamrehemu) mtu huyo mara kumi!

Jee, katika kikao kimoja tu cha maulidi, waliohudhuria humswalia Mtume (s.a.w.w.) mara ngapi? Zidisha mara hizo kwa kumi ujue Mwenyezi Mungu hukurehemu wewe mara ngapi katika kikao hicho. Jee, ni lipi hapo -- kama halitakuwa sunna -- lililo bid'a?

3. Kumhishimu na kumtukuza Bwana Mtume (s.a.w.w.): Katika Qur'ani Tukufu (Sura 7:157), Mwenyezi Mungu anawasifu, na kuweta "wenye kufaulu", wale ambao humtukuza na kumhishimu Mtume Wake (s.a.w.w.), wakamsaidia na kuyafuata yale aliyoyaleta. Lakini tutawezaje kuyafanya hayo kama mtu mwenyewe hatumjui vilivyo?

Waswahili husema: "Jambo usilolijua ni usiku wa kiza"; na "asiyekujua hakuthamini". Kwa hivyo, bila ya kumjua Mtume (s.a.w.w.) vilivyo -- historia yake, sifa zake, cheo chake, utukufu wake, na kadhaalika -- vipi tutaweza kumthamini na kumtukuza? Ndipo wanazuoni, kwa kuwa si kila mtu aweza kusoma vitabu, wakabuni maulidi ili yawe ni chombo cha kumjulisha Bwana Mtume (s.a.w.w.) apate kuhishimiwa na kutukuzwa. Hivyo katika maulidi, watu hupata fursa ya kuelezwa yote ya Mtume (s.a.w.w.). Na kwa kuyajua hayo, watu humpenda; na kama ilivyo dasturi ya kila apendaye kumfuata yule anayempenda, watu humfuata.

Jee, kama maulidi yanasaidia watu kumjua Mtume (s.a.w.w.), kumkumbuka na kumpenda, ni lipi hapo la bid'a?

4. Kumsifu Bwana Mtume (s.a.w.w.): Tunaposoma maisha yake, tunaambiwa kwamba, miongoni mwa maswahaba, walikuwako waliotunga mashairi ya kumsifu Bwana Mtume (s.a.w.w.) ambayo walikwenda nayo mbele zake na kumsomea. Bwana Mtume (s.a.w.w.) hakuwafukuza watu hao wala hakuwakataza, bali aliwasikiliza na kuyafurahia yote waliyomsomea. Kwa kitendo hicho kwa hivyo, Bwana Mtume (s.a.w.w.) alitufungulia mlango wa kumsifu. Tafauti ya pekee iliyoko baina ya maswahaba na sisi ni kwamba wao walimsifu machoni mwake, hali sisi tunamsifu akiwa hayuko na sisi kimwili. Sasa, kwa kitendo hiki, tunafanya jambo gani ambalo halikufanywa na maswahaba na kukubaliwa na mwenyewe Bwana Mtume (s.a.w.w.)?

Kama kufanya hivyo ni bid'a, basi sunna ni ipi?

Kwa leo tukomee hapa. Inshallah wiki ijayo tutaendelea na yaliyobaki.

ABDILAHI NASSIR
P.O. BOX 84603
MOMBASA

23 Rabiuth Thani, 1423
5 Julai, 2002